Monday, July 17, 2017

Nina Mashairi Yote ya John Donne

Nimegundua kuwa nina mashairi yote ya John Donne. Huyu ni mshairi mmoja maarufu sana katika ki-Ingereza, ambaye aliishi miaka ya 1572-1631, na niliwahi kumtaja katika blogu hii. Niliandika habari zake siku niliponunua kitabu kiitwacho The Works of John Donne.

Lakini wikiendi hii, katika kuangalia katika msitu wa vitabu vyangu ofisini, nimegundua kitabu kiitwacho The Complete English Poems of John Donne, kilichohaririwa na C.A. Patrides. Hiki kina mashairi yake yote.

Katika utangulizi wake, Patrides amesema mambo ambayo yamenifungua macho na kunifikirisha. Amesema, kwa mfano, "The text of Donne's poetry can vex an editor into nightmares." Anamaanisha kuwa maandishi ya Donne yanaweza kumchanganya akili mhariri akaishia katika majinamizi. Hii ni kwa sababu miswada ya mashairi ya Donne ni mingi na inahitilafiana.

Niliposoma utangulizi huu, nimewazia maandishi ya William Shakespeare, ambaye aliishi wakati ule ule wa John Donne. Maandishi ya Shakespeare, hasa tamthilia, nayo yanapatikana katika miswada inayohitilafiana, na kwa miaka yote wahariri wamekuwa wakijaribu kurekebisha na kuwasilisha kile ambacho wanaamini ni andiko sahihi la Shakespeare.

Tofauti hizi katika maandishi ya Donne na Shakespeare, haziko katika maneno na sentensi tu, bali pia katika alama kama vile nukta na mikato katika sentensi. Kwa hivyo, tunavyosoma andiko la Shakespeare, tunapaswa kuzingatia kuwa kuna vitu kadha wa kadha ambavyo vimeingizwa na wahariri wa karne moja hadi nyingine.

Hata hivi, kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa mwanzo, nimeona nisome kwa makini mashairi ya Donne, hasa kwa kuzingatia kuwa nilikulia nikiwa nimesikia sana kwamba mashairi yake ni magumu. Nimepata mwamko mpya, wa kutaka kujipima akili kwa kuyakabili haya mashairi yanayosemekana ni magumu. Tena basi, nitapenda hata kujaribu kutafsiri baadhi ya mashairi haya kwa ki-Swahili, kama nilivyowahi kutamka katika blogu hii.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...