Tarehe 9 mwezi huu, nilienda Chuo Kikuu cha Minnesota kutoa mhadhara. Mada niliyoombwa kuongelea ni "Embracing African and African American Culture." Hiyo ilikuwa ni fursa nyingine kwangu kuelezea mtazamo wangu juu ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika. Nilikuwa na mambo manne ya kuelezea: umuhimu wa mada ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika, umuhimu wa kutambua utata na matatizo ya uhusiano huo, umuhimu wa kuelewa tulifikaje hapa tulipo, na umuhimu wa kutafakari namna ya kusonga mbele.
Kuhusu umuhimu wa mada, nilisisitiza kwamba watu weusi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo ya pekee, tofauti na watu wengine. Nilisema kwamba waasisi wa "Pan-Africanism" walitambua jambo hilo vizuri. Kuhusu kipengele cha pili, nilitoa mifano na kufafanua migogoro na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na Wa-Afrika. Kuhusu tulivyofika hapa tulipo, niliongelea historia ya Afrika, tangu mwanzo, ambako tulikuwa jumuia moja, hadi pale watu wa Ulaya, kwa msukumo wa ubepari, walipofika na kuwachukua wa-Afrika kwa mamilioni kuwapeleka utumwani mbali na Afrika na papo hapo, kwa msukumo huo huo wa ubepari, wakavamia bara la Afrika na kulifanya makoloni.
Hapo ndipo wa-Afrika waliopelekwa Marekani wakaanza kuwa na historia tofauti na ile ya wa-Afrika waliobaki Afrika, kwani Marekani kulikuwa na mfumo wa utumwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizwaji wa aina ya pekee. Hapo ndipo tofauti kubwa lilijengeka katika pande hizo mbili katika tamaduni, mitazamo, hisia, na mambo mengi mengine. Chimbuko la misuguano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ni hilo, kwani walipitia njia tofauti. Jukumu lililopo ni kujielimisha. Wa-Afrika wajielimishe kuhusu historia ya wa-Marekani Weusi. Wajielimishe kwa dhati. Wa-Marekani Weusi wajielimishe kuhusu historia ya wa-Afrika. Wajielimishe kwa dhati. Mimi kama mwanafasihi ninafahamu kuwa fasihi ina mchango mkubwa katika elimu hiyo.
Kwa kiasi kikubwa, mhadhara huo ulifuata mwelekeo wa mhadhara niliotoa mwezi Januari katika mkusanyiko wa Nu Skool. Imekuwa ni bahati kupata fursa mbili kuelezea mawazo yangu na kusikiliza na kujadili masuali na maoni mbali mbali.
Showing posts with label Mhadhara. Show all posts
Showing posts with label Mhadhara. Show all posts
Thursday, April 12, 2018
Sunday, December 10, 2017
Maonesho ya St. Dominic Boutique, Northfield, Minnesota
Jana, November 9, shule ya St. Dominic ya hapa Northfield, ilikuwa na wageni wengi. Palifanyika maonesho ya vitu mbali mbali vya matumizi na mapambo ya nyumbani na mavazi na urembo, machapisho, kazi za sanaa. Tamasha hilo lililoitwa St. Dominique Boutique lilijumuisha watengenezaji na wauzaji wa vitu hivyo yapata 60, na watu wengi kutoka maeneo mbali mbali walifika kuangalia na kununua. Mimi nilikuwepo, nikapata fursa ya kuongea na watu juu ya maandishi, mihadhara na utoaji ushauri kuhusu masuala ya tamaduni.
Nilipofika maoneshoni na kuelekezwa kwenye sehemu niliyopangiwa, huyu mzee anayeonekana hapa kushoto alisogea hima na kunisaidia kuandaa meza yangu. Alijitambulisha kuwa alihudhuria mhadhara niliotoa katika kanisa mjini Faribault. Hapo nilikumbuka kuwa niliwahi kutoa mihadhara miwili katika kanisa liitwalo First English Lutheran Church kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni. Waumini walipata fursa ya kununua nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
Mzee huyu, ambaye alininieleza kuwa ni padri mstaafu, alikuwa na meza yake pembeni yangu. Kwa hiyo, tuliweza kuongea muda wote wa maonesho.

Kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane, watu walikuwa wanafika na kuangalia vitu na kununua, na kuongea na sisi tuliokuja kuonesha bidhaa na vitu vyetu vingine.



Huyu dada hapa kushoto alifika kwenye meza yangu na dada yake mkubwa. Tuliongea kirefu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Hatimaye huyu dada alinunua hivi viwili alivyoshika, tukapiga picha. Kama kawaida, nimejionea mwaka hadi mwaka jinsi wa-Marekani wanavyopenda vitabu. Wakishauliza bei na kutajiwa, wanatoa hela hapo hapo na kununua.

Huyu bwana hapa kushoto sikumwelewa mwanzo alipofika mezani pangu, akaangalia na kuondoka bila kusema kitu, pamoja na kwamba nilimsalimia. Baada ya dakika chache alisogea tena na kuangalia, na hakusema kitu. Kisha akakaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni yangu, bila kunisalimia. Akachukua kijidaftari mfukoni mwake, akaanza kuandika sentensi mbili tatu, akanipa. Alikuwa ananiuliza iwapo nimesikia habari za m-Marekani Andrew Foster aliyeanzisha shule Ghana kwa ajili ya wasiosikia. Nilivyosoma na kumwangalia alivyokuwa ananiangalia, nilianza kuhisi kuwa ni mlemavu. Hasikii.
