Saturday, April 18, 2015

Misahafu na Balaa Linaloitwa Dini

Si kila kinachoitwa dini ni dini. Katika historia, kumekuwepo na uovu mwingi ambao umefanyika kwa jina la dini. Hadi leo, uovu wa aina hiyo unaendelea kufanyika. Siku nyingine, panapo majaliwa, nitaleta na kuongelea mifano, kwa uwazi na haki.

Misahafu imetumika na inaendelea kutumika kuhalalisha uovu. Kwa kiasi fulani hii ni kwa sababu mtu anaweza kuzipata nukuu kutoka katika msahafu ambazo zinapingana au zina utata. Lakini vile vile ni suala la tafsiri. Wataalam wa lugha wanatueleza kuwa matumizi ya lugha yanatoa mwanya wa tafsiri mbali mbali.  

Kwa msingi huo, watu waovu wanaweza kutafsiri nukuu za msahafu kwa namna ya kuhalalisha uovu. Katika tamthilia ya Shakespeare, The Merchant of Venice, Antonio anasema, "The devil can cite Scripture for his own purpose." Shetani anaweza kunukuu msahafu kwa faida yake mwenyewe. Historia imethibitisha ukweli huo tena na tena.
 

Tatizo jingine ni imani miongoni mwa waumini wa dini kwamba kila kilichomo katika misahafu sherti kikubaliwe na kufuatwa kilivyo, bila mabadiliko. Imani hii ni chanzo cha matatizo makubwa.

Mtu ukiusoma msahafu wowote bila upendeleo wala ushabiki, utaona kuwa msahafu ulitokea katika mazingira maalum ya kihistoria, kijamii, na kitamaduni. Kuna mambo katika misahafu ambayo yalikusudiwa kwa jamii za zamani, na hayatuhusu sisi watu wa leo.

Kwa msingi huu, ni muhimu tujijengee utamaduni wa kuichambua misahafu ili tuone ni yepi yanatufaa na yepi yaliwafaa watu wa zamani lakini hayatufai sisi watu wa leo.


Mungu ametujalia akili. Tuzitumie. Mungu ametuweka katika dunia tofauti na ile ya watu wa zamani. Tuna ufahamu  na akili tofauti na watu wa zamani, katika masuala kama haki za binadamu.

Utandawazi wa leo na tekinolojia imetupa ufahamu tofauti wa ulimwengu na watu wake, ufahamu wa mahusiano tunayoyahitaji katika dunia ya leo ambayo siku hadi siku inageuka kuwa kijiji.

Je, katika mazingira hayo, ni sahihi kuishikilia misahafu neno kwa neno, kikasuku, badala ya kupambanua yale yanayotuhusu na yale yaliyowahusu watu wa zamani? Je, ukasuku huu, unaosababisha au kuhalalisha balaa juu ya balaa, na maovu ya kila aina, ndio dini?

Kwa kumalizia ujumbe wangu, napenda kusisitiza mtazamo wangu kuwa mijadala ya dini ni muhimu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

 

6 comments:

NN Mhango said...

Kaka hii mada uliyoleta inasisimua. Ukweli ni kwamba dini zilianzishwa na binadamu ili kuwatawala wenzake. Mfano wa karibu ni ile hali ya wamisionari wa Kikristo kutumiwa na wakoloni kama wapelelezi waliwezesha ukoloni kuingia Afrika kirahisi. Ukija kwenye Korani ni yale yale kuwa ni nukuu ya agano la kale iliyoandikwa kishairi ikibadilisha mambo mawili matatu. Kimsingi, dini hazina jipya zaidi ya kuendeleza ukale na kuwagawana watu ili wawatawale kwa kuwapa matumaini hata mengine yasiyoingia akilini. Ukisoma kwenye Biblia unaambiwa tukiingia peponi tutaimba milele kana kwamba wote ni wana muziki.Je wale tunaopenda kusoma kweli tutaweza kuimba badala ya kutafuta maktaba? Ukisoma Quran unaambiwa peponi kutakuwa na mito ya pombe na kila mwanaume atapewa wanawake sitini. Je mwanamke atapewa wanaume wangapi? Je wasiopenda ulevi na ngono watakuwa na lao hapa? Wengine wanasema kutakuwa na mito ya maziwa. Hii inaweza kuwavutia watu wasio na uwezo wa kunywa maziwa kila siku au watoto wachanga. Kwa ufupi ni kwamba dini hazina mchango mkubwa kwa sasa ingawa wengi wanaamini kuwa zinahimiza amani wakati amani ni jambo la mtu binafsi na jamii. Nafikia hitimisho hili kwa kuzingatia kuwa kabla ya kuja hizi dini nyemelezi za kimamboleo zilizotukana na kuharibu utamaduni wetu tuliishi kwa amani kuliko sasa. Naona niishie hapa.Mengi inshallah yatakuwa kwenye kitabu changu kijacho cha Need to decolonize education: Taking on the Grand Narrative.

