Showing posts with label Zanzibar. Show all posts
Showing posts with label Zanzibar. Show all posts

Sunday, January 22, 2017

Maandamano Makubwa Dhidi ya Rais Trump

Jana hapa Marekani yamefanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Donald Trump, ambaye aliapishwa juzi. Maandamano haya yaliyoandaliwa na kukusudiwa kwa wanawake, yanasemekana kuwa makubwa kuliko yote yaliyowahi kufanyika katika historia ya Marekani kwa siku moja. Maandamano haya yamefana sana, kwa mahudhurio na hotuba mbali mbali, na yametoa ujumbe wa wazi kuwa serikali ya Rais Trump isitegemee kuwa itatekeleza ajenda yake bila vipingamizi.

Marekani ni nchi inayoheshimu uhuru wa watu kujieleza. Katiba inalinda uhuru huo. Ndio maana maandamano ya kumpinga Rais Trump yalifanyika nchi nzima bila kipingamizi. Polisi walikuwepo kwa ajili ya kulinda amani, si kuzuia maandamano, wala kuwakamata wahutubiaji waliokuwa wanamrarua Rais Trump. Polisi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa waandamanaji wanayo mazingira muafaka na fursa kamili ya kutekeleza haki yao ya kuandamana na kuelezea mawazo yao.

Ninajua kuna wengine walioshiriki maandamano ya jana ambao si wa-Marekani. Kuna wakimbizi na wahamiaji kutoka nchi mbali mbali ambao walishiriki. Hapa Marekani, huhitaji kuwa raia ili kushiriki maandamano. Mimi sikushiriki, kwa sababu zangu binafsi.

Kwa kuwa mimi si raia wa Marekani, na sijawahi kuwazia kuwa raia, sioni kama nina haki au sababu ya kujihusisha na siasa za ndani za Marekani. Sipigi kura wakati wa uchaguzi wa viongozi. Kwa nini nijihusishe na maamuzi ya hao viongozi? Kama maamuzi yataiathiri nchi yangu, hapo nitaona nina wajibu wa kuisemea nchi yangu. Ninatambua wajibu wangu wa kuitetea nchi yangu popote nilipo.

Ingekuwa maandamano yanahusu masuala ya Tanzania ningeshiriki, kwa sababu Tanzania ni nchi yangu. Serikali ya Tanzania ikifanya mambo yasiyokubalika, halafu wa-Tanzania au marafiki wa Tanzania wakaandaa maandamano ya kupinga au kulaani, ni haki yangu kushiriki. Kule Uingereza, mwaka 2015, wa-Tanzania waliandamana kupinga mwenendo wa uchaguzi Zanzibar. Maandamano kama yale ni haki yangu kushiriki.

Huu utamaduni wa Marekani na nchi kama Uingereza unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Baada ya maandamano haya ya kihistoria ya jana dhidi yake, Rais Trump ametuma ujumbe: "Peaceful protests are a hallmark of our democracy. Even if I don't always agree, I recognize the rights of people to express their views." Tafsiri kwa ki-Swahili ni, "Maandamano ya upinzani ya amani ni kielelezo thabiti cha demokrasia yetu. Hata kama mara nyingine sikubaliani na wahusika, ninatambua haki ya watu kuelezea mawazo yao."

Monday, February 14, 2011

Mwanafunzi Wangu Kaniacha Hoi

Leo kaja ofisini mwanafunzi wangu ambaye amerejea siku chache zilizopita kutoka Tanzania, ambako alikuwa ameenda kujifunza masuala ya huduma za hospitali. Alikuwepo kule kwa mwezi moja.

Kabla ya kwenda Tanzania, alikuwa amechukua somo langu moja. Halafu, alipokuwa anaandaa safari ya Tanzania, tulikutana nikamweleza yale ninayowaelezea wa-Marekani kabla hawajaenda Afrika, kuhusu hali ya Tanzania, na hasa kuhusu tofauti za tamaduni kama nilivyozielezea katika kitabu cha Africans and Americans.

Alivyokuwa Tanzania, alikuwa akiangalia shughuli za madaktari katika hospitali moja mkoa wa Arusha. Kutokana na lengo lake la kuwa daktari, amejifunza mengi. Siku za mapumziko alisafiri hadi Dar es Salaam na Zanzibar, hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Lake Manyara. Pia alipanda Mlima Kilimanjaro.

Tulipomaliza maongezi, alinipa picha, bila mimi kutegemea, aliyopiga akiwa kileleni Mlima Kilimanjaro. Nimeguswa sana na zawadi hii. Raha moja kubwa ya ualimu ni kugusa mioyo, akili, na maisha ya wanafunzi. Nimevutiwa na ubunifu wa mwanafunzi huyu. Sikutegemea kuona jina langu linapepea juu ya Mlima Kilimanjaro. Labda ni changamoto, nijikongoje ili nami siku moja nikafike pale.

Sunday, December 19, 2010

Kitabu Kimetua St. Cloud, Minnesota

Wasomaji wa blogu zangu, hii na ile ya ki-Ingereza, wanafahamu ninavyopenda kujishughulisha na masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa leo.

Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo.

Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault.

Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud. Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO, jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud.

Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans, kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma, na anakipenda. Atawaonyesha wadau wa St. Cloud: halmashauri ya mji, shule na vyuo, idara ya polisi, mahospitali, na kadhalika. Nami nilimhakikishia kuwa ni jambo bora. Badala ya watu kununiana tu au kugombana, ni vema wakaanza utaratibu wa kuzungumzia matatizo kama ilivyofanyika Faribault, na ikapokelewa vizuri.