Tuliendelea kuzungumza kwa maandishi, hadi mwisho, na tulipoagana, nilimwandikia ujumbe wa mwisho kumwuliza kama angependa tupige picha, tukapiga. Nitaandika kuhusu tukio hili siku nyingine, katika blogu hii.

Kama nilivyoandika katika blogu hii, kitabu changu cha Matengo Folktales kilitajwa tarehe 23 Novemba katika "Jeopardy," programu maarufu ya televisheni hapa Marekani. Baada ya kutajwa hivyo na kuleta msisimko hapa Marekani, niliamua kuitumia hiyo kama fursa.
Nilitengeneza bango lenye tamko lililokuwepo kwenye kipindi cha Jeopardy." Ilikuwa ni burudani kuwaonyesha wa-Marekani hili bango na kitabu, huku nikifanya utani kuhusu kitabu changu kuonekana "Jeopardy."

Ninaipongeza shule ya St. Dominic kwa kuandaa maonesho hayo. Ingawa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo, shughuli ilifanikiwa sana. Watu wa aina mbali mbali walifika. Ingawa shule ni ya madhehebu ya Katoliki, hapo kwenye meza yangu pekee niliweza kuongea na watu wa imani mbali mbali. Kwa kadiri nilivyoona, itakuwa vizuri iwapo maonesho haya yatakuwa endelevu kwa siku zijazo.
Saturday, August 5, 2017
Shukrani ya Global Minnesota kwa Mhadhara Wangu
Tarehe 12 Julai, nilitoa mhadhara Global Minnesota, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Nimepata barua ya shukrani kutoka Global Minnesota, iliyoandikwa tarehe 20 Julai, ambayo ni kumbukumbu nzuri kwangu. Imeandikwa:Dear Dr. Mbele
On behalf of Global Minnesota, I would like to thank you for speaking at the Global Conversations program on "African Folktales to Contemporary Authors" at the Minneapolis Central Library on July 12.
Your extensive knowledge and skillful storytelling captured and kept our audience's attention throughout the program. The program was both informative and entertaining, and the feedback we received from the attendees and our partners was extremely positive.
We were also so pleased that you brought your daughters to the program and rekindled an old MIC/GLobal Minnesota connection.
Thank you for partnering with us on this program and helping us in our mission to bring greater awareness and appreciation of African culture to the general public in Minnesota. We look forward to engaging with you again on future Global Minnesota programs!
Kwanza kabisa, mimi nina tabia ya kujitathmini mwenyewe. Pamoja na kusikiliza namna watu wengine wanavyotathmini kazi zangu, tathmini yangu mwenyewe ndiyo inayonisukuma zaidi. Kuna wakati ambapo watu wanaweza kusifia kazi yangu lakini mimi mwenyewe nikawa na mtazamo tofauti.
Pamoja na sifa nilizomwagiwa na Global Minnesota, mimi mwenyewe niliona kuwa muda wa mhadhara ulikuwa mfupi. Kwa hivyo, nilishaamua kuwafahamisha wanipangie siku nyingine na mada nyingine, niweze kuteremsha nondo za kufa mtu, kama wasemavyo wa-Tanzania vijiweni. Sasa, kwa kuwa katika barua yao nao wanapendekeza tuendelee kushirikiana katika programu zao, fursa hiyo sitailazia damu.
Napenda nihitimishe ujumbe wangu kwa kuelezea falsafa inayoniongoza. Jambo la msingi ni kwamba Global Minnesota waliponiuliza kama nitaweza kwenda kutoa mhadhara, nilikubali bila kusita. Ninatambua kuwa mimi ni mwalimu, na ufundishaji hauishii darasani bali unahitajika pia katika jamii nje ya chuo. Vipaji nilivyo navyo nilipewa na Mungu kwa ajili ya wanadamu, si kwa ajili yangu.
Sijivunii vipaji hivyo, bali ninamshukuru Mungu na kumwomba anisaidie kuvitumia kwa namna anavyotaka. Kwamba ninaamka kila asubuhi nikiwa mzima na akili timamu, ni baraka ya Mungu, kuniwezesha kufanya wajibu wangu. Ndio maana, sitilii maanani suala la malipo ninapoalikwa kwenda kutoa mhadhara, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Ninazingatia ufanisi wa hali ya juu katika shughuli ninazofanya. Mengine ni matokeo.
Wednesday, July 12, 2017
Mazungumzo Global Minnesota Kuhusu Fasihi



Leo nilikwenda Minneapolis, kwa mwaliko wa taasisi iitwayo Global Minnesota, kutoa mhadhara juu ya fasihi simulizi na andishi wa Afrika, kuanzia chimbuko lake barani Afrika hadi Marekani, ambako hii fasihi simulizi ililetwa na watu waliosafirishwa kutoka Afrika kama watumwa. Watoa mada tulikuwa wawili, mwingine ni Profesa Mzenga Wanyama anayefundisha katika chuo cha Augsburg.
