Wednesday, March 9, 2011

Mteja ni Mfalme

Kwamba mteja ni mfalme ni dhana inayojulikana, hata kama wengi wenye biashara hawaifuati. Mantiki ya usemi kuwa mteja ni mfalme iko wazi, kwamba mteja akiridhika anakuwa ndio mpiga debe wako, bila wewe kumlipa chochote. Kwa hivi, kama wewe ni mfanyabiashara, ukiwa na tabia ya kumridhisha kila mteja, utafanikiwa.

Kwa kawaida nadharia ni rahisi, ila utekelezaji unaweza kuwa mtihani mgumu. Hayo ninayaona wakati huu ninapoandika makala hii. Kuna mtu ameanza mawasiliano nami, kunialika nikazungumze kwenye kampuni anapofanyia kazi, kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans.

Ingawa nimethibitisha kuwa shughuli hii itafanyika, nimeona kuwa huyu mhusika hana uzoefu mzuri katika kupanga mipango ya aina hii. Nimeanza kupata usumbufu fulni, kwani wakati fulani anasema kitu nami nikadhani nimemwelewa, kumbe baadaye inaonekana hatukuelewana. Hata tarehe aliyopangia tufanya hiyo shughuli ameniambia kuwa imebidi waibadili.

Ninajua kabisa kuwa hatimaye nitaenda kutoa huo mhadhara, lakini usumbufu unanikera. Sasa hapo ndipo suala la mteja ni mfalme linapoingia. Mimi ninatoa huduma ya ushauri katika masuala kama haya niliyoongelea katika kitabu changu. Nimesajili kijikampuni kiitwacho Africonexion hapa Minnesota na huduma nazitoa chini ya kivuli cha kampuni hiyo. Huduma hizo ni pamoja na ushauri, warsha, na vitabu.

Sasa basi, kwa mujibu wa dhana ya kwamba mteja ni mfalme, ni wazi kuwa nawajibika kuwa sambamba na huyu jamaa anayenisumbua, nimsikilize vizuri muda wote na kuongea naye kwa uchangamfu, kama vile hakuna kinachonikera. Kero zake nizione kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu katika kuwashughulikia wateja na kuimarisha sifa ya kikampuni changu.

Najua kuwa pamoja na yote, kikampuni changu kitafaidika. Kwanza, malipo tumeshapatana, na maandalizi yake yameanza. Siku itakapofika, nitaenda kutoa mhadhara wa kusisimua na kuelimisha. Wao watafaidika, nami nitajipatia wapiga debe wengi.
(Katuni ni ya Nathan Mpangala)

5 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kwa Tanzania huu unabakia kuwa ni msemo tu usio na maana; na katuni hii ya Mpangala iko sahihi.

Kila mahali watu wanaangalia hadhi yako kwanza kabla ya kukuhudumia. Ukiwa umevaa vizuri (wanaita kupiga pamba) pengine utapata unafuu kidogo, lakini cha muhimu zaidi ni kufahamika na au kutoa rushwa. Inafikia mahali hata kufungua akaunti benki au kununua tiketi ya ndege tu mtu unasumbuliwa.

Halafu yakija makampuni kutoka nje (mf. jirani zetu Kenya), yanafanya vizuri sana na mwishowe tunaanza kupiga makelele kwamba yanapendelewa. Kumbe, pamoja na mambo mengine, yanajua misingi ya biashara na yanajua kuwa wateja wao ni wafalme.

Sisi hatimaye tunaishia kwenda kwa waganga wa kienyeji ili kusafisha nyota zetu, kumbe nyota hizo tumezitia gubu sisi wenyewe kwa kuwa na kiburi katika biashara zetu. Inabidi tubadilike haraka hasa wakati huu ambapo tumeingia katika Jumuia ya Uchumi ya Afrika Mashariki kwa hali na mali. Vinginevyo tutaendelea kuachwa kwenye mataa!

Mbele said...

Ni kweli, katuni inatoboa ukweli uliopo Tanzania. Kuna ujinga uliokithiri wa kutotambua maana ya mteja ni nini. Mtu anatoa huduma mbovu halafu wateja wakienda kwingine, anasema washindani wake wamemloga.

Kwa hivi anafunga safari kwenda kusafisha nyota yake. Ni ujinga wa kutisha.

Huku ughaibuni, naona vitabu vingi muda wote vinavyofundisha mbinu za biashara na mafanikio. Kila wiki kuna vingine vinachapishwa. Mimi mwenyewe nimekuwa nikinunua kila ninapoweza, na hata bila kununua, huwa navisomasoma kwenye maduka kama Barnes and Noble.

Matokeo yake ni kuwa sitaenda kwa mganga kusafisha nyota ya kikampuni changu. Nyota itasafishika kwa kujielimisha na kwa juhudi ya kutoa huduma bora.

Wakati wa-Tanzania wanawaogopa au kuwasemasema wa-Kenya, mimi sina wasi wasi wowote, na ninapangia kuingia nchini Kenya na kwingineko.

Yasinta Ngonyani said...

Sijui ni lini tutakuja kufunguka na kuona kwamba msingi mkubwa wa maisha na kuendelea ni jitihada. Kutokata moyo na sio kukimbilia kwa waganga wa kienyeji?

Simon Kitururu said...

ili liposananzanialakudharau mteja ingawa nimelikuta sana na nchi za Ulaya mashariki pia hasa zile nchi lilizowahi kuwa chini ya USSR!

Mbele said...

Ndugu Kitururu, hapo nimepata wazo jingine. Nadhani, kwa vile mfanyabiashara wa kwetu anakuwa ameshaenda kwa mganga kusafisha nyota, hawi na wasi wasi tena. Anajiamini kiasi cha kuwadharau wateja.

Wakati wenzetu wanaamini mteja ni mfalme, imani ya kwetu ni kuwa mganga ni mfalme :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...