Friday, March 11, 2011

Mteja Nimefurahi

Juzi niliandika makala fupi, "Mteja ni Mfalme". Leo napenda kuendelea na mada hiyo, kutokana na jambo lililonitokea.

Nilipeleka kigari changu kwenye kampuni ya CarTime, kubadilisha "oil." Kama kawaida, wakati fundi anaendelea na shughuli, nilikuwa kwenye sehemu ya mapumziko ambako wateja hungojea magari yao. Baada ya muda, niliitwa na kuambiwa kuwa gari yangu tayari, nikalipia na kuchukua ufunguo. Kama kawaida, mhudumu wa hapo mapokezi alinishukuru.

Nilienda nje fundi alikopaki gari nikafungua mlango. Kwenye kiti cha mbele alikuwa ameweka karatasi ambayo picha yake nimeiweka hapa juu. Fundi makenika alikuwa ameiweka hapo. Ujumbe wake ni huu: Asante kwa kuchagua CarTime. Tumefurahi kuhudumia gari lako. Kama vile hii haitoshi, fundi ameshukuru tena na kuandika jina lake, Eric.

Katika makala yangu ya juzi niliongelea umuhimu wa kumridhisha mteja. Sasa leo hapa nimeweka mfano hai. Mimi kama mteja nimefurahi kwa huduma niliyopata. Lakini kwa hapa Marekani, hili si jambo la ajabu, kwani wenye biashara wanazingatia suala la huduma kwa mteja. Niliwahi kusema hivyo hata kwenye mahojiano niliyofanyiwa na Radio Mbao.

Kwa vile wanablogu tunafahamu kuwa blogu ni kama shule, na kwa kuzingatia kuwa watu wengi nchini wanasoma hizi blogu, nimeona niweke taarifa hii na mawazo mawili matatu yanayotakiwa kuzingatiwa na wafanyabiashara na watoa huduma wa Tanzania, ambao mara nyingi tunawalalamikia.

Niliwahi kuhudhuria semina ya biashara hapa Minnesota ambapo baadhi ya mambo yaliyosisitizwa ni kuwa unapokuwa na mteja, uwe makini sana. Ujue kuwa mteja huyu akiridhika na kufurahi, atakwenda kukutangazia biashara au huduma yako kwa marafiki na watu wengine.

Sisi wenyewe tunafanya hivyo kila siku. Tukiwa tumevaa nguo nzuri, halafu marafiki wakatuuliza tumenunua wapi, tunawatajia duka. Au watu wakituuliza hoteli nzuri iko wapi, tunawatajia. Waulize watu Dar es Salaam kitimoto safi kinapatikana wapi, watakutajia. Tukiona filamu nzuri, tunawaambia watu wengine na kuwahamasisha nao wakaione. Kwa maana hiyo, tunawapelekea wafanyabishara wateja bila wao kuingia gharama ya matangazo.

Katika semina hiyo hiyo tulionywa kwamba mteja akiudhika, atakwenda kutangaza habari mbaya kuhusu yaliyompata. Habari hiyo itaenea. Wale watakaosikia watawaambia wenzao, na inakuwa kama sumu ambayo itahujumu biashara au huduma yako.

Mimi mwenyewe mwaka jana nilikumbana na wahudumu wa ovyo katika hoteli moja mjini Arusha. Ni hoteli nzuri, na niliiipenda. Nililipia nikapelekwa chumbani. Baada ya muda kidogo nilihitaji msaada wa kurekebishiwa taa. Hapo ndipo nilipokumbana na uzembe usio kifani. Wahudumu walichelewa sana, na huenda hata walisahau. Nikawakumbusha. Bado hawakuja, nimi nikaendelea kuwangoja. Hatimaye nilienda chini walikokuweko nikaanza kuwafokea. Bosi wao naye akaja, nami nikamjumlisha katika mhadhara wangu wa jazba, nikaendelea kutema cheche na kuwapa vidonge wote. Hawakuwa na sababu kabisa ya kushindwa kutekeleza nilichokuwa nimewaambia.

Basi, kutokana na usumbufu walionipa, hata wakati huu ninapoandika sipendi hata kuiwazia hoteli ile. Inakuwa kama vile natonoshwa kidonda. Sina hamu ya kufikia tena katika hoteli ile. Bahati yao ni kuwa hapa sitataja jina lao. Wangenikoma.

Haya ndio mambo ambayo wenye biashara wanapaswa kuyaelewa na kuyazingatia. Inashangaza kwamba wengi nchini mwetu wanaamini kuwa jambo la kufanya ni kwenda kwa waganga wakapate dawa ya kuwavutia wateja. Inakuwaje sisi tuzingatie imani hizo wakati wenzetu kama hao CarTime hawatumii dawa?