Pichani hapa kushoto, tunaonekana kama ifuatavyo. Kutoka kushoto ni Tazo kutoka Zambia, ambaye alihitimu chuo cha St. Olaf mwaka jana, na amajiriwa kwa mwaka huu moja na Global Minnesota. Wa pili ni Carol, rais wa Global Minnesota. Wa tatu ni Profesa Wanyama. Wa nne ni mimi, na wa tano ni Tim, mkurugenzi wa programu wa Global Minnesota, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuniuliza kama ningekuwa tayari kutoa mhadhara Global Minnesota, wakati tulipokutana katika tamasha la Togo miezi michache iliyopita.Hapa kushoto ninaonekana nikiongea. Sina kawaida ya kusoma hotuba, hata kama nimeandika vizuri. Ninashindwa kuangalia karatasi badala ya kuangalia watu. Hata darasani, sisomi nilichoandaa kimaandishi. Katika kujiandaa kwa ajili ya kutoa mihadhara, ninaandika sana hoja na maelezo yangu. Lakini wakati wa kutoa mhadhara, ninatumia kumbukumbu tu ya yale niliyoandika.
Kwa hivyo, katika mhadhara wa leo, nimeongelea chimbuko la binadamu ambalo liliendana na uwezo kutembea wima kwa miguu tu, kutumia lugha, na kutumia na kutengeneza zana za kazi. Hayo yote kwa pamoja yalisababisha kuumbika kwa kiumbe aitwaye binadamu kimwili, kiakili, na kadhalika. Huu ndio msingi wa kukua kwa lugha na fasihi, ambayo ilihitaji ubunifu, kumbukumbu, na uwezo wa kutambua na kuunda sanaa, ikiwemo fasihi, ambayo ni sanaa inayotumia lugha.
Maendeleo ya tekinolojia, ambayo ilianzia na kutengeneza zana za mawe au miti, yalifikia hatua ya binadamu kuvumbua maandishi. Hapo ndipo ikawezekana kuandika yale yaliyokuwa katika fasihi simulizi, na ushahidi tunauona katika Misri ya miaka yapata elfu nne au tano iliyopita. Hadithi zilizoandikwa wakati ule ni kama "The Tale of Two Brothers," "The Story of Sinuhe," na "The Tale of the Ship-wrecked Sailor."
Lakini pia, uandishi ulimwezesha binadamu kutunga fasihi kimaandishi. Waandishi, hasa wa mwanzo, walikuwa wamelelewa katika fasihi simulizi, kiasi kwamba kazi zao andishi zilibeba athari za wazi za fasihi simulizi. Mifano kutoka Afrika ni The Golden Ass (Apuleus), Chaka (Thomas Mofolo), The Palm Wine Drinkard (Amos Tutuola), Things Fall Apart (Chinua Achebe), The Dilemma of a Ghost (Ama Ata Aidoo). Waandishi weusi wa bara la Marekani kama vile Zora Neal Hurston, Toni Morrison, na Edwidge Dandicat.
Baada ya mimi kuongea, alifuata Profesa Mzenga Wanyama, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto. Yeye aliongelea zaidi waandishi weusi wa Marekani, akianzia na Phyllis Wheatley. Aliongelea elimu na itikadi aliyofundishwa msichana na hata alipoandika mashairi yake, akawa anaelezea pia waandishi wa ki-Afrika kama vile Achebe na Ngugi wa Thiong'o, na Chimamanda Ngozi Adichie. Kati ya masuala aliyosisitiza ni utumwa wa fikra na umuhimu wa kujikomboa. Baada ya hotuba zetu, palikuwa na muda mfupi wa masuali na majibu.
Baada ya kikao kwisha, hawakosekani wahudhuriaji wenye kupenda kuongea zaidi na mtoa mada. Hapa kushoto niko na profesa mstaafu wa College of St. Benedict, Minnesota. Ni mzaliwa wa India. Nilimwambia kuwa nilishawahi kualikwa kwenye chuo kile kutoa mihadhara.
Hapa kushoto anaonekana Carol, rais wa Global Minnesota, na binti yangu Assumpta, ambaye aliwahi kufanya kazi na Carol, wakati taasisi ilipokuwa inaitwa International Institute of Minnesota.

Hapa kushoto niko na mama moja kutoka Brazil, ambaye ni mfanyakazi katika Minnesota Department of Human Services. Sikumbuki kama nimewahi kuongea na mama yeyote wa Brazil mwenye asili ya Afrika. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ya pekee.

Hapa kushoto niko na vijana wawili waliohitimu masomo chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha. Huyu wa kushoto kabisa ni raia wa Swaziland, na huyu wa kulia ni Tazo wa Zambia anayeonekana katika picha ya kwanza hapo juu.

Hapo kushoto niko na binti zangu, Assumpta na Zawadi. Ninafurahi wanapokuja kunisikiliza katika mihadhara. Wataweza kuelezea habari zangu kwa yeyote atakayependa kuelewa zaidi shughuli zangu katika jamii.
