Friday, March 4, 2011

Makala Yangu Imepita

Blogu yangu ni sehemu ninapoweka chochote nipendacho, hata mambo binafsi, kama kumbukumbu au hata kujifurahisha. Niliwahi kusema hivyo. Leo nina taarifa ambayo imeniletea furaha moyoni.

Niliandika siku chache zilizopita kwamba mhariri wa jarida la Monday Development alikuwa ameiomba makala yangu, "What is Development?" Baada ya kuikarabati kidogo, niliipeleka.

Ni siku chache tu zimepita, nami nimefurahi kupata ujumbe kutoka kwa msahihisha makala (copy editor) wa jarida hilo. Hakuona kitu cha kusahihisha. Badala yake ameandika: "Thank you for the thoughtful, honest and well-written article."

Kwa huku Marekani, uamuzi wa msahihisha makala ni wa mwisho kabla ya makala kuchapishwa. Taarifa kama hii inaniongezea ari ya kuendelea na jitihada ya kuandika vizuri. Ninajua kuwa ninaweza kuandika vizuri kwa ki-Ingereza. Kama andiko langu likawa si zuri, sababu itakuwa ni uvivu au kukosa muda, sio kutojua ki-Ingereza bora kinakuwaje.

Wakati moja, mwandishi Jim Heynen, ambaye tulikuwa tunafundisha wote katika idara ya ki-Ingereza hapa chuoni St. Olaf, aliiona insha yangu moja fupi, "If You Came Where I was Born," akaomba aitumie katika darasa lake la uandishi kama mfano wa uandishi bora. Aliitumia hivyo hadi alipostaafu. Kutokana na umaarufu wa huyu mwandishi, niliguswa sana na jambo hilo.

Kwa hali hiyo, sikushangaa kupata ujumbe wa msahihisha makala wa Monday Development kuhusu makala yangu. Ila nina furaha sana kutokana na ukweli kwamba mzunguko wa jarida hili ulivyo mpana, makala yangu hii italisambaza jina langu kuliko chochote kingine ambacho nimeandika hadi sasa. Ninahisi hivyo, na ninahisi makala hii fupi itanifungulia milango na fursa mbali mbali, nami sitasita kuweka taarifa hapa katika blogu yangu.

Lakini hayo hayaji kwa muujiza au kwa bahati nasibu. Ni matokeo ya kujituma na kujishughulisha kwa dhati. Pamoja na kuandika, nimejikita katika shughuli ya kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kuangalia na kutathmini uandishi wa wanafunzi na kuona makosa wanayofanya katika kutumia ki-Ingereza na kuyasahihisha imekuwa ni namna ya kujinoa mimi mwenyewe.

Hitimisho langu ni kuwa kama mimi nimefikia hatua hiyo, kutokana na juhudi, kila mtu anaweza pia, katika uwanja wake, kwa kutumia juhudi. Hakuna sababu ya kukata tamaa. Hii ndio habari yangu ya leo, habari binafsi ambayo naamini itawapa moyo wengine, hata kama ni wachache. Inatosha.

7 comments:

Albert Kissima said...

Ni kweli Prof Mbele, habari hii inahamasisha, kushawishi na kukumbusha nini chatakiwa kufanywa hasa kwa waandishi . Binafsi ninajivunia sana na uandishi wako na kupitia uyaandikayo, ni mengi ninajifunza likiwemo hili la namna bora ya uandishi.

Prof, mbali na kujifunza kupitia maandishi yako(namna uwasilishavyo kile ulichokusudia mbali na kile ukusudiacho kuelimisha ktk maandishi yako, ninaomba (kama inawezeka) uwe unatumegea (hapa bloguni) mbinu bora katika swala zima la uandishi kwa kadiri ya muda wako ili tuendelee kujiimarisha zaidi na zaidi katika tasnia hii ya uandishi. Yawezekana hili limeshafanyika na kwa namna moja ama nyingine sikulipata na kwa faida pia ya wengine. Shukrani sana.

Simon Kitururu said...

Nanukuu :``Hitimisho langu ni kuwa kama mimi nimefikia hatua hiyo, kutokana na juhudi, kila mtu anaweza pia, katika uwanja wake, kwa kutumia juhudi. Hakuna sababu ya kukata tamaa.´´- mwisho wa nukuu.

