Thursday, June 2, 2011

Mfano wa Uandishi Bora wa ki-Ingereza

Kusoma kuna faida nyingi. Kusoma vitabu vilivyoandikwa kwa lugha iliyotukuka ni neema. Nina bahati kuwa nafundisha somo la fasihi, na muda wote nawaongoza wanafunzi katika kutafakari na kujadili maandishi bora kabisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wiki chache zilizopita, tulisoma riwaya iitwayo Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera wa Sri Lanka na kusifiwa sana na wahakiki. Ingawa riwaya nzima imeandikwa kwa ki-Ingereza kilichopevuka na kinavutia sana, napenda kunukuu kipande kimoja ambacho kilinigusa kwa namna ya pekee. Mwandishi anaelezea safari ya gari katika kisiwa cha Sri Lanka. Ninaposoma uandishi kama huu, uliosheheni maneno na tamathali murua, hadi kuleta picha kamili na ya kugusa ya kile kinachoelezwa, huwa najiuliza kama kweli sisi wa-Tanzania tutaweza kufikia kiwango hiki. Ni changamoto kubwa na ni kipimo cha kujipima uwezo wetu:

We drove for hours; whistling over a ribbon of tarmac measuring the perpetual embrace of the shore and the sea, bounded by a fretwork of undulating coconut trees, pure unadorned forms framing the seascape into a kaleidoscope of bluish jewels. Above us a tracery of green and yellow leaves arrowed to a vanishing-point we could never reach. At times the road curved as though it were the edge of a wave itself rushing in and then retreating into the ocean. We skittered over these moving surfaces at a speed I had never experienced before. Through the back window I watched the road pour out from under us and settle into a silvery picture of serene timelessness. We overtook the occasional bus belching smoke or a lorry lisping with billowing hay; we blasted through bustling towns and torpid villages. We passed churches and temples, crosses and statues, grey shacks and lattice-work mansions.... (uk. 69)

Pamoja na mengine yote tuliyojadili darasani kwangu, niliwaelekeza wanafunzi kwenye kifungu hiki, kama mfano wa uandishi bora wa ki-Ingereza. Wanafunzi hao ni wa-Marekani, ambao lugha yao ni ki-Ingereza. Inakuwa ni changamoto ya aina yake kwao.

4 comments:

Unknown said...

@Prof. umenifanya nikumbuke tungo za kipelelezi zilizoandikwa kwa kiswahili za Elvis Musiba.

Yaani...ninatamani kuwa mtunzi kama sio mwandishi wa wa waaa vitabu.

Kwa kuwa kibaraza chako kipo, ni kweli kimekuwa ni mhamasishaji mkubwa kila ninapopita hapa nimejikuta ni mtu wa kupiga hatua kwenda mbele.

Usishangae siku moja nika graduate kutokana na blog yako ambayo naichukulia kama chuo.

UISHI MILELE PROF.MBELE.

Mbele said...

Ndugu Mcharia, umenivunja mbavu leo na huo mchapo wa kuhitimu masomo hapa kwenye kablogu kangu :-)

Itabidi niingie mzigoni kuandaa kofia na majoho ya kuvaa wahitimu wangu :-)

Tukirudi kwenye mada ya uandishi, tuna waandishi mahiri sana katika ki-Swahili. Mimi nimejikita zaidi katika uandishi wa zamani, hasa tenzi kama "Inkishafi," "Mwana Kupona," "Ras 'lGhuli," "Liongo Fumo," bila kusahau tungo za akina Shaaban Robert, Ahmed Sheikh Nabhany, Gora Haji Gora, na Amiri Andanenga. Upande wa riwaya, nimekuwa nikisoma sana riwaya za Shaaban Robert.

Maandishi hayo yana mvuto wa pekee kwa upande wa lugha yetu ya ki-Swahili.

Nimepata kufahamiana na hao waandishi wa karibuni zaidi, kama akina Ebrahim Hussein, Kezilahabi, Shafi Adam Shafi, Mbunda Msokile (marehemu), na Edwin Semzaba.

Napendekeza kuwa tujibidishe kuanzia na zile tungo za zamani, maana ndio msingi, na ni tungo zilizofikisha uandishi wa ki-Swahili kieleleni. Kwa ki-Ingereza kuna dhana ya "classics," ambayo itabidi nitafute tafsiri yake kwa ki-Swahili

John Mwaipopo said...

vivumish (adjectives)vimetumika barabara. adjectives/vivumishi zi/vikitumika vema hujenga picha kichwani mwa msomaji. hakika hiki kipande kilichoandikwa vema

Mbele said...

Ndugu Mwaipopo, shukrani kwa ujumbe. Kwa upande wa uandishi wa riwaya au hadithi, mtindo aliotumia huyu mwandishi unavutia sana.

Labda tu tuongeze kuwa kuna aina mbali mbali za uandishi. Ingekuwa ni insha, kwa mfano, tungetegemea mtindo tofauti. Huu ni ukweli hata kwa ki-Swahili. Tatizo letu wa-Swahili wa leo ni kuwa elimu na nidhamu ya lugha tumeiweka pembeni. Aina ya lugha inayotamba ni ile ya udaku. Tunaadika kiudaku hata pale tunapojadili mada muhimu, na hata wanasiasa wetu wanahutubia kiudaku :-)

Tukirudi kwenye hiki kifungu nilichonukuu, tunaona kuwa mwandishi ametumia ubunifu mkubwa. Kwa mfano, tunafahamu kuwa katika hii safari yake, linalokimbia ni gari. Lakini yeye ameleta picha tofauti anapotueleza kuwa ni barabara na miti na ardhi pembeni ya barabara ndizo zinazokwenda kasi. Tena kaifananisha barabara kama mto unaoenda kasii: "Through the back window I watched the road pour out from under us..."

Enzi tulipokuwa tunasoma sisi, kuanzia sekondari kwenda juu, tulikuwa tunatakiiwa kutafakari kwa makini na undani usemi kama huu ulioko katika sentensi ya kwanza "whistling over a ribbon of tarmac..."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...