Nimalizie kwa kusema kuwa wakati tulipokuwa tunaagana, viongozi wa Global Minnesota walielezea nia yao ya kuniita tena kwenye program nyingine. Tim aliongezea kuwa kama angekuwa amekumbuka, vitabu vyangu vingekuwepo kwa ajili ya watu waliohudhuria mkutano wa leo. Nami nilikuwa sijawazia jambo hilo. Siku zijazo litaweza kufanyika.
Friday, July 7, 2017
Wadau Wangu Wapya
Nina furaha kama mwandishi kuwa nimejipatia wadau wapya, na ninawatambulisha hapa kama ilivyo kawaida yangu. Hao ni Brian Faloon na mkewe Kristin, wenyeji wa Rochester, Minnesota. Brian ni rais wa Rochester International Association (RIA). Kristin na mimi ni wanabodi katika bodi ya RIA, ambamo nilijiunga mwaka jana kama nilivyoelezea katika blogu hii.Baada ya mimi kujiunga na bodi, nilipata fursa ya kutoa mhadhara katika chuo kikuu cha Minnesota Rochester, mada ikiwa "Folklore as Expression of Ethics," kama nilivyoeleza katika blogu ya ki-Ingeeza. Brian alihudhuria.
Brian aliuongelea mhadhara ule katika mkutano uliofuata wa bodi ya RIA. Baada ya muda, nilipata mwaliko wa kutoa mhadhara chuo kikuu cha Winona, mwaliko ambao niliuelezea katika blogu hii. Kristin aliniuliza iwapo itawezekana yeye kuhudhuria. Niliwasiliana na waandaaji, kuwauliza iwapo ninaweza kumwalika mgeni kuhudhuria, nikajibiwa kuwa ni ruksa. Nilimweleza Kristin hivyo.
Nilisafiri tarehe 27 Juni hadi Winona, mwendo wa saa mbili. Nilivyoingia ukumbini, niliwakuta Kristi na Brian wameketi, pamoja na wasikilizaji wengine yapata 50. Nilitambulishwa na wenyeji wangu, nikatoa mhadhara kama nilivyoelezea katika blogu ya ki-Ingereza. Nilivyomaliza mhadhara na muda wa masuali na majibu, Kristin na Brian walinisogelea tukaongea. Walifurahia mhadhara. Nilivyowashukuru kwa kusafiri mwendo mrefu na kuhudhuria, walinijibu kuwa wao ni mashabiki wangu. Walichosema ni ukweli, kwani walianza kuwa wadau tangu waliposoma kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
Tarehe 4 Julai, nilipata ujumbe kutoka kwa Kristin. Kati ya mambo aliyoandika ni haya:
We greatly enjoyed hearing your presentation and thought it was very good! Thank you for letting us attend! I believe it would be an excellent presentation to do in our community and schools here in Rochester as we have the same tensions between the two groups....I would like to coordinate something when we have time. We can discuss it at the next meeting if you're interested.
Ninajivunia hao wadau wangu wapya. Moyo wangu wa kutumia ujuzi wangu kwa manufaa ya walimwengu unaniletea fursa kama hii anayoongelea Kristin. Ninazipokea fursa hizi kwa moyo mkunjufu. Ninaamini ni mipango ya Mungu, wala sijali suala la kulipwa au kutolipwa fedha, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Mungu ana mipango yake, na anasawazisha mambo.
Sunday, April 2, 2017
Mhadhara Chuo Kikuu cha Minnesota Juu ya Kitereza
Juzi tarehe 31, Dr. Charlotte (Shoonie) Hartwig na mimi tulitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Minnesota, juu ya mwandishi Aniceti Kitereza. Huyu ni mwandishi muhimu ambaye, hata hivyo, hafahamiki sana. Mama Shoonie amekuwa akiandika kitabu ambacho nami nimechangia, na mhadhara wetu ulihusu kitabu hiki ambacho tunategemea kukichapisha.Kitereza alizaliwa mwaka 1896 katika kisiwa cha Ukerewe kilichomo katika Ziwa Victoria, upande wa Tanzania. Alisomea katika shule za wamisheni, na alipomaliza aliajiriwa kazi kadhaa. Alivyozidi kukua alipata dhamira ya kuhifadhi mila na desturi za zamani za wa-Kerewe, ili zisipotee. Kama sehemu ya juhudi hiyo aliandika riwaya katika lugha ya ki-Kerewe, ambao aliukamilisha mwanzoni mwa mwaka 1945. Andiko hili ni hazina ya mila na destruà za wa-Kerewe wa zamani, ila Kitereza aliandika kwa mtindo wa hadithi ya kubuni, ili wasomaji wasichoke kusoma.
Baada ya juhudi na mahangaiko ya miaka mingi ya kutafuta mchapishaji, na kufuatia ushauri wa marafiki zake wa-Marekani, Kitereza aliutafsiri mswada wake kwa ki-Swahili. Hata hivyo, aliendelea kungoja kwa miaka mingi hadi mwaka 1980 ambapo mswada ulichapishwa kama kitabu, Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buliwhali.
Mama Shoonie ni mtu pekee aliyesalia mwenye taarifa za ndani za Kitereza, kwani yeye na mumewe, Dr. Gerald Hartwig, walimfahamu vizuri Kitereza baada ya kuonana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1968 Ukerewe. Mbali ya kukutana naye mara kwa mara miaka ile ya mwanzo, waliendelea kuandikiana barua hadi miaka ya mwisho wa maisha yake. Kitereza alikuwa hodari wa kuandika barua; ananikumbusha waandishi kama Ernest Hemingway na Shaaban Robert.
