Showing posts with label wa-Marekani Weusi. Show all posts
Showing posts with label wa-Marekani Weusi. Show all posts

Thursday, April 12, 2018

Mhadhara Wangu Chuo Kikuu cha Minnesota

Tarehe 9 mwezi huu, nilienda Chuo Kikuu cha Minnesota kutoa mhadhara. Mada niliyoombwa kuongelea ni "Embracing African and African American Culture." Hiyo ilikuwa ni fursa nyingine kwangu kuelezea mtazamo wangu juu ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika. Nilikuwa na mambo manne ya kuelezea: umuhimu wa mada ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika, umuhimu wa kutambua utata na matatizo ya uhusiano huo, umuhimu wa kuelewa tulifikaje hapa tulipo, na umuhimu wa kutafakari namna ya kusonga mbele.

Kuhusu umuhimu wa mada, nilisisitiza kwamba watu weusi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo ya pekee, tofauti na watu wengine. Nilisema kwamba waasisi wa "Pan-Africanism" walitambua jambo hilo vizuri. Kuhusu kipengele cha pili, nilitoa mifano na kufafanua migogoro na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na Wa-Afrika. Kuhusu tulivyofika hapa tulipo, niliongelea historia ya Afrika, tangu mwanzo, ambako tulikuwa jumuia moja, hadi pale watu wa Ulaya, kwa msukumo wa ubepari, walipofika na kuwachukua wa-Afrika kwa mamilioni kuwapeleka utumwani mbali na Afrika na papo hapo, kwa msukumo huo huo wa ubepari, wakavamia bara la Afrika na kulifanya makoloni.

Hapo ndipo wa-Afrika waliopelekwa Marekani wakaanza kuwa na historia tofauti na ile ya wa-Afrika waliobaki Afrika, kwani Marekani kulikuwa na mfumo wa utumwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizwaji wa aina ya pekee. Hapo ndipo tofauti kubwa lilijengeka katika pande hizo mbili katika tamaduni, mitazamo, hisia, na mambo mengi mengine. Chimbuko la misuguano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ni hilo, kwani walipitia njia tofauti. Jukumu lililopo ni kujielimisha. Wa-Afrika wajielimishe kuhusu historia ya wa-Marekani Weusi. Wajielimishe kwa dhati. Wa-Marekani Weusi wajielimishe kuhusu historia ya wa-Afrika. Wajielimishe kwa dhati. Mimi kama mwanafasihi ninafahamu kuwa fasihi ina mchango mkubwa katika elimu hiyo.

Kwa kiasi kikubwa, mhadhara huo ulifuata mwelekeo wa mhadhara niliotoa mwezi Januari katika mkusanyiko wa Nu Skool. Imekuwa ni bahati kupata fursa mbili kuelezea mawazo yangu na kusikiliza na kujadili masuali na maoni mbali mbali.

Sunday, February 26, 2017

Mpiga Debe Wangu Kutoka Liberia

Nina jadi ya kuwatambulisha wasomaji na wapiga debe maarufu wa vitabu vyangu katika blogu hii. Ninafanya hivyo ili kuwashukuru, nikizingatia kuwa wanachangia mafanikio yangu kwa jinsi wanavyoupokea mchango wangu.

Leo ninapenda kumtambulisha Charles Chanda Dennis, raia wa Liberia ambaye anaishi hapa Marekani, jimbo la Minnesota. Huyu ni mtu maarufu, hasa katika jamii ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Ni mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi kiitwacho African Roots Connection katika KMOJ Radio.

Sikumbuki ni lini nilifahamiana na Charles, lakini nadhani ni miaka karibu kumi iliyopita. Aliwahi kunialika kama mgeni katika kipindi chake tukahojiana juu ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wiki chache zilizopita, alinialika tena, tukafanya mahojiano marefu na ya kina ambayo unaweza kuyasikiliza hapa:

https://www.dropbox.com/home?preview=Story+Telling.mp3

Miaka yapata mitano iliyopita, Charles alialikwa na wanafunzi hapa chuoni St. Olaf kutoa mhadhara juu ya historia ya mahusiano na harakati za watu wa asili ya Afrika. Nilihudhuria mhadhara ule. Charles alithibitisha kuwa ni msomi wa uhakika, mwenye uwezo mkubwa wa kuchambua mambo. Anafahamu vizuri njia waliyopitia watu weusi barani Afrika na nje ya Afrika, hasa Marekani.

