Showing posts with label Siasa. Show all posts
Showing posts with label Siasa. Show all posts

Sunday, July 9, 2017

Wole Soyinka na Madikteta wa Afrika

Wole Soyinka ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika. Ameandika tamthilia, riwaya, mashairi, insha, na wasifu wake. Pia ametafsiri riwaya ya ki-Yoruba ya D.O. Fagunwa. Tafsiri hiyo inaitwa Forest of a Thousand Daemons: A Hunter's Saga.

Pamoja na umahiri wake katika kubuni visa na katika kuimudu lugha ya ki-Ingereza, Soyinka anachota sana mbinu na vipengele vingine vya sanaa na masimulizi ya jadi, hasa ya wa-Yoruba, lakini pia ya mataifa mengine, akienda mbali hadi u-Griki ya kale. Umahiri wake kama mwandishi umetambuliwa kwa namna mbali mbali, ikiwemo tuzo ya Nobel katika fasihi, ambayo alitunukiwa mwaka 1986.

Katika kazi zake, anashughulikia masuala ya aina mbali mbali, kama vile siasa, itikadi, ukoloni, ukoloni mambo leo, utamaduni, na fasihi ya Afrika na kwingineko. Udikteta ni mada ambayo Soyinka ameishughulikia tangu zamani, sio tu katika maandishi na mahojiano, bali pia kama mwanaharakati. Tamthilia ya Kongi's Harvest ni mfano mzuri. Tamthilia hii tuliisoma nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1973-76.

Wiki hii nimesoma A Play of Giants. Ni tamthilia ambayo inazama zaidi katika mada ya madikteta wa Afrika. Nilifahamu jambo hilo tangu zamani, kama nilivyoelezea siku chache zilizopita katika blogu hii. Soyinka anawaumbua madikteta hao. Anatumia kejeli kuelezea fikra na matendo yao, ulevi wa madaraka, uduni wa akili zao, na ukandamizaji wa haki za binadamu. Uduni wa akili zao unadhihirika kwa namna wanavyoongelea mambo yasiyo na maana, na kama wanaongelea mambo ya maana, hoja zao ni za ovyo kupindukia.

Madikteta hao wanaongelea jinsi wanavyoweza kudumu madarakani. Wanabadilishana mawazo na uzoefu wao. Wazo moja ni kutawala kwa mkono wa chuma na kuwafanya raia waishi kwa hofu. Hofu inaweza kujengwa mioyoni mwa raia kwa kutumia ushirikina na kuwafanya waamini kuwa mtawala anaona kila kinachoendelea nchini, Kwa njia hiyo, raia wanaogopa hata kuwazia kupinga utawala, kwani wanaamini kuwa mtawala atajua.

Udikteta ni mada ambayo imeanishwa katika kazi za fasihi tangu zamani sana. Tunaisoma katika The Epic of Gilgamesh, kwa mfano, na katika baadhi ya tamthilia za Shakespeare. Katika kusoma A Play of Giants, nimewazia sana riwaya ya Ngugi wa Thiong'o, Wizard of the Crow, ambamo dikteta anaumbuliwa pamoja na mfumo wa utawala wake kwa njia ya kejeli, sawa na anavyofanya Soyinka.

Ingawa kuna matumizi ya kejeli, A Play of Giants si tamthilia ya kufurahisha, bali inatibua akili na kunifanya nijiulize binadamu tunawezaje kuishi katika himaya ya udikteta. Kejeli ya mwandishi inanifanya mimi msomaji nicheke, lakini si kicheko cha furaha, bali dhihaka juu ya madikteta na aibu juu yetu wanadamu.

Sunday, January 22, 2017

Maandamano Makubwa Dhidi ya Rais Trump

Jana hapa Marekani yamefanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Donald Trump, ambaye aliapishwa juzi. Maandamano haya yaliyoandaliwa na kukusudiwa kwa wanawake, yanasemekana kuwa makubwa kuliko yote yaliyowahi kufanyika katika historia ya Marekani kwa siku moja. Maandamano haya yamefana sana, kwa mahudhurio na hotuba mbali mbali, na yametoa ujumbe wa wazi kuwa serikali ya Rais Trump isitegemee kuwa itatekeleza ajenda yake bila vipingamizi.

Marekani ni nchi inayoheshimu uhuru wa watu kujieleza. Katiba inalinda uhuru huo. Ndio maana maandamano ya kumpinga Rais Trump yalifanyika nchi nzima bila kipingamizi. Polisi walikuwepo kwa ajili ya kulinda amani, si kuzuia maandamano, wala kuwakamata wahutubiaji waliokuwa wanamrarua Rais Trump. Polisi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa waandamanaji wanayo mazingira muafaka na fursa kamili ya kutekeleza haki yao ya kuandamana na kuelezea mawazo yao.