Katika mhadhara wa juzi, Mama Shoonie alielezea maisha ya Kitereza na mambo aliyofanya kama mwandishi. Maelezo yake aliyaambatanisha na picha za Kitereza, mke wake, na familia nzima ya Hartwig. Watoto wa familia ya Hartwig walikuwa wadogo sana wakati huo. Mama Shoonie alielezea kuwa Kitereza alikuwa anajituma sana katika shughuli yake ya kuhifadhi mila na destruà za wahenga kwa kusukumwa na suali ambalo alilitunga mwenyewe, "Tunawajibika kuwafundisha nini watoto wetu?"
Ilipokuja zamu yangu, nilielezea kwa ufupi uandishi wa Kitereza kwa mujibu wa mtazamo wangu kama mwana fasihi. Nilisisitiza masuala kadhaa muhimu yanayojitokeza katika taaluma ya fasihi ya Afrika, hasa suala la uandishi katika lugha za ki-Afrika na suala la tafsiri. Niligusia jinsi riwaya ya Bwana Myombekere inavyoweza kutupa mtazamo mpya kuhusu historia ya riwaya ya ki-Afrika, na jinsi inavyoweza kuchambuliwa sambamba na kazi za waandishi kama Daniel O. Fagunwa na Amos Tutuola wa Nigeria, Gakaara wa Wanjau wa Kenya, na Shaaban Robert wa Tanzania. Huu utakuwa ni mtazamo wa fasihi linganishi.
Nimesoma tafsiri ya Kitereza ya riwaya yake. Ki-Swahili chake, ingawa kinatofautiana na ki-Swahili sanifu, kina ladha na mtiririko wa hadithi simulizi za lugha za ki-Bantu kama vile lugha yangu ya ki-Matengo. Kwa msingi huo, ninaipenda tafsiri ya Kitereza. Riwaya yake imetafsiriwa kwa ki-Faransa na ki-Jermani, lakini tafsiri hizo, kwa mujibu wa Profesa Gabriel Ruhumbika, zina walakini. Kauli ya Profesa Ruhumbika ina uzito sana, kwani lugha mama yake ni ki-Kerewe na pia yeye ni mashuhuri katika uwanja wa kutafsiri.
Profesa Ruhumbika mwenyewe ametafsiri kwa ki-Ingereza riwaya ya Kitereza kama ilivyoandikwa ki-Kikerewe, na tafsiri yake imechapishwa kama Mr. Myombekere and His Wife Bugonoka, Their Son Ntulanalwo and Daughter Buliwhali. Katika kuisoma tafsiri hii, nilivutiwa nayo, sawa na nilivyovutiwa na tafsiri ya ki-Swahili ya Kitereza mwenyewe. Ni tafsiri ambayo ninapendekeza isomwe na yeyote. Hivyo hivyo, ninakipendekeza kitabu cha Mama Shoonie kijacho. Ni kitabu chenye taarifa nyingi, zikiwemo barua na picha, ambazo ulimwengu haujaziona.
Thursday, September 22, 2016
David Robinson Ahutubia Chuo Kikuu cha Minnesota
Leo mchana nilikwenda Chuo Kikuu cha Minnesota, Minneapolis, kumsikiliza David Robinson, m-Marekani Mweusi anayeishi Mbeya, Tanzania, ambako ni mkulima wa kahawa. Huyu ni mtoto wa mwisho wa mwanariadha maarufu sana wa Marekani, Jackie Robinson, ambaye alikuwa pia mpinzani shujaa wa ubaguzi na mtetezi wa haki za wa-Marekani Weusi.David Robinson aliamua kwenda kuishi Tanzania, kwenye kijiji cha Bara wilaya ya Mbozi. Alijitambulisha kwa wanakijiji akajieleza kuwa ni mtoto wa Afrika aliyepotezewa ughaibuni kwa karne kadhaa, katika utumwa, na sasa ameamua kurudi nyumbani. Wanakijiji walimpa shamba akaanza kulima kahawa. Aliungana na wanakijiji wengine, wakaanzisha chama cha ushirika kiitwacho Sweet Unity Farms
Aliongelea shughuli za chama chao cha ushirika, wanavyoshughulikia matatizo na changamoto na kujifunza. Alielezea mahusiano yao na wateja wa nchi mbali mbali, ikiwemo Marekani. Ingawa wao wako kijijini, wanashiriki katika uchumi wa ulimwengu, na ndio hali halisi ya utandawazi. Daima wanatafuta namna ya kujiweka kibiashara, pamoja na uwezo wao mdogo, katika ulimwengu ambao umetawaliwa na makampuni makubwa ya kimataifa.Pichani hapa kushoto anaonekana David Robinson, Limi Simbakalia, mwanafunzi m-Tanzania wa Chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha, na mimi.
Kuna taarifa nyingi mtandaoni juu ya David Robinson na Sweet Unity Farms, yakiwemo mahojiano naye. Taarifa moja nzuri kabisa ni hii hapa. Aidha, kuna taarifa nyingi juu ya baba yake, mwanariadha Jackie Robinson. Mfano mmoja ni filamu hii hapa chini, inayoonyesha magumu aliyopitia na alivyopambana kishujaa katika mazingira ambayo yalikuwa mabaya sana kwa wa-Marekani Weusi.