Alivyonialika kwenye mahojiano safari hii, hatukuongelea angenihoji kuhusu nini hasa, bali nilihisi kuwa alitaka kufuatilia masuala ambayo ninashughulika nayo katika jamii, kama mwalimu na mtoa ushauri kuhusu tamaduni. Niliguswa na masuali yake, kama inavyosikika katika ukanda wa mahojiano niliyoweka hapa juu.

Niliguswa kwa namna ya pekee jinsi Charles alivyonitambulisha kwa wasikilizaji, akinipigia debe kwa bidii na kuwahamasisha watu wasome Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ninamshukuru kwa hilo, nikizingatia umaarufu wa kipindi chake cha African Roots Connection na KMOJ Radio kwa ujumla.

Tuesday, September 20, 2016

"The Dilemma of a Ghost:" Tamthilia ya Ama Ata Aidoo

The Dilemma of a Ghost ni tamthilia ya kwanza ya Ama Ata Aidoo wa Ghana. Aliitunga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Ghana, Legon, ikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1964, na kuchapishwa mwaka 1965. Ama Ata Aidoo aliendelea kuandika na bado anaandika, na kazi zake ni pamoja na tamthilia nyingine iitwayo Anowa, ambayo ilichapishwa mwaka 1970, hadithi fupi, na riwaya kadhaa.

The Dilemma of a Ghost inaongelea juu ya kijana wa Ghana aitwaye Ato aliyekwenda masomoni Marekani na huko akakutana na Eulalie, binti Mwamerika Mweusi. Huyu ni kati ya wale wa-Marekani Weusi wanaoiwazia Afrika kwa hamu kama mtu aliyeko ugenini anavyowazia nyumbani kwake.

Ato na Eulalie wanaoana na kurejea Ghana, ambako wanakumbana na mambo magumu. Kwanza ndugu zake Ato wanashtuka kusikia kuwa Ato ameoa bila kuwashirikisha. Halafu binti mwenyewe hana kabila wanalolitambua, na hata jina lake wanashindwa kulitamka, na kibaya zaidi, kwa mtazamo wao, ni kuwa binti huyo ni kizalia cha watumwa. Wanaukoo wanaona Ato amewasaliti.

Halafu, Eulalie naye anashindwa kuelewa na kufuata mila na desturi za hao ndugu. Wao wanamwona kama kizuka, kwa tabia zake, ikiwemo kukataa kunywesha dawa za kienyeji za kumwezesha kupata mimba. Mama mkwe wake, Esi Kom, anapofanya ukarimu wa kumletea konokono, ambao ni chakula cha heshima, Eulalie anashtuka, na haamini macho yake, na hatimaye anawatupilia mbali hao konokono. Jambo jingine linalowashangaza ndugu hao ni jinsi Eulalie anavyovuta sigara. Basi, inakuwa shida juu ya shida, na hatimaye binti anajikuta katika upweke na msongo wa mawazo.

Lakini, hatimaye, mama yake Ato anaridhia kumpokea huyu mkwe wake na anachukua hatua za kuwashawishi ndugu wote wampokee, kwa hoja kwamba mgeni hastahili kulaumiwa, bali mwenye lawama ni mwenyeji, yaani Ato. Ato anajikuta akiwa mpweke, aliyesongwa na mawazo, karibu kuchanganyikiwa. Ndivyo tamthilia inavyokwisha.

The Dilemma of a Ghost imejengeka katika mfumo wa hadithi za jadi ambazo huitwa "dilemma tales" ambao ni muundo unaowaacha wasikilizaji wakiwa na masuali yasiyojibika kirahisi. Katika tamthilia hii, suali moja muhimu ni nani wa kulaumiwa kwa matatizo yanayoibuka. Tamthilia hii inatumia pia aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo na methali. Vile vile kuna imani za jadi, kama vile juu ya mizimu na matambiko.

Ama Ata Aidoo ni mmoja wa waandishi wa ki-Afrika ambao ni hodari wa kutumia miundo na dhamira za masimulizi ya jadi. Hilo suala la kijana kujifanyia mwenyewe uamuzi wa kuoa au kuolewa bila kuwahusisha wazazi ni dhamira maarufu katika fasihi simulizi za Afrika, na matokeo ya kiburi hiki huwa si mema. Katika tamthilia ya Anowa, Ama Ata Aidoo ameiweka pia dhamira hiyo. Msichana Anowa anaamua kuolewa na kijana aliyemkuta bila wazazi kuhusika.

Tangu mwanzo, nilivutiwa na mtindo huu katika uandishi wa Ama Ata Aidoo, ambaye miaka ile alikuwa anajulikana kwa jina la Christina Ama Ata Aidoo. Ninakumbuka vizuri, kwa mfano, hadithi yake moja ya mwanzo kabisa iitwayo "In the Cutting of a Drink" ambayo niliisoma kwa mara ya kwanza miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari.

