Showing posts with label mteja. Show all posts
Showing posts with label mteja. Show all posts

Tuesday, February 6, 2018

Mteja Anapokupigia Debe

Tarehe 3 Februari, nilipata ujumbe wa barua pepe kutoka kwa dada au mama ambaye amejitambulisha kwa jina la Cynthia, ila simjui. Ameandika kuulizia kitabu changu namna hii:

Hello,

I am planning a trip to Tanzania and someone recommended your book about cultural differences between Africans and Americans. How can I purchase your book? Thank you very much.

Kwa wasiojua ki-Ingereza, tafsiri yake ni hii:

Habari

Ninapanga safari ya kwenda Tanzania na mtu fulani alikipendekeza kitabu chako juu ya tofauti za tamaduni za wa-Afrika na wa-Marekani. Nitakinunuaje kitabu chako? Shukrani sana.

Kwa mwandishi, habari ya aina hii ni habari njema. Kwamba mtu fulani ambaye alitumia hela zake kununulia kitabu chako alikisoma akaridhika au kufurahi kiasi cha kukipendekeza kwa mwingine, si jambo jepesi. Mtu anapopendekeza kitu kwa mwingine namna hii, anajiweka katika hali ya kueleweka vibaya, iwapo kile anachopendekeza hakitamridhisha huyu mwingine. Tunapendekeza vitu kwa marafiki zetu tukiwa na uhakika na hicho tunachopendekeza.

Sisi wote ni wateja wa hiki au kile, iwe ni vitu au huduma. Muda wote tunawashawishi wenzetu wakanunue kitu fulani au wanapohitaji huduma, tunawaelekeza sehemu ambayo tunaiamini. Tunapopendekeza kitu au huduma tunatoa tamko kuhusu ubora wa kile tunachopendekeza. Nimekuwa nikielezea masuala haya katika blogu hii.

Muda wote sisi binadamu tunafanya hii shughuli ya kupiga debe bila malipo. Tunafanya hiki kibarua kisicho na malipo bila hata kujitambua. Ni sehemu ya mazungumzo yetu na marafiki au watu wengine. Mwenye kuuza bidhaa au kutoa huduma anafaidika bila kutumia hela kulipia matangazo.

Hayo ni baadhi ya mawazo yangu wakati huu ninapotafakari suala la huyu mpiga debe asiyejulikana ambaye amekipendekeza kitabu changu kwa mtu huyu aitwaye Cynthia, ambaye naye simjui. Nimemjibu Cynthia nikamwambia sijui mahali alipo, lakini kitabu anaweza kukipata mtandaoni.

Wednesday, October 25, 2017

Ninangojea Mwaliko Kuelezea Tamaduni

Nimeona tangazo la chuo kimoja cha hapa Minnesota kwamba wanajiandaa kuwapeleka wanafunzi kwenye nchi moja ya Afrika. Ni programu ambayo wamekuwa nayo kwa miaka kadhaa. Kila mara, wamekuwa wakitumia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences katika maandalizi hayo, ili kufahamu mambo ya msingi ya tofauti za tamaduni. Wamekuwa wakinialika kuongea nao kabla ya safari.

Nilivyoona tangazo nilijisemea kuwa hawa watu lazima watatafuta kitabu changu tena, na watanitafuta tena, kutokana na nilivyoona siku zilizopita. Nimejifunza tangu zamani kuwa unapotoa huduma kwa mteja, toa huduma bora kiasi cha kumfanya mteja asiwe na sababu ya kutafuta huduma kwingine.

Kwa upande wangu, nilijenga uhusiano huu na wateja kwa awamu. Mwanzoni, nilikuwa ninatoa ushauri tu, hasa katika program za kupeleka wanafunzi Afrika, zinazoendeshwa na vyuo mbali mbali vya Marekani. Baadaye, nilichapisha kitabu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences,  na hicho kikawa kinawavutia wateja wapya. Si kwamba kitabu hiki kina kila kitu. Vile vile, wanaonialika hawanialiki nikawasomee hiki kitabu. Wanakuwa wameshakisoma, ila wanakuwa na shauku ya kujua zaidi kutoka kwangu mwandishi. Kitabu ni kama chambo na kianzio cha mazungumzo.