Friday, June 12, 2015
Siku ya Mhadhara Chuo Kikuu Winona Inakaribia
Leo nimeamka nikiwa nauwazia mhadhara huu kwa dhati. Nimejikuta nikijikumbusha mambo muhimu. Ninataka kwenda kutoa mhadhara madhubuti, wa kusisimua na kuelimisha. Hili huwa ni lengo langu kila ninapokubali mwaliko kama huu wa kwenda kutoa mhadhara popote.
Ninatambua wajibu wangu wa kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kama mtafiti na mwalimu kuitendea haki taaluma. Ni wajibu wangu kuwa mfano wa kuigwa na vijana wanaotafuta elimu, kama hao vijana watakaonisikiliza Chuoni Winona.
Ninatambua wajibu wangu wa kuwathibitishia wanaonialika kwamba hawakukosea kwa kunialika. Ninataka wasikilizaji wangu wakiri kuwa uamuzi wa kunialika ulikuwa sahihi. Sitaki wanaonialika na wanaonisikiliza niwaache wakisema kuwa afadhali wangemwalika mtu mwingine. Sitaki. Nataka wote wakiri kuwa mimi ndiye niliyefaa kutoa mhadhara ule. Wakiri kuwa mimi ndiye niliyefaa kujibu au kujadili masuali yao.
Ninatambua wajibu wangu mbele ya Mungu. Uhai wangu siku hadi siku, akili timamu, na vipaji alivyonipa Mungu ni dhamana kwa faida ya wanadamu. Ninapovitumia vipaji hivi ipasavyo, ninatimiza wajibu wangu kwa Mungu. Ninamtukuza Mungu. Ni furaha kwangu kutambua kwamba kutumia vipaji kwa namna hii ni kumtukuza Mungu, sawa na kusali.
Hayo ndiyo mawazo ambayo yamekuwa yakizunguka akilini mwangu tangu asubuhi. Ni aina ya mawazo yanayonisukuma nyakati kama hizi, ninapojiandaa kutekeleza mialiko. Ninapokubali mwaliko, ninafanya hivyo kwa dhati. Nikiona sitaweza kwa vigezo nilivyofafanua hapa juu, huwa nakiri tangu mwanzo ili wahusika wamtafute mtu mwingine, hata kama kwa kufanya hivyo ninajikosesha malipo yanayoendana na mwaliko.
Tuesday, April 7, 2015
Mhadhara Ujao, Lands Lutheran Church
Mama aliyenialika, kwa niaba ya kamati ya maandalizi, alisema kuwa wangependa niongelee masuala ambayo yameanza kujitokeza katika sharika mbali mbali za sinodi kutokana na kuingia kwa watu kutoka tamaduni mbali mbali. Aliniambia kuwa aliwahi kunisikiliza miaka kadhaa iliyopita katika kanisa lake la First English Lutheran Church, mjini Farbault, nikiongelea masuala hayo, akanunua kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
Wiki zilizofuata, mama huyu nami tuliwasiliana ili kupanga mada ya mhadhara wangu. Nilitoa mapendekezo, naye aliyawasilisha kwenye kamati yao. Pendekezo walilolichagua ni "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunities."
Niliandika taarifa ya mwaliko katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Sasa siku imekarbia, nami nangojea kwa hamu kwenda kujumuika na waumini hao kutoka makanisa mbali mbali, na kuwapa mawazo na mawaidha yangu kuhusu hali wanayoikabili ya kujikuta wana watu wa tamaduni mbali mbali. Azma yao ya kutaka kujua nini cha kufanya ni mfano wa kuigwa.
Kadiri dunia inavyoendelea kubadilika kutokana na utandawazi wa leo, jamii zote zitalazimika kutafuta njia za kuishi pamoja na watu wa tamaduni tofauti. Hili ni suala ambalo nimelitafiti, kulitafakari, na kuliongelea kwa miaka mingi.
Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani. Nilijibu kama nilivyozoea, kwamba waamue wenyewe, kufuatana na uwezo wao. Nasukumwa na dhamiri yangu, kutumia vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu. Pesa si msingi.
Ningekuwa na uchu wa pesa, kama fisadi, ningesema ngoja niwakamue. Lakini mtu unayemtegemea Mungu unajiuliza: Je, tunabarikiwa kwa kutanguliza pesa mbele badala ya ubinadamu? Ninashukuru ninavyofanikiwa kuwagusa wanadamu.
Sunday, March 1, 2015
Imekuwa Wiki ya Mafanikio
Wiki hii inayoisha imekuwa ya mafanikio makubwa kwangu. Napenda kwanza nifafanue kuwa dhana yangu ya mafanikio ni tofauti na ya wale wanaowazia fedha. Mimi ni mwelimishaji, darasani na katika jamii. Ni mtoa ushauri katika masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake, hasa katika dunia ya tandawazi wa leo. Ushauri huo natoa kwa njia mbali mbali, hasa maandishi na mazungumzo na watu binafsi au vikundi. Dhana yangu ya mafanikio imejengeka katika shughuli hizo.
