Thursday, April 9, 2015

Mipango ya Mhadhara wa Keshokutwa Imekamilika

Jioni hii, nimepigiwa simu na Marci Irby wa First English Lutheran Church, Faribault, kunipa taarifa kuwa mipango ya mhadhara wangu wa keshokutwa, imekamilika. Mada yangu itakuwa kama ilivyopangwa, "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunities."

Hadi leo, watu 40 wameshajiandikisha kuhudhuria mkutano. Lakini, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wengine hungoja mpaka dakika ya mwisho, na wengine hujisajili hapo hapo kwenye mkutano.

Mama Irby kaniuliza aseme nini juu yangu wakati wa kunitambulisha. Nimemwambia kuwa ninapenda kutambulishwa au kujitambulisha kifupi, bila madoido mengi. Itatosha akitaja jina langu, uraia wangu kama m-Tanzania, na kwamba ninafundisha Chuo cha St. Olaf.

Anaweza kuongeza kuwa, zaidi ya kufundisha darasani, ninatoa ushauri kuhusu masuala ya utamaduni kwa wa-Marekani wanaoenda Afrika, iwe ni kusoma, kujitolea, au kutalii, na ninatoa ushauri huo kwa wa-Afrika wanaofika au wanaoishi Marekani.

 Mkutano utaanza saa tatu asubuhi, kama ilivyopangwa. Kwa kuzingatia kwamba zitakuwepo shughuli nyingine pia, tangu hiyo saa tatu hadi saa sita na nusu mchana, nitakuwa na muda wa nusu saa hivi kwa ajili ya mhadhara wangu. Huenda yakatokea mabadiliko.

Amesema amemaliza tu kusoma upya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaburudika na michapo iliyomo. Kwenye mkutano ataweka meza niweke vitabu hivi, kwa ajili ya wale watakaopenda kuvinunua.

Kuna uwezekano kuwa nitaonana na watu ambao wameshafika Tanzania, kama yeye mwenyewe Mama Irby, na labda wawili watatu ambao tumewahi kuonana, kama Mchungaji Joy Bussert, ambaye aliwahi kunialika kutoa mhadhara kuhusu kitabu changu kanisani kwake Immanuel Lutheran mjini St. Paul, kisha akatembelea Tanzania akiwa na binti yake mdogo.

3 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nakuombea kila la heri nenda na kurejea salama.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Shughuli ilikwenda vizuri.

Walikuwa na program ya taarifa mbali mbali, muziki na nyimbo za kidini, na halafu mimi nikatambulishwa, kama mzungumzaji rasmi wa mkutano ule.

Hapo nilienda mbele na kutoa mawazo, maoni, na mawaidha, ingawaje kwa kifupi, kwa kuzingatia muda.

Nawazia kuandika ripoti katika blogu hii, kwani, pamoja na mimi kuwatajirisha kifikra na kimtazamo, nami wamenitajirisha kwa namna hiyo hiyo.

Mbele said...

Leo nimeona taarifa kuwa Mama Marcy alifariki mwezi Aprili. Apumzike kwa amani:
https://www.parkerkohlfuneralhome.com/obituary/MarcellaMarcy-Irby#tributewall

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...