
Jana jioni nilikuwa nyumbani kwa familia inayoonekana katika hii picha. Ni familia ya
Shannon Gibney, mwandishi chipukizi ambaye tayari ni maarufu.
Miaka michache iliyopita, Shannon Gibney alisoma kitabu changu cha
Africans and Americans, akaandika mapitio katika
Minnesota Spokesman Recorder, kama nilivyosema
hapa.
Siku chache zilizopita alinialika nyumbani kwake kwa chakula cha jioni, tukapanga hiyo tarehe ya jana. Aliniambia kuwa mume wake, ambaye anatoka Liberia, na bado ni mgeni hapa Marekani, amekuwa akisoma
kitabu changu.
Nilifurahi kukutana na familia hii. Kwa zaidi ya saa mbili nilizokuwa nao, maongezi yetu yalihusu masuala niliyoongelea katika kitabu, yaani tofauti za tamaduni za wa-Marekani na wa-Afrika. Wote wawili wanakifahamu vizuri sana
kitabu hiki, na walikuwa wananikumbusha mengi, ingawa mimi ndiye mwandishi.
Huyu bwana aliezea mshangao wake kwa jinsi maelezo ya
kitabu hiki yanavyofanana na hali ya Liberia, ingawa mimi mwandishi sijafika kule. Niliguswa na furaha yake kwamba niliyoandika yamemwelewesha mambo ya wa-Marekani ambayo yalikuwa yanamtatiza. Nami nashukuru kwa hilo.
Familia hii ilinikarimu vizuri sana, nami nimebaki nashangaa kwa jinsi uandishi wa kitabu unavyoweza kukujengea urafiki na watu kiasi hicho.