Thursday, May 25, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo nikitokea Minneapolis, nilipita Apple Valley, katika duka la vitabu la Half Price Books. Nilikuwa nimepania kununua kitabu juu ya Hemingway, Hemingway's Boat: Everything He Loved in Life, And Lost, kilichotungwa na Paul Hendrickson, ambacho nilikifahamu kwa miezi, na hivi karibuni nilikiona katika duka hilo, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Kwa hivi, leo niliombea nikikute hiki kitabu, na kwa bahati nzuri nilikikuta. Baada ya kukichukua mahali kilipokuwepo, nilienda sehemu panapouzwa vitabu kwa bei ndogo zaidi. Bila kuhangaika sana, niliona kitabu kiitwacho F. Scott Fitzgerald, kilichotungwa na Arthur Mizener.  Nilifungua kurasa mbili tatu, nikakichukua.

Nilifahamu kwa muda mrefu kuwa Fitzgerald alizaliwa St. Paul, Minnesota, mji ninaoutembelea mara kwa mara. Nilishasoma riwaya yake maarufu, The Great Gatsby. Halafu, miaka hii ambapo nimekuwa nikisoma sana maandishi na habari za Ernest Hemingway, nimeelewa kuwa haiwezekani kumtenganisha Hemingway na Fitzgerald.

Hemingway alipokuwa kijana, akiishi Paris kama ripota wa gazeti la Toronto Star na pia kama mwandishi wa hadithi fupi na riwaya, alikuwa na mahusiano ya karibu na waandishi wengine waliokuwepo Paris, kama vile Gertrude Stein, Ezra Pound, na huyu F. Scott Fitzgerald. Fitzgerald alifanya bidii kumwezesha Hemingway kuanza kuandika riwaya, akafanya juhudi zilizomfanya Marx Perkins, mhariri maarufu wa kampuni ya Scribners Sons, akachapisha riwaya ya Hemingway, The Sun Also Rises. Hayo ndiyo mawazo yaliyonifanya nikanunua kitabu hiki.

Hapo hapo, nilivutiwa na kitabu kiitwacho The Works of John Donne, kilichoandaliwa na The Wordsworth Poetry Library. Sikuwa ninakifahamu kitabu hiki. Jina la mshairi John Donne nimelifahamu tangu zamani, labda nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari. Nadhani nilishasoma mashairi yake mawili matatu, lakini sio zaidi.

Ila kwa kusoma maandishi ya wahakiki na wanataaluma, nilifahamu kuwa Donne anahesabiwa kama mshairi anayeandika mashairi magumu kuyaelewa. Habari hii ilichangia kunifanya nisiwe mwepesi wa kusoma mashairi yake. Nadhani si jambo zuri kwa mwandishi kuvumishiwa sifa kwamba tungo zake ni ngumu kueleweka. Inaweza kuwakatisha wasomaji hamu ya kujisomea maandishi ya mwandishi huyo.

Kwa Afrika, mashairi ya Christopher Okigbo yamepewa sifa hiyo. Pia mashairi ya Wole Soyinka. Lakini kwa umri nilio nao, na uzoefu wangu wa kusoma na kufundisha fasihi, naona ni vema kuwahimiza watu wajisomee wenyewe tungo zozote, kwani kwa kufanya hivyo, na kama wanafanya juhudi ya dhati, ni lazima wataambulia chochote. Nazingatia nadharia inayosema kwamba utungo wa fasihi una uwezo wa kuzalisha maana na tafsiri nyingi bila kikomo. Nadharia hii imefafanuliwa na wataalam kama Roland Barthes.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...