Ninaandaa kitabu kingine cha kuendeleza yaliyomo katika Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitakuwa na mwelekeo ule ule na mtindo ule ule, ila kitaibua mambo mapya. Tayari nimeshakipa jina, Chickens in the Bus, ambacho ni kichwa cha sura mojawapo katika kitabu hiki.

Friday, January 6, 2017

Namshukuru Mteja

Leo nimepita kwenye mtandao wa Amazon kuangalia vinapopatikana vitabu vyangu, nikaona ujumbe ulioandikwa jana na mteja kuhusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ni mmoja wa wateja ambao baada ya kununua na kusoma kitabu, huweka maoni yao kuhusu kitabu hapo mtandaoni.

Ninaguswa na wateja hawa na ninapenda kuwashukuru. Ninazingatia kuwa hela walizotumia kununulia kitabu changu wangeweza kuzitumia kwa mahitaji mengine. Halafu, ninawashukuru kwa kitendo chao cha kuandika maoni. Wananitangazia kitabu bila malipo bali kwa hisani yao.

Huyu mteja aliyeandika jana, anaonekana ni m-Marekani, na amesema:

Great book to compare things we do in the United States and how it differs in Africa. Some of the differences would be insulting to Africans and I would not have known it Highly recommend this book if you are traveling to Tanzania as author is from there. It is a short, easy read.

Natafsiri

Kitabu bora kwa ajili ya kufananisha mambo tufanyayo Marekani na yalivyo tofauti kwa Afrika. Baadhi ya tofauti hizo zingetafsiriwa kama utovu wa heshima kwa vigezo vya wa-Afrika, nami nisingejua. Ninakipendekeza sana kitabu hiki iwapo unasafiria Tanzania, kwani mwandishi anatoka kule. Ni kitabu kifupi, rahisi kusomwa.

Ninamshukuru mteja huyu kwa moyo wake wa kutaka kuwasaidia wengine wawe katika mstari sahihi wakiwa wageni Afrika.

Friday, June 19, 2015

Mteja Nimefurahia Huduma

Leo nilipeleka gari langu kwenye kituo cha Car Time hapa mjini Northfield kubadilishiwa "oil." Kwa hapa Marekani, inashauriwa kubadili "oil" kila baada ya kuendesha gari maili 3000. Sijui utaratibu wa Tanzania.

Kama ilivyo kawaida, nilipokewa vizuri, nikakaa sehemu ambapo wateja hungojea huduma. Baada ya dakika kama ishirini hivi, mtu aliyenipokea sehemu ya mapokezi alifika nilipokaa akachuchumaa kwa heshima zote na kuniambia kuwa mafundi walikuwa wamegundua kuwa gari langu linahitaji pia "tire rotation."

Kwa kuogopa kuwa labda ingekuwa gharama ambayo sikujiandaa kuimudu, nilimwuliza kwa utaratibu iwapo itakuwa gharama kiasi gani. Alinijibu kuwa hiyo "tire rotation" haitanigharimu. Nilimjibu kuwa nashukuru kwa huduma hiyo.

Dakika kama kumi tu baadaye. huyu jamaa aliiniita, kuniambia kuwa gari lilikuwa tayari. Alinikabidhi ufunguo na bili yangu, nikalipia, kisha nikashukuru na kuondoka zangu.

Huu ndio utamaduni niliouona hapa Marekani wa kuhudumia wateja. Nimewahi kuandika kuhusu huduma ya Car Time katika blogu hii,. Kila mahali nilipopita, hapa Marekani nimeona utamaduni huu wa kumjali mteja.

Sio mimi pekee mwenye uzoefu huo. Katika mahojiano yangu na Deus Gunza, m-Tanzania mwenzangu, tuliongelea suala hilo, tukakubaliana kuwa huu ndio utamaduni tunaouona hapa Marekani. Kwa upande wangu, nimejionea kuwa hata ukiingia baa, kama mhudumu yuko sehemu nyingine, ni kawaida kumwona meneja anakuja kwenye meza yako, kusafisha na kukuhudumia.