7 comments:

Simon Kitururu said...

@Prof. : Labda kuna mtu ataamini hicho kikaratasi SI BURE ni aina ya kizizi kilichowangiwa na mganga fulanin unajua!:-)

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kumbe jana tulikuwa tunafanya kazi sawa. Mimi pia nilipeleka mkweche wangu kubadilisha oil. Nilipoingia kwenye gari tayari kuondoka niliona kimfuko fulani cheupe kimewekwa kitini na ndanimwe mlikuwa na vitu vya kuchezea watoto - kifarasi kidogo kinachonengua shingo unapokibinya na karata. Kulikuwa pia na ujumbe usemao "we will see you again after 3,000 miles!"

Niliondoka hapo nikitabasamu, na pengine kweli nitarudi tena baada ya hizo maili 3,000. Biashara ni saikolojia na matendo madogo kama haya yanatosha kumridhisha mteja na kumfanya aone kuwa amethaminiwa na kutendewa vyema. Hata sasa binti yangu mdogo yupo hapa anacheza na hiki kifarasi kidogo cheupe chenye shingo ya kunesanesa.

Sisi tutajifunza lini kumheshimu na kumthamini mteja?

Mbele said...

Nina kijikampuni changu kiitwacho Africonexion: Cultural Consultants ambacho nilikisajili hapa Minnesota mwezi Machi 2002. Sina mwajiriwa yeyote; kila kitu ni mimi mwenyewe, kuanzia mkurugenzi, mhasibu, afisa uhusiano, afisa mauzo, machinga, na m-Makonde wa kulinda :-)

Kampuni ya namna hii hapa Marekani inasajiliwa kama "sole proprietorship," yaani umiliki wake ni wa mtu moja.

Pamoja na hivyo, kisheria kakampuni haka kana wadhifa wa kufanya biashara na taasisi, kampuni, au mfanyabishara yeyote. Kwa mujibu wa sheria pia kakampuni haka kanatakiwa kulipa kodi kama kampuni nyingine.

Kwa nini naeleza yote hayo? Ni kwamba nimeona kuwa kuendesha kakampuni haka ni shule kabisa kwangu. Najifunza mengi na najipatia uzoefu mwingi, ikiwemo uzoefu wa kushughulika na wateja na jamii kwa ujumla. Ninanunua na kusoma vitabu, na pia nalipia warsha na kwenda kuhudhuria ili nielimike zaidi. Najifunza kwa nadharia na vitendo.

Nina uzoefu na fikra tofauti na wa-Tanzania ambao hawaendi warsha mpaka wapewe posho :-)

Ninapangia kukaingiza kakampuni haka Tanzania siku zijazo. Ndoto yangu si tu kutoa huduma kwa wananchi katika masuala muhimu ninayoshughulika nayo, bali kuwafundisha watu kuwa msingi wa mafanikio si mizizi, bali elimu, ujuzi na maarifa.

Ngoja niendelee na hii shule, maana wahenga walisema maneno mengi hayavunji mfupa :-)

chib said...

Somo hili linatakiwa kuletwa hapa Rwanda, kwani mimi naona sehemu nyingi mteja ni karaha!

Mbele said...

Ndugu Chib, shukrani kwa kutupanua upeo wa mawazo yetu.

Unknown said...

Prof. unaendelea kunifumbua macho hasa hapa kwetu TZ wahudumu wengi hasa mahotelini wanashindwa kuwahudumia wateja wao vizuri kwa hasa kiachoitwa uzembe wa usimamizi wa shughuli.
unaweza kuagiza pengine chai ambayo kikombe ni tsh 500 , lakini mhudumu akakwambia kama hauna chanchi chai ni tsh 1,000. kweli jamii tunahitajika kubadili mtazamo wa shughuli yoyote tunayoifanya kila siku ili kuleta tija

Mbele said...

Ndugu Emmanuel Karengi,

Shukrani kwa kutembelea "hapa kwetu" na kuacha ujumbe. Ukipitia pitia blogu hii utagundua kuwa ninaongelea sana vitabu na kuhimiza usomaji wa vitabu. Wafanya biashara wetu, wajasiriamali, watoa huduma, wangeweza kujifunza mengi ya manufaa kwa kusoma vitabu. Tuko, na tunaendelea kuingia, katika ulimwengu ambao ni wa "knowledge economy," nami nimekuwa nikielezea hayo katika blogu hii. Inasikitisha kuwa ukweli huu kuhusu " knowledge economy" kwa ujumla haufahamiki Tanzania. Watu wanatarajia mafanikio makubwa wakati wamezama katika Ujinga, ubabaishaji, na ushirikina. Hata blogu ambayo inahamasisha usomaji wa vitabu na utafutaji wa elimu haiwavutii wasomaji kama blogu za udaku.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...