Agosti 6, mwaka jana, nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Irente. Nilishawahi kusafiri hadi Irente miaka michache kabla, nikitumia teksi. Lakini mwaka jana niligundua kuwa ningeweza kusafiri kwa bajaji. Bajaji yenyewe ndio hii inayoonekana katika picha, na dreva wake. Bajai hii ilikuwa maarufu mjini Lushoto.
Niliziona bajaji kwa mara ya kwanza nilipokuwa India, mwezi Aprili mwaka 1991. Wakati huo hapakuwa na bajaji Tanzania. Lakini kidogo kidogo, miaka iliyofuatia, bajaji zilianza kuonekana, na leo zimejaa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Sasa zinaonekana hata kwenye miji midogo kama Lushoto. Ndio mambo ya ulimwengu katika utandawazi wa leo.
Safari ilikuwa murua. Bajaji ilikula milima na kukwepa mifereji na mashimo kama mchezo. Tulipofika Irente, nilianza kuwatafuta vijana wawili mapacha ambao niliwafahamu miaka iliyotangulia, wakati nafanya utafiti kuhusu masimulizi juu ya Osale Otango na Paulo Hamisi. Osale Otango na Paulo Hamisi ni maarufu katika historia ya miaka ya hamsini na kitu, walipokuwa wakisakwa na serikali ya wa-Ingereza kwa ujambazi. Walikuwa wakizunguka na kujificha maeneo hayo ya Irente.
Kwa bahati nzuri siku hiyo, hao mapacha walikuwa kijiji cha jirani wakati bajaji yangu ilipofika hapo. Tulifurahi kukutana, tukapandisha njia hadi nyumbani kwao.
Nilipiga picha hii wakati tunateremka kutoka kanisani. Hao marafiki zangu wametangulia. Bajaji ilikuwa imepaki kwenye nyumba zinazoonekana kule ng'ambo. Upande wa kulia, kule ukingoni, ndipo penye mwamba ambapo watalii na wageni wengine hufika kuangalia mandhari ya sehemu hizo na sehemu za mbali. Panaitwa Irente Viewpoint. Kuna picha nyingi za mahali hapo mtandaoni. Ni mahali maarufu kiasi kwamba kama hujafika hapo, inakuwa kama vile hujafika Lushoto.
Hapa ninaonekana nikiwa na hao marafiki zangu mapacha. Kule nyuma yetu ni miamba ambayo nayo imepigwa picha sana na watalii na wageni wanaofika hapa Irente. Kuna miteremko ya kutisha maeneo hayo. Hata mimi ambaye natoka sehemu za milimani, Umatengo, kwenye milima na miteremko, ninatishika na miteremko ya Irente.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Shikamoo profesa.Nimeingia kwenye blogu yako kwa mara ya kwanza leo na nimeipenda. Lengo lilikuwa kupata historia ya huyu mtu Otango Osale na mapango ya Amboni.Kwa bahati mbaya sijaona maelezo ya ziada na kwa mawazo yangu bado unaendelea na utafiti huu. Kama ni hivyo naomba utakapomaliza na mimi niupate. Nakutakia siku njema. Caleb
Naona Profesa hadi leo hajakamilisha utafiti wake. Ila naona ni muda mrefu
Post a Comment