Tangu wiki mbili zilizopita, blogu yangu hii imepanda chati ghafla. Ninaongelea kigezo cha "pageviews," ambazo ninaziangalia kila nitakapo. Kwa miaka na miaka, "pageviews" za blogu hii kwa siku zilikuwa kama 130, sio zaidi sana na sio pungufu sana.
Lakini, kuanzia wiki mbili hivi zilizopita, "pageviews" zimeongezeka ghafla kwa kiwango kikubwa, na sasa ni yapata 900 au zaidi kila siku. Sielewi ni nini kimesababisha ongezeko hilo. Mkondo wa mada zangu haujabadilika. Kwa kiasi kikubwa ninashughulika na masuala ya elimu na utamaduni.
Nimeona kuwa ongezeko hilo la "pageviews," limetokea hapa Marekani. Kwa nchi zingine, kama vile Tanzania na Kenya, hali haijabadilika. Ni ajabu kiasi kwamba blogu ya ki-Swahili inasomwa zaidi Marekani kuliko Afrika Mashariki.
Mtu unaweza kujiuliza ni watu gani wanaosoma hii blogu ya ki-Swahili kwa wingi namna hii hapa Marekani. Ukweli ni kuwa kuna watu wengi hapa, hasa kutoka Kenya na Tanzania, wanaokifahamu ki-Swahili. Wako pia watu kutoka Burundi, Uganda, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Vile vile, kuna wa-Marekani ambao wameishi Afrika Mashariki na wanakifahamu ki-Swahili. Pia kuna wa-Marekani wengi ambao wamejifunza au wanajifunza ki-Swahili katika vyuo vikuu mbali mbali hapa hapa Marekani. Ninahisi kuwa hao nao ni kati ya wasomaji wa blogu hii.
Ninavyowazia suala hili la ukuaji wa idadi ya "pageviews" katika blogu, ninawazia jinsi watu wanavyotumia blogu kwa matangazo, hasa ya biashara. Katika ulimwengu wa leo ambamo tekinolojia za mawasiliano zinaendelea kusambaa na kuimarika, wafanya biashara na wajasiriamali wanatumia fursa za mitandao kama vile blogu kutangaza shughuli zao.
Kwa upande wangu, sijajiingiza katika matumizi haya ya blogu, ukiachilia mbali matangazo ya vitabu vyangu na mihadhara ninayotoa au matamasha ninayoshiriki. Lakini, endapo nitabadili msimamo, bila shaka nitakaribisha matangazo ya waandishi, wachapishaji, na wauzaji wa vitabu, kwa sababu blogu yangu inajitambulisha kwa masuala ya aina hiyo.
Showing posts with label vyuo vikuu. Show all posts
Showing posts with label vyuo vikuu. Show all posts
Wednesday, April 12, 2017
Thursday, August 20, 2015
Tumemaliza Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma

Jana tulijadili sura za 1, 5, na 8 za Professors and Their Politics, kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons. Insha zilizomo katika kitabu hiki zinabainisha vizuri aina mbali mbali za mitzamo ya kisiasa inayoongoza fikra, utafiti, uongozi, na mambo mengine katika vyuo vikuu vya Marekani. Kitabu hiki kinajadili soshiolojia ya wanataaluma, kwa kuchambua mahusiano miongoni mwao na siasa zinazoendesha vyuo. Kinatoa mwanga juu ya mahusiano baina ya wanataaluma na jamii kwa ujumla, ikiwemo ushiriki wa waalimu na wahitimu katika masuala ya siasa za Marekani.
Tulisoma pia maandishi mengine ambayo hayamo katika kitabu hiki, tukayajumlisha katika mjadala. Andiko mojawapo ni "The Coddling of the American Mind." Mjadala ulikuwa wa kufikirisha na kuelimisha, sawa na mijadala ya siku mbili zilizotangulia.
Leo, tulijadili sura ya 2, 5, na 8 za Compromising Scholarship. Kwa kiasi fulani, mambo yaliyojitokeza leo ni mwendelezo wa yale tuliyoyajadili jana, ingawa kitabu hiki kinakwenda mbali katika kutufanya tujitambue kwamba tunapoangalia suala lolote, tunaliangalia kwa kutumia misingi, mitazamo, au kasumba tulizo nazo vichwani. Kwa mtu ambaye anafahamu angalau kiasi falsafa ya watu akina Immanuel Kant, au nadharia za kisasa za fasihi, msisitizo kwamba sisi sote tuna misingi hiyo vichwani mwetu, kitabu hiki si kigumu kukielewa.
Mjadala wa leo ulionekana kuamsha hisia za ndani na hamasa miongoni mwa wengi wetu. Labda ni kwa sababu ya aina ya masuala tuliyokuwa tunazungumzia, au labda ni kwa sababu tumezoeana baada ya siku tatu za kukaa pamoja na kujadili masuala, mjadala wa leo haukuwa wa kawaida. Ingekuwa warsha inaendelea kesho na keshokutwa, kwa mfano, joto la mjadala lingezidi kupanda.
Nimejifunza mengi katika warsha hii. Kama nilivyosema awali katika blogu hii, nafurahi kujipatia vitabu muhimu bila gharama, ambavyo nitavisoma kwa wakati wangu. Elimu ya bure namna hii, na vitabu muhimu, ni marupurupu adhimu ya ualimu.
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...

-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
-
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...