Katika baa za Tanzania, sijawahi kumwona meneja akifanya jambo kama hilo. Utamwona amekaa mahali anapiga gumzo na ulabu na marafiki zake, na akiona mteja umeingia na unangojea huduma, atakachofanya ni kuwaita wahudumu na kuwafokea kwa kukukalisha bila huduma. Sijawahi kumwona meneja akichukua kitambaa na kusafisha meza kwa ajili ya mteja na halafu kumletea kinywaji. Ni kama mwiko.

Kwa nini ninasimulia yote hayo? Ni kwa sababu nina nia ya dhati ya kuwasaidia wafanya biashara na watoa huduma wa Tanzania. Huduma bora kwa mteja ni msingi muhimu wa mafanikio. Hii imani kwamba mafanikio yanatokana na kwenda kwa mganga kusafisha nyota au kupata dawa ya mafanikio ni upuuzi.

Sijaona kampuni yoyote hapa Marekani inayoenda kwa waganga kutafuta dawa. Dawa muhimu ya uhakika ni kumridhisha au kumfurahisha mteja. Kama unauza bidhaa, uhakikishe bidhaa yako ni bora. Na kama biashara yako ni ya kutoa huduma, kama ile ushauri, uhakikishe huduma yako ni bora. Kwa vyovyote vile hakikisha mteja ameridhika au amefurahi. Huyu atakuwa mpiga debe wako. Ukimwudhi ataeneza habari kwa wengine na biashara yako itadhurika. Wataalam wanasema kuwa matangazo haya ya mdomo wanayofanya wateja ni msingi mkuu wa kufanikiwa au kuanguka kwa biashara.

Leo, niliporejea kutoka Car Time, nimemwelezea binti yangu Zawadi na mama watoto yote yaliyojiri, kwa furaha kubwa. Halafu jionee nilivyoandika hapa katika blogu. Nimekuwa mpiga debe wa Car Time bila wao kunilipa. Na ndivyo ilivyo katika maisha yetu. Utamsikia m-Tanzania anaisifia simu yake mpya ya "iPhone" au "smartphone" au "laptop" yake au kitu kingine, bila kutambua kuwa anaipigia debe kampuni ambayo haimlipi chochote, haimjui na wala haichangii uchumi wa Tanzania bali inajitajirisha. Tuna uwezo mkubwa sisi wateja. Laiti tungeutumia kuzitangaza bidhaa na huduma za ki-Tanzania.

Nimejifunza mengi katika kuishi hapa Marekani. Hili nililolieleza ni jambo moja. Ni elimu ambayo ninaitumia katika kuendeleza kampuni yangu ya ushauri ya Africonexion. Ninazingatia sana umuhimu wa kutoa huduma bora, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Friday, November 11, 2011

Nitakutana na Mteja Maarufu

Mara kwa mara napata fursa ya kukutana na wateja. Hao ni watu waliosoma vitabu vyangu au wanapangia kufanya hivyo au wamehudhuria mihadhara yangu. Wengine, ambao hatupati fursa ya kukutana uso kwa uso, wanawasiliana nami kwa barua pepe. Kwangu ni jambo la kushukuru, kwamba Mungu kanijalia uwezo na fursa hizo.

Siku chache zilizopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja akisema kuwa alipata taarifa zangu kutoka kwa mama mwingine wa Shepherd of the Valley Lutheran Church. Nilivyoangalia mtandaoni, nimegundua kuwa huyu aliyeniandikia ni mtu maarufu.

Wakati anaulizia kama tungeweza kukutana, alisema kuwa amenunua kitabu changu cha Africans and Americans na atakisoma hima. Anapangia kuandika kitabu kingine, na anapenda kusikia mawaidha yangu kuhusu masuala ya utamaduni katika malezi ya watoto.

Huyu namhesabu kama mteja maarufu, kwa vile anafahamika sana kutokana na shughuli zake za kuandika na kuelimisha umma. Nangojea siku tuliyopanga kukutana, wiki ijayo, nikizingatia kuwa mteja ni mfalme.