Kwanza, nilijiandaa kwa ziara ya chuo cha South Central, mjini Mankato, ambako nilifanya mazungumzo na darasa la wanafunzi wanaojiandaa kwenda Afrika Kusini kimasomo, na halafu nikatoa mhadhara kwa wanajumuia hapo chuoni, ambao mada yake ilikuwa "Writing About Americans."
Maandalizi ya mazungumzo hayo yote yalikhusu kukusanya fikra zilizokuwa akilini mwangu na kuziweka pamoja ili kukidhi mahitaji ya mazungumzo yale. Ilikuwa rahisi kujitayarisha kwa maongezi na wanafunzi waendao Afrika Kusini. Nmaongezi ya aina hiyo na wa-Marekani wengi katika maandalizi ya kwenda Afrika.
Katika kuandaa mhadhara wa "Writing About Americans," nilijikuta ninatafakari namna ya kuwasilisha mada yangu. Hatimaye, niliamua kuzingatia uzoefu wangu wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliamua nielezee chimbuko la wazo na azma ya kuandika kitabu hicho, mchakato wa kuandika, na mambo niliyojifunza katika kuandika huko. Baada ya kuamua hivyo, nilikaa chini nikatmia dakika chache tu kuandika dondoo ambazo ningetumia katika mhadhara.
Nilipoziangalia dondoo hizo, nilijua kwa hakika kwamba nitatoa mhadhara mzuri. Na ndivyo ilivyokuwa, kama alivyoeleza Mwalimu Becky Fjelland Davis katika blogu yake. Baada ya ziara yangu, niliandika katika blogu yangu kwamba nilitegemea kuwa tathmini ya ziara yangu ingeendelea miongoni mwa wale waliohidhuria.
Ukweli wa dhana yangu umeendelea kujitokeza, na hapa napenda kuleta ujumbe ulioandikwa na mtu aliyehudhuria mhadhara wangu:
Dr. Mbele,
I attended the talk you gave at South Central and found it to be very interesting and insightful. You showed how valuable writing is in itself, by giving us a mirror of ourselves as authors.
Thank you for your willingness to share you observations of Africans and Americans as well as your own self-assessments.
I thoroughly enjoyed your talk and only wish that I could have remained loner to hear the questions from the audience.
Thank you for sharing your life and writing experiences with us at South Central College.
Baada ya ziara ya Mankato, nilijikuta nikiongea kwa njia ya Skype na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Montana, ambao walikuwa wanasoma kitabu changu cha Matengo Folktales. Niliandika kuhusu mazungumzo hayo katika blogu hii. Mazungumzo yale yalikwenda vizuri sana. Wanafunzi na mwalimu wao walifurahi, na mimi pia.
Wameendelea kuelezea furaha yao. Mwanafunzi mmoja ameniandikia hivi:
Hello Dr. Mbele!
I was a student from Professor Olsen's Skype class earlier today, my name is Sara Saxton. I'm I just wanted to say thank you so much for your time and expressing your mind to our class! I really enjoyed hearing about your definition of a classroom. I agree with the aspect of having a classroom be a "safe place" for learning. I feel as though I have experienced many things outside of the classroom, but there is nothing that compares to being able to ask questions you've always wanted to ask in a classroom. Anyway, I just wanted to let you know I really enjoyed hearing about your tales and watching you preform them. It was great!
Thank you again!!
Mwanafunzi mwingine kaniandikia hivi:
Shikamoo Dr. Mbele,
I hope I have used the greeting properly. I wanted to say thank you taking the time to speak with, and preform for our class today over Skype. Growing up in Montana there are not many oppertunities to experience the vastness of culture the world has to offer and your time and knowledge was greatly appreciated. I hope to have the chance to speak with you again someday.
Asante sana!
Kama ninavyosema mara kwa mara, blogu yangu hii ni mahali ambapo nahifadhi mambo yangu, kama vile mawazo, hisia na kumbukumbu. Nafurahi nimeandika hayo niliyoandika, muhtasari wa mafanikio niliyoyapa wiki hii inayoisha. Ni mafanikio yanayougusa moyo wangu na yenye maana kwangu kuliko fedha.
Kwanza, nilijiandaa kwa ziara ya chuo cha South Central, mjini Mankato, ambako nilifanya mazungumzo na darasa la wanafunzi wanaojiandaa kwenda Afrika Kusini kimasomo, na halafu nikatoa mhadhara kwa wanajumuia hapo chuoni, ambao mada yake ilikuwa "Writing About Americans."
Maandalizi ya mazungumzo hayo yote yalikhusu kukusanya fikra zilizokuwa akilini mwangu na kuziweka pamoja ili kukidhi mahitaji ya mazungumzo yale. Ilikuwa rahisi kujitayarisha kwa maongezi na wanafunzi waendao Afrika Kusini. Nmaongezi ya aina hiyo na wa-Marekani wengi katika maandalizi ya kwenda Afrika.
Katika kuandaa mhadhara wa "Writing About Americans," nilijikuta ninatafakari namna ya kuwasilisha mada yangu. Hatimaye, niliamua kuzingatia uzoefu wangu wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Niliamua nielezee chimbuko la wazo na azma ya kuandika kitabu hicho, mchakato wa kuandika, na mambo niliyojifunza katika kuandika huko. Baada ya kuamua hivyo, nilikaa chini nikatmia dakika chache tu kuandika dondoo ambazo ningetumia katika mhadhara.
