Friday, May 20, 2011

"Mama m-Katoliki" (shairi kutoka India)

Uandishi wa ki-Ingereza wa India unafahamika zaidi katika tanzu ya riwaya na hadithi fupi, ingawa waandishi wa mashairi pia wapo, kama vile Kamala Das, Nissim Ezekiel na Jayanta Mahapatra. Leo wanafunzi wangu wa somo la fasihi ya Asia Kusini walifanya mtihani wa mwisho, na suali moja nililowapa lilihusu shairi la "Catholic Mother," lililotungwa na Eunice de Souza.

Suali nililowapa ni hili: "Discuss the poem, "Catholic Mother," by Eunice de Souza. Say what you want about it. In addition, compare the woman in this poem with Anil, a key character in Michael Ondaatje's Anil's Ghost."

Sijui kwa nini, baada ya mtihani kumalizika, nimepata wazo la kulitafsiri shairi hili na kuliweka hapa kwenye blogu yangu. Ingawa lugha aliyotumia mtunzi inaonekana ni ya kawaida tu, ameingiza tamathali za usemi kiurahisi, lakini kwa uhodari na kufikirisha. Amepenyeza na kuchochea uchambuzi wa masuala muhimu ya jamii, kama vile dini, udini na jinsia.

Vile vile, nimekuwa nikiangalia jinsi anavyotumia herufi kubwa na wakati mwingine herufi ndogo. Hili nalo ni suala la kufikiriwa. Kuna kejeli nzuri na ucheshi fulani ndani yake.

Kutafsiri kazi ya fasihi--iwe ni hadithi, riwaya, au shairi--ni suala tata na mtihani mkubwa. Ninajua ninalosema, kutokana na kusoma mawazo ya watalaam na pia kutokana na uzoefu wangu. Kwa kweli, dhana yenyewe ya tafsiri ni ndoto, kwani lugha zinatofautiana, na tafsiri yoyote ni lazima itofautiane kwa namna mbali mbali na utungo unaotafsiriwa. Hali hiyo inajitokeza katika tafsiri yangu ya shairi la "Catholic Mother."

Msomaji ambaye anafahamu vizuri ki-Ingereza na ki-Swahili ataweza kutambua namna ambayo yeye angetafsiri shairi hili. Ingekuwa vizuri kuona wengine wangetafsiri vipi shairi hili, nami nakaribisha michango hiyo.

Mimi kama m-Mkatoliki nimevutiwa na shairi hili. Nimejikuta nikitabasamu kwa jinsi mshairi anavyotusanifu sisi wa-Katoliki. Mshairi Eunice de Souza ni mwanamke, na ni m-Katoliki kutoka jamii ya wa-Goa. Alizaliwa Pune, India, mwaka 1940. Amestaafu kazi ya ualimu wa ki-Ingereza katika chuo cha Mtakatifu Xavier, mjini Mumbai. Soma hilo shairi lake, na tafsiri yangu:


Catholic Mother

Francis X. D’Souza
father of the year.
Here he is top left
the one smiling.
By the Grace of God he says
we’ve had seven children
(in seven years)
We’re One Big Happy Family
God Always Provides
India will Suffer for
her Wicked Ways
(these Hindu buggers got no ethics)

Pillar of the Church
says the parish priest
Lovely Catholic Family
says Mother Superior

the pillar's wife
says nothing.

---------------------------

Mama m-Katoliki

Francis X. D’Souza
baba wa mwaka.
Yuko hapa juu kushoto
anayetabasamu.
Kwa Neema ya Mungu anasema
tumejaaliwa watoto saba
(katika miaka saba)
Sisi ni Familia Moja Kubwa Yenye Furaha
Mungu Daima Anaruzuku
India Itateseka
kwa Mwenendo Wake Mbaya
(hao wa-Hindu mabwege hawana maadili)

Ni Nguzo ya Kanisa
asema baba paroko
Familia Murua ya ki-Katoliki
asema Mkuu wa Masista

mkewe nguzo
hasemi lolote.

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Ushairi ni ugonjwa wangu. Nimefurahi sana kusoma Mama wa Kikatoliki. Nimejifunza mengi hapa. Ahsante sana Prof Mbele.

Mbele said...

Shukrani ndugu Mtanga kwa ujumbe wako. Hili shairi la Eunice de Souza lina utajiri mkubwa wa fani na maudhui. Mtu makini anaweza kuandika insha ndefu kuhusu shairi hili, akafafanua kipengele kwa kipengele, neno kwa neno.

Lakini hayo yanahitaji fikra pevu, nidhamu ya akili, na ufahamu mzuri wa lugha, vitu ambavyo vinaendelea kuwa nadra katika jamii ya wa-Tanzania, ambayo inataka njia ya mkato.

Kuthibitisha kauli yangu, napenda kunukuu ubeti wa kwanza wa shairi lako la "Penzi letu la wawili." Ni ubeti uliopangika vizuri.

Napenda wadau wautafakari halafu wautafsiri kwa lugha yoyote ambayo wanadhani wanaijua, iwe ni ki-Ingereza, ki-Chagga, ki-Kuria, ki-Nyasa, ki-Luguru na kadhalika.

Katika kutafsiri, watagundua matatizo mengi. Wataumia kichwa na pengine kukata tamaa. Itakuwa vizuri wakielezea yote hayo, kwani ni fundisho na elimu nzito.

Ubeti wenyewe ni huu:

Majira hubadilika,
Miaka inasogea,
Nyasi nazo hunyauka,
Mimea kujiozea,
Lakini nina hakika,
Wewe hutonipotea.

Simon Kitururu said...

Mmmh!

Christian Sikapundwa said...

Lugha ya ushairi ni tata hasa ukiichukulia kama mtunzi alivyoandika.Prf.Shairi la ' mama m- Katoliki'kutoka India limenikumbusha enzi zangu nikiwa mwanafunzi.Nikiwa middle school nilisoma tulijifunza mashairi mengi ni siku nyingi lakini moja lilisema 'Fitina kaua mbele,adui heri mchawi'.

Nimekumbuka nilivyo soma Ubeti huo wa mwisho.ambao una fundisha jamii,kuwa hali ya maisha hubadilika haibakii pale pale.

Pia Linajikita kwenye siasa,maisha wakati wa kudai Uhuru na baada ya uhuru sasa miaka 50 je kuna mabadiliko ya maisha ya m- Tanzania.

Nakushukuru sana kwa kuielimisha jamii kwa lugha fupi lakini ina mantiki kwa wanajamii wengi.Mwalimu hachoki kuelimisha jamii yake popote pale alipo.

Mungu akuzidishie baraka ya kuendelea kutumia taalamu uliyosomea.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...