Showing posts with label taaluma. Show all posts
Showing posts with label taaluma. Show all posts

Thursday, September 15, 2016

Ujumbe kwa Ndugu na Marafiki

Napenda kuwajulisha ndugu na marafiki kuwa leo tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nimeanza vizuri, kama nilivyogusia katika blogu hii, kwa ari kubwa. Wanafunzi wanaonekana wenye ari ya kujifunza. Sitawaangusha.

Tarehe 17 mwezi uliopita ilikuwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu. Nilitimiza miaka 65 ya maisha yangu. Ninavyoingia mwaka wa 66, ninamshukuru Mungu kwa kuniweka hai na mwenye uwezo wa kutekeleza majukumu yangu kama nilivyozoea.

Uhai na afya ni baraka kutoka kwa Mungu. Nitaendelea kutumia fursa hii, ambayo ni dhamana, kwa kufanya kazi zangu za kufundisha kwa juhudi yote na uadilifu, kusoma kwa bidii, na kuandika ili kuuneemesha ulimwengu kwa elimu.

Nawaombeni ndugu na marafiki mniombee ili nizingatie mwelekeo huo, nami nawaombea baraka na mafanikio.

Wednesday, October 28, 2015

Maprofesa na Wajibu wa Kuandika

Profesa ni mtu aliyefikia kiwango cha juu cha ufanisi katika ufundishaji, utafiti, uandishi, na kutoa ushauri kwa jamii katika masuala mbali mbali yanayohusiana na utaalam wake. Siwezi kuongelea hapa vipengele vyote vya suala hili, kama vile vigezo vinavyotumika katika kupima ufanisi wa mhusika hadi kumfikisha kwenye hadhi ya uprofesa. Ninakumbushia tu suala la wajibu wa profesa wa kuandika.

Baadhi yetu wa-Tanzania tumeliwazia na kuliongelea suala hili kwa miaka mingi, kwa manufaa ya jamii, tukiliunganisha na masuala kama sera ya elimu, matatizo ya uchapishaji, na kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu.

Kilichonifanya nirejeshe mada hii leo ni kwamba nimejikumbusha tamko la Rais Kikwete, "Maprofesa Wananisikitisha," ambalo lilijadiliwa katika blogu yangu hii na blogu ya Profesa Matondo. Mambo yaliyosemwa katika majadiliano yale ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu. Wajibu wa profesa wa kuandika, kama njia mojawapo ya kufundisha na kuchangia maendeleo ya taaluma ni jambo lililo wazi.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa dunia inabadilika muda wote, kuna umuhimu wa kulitafakari suala hili kwa mtazamo unaozingatia mabadiliko haya. Fikra zilizokuwa sahihi miaka michache iliyopita, huenda zimepitwa na wakati. Wataalam katika nyanja mbali mbali, kama vile ujasiriamali, elimu, na biashara wanatufundisha kuwa mabadiliko yanatulazimisha kuwa wabunifu na wepesi wa kubadilisha fikra, mahusiano, mbinu na utendaji wetu. Ndio maana ni muhimu kusoma daima na kujielimisha kwa njia zingine.

Katika dunia ya utandawazi wa leo, ambamo tekinolojia mbali mbali zinastawi, zikiwemo tekinolojia za mawasiliano, tunawajibika kuwa na fikra mpya kuhusu usomaji, uchapishaji na uuzaji wa vitabu, na kadhalika. Shughuli nyingi sasa zinafanyika mtandaoni, ikiwemo ufundishaji, kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii. Tunawajibika kufunguka akili na kuacha kujifungia katika hiki tunachokiita sera ya elimu ya Tanzania. Je, inawezekana kuandika kitabu chenye umuhimu kwa Tanzania lakini si kwa ulimwengu? Taaluma inaweza kufungiwa katika mipaka ya nchi? Kuna dhana katika ki-Ingereza tunayopaswa kuitafakari: "The local is global."

Naona ni jambo jema kuirejesha mada hii, tuendelee kuitafakari katika mazingira ya leo. Lakini, naona tusome kwanza mjadala uliofanyika katika blogu hii na blogu ya Profesa Matondo.

Thursday, August 20, 2015

Tumemaliza Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma

Leo, hapa chuoni St. Olaf, tumemaliza warsha yetu kuhusu jamii na taaluma. Nimeshaandika kuhusu warsha hii katika blogu hii. Tumehitimisha warsha kwa kujadili kitabu cha George Yancey, Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education. Lakini, kabla ya kuongelea mjadala wa leo, napenda kwanza kugusia mjadala wa jana.

