Wednesday, July 12, 2017

Mazungumzo Global Minnesota Kuhusu Fasihi

Leo nilikwenda Minneapolis, kwa mwaliko wa taasisi iitwayo Global Minnesota, kutoa mhadhara juu ya fasihi simulizi na andishi wa Afrika, kuanzia chimbuko lake barani Afrika hadi Marekani, ambako hii fasihi simulizi ililetwa na watu waliosafirishwa kutoka Afrika kama watumwa. Watoa mada tulikuwa wawili, mwingine ni Profesa Mzenga Wanyama anayefundisha katika chuo cha Augsburg.


Pichani hapa kushoto, tunaonekana kama ifuatavyo. Kutoka kushoto ni Tazo kutoka Zambia, ambaye alihitimu chuo cha St. Olaf  mwaka jana, na amajiriwa kwa mwaka huu moja na Global Minnesota. Wa pili ni Carol, rais wa Global Minnesota. Wa tatu ni Profesa Wanyama. Wa nne ni mimi, na wa tano ni Tim, mkurugenzi wa programu wa Global Minnesota, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuniuliza kama ningekuwa tayari kutoa mhadhara Global Minnesota, wakati tulipokutana katika tamasha la Togo miezi michache iliyopita.


Hapa kushoto ninaonekana nikiongea. Sina kawaida ya kusoma hotuba, hata kama nimeandika vizuri. Ninashindwa kuangalia karatasi badala ya kuangalia watu. Hata darasani, sisomi nilichoandaa kimaandishi. Katika kujiandaa kwa ajili ya kutoa mihadhara, ninaandika sana hoja na maelezo yangu. Lakini wakati wa kutoa mhadhara, ninatumia kumbukumbu tu ya yale niliyoandika.

Kwa hivyo, katika mhadhara wa leo, nimeongelea chimbuko la binadamu ambalo liliendana na uwezo kutembea wima kwa miguu tu, kutumia lugha, na  kutumia na kutengeneza zana za kazi. Hayo yote kwa pamoja yalisababisha kuumbika kwa kiumbe aitwaye binadamu kimwili, kiakili, na kadhalika. Huu ndio msingi wa kukua kwa lugha na fasihi, ambayo ilihitaji ubunifu, kumbukumbu, na uwezo wa kutambua na kuunda sanaa,  ikiwemo fasihi, ambayo ni sanaa inayotumia lugha.

Maendeleo ya tekinolojia, ambayo ilianzia na kutengeneza zana za mawe au miti, yalifikia hatua ya binadamu kuvumbua maandishi. Hapo ndipo ikawezekana kuandika yale yaliyokuwa katika fasihi simulizi, na ushahidi tunauona katika Misri ya miaka yapata elfu nne au tano iliyopita. Hadithi zilizoandikwa wakati ule ni kama "The Tale of Two Brothers," "The Story of Sinuhe," na "The Tale of the Ship-wrecked Sailor."

Lakini pia, uandishi ulimwezesha binadamu kutunga fasihi kimaandishi. Waandishi, hasa wa mwanzo, walikuwa wamelelewa katika fasihi simulizi, kiasi kwamba kazi zao andishi zilibeba athari za wazi za fasihi simulizi. Mifano kutoka Afrika ni The Golden Ass (Apuleus), Chaka (Thomas Mofolo), The Palm Wine Drinkard (Amos Tutuola), Things Fall Apart (Chinua Achebe), The Dilemma of a Ghost (Ama Ata Aidoo). Waandishi weusi wa bara la Marekani kama vile Zora Neal Hurston, Toni Morrison, na Edwidge Dandicat.
Baada ya mimi kuongea, alifuata Profesa Mzenga Wanyama, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto. Yeye aliongelea zaidi waandishi weusi wa Marekani, akianzia na Phyllis Wheatley. Aliongelea elimu na itikadi aliyofundishwa msichana na hata alipoandika mashairi yake, akawa anaelezea pia waandishi wa ki-Afrika kama vile Achebe na Ngugi wa Thiong'o, na Chimamanda Ngozi Adichie. Kati ya masuala aliyosisitiza ni utumwa wa fikra na umuhimu wa kujikomboa. Baada ya hotuba zetu, palikuwa na muda mfupi wa masuali na majibu.

Baada ya kikao kwisha, hawakosekani wahudhuriaji wenye kupenda kuongea zaidi na mtoa mada. Hapa kushoto niko na profesa mstaafu wa College of St. Benedict, Minnesota. Ni mzaliwa wa India. Nilimwambia kuwa nilishawahi kualikwa kwenye chuo kile kutoa mihadhara.

Hapa kushoto anaonekana Carol, rais wa Global Minnesota, na binti yangu Assumpta, ambaye aliwahi kufanya kazi na Carol, wakati taasisi ilipokuwa inaitwa International Institute of Minnesota.Hapa kushoto niko na mama moja kutoka Brazil, ambaye ni mfanyakazi katika Minnesota Department of Human Services. Sikumbuki kama nimewahi kuongea na mama yeyote wa Brazil mwenye asili ya Afrika. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ya pekee.
Hapa kushoto niko na vijana wawili waliohitimu masomo chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha. Huyu wa kushoto kabisa ni raia wa Swaziland, na huyu wa kulia ni Tazo wa Zambia anayeonekana katika picha ya kwanza hapo juu.

Hapo kushoto niko na binti zangu, Assumpta na Zawadi. Ninafurahi wanapokuja kunisikiliza katika mihadhara. Wataweza kuelezea habari zangu kwa yeyote atakayependa kuelewa zaidi shughuli zangu katika jamii.

Nimalizie kwa kusema kuwa wakati tulipokuwa tunaagana, viongozi wa Global Minnesota walielezea nia yao ya kuniita tena kwenye program nyingine. Tim aliongezea kuwa kama  angekuwa amekumbuka, vitabu vyangu vingekuwepo kwa ajili ya watu waliohudhuria mkutano wa leo. Nami nilikuwa sijawazia jambo hilo. Siku zijazo litaweza kufanyika.

2 comments:

Unknown said...

Hongera sana prof. Mbele nipo nyuma najipanga kurithi mikoba. Ninafurahi sana!

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako, Daudi Mlengela. Ninavutiwa na juhudi zako. Nilivutiwa kuona umeshika andiko la Derek Walcott, "Omeros." Ukitpenda, tutaweza kubadilishana mawazo. Walcott nimemsoma kuliko waandishi wengi, na nimefundisha kazi zake hapa chuoni St. Olaf.

Msomaji na Mpiga Debe Wangu Aikwaa Tuzo

Jana niliandika taarifa za msomaji na mpiga debe wangu Joy Zenz, mKenya aishiye uJerumani. Napenda niseme kuwa juhudi zake za kuwaunganisha ...