Anonymous said...

Anyonymous nimerejea tena, nashukuru sana prof mbele kwa mada yako. Kwa kukolezea ni kuwa; tatizo la waumini wengi ni kufanya dini kama ushabiki, na kuweka akili mfukoni.
Kutokana na kiwango duni cha elimu ambacho muumini anakipata(hasa nchi maskini), imepelekea wengi kushindwa kufikira ipasavyo. Na hii ndio chanzo cha machafuko mengi ya dini na vurugu.
Pia na ungana na NN Mhango, kuhusu asili yetu, ambazo pamoja na ujima wake, bado zilikuwa na mengi mazuri. Hizi dini za kuletwa zimesababisha mgawanyiko mkubwa kati ya waafrika kuliko hata ukabila. Mtu anajiona yu karibu na ataonesha kumjali na kumtetea muumini mwenzake aliyeko umbali wa kilomita 5000, na atamchukia jirani yake wa nyumba ya pili. Nini hiki kama si ujuha?. Inahitaji elimu ya kufikirisha kuondokana na haya.

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani kwa mchango wako. Binafsi, navutiwa na nahimiza kila fikra inayochangamsha akili.

Mimi ni m-Katoliki. Lakini, ni mtu ninayeziheshimu dini zote. Nawaheshimu wale wasio na dini, kama ninavyowaheshimu wenye dini, kwani ninazingatia kuwa wanadamu wote ni sawa, na kila mmoja ana haki na uhuru kamili kuamini dini atakayo, kubadili dini, au kutokuwa na dini.

Masuali uliyouliza yanachangamsha akili. Ni kweli, kwa mfano, ukisikiliza jinsi hizi dini zinavyoelezea jehenam, ahera, na kadhalika utaona ni kama burudani fulani hivi.

Ingekuwa hawaishii katika magomvi na uvunjifu wa amani, hayo malumbano yao yangebaki kuwa burudani. Tatizo ni pale wanapozua uhasama, machafuko, na vita, eti wanatetea dini.

Wakati wanapopigana, hata kama ni watu wa dini moja, kila upande unamwomba Mungu aupe nguvu na ushindi. Unaona wazi namna hizi dini zinavyoweza kupumbaza akili.

Mambo ni mengi ya kuongelea. Afadhali uendelee na uandishi wa hiki kitabu, kwani kitabu angalau kinakupa fursa ya kujieleza kirefu na kwa kina.

Mbele said...


Ndugu Anonymous,

Kwa mtazamo wangu, naona umekoleza kweli tafakuri hii, na umetoa mchango ambao ni chachu ya watu kujitambua.

Kona ya Uungwana said...

Ni mada nzuri na yenye kuelimisha. Tatizo la watu wengi ni uoga wa kufikiri na kuhoji ati tu kwakuwa hii ni sehemu ya dini yake. Wengi tumeshindwa kukemea maovu ati tu kwakuwa shina na uovu huo ni dini yake. Angalia jinsi dini zilivyoingia kwetu Afrika, mababu zetu walibatizwa na kupewa Baraka tele kabla ya kupandishwa kwenye meli ni kupelekwa Amerika. Pia kuna uovu mwingi ambao ulifanywa na waarabu wakati walipokuwa wakiwakamata mababu zetu na kuwauza utumwani sawia na kutuletea dini yao. Natamani siku ambayo waafrika tutaamka usingizini na kuhoji uhalali na uovu uliopo chini ya blanketi la dini.

Mbele said...

Kona ya Uungwana, shukrani kwa ujumbe wako. Nimeona ulivyoweka ujumbe wangu katika blogu yako. Nashukuru kwa kunisaidia kuueneza mtazamo wangu.

Ni kweli kuwa mijadala ya dini haina wachangiaji wengi. Lakini, kwa bahati nzuri, hali hii haiwezi kutuzuia sisi tunaotaka kueneza mitazamo yetu.

Tekinolojia hizi za mawasiliano ziko na ni huru kwa yeyote. Nami nitaendelea kutoa mawazo yangu kwa uhuru kila nitakapojisikia kufanya hivyo, na papo hapo nawahakikishia wasomaji kuwa wana uhuru wa kuandika maoni yao katika blogu yangu hii.

Maoni yakiwa mengi, ya aina mbali mbali, yanayotofautiana na kupingana, tutatambua ukweli uko wapi. Wote tutafaidika.