Nilivutiwa sana na hadithi hiyo kwa mtiririko wake sawa na wa mtambaji hadithi. Miaka ya baadaye, nilipojifunza somo la fasihi simulizi, nilianza kuelewa vizuri jinsi waandishi kama Ama Ata Aidoo wanavyotumia jadi hiyo.

Jambo muhimu sana jingine kuhusu Ama Ata Aidoo ni kuwa ni mwandishi mwenye kuchambua masuala ya jamii. Alivyokuwa anatunga The Dilemma of a Ghost, masuala kama ya mshikamano na mahusiano ya watu weusi ulimwenguni yaani "Pan-Africanism," yalikuwa yakivuma na kuwashughulisha viongozi maarufu kama George Padmore, W.B. Dubois, Kwame Nkrumah, Ahmed Sekou Toure, Jomo Kenyatta, na Julius Nyerere. Miaka iliyofuatia, Ama Ata Aidoo amekuwa akienda na wakati kama mwanaharakati katika masuala ya ukoloni mambo leo, haki za wanawake, na hata ujamaa. Sawa na ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere, Ama Ata Aidoo ni muumini wa fikra za kijamaa.

Saturday, June 20, 2015

Msomaji Amenilalamikia

Leo alasiri nilikwenda Brooklyn Park, Minnesota, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Tulifanyia mkutano wetu katika maktaba ya Brookdale.

Baada ya mkutano, nilipotoka nje kuelekea sehemu nilipopaki gari, alinikimbilia dada Latonya anayeonekana katika picha hapa kushoto, ambayo tulipiga miaka mitano iliyopita kwenye tamasha la Afrifest. Ni m-Marekani Mweusi kutoka Chicago, ila anaishi Minneapolis. Tulifahamiana miaka ile kwa kuwa naye alikuwa katika bodi ya Afrifest Foundation.

Hatukutegemea kama tungeonana leo, ghafla namna ile. Kwa hivi tulifurahi sana. Lakini hakupoteza muda, alianza kunihoji kwa nini siandiki sana katika blogu yangu ya ki-Ingereza kama zamani. Alisema, akimaanisha maandishi yangu ya kiSwahili, "Tunaona unaandika sana, na tunajua unaandika mambo ya maana, ila hatujui unachoandika. Inakuwa kama unatusahau marafiki zako wa-Marekani Weusi."

Kwa kweli, ingawa mazungumzo yalikuwa ya kirafiki, na hata kiutani, niliona kuwa alikuwa anaongea kwa dhati. Na sisi wa-Afrika ambao tunaishi Marekani tunafahamu kuwa wako wa-Marekani Weusi wengi ambao wanategemea sisi wa-Afrika tuwe na mshikamano nao, kama ndugu. Kwa hivi, sikuyachukulia malalamiko ya Latonya kama mzaha. Nilijikuta nikikiri kosa na kuahidi kuwa nitakuwa naandika kama zamani. Alivyowataja wa-Marekani Weusi hakuwa anatunga hadithi. Ninafahamu kuwa wanasoma maandishi yangu.

Latonya mwenyewe ni mmoja wa wafuatiliaji wa dhati wa maandishi yangu. Hapo pichani, anaonekana ameshika kitabu changu cha Africans and Americans:Embracing Cultural Differences, mara baada ya kukinunua. Maneno aliyoniambia leo yameniingia. Nilimwambia hivyo, nikaahidi kujirekebisha.

Tuesday, December 4, 2012

Nimekutana na Kobina Aidoo

Siku chache zilizopita, Kobina Aidoo kutoka Ghana alitembelea hapa Chuoni St Olaf kutoa mhadhara kama sehemu ya maazimisho ya Africa Weeks. Maazimisho hayo huandaliwa kila mwaka na jumuia ya wanafunzi iitwayo Karibu.

Sikuwa nimesikia jina la Kobina Aidoo, ila nilihudhuria mhadhara wake. Ni kijana mwenye kipaji anayeinukia katika nyanja za filamu na uanaharakati katika kuelimisha jamii.

Aliongelea suala la nani ni mw-Amerika Mweusi, akaleta changamoto nyingi zinazowakabili watu weusi wanaoishi hapa Marekani katika kujitambua na kujitambulisha. Baada ya kusema machache, alituonyesha DVD yake ambayo imajaa kauli na mitazamo ya watu weusi wanaoishi Marekani, wakiwa wametokea nchi mbali mbali za Afrika na bara la Marekani.

