Showing posts with label shule. Show all posts
Showing posts with label shule. Show all posts

Sunday, December 10, 2017

Maonesho ya St. Dominic Boutique, Northfield, Minnesota

Jana, November 9, shule ya St. Dominic ya hapa Northfield, ilikuwa na wageni wengi. Palifanyika maonesho ya vitu mbali mbali vya matumizi na mapambo ya nyumbani na mavazi na urembo, machapisho, kazi za sanaa. Tamasha hilo lililoitwa St. Dominique Boutique lilijumuisha watengenezaji na wauzaji wa vitu hivyo yapata 60, na watu wengi kutoka maeneo mbali mbali walifika kuangalia na kununua. Mimi nilikuwepo, nikapata fursa ya kuongea na watu juu ya maandishi, mihadhara na utoaji ushauri kuhusu masuala ya tamaduni.




Nilipofika maoneshoni na kuelekezwa kwenye sehemu niliyopangiwa, huyu mzee anayeonekana hapa kushoto alisogea hima na kunisaidia kuandaa meza yangu. Alijitambulisha kuwa alihudhuria mhadhara niliotoa katika kanisa mjini Faribault. Hapo nilikumbuka kuwa niliwahi kutoa mihadhara miwili katika kanisa liitwalo First English Lutheran Church kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni. Waumini walipata fursa ya kununua nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Mzee huyu, ambaye alininieleza kuwa ni padri mstaafu, alikuwa na meza yake pembeni yangu. Kwa hiyo, tuliweza kuongea muda wote wa maonesho.






Kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane, watu walikuwa wanafika na kuangalia vitu na kununua, na kuongea na sisi tuliokuja kuonesha bidhaa na vitu vyetu vingine.







































Huyu dada hapa kushoto alifika kwenye meza yangu na dada yake mkubwa. Tuliongea kirefu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Hatimaye huyu dada alinunua hivi viwili alivyoshika, tukapiga picha. Kama kawaida, nimejionea mwaka hadi mwaka jinsi wa-Marekani wanavyopenda vitabu. Wakishauliza bei na kutajiwa, wanatoa hela hapo hapo na kununua.












Huyu bwana hapa kushoto sikumwelewa mwanzo alipofika mezani pangu, akaangalia na kuondoka bila kusema kitu, pamoja na kwamba nilimsalimia. Baada ya dakika chache alisogea tena na kuangalia, na hakusema kitu. Kisha akakaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni yangu, bila kunisalimia. Akachukua kijidaftari mfukoni mwake, akaanza kuandika sentensi mbili tatu, akanipa. Alikuwa ananiuliza iwapo nimesikia habari za m-Marekani Andrew Foster aliyeanzisha shule Ghana kwa ajili ya wasiosikia. Nilivyosoma na kumwangalia alivyokuwa ananiangalia, nilianza kuhisi kuwa ni mlemavu. Hasikii.

Tuliendelea kuzungumza kwa maandishi, hadi mwisho, na tulipoagana, nilimwandikia ujumbe wa mwisho kumwuliza kama angependa tupige picha, tukapiga. Nitaandika kuhusu tukio hili siku nyingine, katika blogu hii.


Kama nilivyoandika katika blogu hii, kitabu changu cha Matengo Folktales kilitajwa tarehe 23 Novemba katika "Jeopardy," programu  maarufu ya televisheni hapa Marekani. Baada ya kutajwa hivyo na kuleta msisimko hapa Marekani, niliamua kuitumia hiyo kama fursa.

Nilitengeneza bango lenye tamko lililokuwepo kwenye kipindi cha Jeopardy."  Ilikuwa ni burudani kuwaonyesha wa-Marekani hili bango na kitabu, huku nikifanya utani kuhusu kitabu changu kuonekana "Jeopardy."



Ninaipongeza shule ya St. Dominic kwa kuandaa maonesho hayo. Ingawa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo, shughuli ilifanikiwa sana. Watu wa aina mbali mbali walifika. Ingawa shule ni ya madhehebu ya Katoliki, hapo kwenye meza yangu pekee niliweza kuongea na watu wa imani mbali mbali. Kwa kadiri nilivyoona, itakuwa vizuri iwapo maonesho haya yatakuwa endelevu kwa siku zijazo. 

Sunday, August 9, 2015

Shaaban Robert na Mbaraka Mwinshehe Waliongelea Umuhimu wa Shule

Nikiachilia mbali jinsi wazazi wangu walivyohimiza elimu, nikiachilia mbali jinsi Mwalimu Nyerere alivyohimiza elimu, naukumbuka kwa namna ya pekee mchango wa mwandishi Shaaban Robert na mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe katika kuhimiza elimu.

Ninakumbuka jinsi baba yangu, nilipokuwa shule ya msingi, alivyokuwa ananitia msukosuko iwapo nilishindwa kupata 100% katika zoezi lolote au mtihani wowote. Ninakumbuka pia jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anahimiza elimu, kwa watu wote, kuanzia watoto hadi wazee, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Shaaban Robert ni mtu anayenifanya nimkumbuke baba yangu. Nilijionea hayo niliposoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert, ambacho habari zake niliziandika katika blogu hii. Humo tunaona jinsi Shaaban Robert alivyokuwa anamhamasisha mdogo wake Yusuf Ulenge afanye bidii katika elimu, akimtimizia mahitaji yote ya shule. Kwa wazazi na walezi, Shaaban Robert ni mfano wa kuigwa.

Mbaraka Mwinshehe, mwanamuziki ambaye wakati wa ujana wangu alitingisha Afrika Mashariki, ya Kati, na Kusini kwa nyimbo na muziki wake, aliimba wimbo maarufu wa kuwaasa vijana wazingatie elimu. Wimbo huo, "Enyi Vijana Sikilizeni," unaweza kuusikiliza hapa:

https://archive.org/details/EnyiVijanaSikilizeni

Friday, February 24, 2012

Ualimu Kazi Ngumu

Mimi ni mmoja wa walimu ambao tunapenda ualimu. Moyo wangu daima umekuwa kwenye ualimu, na sijawahi kuwazia kubadili mwelekeo.

Walimu wanakumbana na vipingamizi kadhaa, kuanzia sera katika sekta ya elimu, hadi tabia za baadhi ya watoto na wazazi. Namsikitikia mwalimu anayeonekana katika hii katuni. Huenda wizara imeamua kuwa watoto wafundishwe dhana kama istilahi, kutohoa au kifyonzeo kabla ya wakati ufaao. Kila somo lazima liende hatua kwa hatua, kufuatana na umri wa mtoto. Utaratibu huu ukifuatwa, itadhihirika kwamba hakuna somo gumu.
(Namshukuru mchoraji wa katuni hii, ingawa nimeshindwa kumtambua na kumtaja ipasavyo).

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...