Nilipoziangalia dondoo hizo, nilijua kwa hakika kwamba nitatoa mhadhara mzuri. Na ndivyo ilivyokuwa, kama alivyoeleza Mwalimu Becky Fjelland Davis katika blogu yake. Baada ya ziara yangu, niliandika katika blogu yangu kwamba nilitegemea kuwa tathmini ya ziara yangu ingeendelea miongoni mwa wale waliohidhuria.
Ukweli wa dhana yangu umeendelea kujitokeza, na hapa napenda kuleta ujumbe ulioandikwa na mtu aliyehudhuria mhadhara wangu:
Dr. Mbele,
I attended the talk you gave at South Central and found it to be very interesting and insightful. You showed how valuable writing is in itself, by giving us a mirror of ourselves as authors.
Thank you for your willingness to share you observations of Africans and Americans as well as your own self-assessments.
I thoroughly enjoyed your talk and only wish that I could have remained loner to hear the questions from the audience.
Thank you for sharing your life and writing experiences with us at South Central College.
Baada ya ziara ya Mankato, nilijikuta nikiongea kwa njia ya Skype na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Montana, ambao walikuwa wanasoma kitabu changu cha Matengo Folktales. Niliandika kuhusu mazungumzo hayo katika blogu hii. Mazungumzo yale yalikwenda vizuri sana. Wanafunzi na mwalimu wao walifurahi, na mimi pia.
Wameendelea kuelezea furaha yao. Mwanafunzi mmoja ameniandikia hivi:
Hello Dr. Mbele!
I was a student from Professor Olsen's Skype class earlier today, my name is Sara Saxton. I'm I just wanted to say thank you so much for your time and expressing your mind to our class! I really enjoyed hearing about your definition of a classroom. I agree with the aspect of having a classroom be a "safe place" for learning. I feel as though I have experienced many things outside of the classroom, but there is nothing that compares to being able to ask questions you've always wanted to ask in a classroom. Anyway, I just wanted to let you know I really enjoyed hearing about your tales and watching you preform them. It was great!
Thank you again!!
Mwanafunzi mwingine kaniandikia hivi:
Shikamoo Dr. Mbele,
I hope I have used the greeting properly. I wanted to say thank you taking the time to speak with, and preform for our class today over Skype. Growing up in Montana there are not many oppertunities to experience the vastness of culture the world has to offer and your time and knowledge was greatly appreciated. I hope to have the chance to speak with you again someday.
Asante sana!
Kama ninavyosema mara kwa mara, blogu yangu hii ni mahali ambapo nahifadhi mambo yangu, kama vile mawazo, hisia na kumbukumbu. Nafurahi nimeandika hayo niliyoandika, muhtasari wa mafanikio niliyoyapa wiki hii inayoisha. Ni mafanikio yanayougusa moyo wangu na yenye maana kwangu kuliko fedha.
Wednesday, March 9, 2011
Mteja ni Mfalme
Kwa kawaida nadharia ni rahisi, ila utekelezaji unaweza kuwa mtihani mgumu. Hayo ninayaona wakati huu ninapoandika makala hii. Kuna mtu ameanza mawasiliano nami, kunialika nikazungumze kwenye kampuni anapofanyia kazi, kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans.
Ingawa nimethibitisha kuwa shughuli hii itafanyika, nimeona kuwa huyu mhusika hana uzoefu mzuri katika kupanga mipango ya aina hii. Nimeanza kupata usumbufu fulni, kwani wakati fulani anasema kitu nami nikadhani nimemwelewa, kumbe baadaye inaonekana hatukuelewana. Hata tarehe aliyopangia tufanya hiyo shughuli ameniambia kuwa imebidi waibadili.
Ninajua kabisa kuwa hatimaye nitaenda kutoa huo mhadhara, lakini usumbufu unanikera. Sasa hapo ndipo suala la mteja ni mfalme linapoingia. Mimi ninatoa huduma ya ushauri katika masuala kama haya niliyoongelea katika kitabu changu. Nimesajili kijikampuni kiitwacho Africonexion hapa Minnesota na huduma nazitoa chini ya kivuli cha kampuni hiyo. Huduma hizo ni pamoja na ushauri, warsha, na vitabu.
Sasa basi, kwa mujibu wa dhana ya kwamba mteja ni mfalme, ni wazi kuwa nawajibika kuwa sambamba na huyu jamaa anayenisumbua, nimsikilize vizuri muda wote na kuongea naye kwa uchangamfu, kama vile hakuna kinachonikera. Kero zake nizione kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu katika kuwashughulikia wateja na kuimarisha sifa ya kikampuni changu.
Najua kuwa pamoja na yote, kikampuni changu kitafaidika. Kwanza, malipo tumeshapatana, na maandalizi yake yameanza. Siku itakapofika, nitaenda kutoa mhadhara wa kusisimua na kuelimisha. Wao watafaidika, nami nitajipatia wapiga debe wengi.
(Katuni ni ya Nathan Mpangala)
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...