Ni mitazamo inayofikirisha na kuchangamsha akili. Inatupanua mawazo kuhusu utata wa suala hilo la nani ni m-Marekani Mweusi, na kwa ambaye hakufahamu, inashtua kuona migogoro baina ya waMarekani weusi wa asili na watu weusi ambao ni wahamiaji wa miaka ya karibuni nchini Marekani.

Katika picha hapo juu ninaonekana na Kobina, baada ya mhadhara wake. Tulipiga picha hii mara baada ya mimi kumkabidhi nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambayo anaonekana ameishika, na yeye akawa amenikabidhi nakala ya DVD yake.

Saturday, June 11, 2011

Waandishi Tumekutana Leo

Leo nilienda Minneapolis kushiriki mkutano wa waandishi wa-Marekani Weusi, kama nilivyoandika hapa. Mkutano huu, uliofanyika katika Center for Families, ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya vitabu ya tarehe 16 mwezi huu, katika maktaba ya Magers and Quinn. Waandaaji wa shughuli zote hizi ni Jeffrey Groves na Shatona Kilgore-Groves, wanaoonekana hapa juu.

Mkutano wa leo ulikuwa ni wa kufahamiana. Kila mtu alipata fursa ya kutoa maelezo mafupi kuhusu maisha na shughuli zake za uandishi. Baadhi ni chipukizi, ambao wamechapisha kitabu kimoja tu, na baadhi ni wazoefu, waliochapisha vitabu kadhaa. Baadhi ya vitabu vinahusu maisha binafsi; vingine vinahusu mafunzo mbali mbali, hadithi za kubuni, mashairi, na falsafa. Wengine wameandika vitabu vya watoto. Nami nilipata fursa ya kuongelea vitabu nilivyoandika.
Watu waliongelea maisha yao na kwa nini wanaandika. Baadhi, kama hao akina mama wanoonekana kushoto, wamepitia maisha machungu yasiyoelezeka, yanayowafanya baadhi ya wanadamu wajiue. Kuandika ni namna ya kujiponya ili kuendelea na maisha
Baadhi ya waandishi nilikuwa nimefahamiana nao kabla, kama vile Mahmoud el Kati, Joyce Marrie, Gerard Montgomery, na Jeff na Shatona Groves, ambao kitabu chao, A Black Parent's Memoir, ninakiandikia mapitio. Lakini imekuwa bahati leo kufahamiana na waandishi wengi kwa mpigo.

Mkutano wa leo umeleta msisimko mkubwa miongoni mwa washiriki. Tumekubaliana kuwa kukutana kwa namna hii ni hatua nzuri na muhimu; inatakiwa iwe jadi ya kuendelezwa. Kutokana na mafanikio ya mkutano wa leo, sote tunayangojea kwa hamu maonesho ya Juni 16, ambayo watu wengi wanategemewa kuhudhuria.

Tuesday, June 7, 2011

Mwaliko Nyumbani kwa Wateja Wangu

Jana jioni nilikuwa nyumbani kwa familia inayoonekana katika hii picha. Ni familia ya Shannon Gibney, mwandishi chipukizi ambaye tayari ni maarufu.

Miaka michache iliyopita, Shannon Gibney alisoma kitabu changu cha Africans and Americans, akaandika mapitio katika Minnesota Spokesman Recorder, kama nilivyosema hapa.

Siku chache zilizopita alinialika nyumbani kwake kwa chakula cha jioni, tukapanga hiyo tarehe ya jana. Aliniambia kuwa mume wake, ambaye anatoka Liberia, na bado ni mgeni hapa Marekani, amekuwa akisoma kitabu changu.

Nilifurahi kukutana na familia hii. Kwa zaidi ya saa mbili nilizokuwa nao, maongezi yetu yalihusu masuala niliyoongelea katika kitabu, yaani tofauti za tamaduni za wa-Marekani na wa-Afrika. Wote wawili wanakifahamu vizuri sana kitabu hiki, na walikuwa wananikumbusha mengi, ingawa mimi ndiye mwandishi.

Huyu bwana aliezea mshangao wake kwa jinsi maelezo ya kitabu hiki yanavyofanana na hali ya Liberia, ingawa mimi mwandishi sijafika kule. Niliguswa na furaha yake kwamba niliyoandika yamemwelewesha mambo ya wa-Marekani ambayo yalikuwa yanamtatiza. Nami nashukuru kwa hilo.

Familia hii ilinikarimu vizuri sana, nami nimebaki nashangaa kwa jinsi uandishi wa kitabu unavyoweza kukujengea urafiki na watu kiasi hicho.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...