Monday, June 13, 2011

Maonesho ya Utamaduni wa Afrika, Brooklyn Park

Tarehe 11 Juni, katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota, yalifanyika maonesho ya utamaduni wa Afrika, kama nilivyowahi kutangaza katika blogu hii. Kulikuwa na hotuba mbali mbali kuhusu masuala kama afya na mengine mengi.
Kulikuwa na ngoma za watu wa Kamerun ambao wanaonekana hapa kushoto. Tena mmoja wa wachezaji ni mwanasheria maarufu hapa Minnesota, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Alikuwa anayarudi magoma sawa na mtu wa kule kijijini.








Wadau wa aina aina walikuja kwenye maonesho hayo. Kwa upande wa Afrika Mashariki, walikuja wa-Kenya wengi na wa-Ganda, na kulikuwa na meza zao ambapo waliweka majina ya nchi zao. Hapakuwa na meza ya Tanzania, yenye bendera ya nchi kama ilivyokuwa kwa wenzetu. Mdau mmoja kutoka Ethiopia aliniuliza inakuwaje hakuna meza ya wa-Tanzania, wakati wengine wa Afrika Mashariki wana meza. Mimi natoka mji wa mbali, na nilikuwa nimejilipia maonesho hayo kama mtu binafsi sio kama mwakilishi wa Tanzania. Labda wa-Tanzania tusaidiane kutoa maelezo, maana nimeongelea sana kwenye blogu hii na zingine suala la wa-Tanzania kutoonekana kwenye shughuli za aina hii, zinazojumuisha mataifa mbali mbali. Tunakwenda kinyume na alivyotufundisha Mwalimu Nyerere.


Shirika moja dogo la wa-Marekani linaloshughulikia tatizo la kipindupindu Tanzania lilikuwa na meza ambapo taarifa mbali mbali zilikuwepo. Niliongea sana dada Katie JohnsTon ambaye ni mhusika. Yeye na mwenzake mmoja wanajiandaa kwa safari ya Tanzania.






Hapa kushoto kuna meza ya vitu kutoka Kamerun.













Akina mama kutoka Senegal na Togo walionesha vitu mbali mbali vya kwao, zikiwemo nguo, vikapu na vinyago.










Kulikuwepo pia na maonesho ya mitindo ya mavazi. Hapa kushoto anaonekana mwendeshaji wa shughuli hii, Dr. Woldu, aliyevaa nguo nyeupe, na msichana akipita na vazi mojawapo.













Fasihi simulizi na andishi ni sehemu muhimu ya utamaduni. Mimi kama mtafiti hurekodi urithi huo na kuuandikia makala na vitabu. Hapa kushoto anaonekana binti yangu akinisaidia kuonesha na kuelezea kazi zangu hizo. Nimemzoesha tangu alipokuwa mdogo zaidi, na anaweza kuniwakilisha hata kama nimesafiri.





Hapa kushoto niko na mwendeshaji mojawapo wa maonesho haya, Dr. Samuel Woldu kutoka Ethiopia. Mwenye shati la kitenge ni Bwana Albert Nyembwe kutoka Kongo Kinshasa. Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa taasisi ya Cilongo. Pia ni shabiki na mpiga debe mkubwa wa maandishi yangu.







Watoto wa umri mbali mbali, walikuwepo. Hawakuwa watazamaji tu, bali wengine walishiriki kwa vitendo, kama vile nyimbo.










Kwaya ya wa-Kenya iliimba nyimbo mbali mbali, tena kwa kiSwahili. Tukizingatia kuwa lugha ni msingi mkubwa wa utamaduni, hao wa-Kenya walituwakilisha vizuri sisi watu wa Afrika Mashariki.











Kule nyuma kwenye kibanda cha Knight's Cafe akina mama walikuwa wanauza vyakula kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Hapo nilinunua na kuonja chakula kutoka Togo. Sio jambo gumu kuelewa jinsi utamaduni ulivyofungamana na chakula. Kwa kiasi kikubwa chakula ni utambulisho wa utamaduni.

5 comments:

MICHUZI BLOG said...

Prof vipi Wamatumbi mbona siwaoni? Hamkualikwa>

Mbele said...

Kwa kweli Ankal hapa maeneo ya katikati ya Marekani tuna tatizo. Kwa ujumla, wa-Matumbi wa hapa huwa hatushiriki shughuli za aina hii. Sijui wenzetu wa-Ndengereko wa sehemu kama Washington, Texas au California.

Goodman Manyanya Phiri said...

Prof, nimesoma yote hapa. Kazi unayo; tena yataka moyo. Lakini moyo pia kwa ukweli, unao tu!

Nimefurahi sana uliposema binti umemlea ili aelewe shughuli zako hizo. Nami watoto wangu wakwanza wawili ni mabinti na hapo umenipa mfano wa kuigwa kweli.

Mungu akustiri wewe na familia yako nzima pia akupe nguvu zaidi za kuutambulisha Uafrika wako!

Mbele said...

Mbele said...
Mzee Phiri, asante sana kwa ujumbe wako. Ninafurahia sana shughuli hizi. Kila ninaposhiriki nakutana na watu wa aina mbali mbali, wenye uzoefu, mitazamo, na fikra mbali mbali. Kuongea nao ni kuelimika. Kwa maana hiyo, ninajisikia kuwa niko mbali sana kielimu kutokana na mchango wa watu hao katika maongezi yetu.

Kuhusu kuwalea watoto waelewe tunachofanya, nimejifunza kutoka kwa wmwandishi Ernest Hemingway. Watoto wake alikuwa nao sambamba na baada ya yeye kufariki, walikuwa mahiri wa kuuelezea ulimwengu habari zake. Walionekana kujua mengi sana kuhusu maandishi ya baba yao na walikuwa mstari wa mbele katika kuyachapisha hata yale ambayo yeye mwenyewe hakuwa amechapisha.

Siwezi na sitaweza kujifananisha na Hemingway, maana itakuwa ni sawa na sisimizi kujaribu kujifanisha na tembo. Yeye alipata tuzo ya Nobel kwa uandishi. Lakini angalau hiki kipengele cha kuwafanya watoto watuelewe naona ni kizuri na tunakiweza.

Hata hivi, inakuwa ni bahati, maana watoto unaweza kuwa nao, lakini ikawa wao wanapenda vitu tofauti na vyako. Hatuwezi kuwalazimisha, wala kuwalaumu. Huyu wa kwangu nilimwona anapenda shughuli zangu yeye mwenyewe. Tena wakati mwingine, tangu utoto wake, alikuwa anawaleta pia watoto wenzake, ambao ni wa-Marekani, kwenye maonesho ambayo nilikuwa nashiriki.

Matokeo yake yakawa kwamba wale watoto nao wakajijengea upendo kwa mambo ya ki-Afrika, kuanzia miziki na hadi hadithi hadi duku duku ya kwenda kuiona Afrika. Kizuizi ni gharama tu.

Goodman Manyanya Phiri said...

Asante, Prof! Wacha tena niende nikakitafute kitabu cha Hemingway!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...