Nimalizie tu kwa kusema kuwa niliwahi kwenda Shepherd of the Valley kuongelea suala la tofauti za tamadununi. Kanisa hili lina ushirikiano na waumini wa Tungamalenga, Iringa. Nilifanya hiyo shughuli, na sikutegemea kuwa ingezua hayo niliyoeleza hapa juu. Ndivyo mambo yanavyokwenda hapa duniani. Unaweza kufanya jambo, usijue litazua nini, litaishia wapi au vipi.

Wednesday, March 9, 2011

Mteja ni Mfalme

Kwamba mteja ni mfalme ni dhana inayojulikana, hata kama wengi wenye biashara hawaifuati. Mantiki ya usemi kuwa mteja ni mfalme iko wazi, kwamba mteja akiridhika anakuwa ndio mpiga debe wako, bila wewe kumlipa chochote. Kwa hivi, kama wewe ni mfanyabiashara, ukiwa na tabia ya kumridhisha kila mteja, utafanikiwa.

Kwa kawaida nadharia ni rahisi, ila utekelezaji unaweza kuwa mtihani mgumu. Hayo ninayaona wakati huu ninapoandika makala hii. Kuna mtu ameanza mawasiliano nami, kunialika nikazungumze kwenye kampuni anapofanyia kazi, kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans.

Ingawa nimethibitisha kuwa shughuli hii itafanyika, nimeona kuwa huyu mhusika hana uzoefu mzuri katika kupanga mipango ya aina hii. Nimeanza kupata usumbufu fulni, kwani wakati fulani anasema kitu nami nikadhani nimemwelewa, kumbe baadaye inaonekana hatukuelewana. Hata tarehe aliyopangia tufanya hiyo shughuli ameniambia kuwa imebidi waibadili.

Ninajua kabisa kuwa hatimaye nitaenda kutoa huo mhadhara, lakini usumbufu unanikera. Sasa hapo ndipo suala la mteja ni mfalme linapoingia. Mimi ninatoa huduma ya ushauri katika masuala kama haya niliyoongelea katika kitabu changu. Nimesajili kijikampuni kiitwacho Africonexion hapa Minnesota na huduma nazitoa chini ya kivuli cha kampuni hiyo. Huduma hizo ni pamoja na ushauri, warsha, na vitabu.

Sasa basi, kwa mujibu wa dhana ya kwamba mteja ni mfalme, ni wazi kuwa nawajibika kuwa sambamba na huyu jamaa anayenisumbua, nimsikilize vizuri muda wote na kuongea naye kwa uchangamfu, kama vile hakuna kinachonikera. Kero zake nizione kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu katika kuwashughulikia wateja na kuimarisha sifa ya kikampuni changu.

Najua kuwa pamoja na yote, kikampuni changu kitafaidika. Kwanza, malipo tumeshapatana, na maandalizi yake yameanza. Siku itakapofika, nitaenda kutoa mhadhara wa kusisimua na kuelimisha. Wao watafaidika, nami nitajipatia wapiga debe wengi.
(Katuni ni ya Nathan Mpangala)

Friday, May 21, 2010

Mteja wa Pili wa CHANGAMOTO

Kitabu cha Changamoto kimepata mteja wa pili leo, hapo mtandaoni kinapochapishwa. Amenunua nakala tano.

Kwanza ninamshukuru mteja huyu kwa imani yake juu ya kitabu hiki, kama nilivyomshukuru mteja wa kwanza. Jambo la pili ni kuwa nafurahi kuona kuwa habari za kitabu hiki zinaenea. Hii ni ndoto na mategemeo ya kila mwandishi. Kwa upande wangu, nangojea kwa hamu mijadala itakayotokana na changamoto niliyotoa katika masuala mbali mbali ya jamii ya Tanzania na dunia ya leo.

Nikizingatia imani ya wateja, namalizia kwa kuahidi kuwa nitaendelea kujibidisha katika kuifahamu zaidi lugha hii ya ki-Swahili, ili niweze kuitumia kwa ufasaha zaidi na kuandika maandishi bora zaidi. Hii ndio shukrani yangu kwao.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...