Ninajua kuna wengine walioshiriki maandamano ya jana ambao si wa-Marekani. Kuna wakimbizi na wahamiaji kutoka nchi mbali mbali ambao walishiriki. Hapa Marekani, huhitaji kuwa raia ili kushiriki maandamano. Mimi sikushiriki, kwa sababu zangu binafsi.

Kwa kuwa mimi si raia wa Marekani, na sijawahi kuwazia kuwa raia, sioni kama nina haki au sababu ya kujihusisha na siasa za ndani za Marekani. Sipigi kura wakati wa uchaguzi wa viongozi. Kwa nini nijihusishe na maamuzi ya hao viongozi? Kama maamuzi yataiathiri nchi yangu, hapo nitaona nina wajibu wa kuisemea nchi yangu. Ninatambua wajibu wangu wa kuitetea nchi yangu popote nilipo.

Ingekuwa maandamano yanahusu masuala ya Tanzania ningeshiriki, kwa sababu Tanzania ni nchi yangu. Serikali ya Tanzania ikifanya mambo yasiyokubalika, halafu wa-Tanzania au marafiki wa Tanzania wakaandaa maandamano ya kupinga au kulaani, ni haki yangu kushiriki. Kule Uingereza, mwaka 2015, wa-Tanzania waliandamana kupinga mwenendo wa uchaguzi Zanzibar. Maandamano kama yale ni haki yangu kushiriki.

Huu utamaduni wa Marekani na nchi kama Uingereza unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Baada ya maandamano haya ya kihistoria ya jana dhidi yake, Rais Trump ametuma ujumbe: "Peaceful protests are a hallmark of our democracy. Even if I don't always agree, I recognize the rights of people to express their views." Tafsiri kwa ki-Swahili ni, "Maandamano ya upinzani ya amani ni kielelezo thabiti cha demokrasia yetu. Hata kama mara nyingine sikubaliani na wahusika, ninatambua haki ya watu kuelezea mawazo yao."

Thursday, August 20, 2015

Tumemaliza Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma

Leo, hapa chuoni St. Olaf, tumemaliza warsha yetu kuhusu jamii na taaluma. Nimeshaandika kuhusu warsha hii katika blogu hii. Tumehitimisha warsha kwa kujadili kitabu cha George Yancey, Compromising Scholarship: Religious and Political Bias in American Higher Education. Lakini, kabla ya kuongelea mjadala wa leo, napenda kwanza kugusia mjadala wa jana.

Jana tulijadili sura za 1, 5, na 8 za Professors and Their Politics, kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons. Insha zilizomo katika kitabu hiki zinabainisha vizuri aina mbali mbali za mitzamo ya kisiasa inayoongoza fikra, utafiti, uongozi, na mambo mengine katika vyuo vikuu vya Marekani. Kitabu hiki kinajadili soshiolojia ya wanataaluma, kwa kuchambua mahusiano miongoni mwao na siasa zinazoendesha vyuo. Kinatoa mwanga juu ya mahusiano baina ya wanataaluma na jamii kwa ujumla, ikiwemo ushiriki wa waalimu na wahitimu katika masuala ya siasa za Marekani.

Tulisoma pia maandishi mengine ambayo hayamo katika kitabu hiki, tukayajumlisha katika mjadala. Andiko mojawapo ni "The Coddling of the American Mind." Mjadala ulikuwa wa kufikirisha na kuelimisha, sawa na mijadala ya siku mbili zilizotangulia.

Leo, tulijadili sura ya 2, 5, na 8 za Compromising Scholarship. Kwa kiasi fulani, mambo yaliyojitokeza leo ni mwendelezo wa yale tuliyoyajadili jana, ingawa kitabu hiki kinakwenda mbali katika kutufanya tujitambue kwamba tunapoangalia suala lolote, tunaliangalia kwa kutumia misingi, mitazamo, au kasumba tulizo nazo vichwani. Kwa mtu ambaye anafahamu angalau kiasi falsafa ya watu akina Immanuel Kant, au nadharia za kisasa za fasihi, msisitizo kwamba sisi sote tuna misingi hiyo vichwani mwetu, kitabu hiki si kigumu kukielewa.

Mjadala wa leo ulionekana kuamsha hisia za ndani na hamasa miongoni mwa wengi wetu. Labda ni kwa sababu ya aina ya masuala tuliyokuwa tunazungumzia, au labda ni kwa sababu tumezoeana baada ya siku tatu za kukaa pamoja na kujadili masuala, mjadala wa leo haukuwa wa kawaida. Ingekuwa warsha inaendelea kesho na keshokutwa, kwa mfano, joto la mjadala lingezidi kupanda.

