Tuesday, April 7, 2015

Mhadhara Ujao, Lands Lutheran Church

Siku zimekwenda kasi. Wiki kadhaa zimepita tangu nilipopata mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara katika mkutano wa Sinodi ya Kusini Mashariki ya Minnesota. Mkutano ulipangwa kufanyika mjini Zumbrota, kwenye Kanisa la Lands Lutheran, tarehe 11 Aprili.

Mama aliyenialika, kwa niaba ya kamati ya maandalizi, alisema kuwa wangependa niongelee masuala ambayo yameanza kujitokeza katika sharika mbali mbali za sinodi kutokana na kuingia kwa watu kutoka tamaduni mbali mbali. Aliniambia kuwa aliwahi kunisikiliza miaka kadhaa iliyopita katika kanisa lake la First English Lutheran Church, mjini Farbault, nikiongelea masuala hayo, akanunua kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Wiki zilizofuata, mama huyu nami tuliwasiliana ili kupanga mada ya mhadhara wangu. Nilitoa mapendekezo, naye aliyawasilisha kwenye kamati yao. Pendekezo walilolichagua ni "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunities."

Niliandika taarifa ya mwaliko katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Sasa siku imekarbia, nami nangojea kwa hamu kwenda kujumuika na waumini hao kutoka makanisa mbali mbali, na kuwapa mawazo na mawaidha yangu kuhusu hali wanayoikabili ya kujikuta wana watu wa tamaduni mbali mbali. Azma yao ya kutaka kujua nini cha kufanya ni mfano wa kuigwa.

Kadiri dunia inavyoendelea kubadilika kutokana na utandawazi wa leo, jamii zote zitalazimika kutafuta njia za kuishi pamoja na watu wa tamaduni tofauti. Hili ni suala ambalo nimelitafiti, kulitafakari, na kuliongelea kwa miaka mingi.

Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani. Nilijibu kama nilivyozoea, kwamba waamue wenyewe, kufuatana na uwezo wao. Nasukumwa na dhamiri yangu, kutumia vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu. Pesa si msingi.

Ningekuwa na uchu wa pesa, kama fisadi, ningesema ngoja niwakamue. Lakini mtu unayemtegemea Mungu unajiuliza: Je, tunabarikiwa kwa kutanguliza pesa mbele badala ya ubinadamu? Ninashukuru ninavyofanikiwa kuwagusa wanadamu.

No comments: