Tuesday, May 24, 2011

Nataka Tanzania Isitawalike Kamwe

Nataka Tanzania isitawalike kamwe. Kama hupendi kusikia hayo, shauri lako. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila nataka Tanzania isitawalike.

Nataka Tanzania iwe na viongozi, sio watawala. Wanaotaka kutawala wasipate nafasi hiyo. Uongozi unahitaji busara na ushawishi, kukubalika na jamii husika. Kama ni kutawaliwa, tulitawaliwa na wakoloni. Masultani walikuwa wanatawala. Walikuwa wakandamizaji, sawa na wakoloni. Wazee wetu walipambana hadi Uhuru ukapatikana.

Nataka nchi yetu iimarishe misingi ya Uhuru na demokrasia. Kutawala ni suala la mabavu, kwani hakuna jamii inayokubali kutawaliwa, labda iwe ni jamii ya wajinga, au waoga, au ambao wamelishwa sana kasumba ili wasitambue haki zao.

Lakini jamii inayojitambua, inayotambua maana ya uhuru, haki, na demokrasia, jamii inayothamini na kutetea hayo, haiwezi kutawalika, labda kwa mabavu na vitisho. Itakuwa ni jambo la kuhuzunisha iwapo Tanzania itatawalika. Nataka tuwe macho, tuwe makini, nchi yetu isitawalike, kamwe.

6 comments:

tz biashara said...

Ni kweli kutawaliwa sio kitu kizuri lakini mpaka leo ni nusu karne tokea uhuru upatikane.Sijui kama leo profesa uliingia kwa mjengwa hebu chungulia uone picha za kusikitisha na kuonyesha uhalisi wa maisha ya watu wenye kupata shida.Hapo sijajua kuwa na uhuru au kutokuwa na uhuru au democrasia inatumika kwa nani au wakati gani.Tunajuwa kama viongozi wetu wanakopeshwa magari ya thamani na nyumba za thamani na pia watoto wao wanasoma ktk shule za kulipia na hata wakipata maradhi vilevile wanakwenda ktk hospitali nzuri au nje ya nchi.Sasa je hawa maskini ya mungu hawajui chakula gani watakula leo,watoto hawana hata viti vya kukalia mashuleni wala meza za kusomea,Hawana hata vitanda ktk kijizahanati yaani kwa ufupi sitoweza kumaliza leo maelezo yote.Sasa sifahamu mpaka leo ni nani alietawala ktk nchi ni vizuri kumjua japokuwa tunamjua raisi lakini lazima kuna mkubwa anaeongoza hii nchi haiwezekani.Na wananchi hawajijui wala hawajitambui kwa ulabu,ilimradi mtu ahangaikie pesa ya kujirusha usiku.Sasa hayo kweli ndio maisha jamani.

Mbele said...

tz biashara, shukrani kwa mchango wako. Masuali yako ni mazito na mazuri, nami naona unasema ukweli. Demokrasia haiwezekani bila mfumo wa kiuchumi wa haki kwa wote.

Tafakari yako imenikumbusha maandishi ya akina Karl Marx, Engels, na Lenin, ambao walisema kuwa mfumo wa uchumi ndio hasa msingi wa hayo mambo kama mahusiano ya jamii, itikadi na imani. Demokrasia ni itikadi mojawapo.

Katika jamii yenye matabaka, kinachotokea ni tabaka tawala kuhodhi madaraka na nguvu za dola ili kuendeleza maslahi yake na kuwakandamiza walalahoi wasio nacho. Hapawezi kuwa na demokrasia kwa maana ile ya utawala wa walio wengi, kwa maslahi ya walio wengi.

Tunaweza kuanzisha vyama vya siasa, uchaguzi kila baada ya miaka kadhaa, vyombo vya habari vingi na huru, lakini pasiwe na demokrasia ya umma.

Marekani kuna vyombo vya habari vingi, vyama vya siasa, na kadhalika, lakini tabaka lenye kushika hatamu ni la mabepari, si walalahoi. Na Tanzania tunaelekea huko huko.

Albert Kissima said...