Jana tulijadili sura za 1, 5, na 8 za Professors and Their Politics, kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons. Insha zilizomo katika kitabu hiki zinabainisha vizuri aina mbali mbali za mitzamo ya kisiasa inayoongoza fikra, utafiti, uongozi, na mambo mengine katika vyuo vikuu vya Marekani. Kitabu hiki kinajadili soshiolojia ya wanataaluma, kwa kuchambua mahusiano miongoni mwao na siasa zinazoendesha vyuo. Kinatoa mwanga juu ya mahusiano baina ya wanataaluma na jamii kwa ujumla, ikiwemo ushiriki wa waalimu na wahitimu katika masuala ya siasa za Marekani.

Tulisoma pia maandishi mengine ambayo hayamo katika kitabu hiki, tukayajumlisha katika mjadala. Andiko mojawapo ni "The Coddling of the American Mind." Mjadala ulikuwa wa kufikirisha na kuelimisha, sawa na mijadala ya siku mbili zilizotangulia.

Leo, tulijadili sura ya 2, 5, na 8 za Compromising Scholarship. Kwa kiasi fulani, mambo yaliyojitokeza leo ni mwendelezo wa yale tuliyoyajadili jana, ingawa kitabu hiki kinakwenda mbali katika kutufanya tujitambue kwamba tunapoangalia suala lolote, tunaliangalia kwa kutumia misingi, mitazamo, au kasumba tulizo nazo vichwani. Kwa mtu ambaye anafahamu angalau kiasi falsafa ya watu akina Immanuel Kant, au nadharia za kisasa za fasihi, msisitizo kwamba sisi sote tuna misingi hiyo vichwani mwetu, kitabu hiki si kigumu kukielewa.

Mjadala wa leo ulionekana kuamsha hisia za ndani na hamasa miongoni mwa wengi wetu. Labda ni kwa sababu ya aina ya masuala tuliyokuwa tunazungumzia, au labda ni kwa sababu tumezoeana baada ya siku tatu za kukaa pamoja na kujadili masuala, mjadala wa leo haukuwa wa kawaida. Ingekuwa warsha inaendelea kesho na keshokutwa, kwa mfano, joto la mjadala lingezidi kupanda.

Nimejifunza mengi katika warsha hii. Kama nilivyosema awali katika blogu hii, nafurahi kujipatia vitabu muhimu bila gharama, ambavyo nitavisoma kwa wakati wangu. Elimu ya bure namna hii, na vitabu muhimu, ni marupurupu adhimu ya ualimu.

Thursday, July 30, 2015

Nimepata Vitabu vya Warsha: Jamii na Taaluma

Leo nimepata vitabu vya warsha itakayofanyika hapa chuoni St. Olaf tarehe 17-20, mwezi Agosti, kuhusu jamii na taaluma. Warsha itawahusisha maprofesa wachache, kuongelea masuala kama nafasi ya mwanataaluma katika jamii, itikadi katika taaluma, na uhuru wa taaluma.

Washiriki wa warsha tunapata vitabu vya bure, ambavyo tutavijadili katika warsha. Tutaanza na viwili. Kimoja ni Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities, kilichotungwa na Martha C. Nussbaum. Cha pili ni Versions of Academic Freedom, kilichoandikwa na Stanley Fish. Kwetu tuliomo katika masomo ya nadharia ya fasihi, maandishi ya Stanley Fish katika uwanja huo ni maarufu sana.

Baada ya vitabu hivyo, tutajadili Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education, kitabu cha George Yancey, na Professors and Their Politics, ambacho kimehaririwa na Neil Gross na Solon Simmon. Hiki cha pili ni mkusanyo wa insha za wataalam mbali mbali.

Warsha itakuwa nzito, sawa na masomo ya kiwango cha juu kabisa. Tutakuwa tunasoma kurasa nyingi kila siku kwa maandalizi ya mjadala wa masaa mawili kila siku. Ni fursa ya kujinoa katika fikra na mitazamo juu ya masuala muhimu ya taaluma, ufundishaji, na nafasi na mchango wetu katika jamii. Ni fursa pia ya sisi wenyewe kubadilishana mawazo na kufahamiana. Cha zaidi ni kuwa ninapenda vitabu vya kufikirisha na kuelimisha, na kuvipata vya bure si jambo dogo.

Monday, June 1, 2015

Blogu Zangu Zimenisaidia

Hapa Chuoni St. Olaf kuna utaratibu unaomtaka kila mwalimu kuandika ripoti ya shughuli alizofanya katika mwaka wa shule unaoisha. Hizo ni shughuli za kitaaluma, yaani vitabu ulivyochapishwa, makala ulizochapisha, ushiriki wako katika mikutano ya kitaaluma, kazi ulizofanya katika uongozi wa vyama vya kitaaluma, kozi ulizotunga na kufundisha, uhariri katika majarida ya kitaaluma. Vile vile unaorodhesha huduma ulizotoa katika jamii nje ya chuo, kama vile ushauri ("consultancy"), na mihadhara katika mikutano ya vikundi na jumuia.

Nimekuwa na jadi ya kuandika mambo ya aina hiyo katika blogu hii ya hapakwetu na blogu ya ki-Ingereza. Katika kuandika ripoti yangu ya mwaka unaoisha, blogu zangu zimekuwa hazina ya kumbukumbu na taarifa nilizohitaji. Huu ni uthibitisho wa manufaa ya shughuli ninayofanya ya kublogu. Ninakumbuka kuwa niliwahi kuelezea namna blogu ilivyonisaidia darasani.

Watu wengine wanaandika kumbukumbu zao katika "diary." Lakini mimi kwa vile sina mazoea ya kufanya hivyo, nitaendelea kublogu kama ninavyofanya. Lengo ni kuhifadhi kumbukumbu. Tena, kwa kuwa nimezoea kuelezea shughuli zangu kwa upana, tangu chimbuko hadi matokeo, taarifa zangu zitaweza kutumika hata kwa kuandika kitabu. Ndoto ya kuandika kitabu cha aina hiyo nimekuwa nayo kitambo. Panapo majaliwa, nitaitekeleza.

Wednesday, March 23, 2011

Eti Wahadhiri Waeneza Siasa za Chuki Vyuoni

Niomeona taarifa hii hapa chini nikaona lazima niseme moja mawili, nikitumia wadhifa wangu kama mwanataaluma na mzoefu wa kufundisha au kutoa mihadhara vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia.

Sio kazi ya serikali kuingia darasani chuo kikuu ili kuchunguza mwalimu anafundisha nini au anafundishaje. Hii ni kazi ya wanataaluma na wahadhiri, kufuatana na taratibu zinazotambulika katika jumuia ya wanataaluma. Taratibu hizi ni za kulinda, kutathmini, kuratibu na kuboresha viwango vya utafiti, ufundishaji na taaluma kwa ujumla.

Serikali inapaswa kutambua kuwa dhana ya chuo kikuu, duniani pote, inaendana na haitengeki na uhuru wa kitaaluma. Walimu wa vyuo vikuu sio tu wana wajibu, bali uhuru wa kufukuzia taaluma bila vipingamizi, kwa mujibu wa vigezo vya taaluma hizo vinavyotambulika miongoni mwa wanataaluma kimataifa.

Kama kuna walakini katika utendaji kazi wa mwalimu wa chuo kikuu, kama vile kutofundisha somo inavyotegemewa, wanaowajibika kuchunguza ni wanataaluma wenzake, si serikali. Serikali haitegemewi wala kuruhusiwa kuingilia uhuru wa walimu na watafiti chuo kikuu katika kufanya utafiti, ufundishaji, uandishi na kadhalika kwa misingi na viwango vinavyotambuliwa kitaaluma.

Jambo jingine la msingi kabisa kuhusu chuo kikuu ni kuwa hapa ni mahala pa tafakari na malumbano kuhusu masuala mbali mbali, kwa kiwango cha juu kabisa. Ni mahala ambapo fikra za kila aina na hoja za kila aina zinapaswa kusikika na kuchambuliwa.

Chuo kikuu cha kweli, chenye hadhi ya chuo kikuu, ni maskani ya wachochezi wa fikra na hoja, katika taaluma mbali mbali, ikiwemo siasa. Huwezi kumwambia mtafiti au mhadhiri asiiponde serikali iliyoko madarakani iwapo utafiti na tafakari yake inampeleka huko.

Dhana ya kwamba kuna wanaoeneza siasa za chuki miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu ni dhana ya kusikitisha. Inamaanisha kuwa hao wanafunzi ni wajinga sana, au ni wavivu sana, ambao hawana uwezo au dhamira ya kujibidisha katika kusoma na kutafakari mambo ili waweze kugundua mapungufu ya hoja wanazosikia, na kupambana kwa hoja. Inamaanisha hao ni wanafunzi mbumbumbu, wasio na akili au wasiotumia akili. Kitendawili ni je, walifikaje hapo chuoni, kama si kwa njia za panya?

Wanafunzi wa chuo kikuu wanawajibika kuwa tayari na makini katika kupambana kwa hoja na wanafunzi wenzao na pia na walimu wao. Ni fedheha iwapo wanafunzi hao kiwango chao ni duni kiasi cha kuweza kupotoshwa na walimu wao. Hawastahili kuitwa wanafunzi wa chuo kikuu, na hicho chuo chenyewe hakistahili kuitwa chuo kikuu. Na ni fedheha kama tumefikia mahali ambapo serikali inaona ije darasani kuwanusuru hao wanafunzi feki.


------------------------------------------------------------------------------------
WAHADHIRI WAENEZA SIASA ZA CHUKI VYUONI


Chanzo:Habari Leo

Wahadhiri waeneza siasa za chuki vyuoni
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko; Tarehe: 23rd March 2011


SERIKALI inawachunguza wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wanaotumia muda mrefu madarasani kuzungumzia siasa badala ya kufanya kazi zinazohusu taaluma.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, Serikali ina taarifa kuwa, baadhi ya wahadhiri wanatumia muda wa kutoa mihadhara ya masomo kwa kuzungumzia siasa hasa kupiga vita Serikali iliyopo madarakani.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kuwabaini baadhi ya wahadhiri wanaojihusisha na siasa kwa kuingia madarasani na kuzungumzia siasa kwa dakika kumi kabla ya kuanza kufundisha,” amesema Mulugo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, lengo la wahadhiri hao ni kuwafanya wanafunzi kuchochea migomo na maandamano na kupandikiza chuki baina ya Serikali na wanafunzi.

Naibu Waziri ameyasema hayo katika mkutano kati ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Dar es Salaam.

Mulugo amesema, ingawa si katika chuo hicho, lakini kuna taarifa katika baadhi ya vyuo vikuu, wahadhiri wanafanya hivyo na kuwaonya kuwa kazi yao ni kuelimisha na si kuwavuruga wanafunzi akili kwa kuchanganya yale wanaojifunza na siasa na akawataka kujiepusha na siasa kwa kuwa wao ni wataalamu.

“Tena siasa zenyewe ni za kupiga vita Serikali iliyopo madarakani, tutawachukulia hatua,” alisisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri Kawambwa ambaye aliongeza kuwa wahadhiri wasipojihusisha katika siasa, watasaidia kuweka utulivu katika vyuo na kuepusha migogoro.

Awali, kabla ya onyo hilo, Dk. Kawambwa alisema Baraza la Mawaziri limeazimia kuanzia Machi mwaka huu wahadhiri wastaafu walipwe pensheni sawa na wastaafu wengine serikalini.

Alifafanua kwamba uamuzi huo unatokana na malalamiko ya wahadhiri wastaafu kwamba wanapata mafao finyu kutoka Mfuko wa Pensheni wa PPF tofauti na wanaostaafu kutoka Serikali Kuu ambao hupata mafao yenye neema kutoka Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GSPF).

Mbali na Dk. Kawambwa, pia Rais Jakaya Kikwete katika shughuli tofauti ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) jana, aligusia malalamiko ya wafanyakazi wote kuhusu tofauti kubwa ya sana katika utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni.

“Utakuta wafanyakazi wenye viwango sawa vya mshahara, muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata hadi mara tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine,” alisema Rais Kikwete.

Kutokana na tofauti hiyo aliyosema imelalamikiwa na vyama vingi vya wafanyakazi, Rais Kikwete aliagiza SSRA iangalie tofauti hiyo kwa makini na kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa mafao kati ya mfuko na mfuko, lakini akawataka pia wazingatie ustawi wa mfuko huo.

Lakini kuhusu maombi ya wahadhiri wa Muhas, kutaka kulipwa mafao kwa mkupuo kwa asilimia 50 ya mafao yao na kulipwa kwa miaka 15 baada ya kupokea mafao ya mkupuo, Dk. Kawambwa alisema bado yanafanyiwa kazi.

Kati hilo, Dk. Kawambwa alibainisha wataalamu wanaangalia suala la malipo hayo kwa kuwa limeonekana na utata unaoweza kusababisha baadhi ya mifuko kufa iwapo itapata wastaafu wengi hivyo unaangaliwa mfumo utakaotumiwa na mifuko yote.

Akizungumzia madai ya wahadhiri wa chuo hicho kuhusu posho ya nyumba ambazo hawajalipwa kuanzia mwaka jana, alisema hali hiyo ilitokana na ufinyu wa bajeti, lakini tayari wamepeleka malalamiko yao kwa Wizara ya Fedha ili walipwe katika bajeti ijayo.

Kabla ya kauli hizo za mawaziri, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Kisali Pallangyo alielezea changamoto anazopata ikiwemo ya miundombinu michache ya chuo hicho.

Kutokana na uhaba huo wa miundombinu, kati ya wanafunzi wanne wanaostahili kujiunga na chuo hicho, ni mmoja tu anayepata nafasi wakati Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya.

Dk. Kawambwa akijibu hoja hiyo, alisema, katika kuongeza wataalamu hasa katika masomo ya sayansi, Serikali imejipanga katika mpango wa maendeleo ya elimu ya juu kuboresha miundombinu ya vyuo hivyo ili wanafunzi wote wenye sifa wajiunge na vyuo stahili.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...