Nimejifunza mengi katika warsha hii. Kama nilivyosema awali katika blogu hii, nafurahi kujipatia vitabu muhimu bila gharama, ambavyo nitavisoma kwa wakati wangu. Elimu ya bure namna hii, na vitabu muhimu, ni marupurupu adhimu ya ualimu.

Tuesday, August 18, 2015

Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma Inaendelea

Siku chache zilizopia niliandika katika blogu hii kuhusu warsha tuliyokuwa tunaisibiri hapa chuoni St. Olaf juu ya jamii na taaluma. Warsha hiyo ilianza jana; tulijadili sura kadhaa za kitabu cha Martha C. Nussbaum, Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities.

Kitabu hiki kinaelezea namna mwelekeo wa elimu ya juu unavyochepuka kutoka katika hali yake ya asili na unavyoingia katika mkondo wa kibiashara. Malengo ya elimu, ambayo yanapaswa kuwa kumjenga mtu na jamii katika tabia ya kutafakari, kuhoji mambo, kujitambua, na kuwa na mahusiano mema, ya ushirikiano na kusaidiana, yamekuwa yakibadilika. Malengo hayo sasa ni kuwaandaa watu kwa ajira na uzalishaji wa mali.

Not for Profit kinaongelea umuhimu wa elimu katika demokrasia. Kwa kuiingiza elimu katika mfumo wa biashara, tunahujumu demokrasia na mahusiano bora ulimwenguni. Nilifurahi kusoma katika kitabu hiki nadharia za mabingwa niliowasoma nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Socrates, Jean Jacques Rousseau, Johann Pestalozzi, na John Dewey. Ningefurahi zaidi iwapo nadharia za Paulo Freire zingekuwemo pia, kwani huyu ni mwelimishaji maarufu aliyeonyesha njia ya kuifanya elimu kuwa nyenzo ya mapinduzi.

Nilifunguka akili niliposoma kuwa Rabindranath Tagore alikuwa mwelimishaji, sio tu kinadharia, bali kwa kuanzisha na kuendesha vyuo. Tangu zamani nilimfahamu Tagore kama mwandishi maarufu wa riwaya, tamthilia na mashairi, aliyepata tuzo ya Nobel mwaka 1913. Niliwahi kufundisha kitabu chake maarufu, Gitanjali, hapa chuoni St. Olaf. Lakini sikuwa nimefuatilia mchango wake ulivyoelezwa katika Not for Profit.

Leo tumejadili sura kadhaa za kitabu cha Stanley Fish, Versions of Academic Freedom: From Professionalism to Revolution. Fish anafafanua vizuri dhana ya uhuru wa taaluma, kwa kuangalia mitazamo mbali mbali iliyopo kuhusu dhana hiyo. Ameweka wazi masuali muhimu kuhusu dhana ya uhuru wa taaluma. Kwa mfano, uhuru wa taaluma ni haki ya kikatiba? Kwa nini waalimu katika elimu ya juu wanaamini wana haki ya kuwa na uhuru wa taaluma mpana kuliko uhuru walio nao wananchi wengine? Wanafunzi nao wanao au wanastahili uhuru huo?

Fish anaongelea pia masuala ya mtazamo wa kisiasa wa waalimu katika vyuo vikuu, na uhusiano wa maadili na uhuru wa taaluma. Tulipokuwa tunajadili suala hilo la maadili, profesa mwenzetu mmoja alielezea alivyowahi kukataa kuchora michoro ya kuboresha muundo wa ndege za kivita za jeshi la Marekani.

Kama ilivyokuwa jana, mjadala wa leo ulikuwa mzuri na wa kuelimisha. Nimefurahi kuvisoma vitabu viwili nilivyovitaja hapo juu. Kesho tutajadili Professors and their Politics, kitabu kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons.

Sunday, May 24, 2015

Angalizo kwa Wenye Vyama: Tanzania ni Yetu Wote

Mimi ni m-Tanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Natoa angalizo kwa wa-Tanzania wenye vyama, hasa CCM, wazingatie kuwa Tanzania ni yetu wote. Naitaja CCM namna hii kwa sababu ni chama tawala, chenye wajibu wa kuongoza njia na kuwa mfano kwa wengine.

Wa-Tanzania wenye vyama wakumbuke kuwa wao ni wachache kwa kufananisha na idadi ya wa-Tanzania kwa ujumla. Wafanye siasa zao, ila wasisahau jambo hilo. Nasema hivyo kwa sababu wana tabia ya kujiona kuwa wao ndio Tanzania, na Tanzania ni wao.