Prof Mbele, malengo/madhumuni ama misingi ya uhuru ule wa mwaka 1961 hatunayo tena. Maana ya ule uhuru imepotea. Kinyume chake, Tanzania tumejikuta kwenye ukoloni mbaya kabisa; ukoloni ambao wakoloni ni "wazawa". Sasa tunahitaji kutangaza vita nyingine; vita ya wenyewe kwa wenyewe. Vita ya kuvunja matabaka yanayosababisha kuwepo kwa watawala na watawaliwa (miongoni mwetu wazawa) na si viongozi na wawezeshwaji.

Tanzania tunahitaji uhuru wa kizalendo. Maana mzalendo haujumu nchi yake wala kutawala, kwa maana ya kuonea, kukandamiza na kunyanyasa watawaliwa.

Hata mimi sitaki Tanzania itawalike, japo kuwa huu ndio uhalisia wa nchi yangu kwa sasa. Hili linadhihirika kwa sera za vyama vya siasa ambazo kwa kiasi kikubwa ni ahadi. Zinamtaka mtanzania asubiri ahadi hizo zitekelezwe ili afaidike. Hazimuhusishi mtanzania moja kwa moja, hivyo hawezeshwi, kwa maana ya kuwa haongozwi, bali anatawaliwa.

Mbele said...

Ndugu Kissima, shukrani kwa ujumbe wako. Tuko pamoja.

Nimekuwa nikifuatilia idadi ya wasomaji wanaomiminika kwenye makala hii, na nimebaki nacheka.

Nafahamu kuwa kichwa cha ujumbe wangu tayari ni kivutio, maana kwa jinsi walivyozoea wa-Tanzania, kichwa hicho kinaashiria kile kinachoitwa uchochezi.

Nadhani watu wanatinga kwenye blogu yangu wajioneee ninavyochochea uvunjifu wa amani :-)

Kumbe, kwa kusema nataka nchi isitawalike, mimi nilitaka kuleta dhana yangu ambayo ni tofauti na yao. Kazi kweli :-)

Anonymous said...

okey sawa wachangiaji,hapo juu swali langu ni kwamba,nini maana ya kutawaliwa?mimi ninavyojua kutawaliwa ni moja ya kuwa na viongozi wanao hakiki na kusimamia shughuli zote za kitaifa,ama serikali kwa ujumla!sasa mnavyosema tanzania tusitawaliwe mna maanisha nini??prof hwebu weka hii wazi,mdau uk

Mbele said...

Anonymous, shukrani kwa ujumbe wako. Suala la uongozi limefanyiwa tafakari kwa muda mrefu na wataalam, na kuna maandishi mengi juu yake vitabuni na katika majarida.

Lakini kwa hapa napenda kutaja dhana ya aina mbali mbali za akili. Utafiti unasema kuwa kuna aina nyingi za akili. Na kwa uongozi, akili inayohitajika au inayomfanya mtu awe kiongozi bora, ni ile inayoitwa "emotional intelligence." (Sijui kwa ki-Swahili niite "akili hisia," lakini wataalam wanaweza kututafsiria vizuri).

Katika jamii kama yetu, hata huo utafiti ninaoongelea, nadhani watu hawaujui. Wataujuaje wakati vitabu hawasomi? Tunawapa watu madaraka, iwe ni kwenye taasisi, vyama, wizara, kampuni, vyuo na kadhalika, bila kuwazia sifa hii ninayoongelea.

Matokeo yake ni kuwa mhusika akishayakwaa madaraka, kazi yake ni kumwaga mbwembwe, kujikuza, kuwaonyesha wengine kuwa yeye ni bosi, na kadhalika. Watu wanaogopa hata kuingia ofisini kwa bosi, maana ni tishio.

Mtu mwenye "emotional intelligence" anakuwa na mvuto na ushawishi. Penye migogoro, kuwepo kwake kunaleta suluhu. Yeye ni kiungo hata baina ya wagombanao. Ni msuluhishi anayewavutia hao wengine.

Kwetu, utakuta huyo tunayemwita kiongozi naye anashabikia upande mojawapo wa wagombanao. Utakuta yeye naye ni mpiga majungu namba wani.

Kwa hivi, kutokana na watu kutothamini elimu, hata ukigusia kama nilivyogusia, tofauti kati ya uongozi na utawala, watu wanashindwa kuelewa.

Pendekezo langu ni kuwa huko kwenye semina elekezi itakuwa vizuri wawe wanasoma na kujadili pia suala hili la "emotional entilligence." Ni suala pana, kubwa, lenye mantiki na mafundisho mazuri sana.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...