Nimefarijika sana na maneno yako hayo Prof.

Simon Kitururu said...

Samahani sikumalizia!

Asante sana Mkuu kwa kututia moyo bila kuchoka!

Mbele said...

Ndugu Kissima na Kitururu, shukrani kwa mchango wenu. Ni faraja kuona jinsi mlivyouchukulia ujumbe wangu kwa namna ya kuzingatia kuwa lengo lake lilikuwa kuwasaidia wengine.

Kama tunavyojua, watu wengine wakisoma ujumbe kama huo nilioandika wanakuwa na hisia na mtazamo tofauti, ambao Ankal Michuzi anauita usenene. Hawaamini kuwa mtu anaweza kuwa na lengo la kuwasaidia wengine, ili nao wapate mafanikio. Siku zijazo, nitaandika zaidi kuhusu suala hili na kutoa mifano hai, ili kuwavuta wengi zaidi wenye mtazamo kama wenu.

Ndugu Kissima, nitazingatia ombi lako la kutoa ushauri zaidi kuhusu uandishi. Ajabu ni kwamba, ninapofundisha somo la uandishi bora wa ki-Ingereza (na wanafunzi wenyewe ni wa-Marekani, ambao hii ndio lugha yao), huwa nawaambia kuwa ninafundisha kwa vile mimi mwenyewe ninaona mafanikio katika maisha yangu.

Siwapi nadharia tu, kuhusu umuhimu wa kuandika vizuri, bali mfano hai wa mafanikio yangu mwenyewe maishani. Habari hii ya makala yangu katika jarida la "Monday Development" nimeshawaambia, kama kielelezo kimojawapo. Matokeo yake ni kuwa vijana wananisikiliza kwa makini.

Hata ninapoongea na vijana Tanzania, ninawatolea mifano hai kutokana na maisha yangu. Ni faraja kubwa kwangu pale ninapofanikiwa kugusa mioyo yao. Kwa mfano soma hapa.

mnkadebe said...

Asante Prof. Mbele. Umetutia moyo. Ombi langu ni kwamba urudi nyumbani...tunakuitaji huku,kuliko huko. Hebu angalia hii ripoti:
http://www.uwezo.net/index.php?i=139

Sijui kama wanaotufuata wataweza kuitikia wito kama usiporudi huku kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye vyuo vya juu kwa kutufundisha wafundishi!

Christian Sikapundwa said...

Ni jambo la busara Profesa,na pia linatia moyo kwa makala yako kupita.Uandishi unakarama zake kama ulizo nazo hivyo nasi wengine hatuna budi kufuata nyayo zako ingawa si kitu rahisi.

Ili kufanikiwa ni lazima kukubali kupokea masahihisho ya hapa na pale ili baadaye ufike na kitu kinacho vutia msomaji

Mbele said...

Ndugu Kadebe, shukrani kwa mawaidha yako. Ukijitahidi kutafuta habari zangu, hasa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, utapata mwanga mzuri kuhusu hayo unayoongelea.

Mimi nilifundisha pale kuanzia mwaka 1976. Hatimaye nilikuja kusoma Marekani. Baada ya masomo hayo nilirudi tena kufundisha pale. Yaliyotokea pale utaelezwa na kisa cha mimi kuondoka utaelezwa. Huwa sipendi kuelezea mimi mwenyewe.

Kukaa nje si hoja. Cha msingi ni mtu kuwa na mapenzi kwa nchi yako. Unaweza kuitumikia popote ulipo. Una wajibu wa kuitumikia popote ulipo. Napenda kukuhakikishia kuwa naitumikia nchi kwa kadiri inavyowezekana, ingawa niko hapa Marekani.

Kwa mzalendo, kukaa nchini kunaweza kuwa ni fursa ya kuitumikia nchi kwa namna hii au ile. Lakini vile vile, kuna wahujumu wa nchi na mafisadi ambao wamejichimbia hapo hapo nchini, na hawabanduki kwa sababu wanaitafuna nchi kwa urahisi kwa kuwepo hapo nchini.

Shukrani kwa kunimegea hicho kiunganishi cha tovuti. Nimepitia kidogo, ila nitaenda nipitie kila kitu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...