Kinachonikera zaidi ni fujo. Wa-Tanzania wenye vyama wana tabia ya kuleta fujo na kuhujumu amani, hasa kinapokaribia kipindi cha uchaguzi. Ni aibu sana kwamba, kutokana na fujo za wa-Tanzania wenye vyama, tumefikia mahali sasa ambapo watu wanasali na kufanya ibada kuombea amani. Hii ni fedheha ambayo tumeletewa na wa-Tanzania wenye vyama.

Ni sahihi kumwomba Mungu atupate mvua ya kutosha kwa mazao yetu. Ni sahihi kumwomba atuepushe na majanga kama vile matetemeko ya ardhi. Ni sahihi kumwomba atupe uzima siku hadi siku tuweze kujenga nchi yetu na kutimiza majukumu yetu mengine.

Lakini kuombea amani kwa kuwa inatishiwa na utovu wa nidhamu unaofanywa na wa-Tanzania wenye vyama ni jambo lisilokubalika. Kuombea amani kwa sababu ya utovu wa busara wa watu hao ambao wanadhani nchi hii ni yao peke yao, wanaodhani wana haki ya kujifanyia watakalo katika nchi hii, ni jambo lisilokubalika. Hili si suala la kuombea amani. Ni suala la kupambana na hao wahujumu wa amani.

Inashangaza kwamba hata Ikulu imeshindwa kutambua hilo. Haijawahi kutokea Ikulu ikawaita wa-Tanzania wasio na vyama kwa mazungumzo na mashauriano. Ikulu imekuwa tayari kuwaita wenye vyama na kuongea nao, lakini sio sisi tusio na vyama, ambao ndio wengi zaidi na ni mfano wa kuigwa.

Wa-Tanzania wenye vyama wazingatie kuwa sisi tusio na vyama hatujawahi na hatuna mpango wa kuhujumu amani ya Tanzania kama wanavyofanya wao. Tumetunza heshima ya Tanzania wakati wao wanaihujumu. Wajifunze kutoka kwetu ili wote tudumishe amani na tuipe nchi yetu heshima inayostahili.

Wednesday, April 1, 2015

Tunahitaji Demokrasia, Lakini Tunahitaji Vyama vya Siasa?

Bila shaka tutakubaliana kuwa tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao ni wa umma, unaendeshwa na umma, kwa maslahi ya umma. Kwa ki-Ingereza wanasema "rule of the people, by the people and for the people."

Hii ndio maana na tafsiri ya demokrasia. Lakini je, tunahitaji chama cha siasa? Tunahitaji vyama vya siasa? Ni lini wa-Tanzania walikaa na kulitafakari suali hili? Kwa kweli hawajawahi kufanya tafakari hii. Badala yake wamekurupuka na wazo la chama au vyama, kikasuku tu.

Hata wale tunaowaita wasomi wetu nao wameshindwa kuhoji hali hii. Wameshindwa kujinasua kutokana na mtazamo huu, badala ya kufanya kile kinachoitwa kwa ki-Ingereza "thinking outside the box."

Nimeelezea zaidi huu ukurupukaji, mkanganyiko, na ukasuku wa wa-Tanzania katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Tuesday, May 24, 2011

Nataka Tanzania Isitawalike Kamwe

Nataka Tanzania isitawalike kamwe. Kama hupendi kusikia hayo, shauri lako. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nataka Tanzania isitawalike.

Nataka Tanzania iwe na viongozi, sio watawala. Wanaotaka kutawala wasipate nafasi hiyo. Uongozi unahitaji busara na ushawishi, kukubalika na jamii husika. Kama ni kutawaliwa, tulitawaliwa na wakoloni. Masultani walikuwa wanatawala. Walikuwa wakandamizaji, sawa na wakoloni. Wazee wetu walipambana hadi Uhuru ukapatikana.

Nataka nchi yetu iimarishe misingi ya Uhuru na demokrasia. Kutawala ni suala la mabavu, kwani hakuna jamii inayokubali kutawaliwa, labda iwe ni jamii ya wajinga, au waoga, au ambao wamelishwa sana kasumba ili wasitambue haki zao.

Lakini jamii inayojitambua, inayotambua maana ya uhuru, haki, na demokrasia, jamii inayothamini na kutetea hayo, haiwezi kutawalika, labda kwa mabavu na vitisho. Itakuwa ni jambo la kuhuzunisha iwapo Tanzania itatawalika. Nataka tuwe macho, tuwe makini, nchi yetu isitawalike, kamwe.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...