Kama ninavyosema katika mihadhara, blogu na maandishi mengine, matatizo ya aina hii yanayoikumba miji ya Faribault na St. Cloud yanajitokeza katika miji na jamii nyingine duniani: Afrika, Asia, Australia, Marekani, Ulaya, na kwingineko, na yataongezeka, kutokana na mwenendo wa utandawazi wa leo. Ninapokuwa Dar es Salaam, kwa mfano, nasikiliza na kutafakari minong'ono na majungu kuhusu wa-China, ambao wanaendelea kuja katika mji ule. Niliwahi pia kuongelea tafrani iliyotokea Zanzibar. Kinachobaki ni sisi kujizatiti kwa kuelimishana kuhusu tofauti zetu na kutafuta namna ya kuishi bila matatizo.

Najiandaa kushiriki katika masuala ya St. Cloud. Mbali ya umuhimu wake kwa jinsi hali ilivyo, ni fursa ya mimi kujiongezea ujuzi na uzoefu nitakaoutumia katika kuwasaidia wengine.

Friday, November 19, 2010

Wabunge wa CCM Wanakera

Wabunge wa CCM wanakera. Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa.

Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo kile ni ishara ya tabia na mwenendo watakaofuata kwa miaka mitano ijayo.

Tukirudi nyuma, kwenye awamu iliyopita, wabunge wa CCM walikera. Ni nani atakayesahau yaliyotokea wakati Dr. Slaa alipoanza kutamka kuwa kuna ufisadi katika nchi yetu? Wabunge wote wa CCM walimpinga vikali na kumtupia shutuma nzito kwamba alikuwa mzushi.

Dr. Slaa hakuyumba, bali aliendelea kutoa madai yake. Hatimaye, ilianza kuthibitika kuwa aliyokuwa anayasema ni kweli, kwamba tuna mafisadi. Baada ya wananchi kuanza kuona ukweli huo, ukawa haupingiki tena, tuliwaona baadhi ya wabunge wa CCM wakijitokeza na kuanza kujinadi kuwa nao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi. Sijui kama walikuwa wanaongea kwa dhati au kwa lengo jingine.

Tukirudi nyuma zaidi, tunakumbuka suala la machafuko yaliyotokea Visiwani mwaka 2001. Machafuko yale, yaliyotokana na CCM, chama tawala, kushindwa kutumia haki na busara, yaliiletea Tanzania aibu kubwa duniani. Kwa uthibitisho, soma hapa.

Lakini, pamoja na maovu yote yaliyofanyika Visiwani, pamoja na fedheha yote iliyoiangukia Tanzania, wabunge wa CCM hawakukubali kuwa serikali ya CCM ilikuwa na makosa, wala hawakukubali kuwa Tanzania ilikuwa inafedheheka. Wao waliitetea serikali ya CCM. Maadam palikuwa na suala lililohusu chama cha upinzani, yaani CUF, wabunge wa CCM waliamua kuikingia kifua serikali ya CCM, badala ya kusimamia haki za binadamu na heshima ya Tanzania.

Je, kuna kero kubwa zaidi ya hii ya kutojali maslahi ya Taifa na badala yake kuangalia maslahi ya kikundi fulani?

Wednesday, March 17, 2010

Naishangilia Zanzibar

Siku kadhaa zilizopita nilipata fursa ya kusikiliza hotuba aliyotoa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff, kule Uingereza, akielezea makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Karume. Bofya hapa.

Nimeipenda sana hotuba ile, kwa jinsi ilivyojaa kumbukumbu, mawazo, tathmini na mawaidha kuhusu siasa Zanzibar. Nimevutiwa na jinsi Zanzibar ilivyofikia hatua ya kutathmini maana ya mfumo wa siasa ambao umetumika kwa yapata nusu karne na wakauona kuwa una dosari na ni chanzo cha matatizo. Mfumo huo ni wa vyama vya siasa.

Mimi mwenyewe nimehoji sana mantiki ya dhana nzima ya chama au vyama vya siasa. Mwaka jana niliandika makala nikihoji kama chama cha siasa au vyama vya siasa ni kitu cha lazima katika kujenga demokrasia. Nilisema kuwa tumeiga hii dhana kikasuku, na tunashinikizwa na mataifa mengine. Nilitamka kuwa labda kuna umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kujenga demokrasia bila chama au bila vyama. Bofya hapa. Mawazo yangu, ambayo yanahoji mambo tuliyozoea, katika siasa, uchumi, utamaduni, elimu na kadhalika, yamo katika kitabu cha Changamoto.

Nimefurahi kusikia maelezo ya Maalim Seif kuhusu tathmini waliyoifanya Zanzibar, hadi wakafikia hatua ya kujenga ushirikiano baina ya CUF na CCM, na kuondokana na historia ya uhasama, kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar. Wamefanya uamuzi wa maana, na nimefurahi kuona jinsi wanavyojipanga kuunganisha nguvu za wa-Zanzibar wote, walioko nchini na nje ya nchi, ili wajenge Zanzibar, ambayo zamani ilikuwa na historia na heshima kubwa duniani.

Naamini kuwa kwa Zanzibar kuchukua uamuzi huu, sote tutafaidika. Kuimarika kwa Zanzibar ni neema kwa Muungano. Wale waliokuwa wanaitumia Zanzibar kwa manufaa yao, wakawa wanaendekeza siasa za mfarakano, ndio pekee watakaoambulia patupu. Wale waliokuwa wanaendekeza ubabe wa kutumia nguvu ya chama au vyama, wamepewa somo kubwa. Nategemea watajifunza.

Hotuba hii ya Maalim Seif nimeona ni muhimu kuliko zote ambazo nimewahi kuzisikia kutoka kwa wanasiasa wetu tangu aondoke Mwalimu Nyerere.

Wednesday, March 3, 2010

Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad

Mwaka jana, nilipokuwa Dar es Salaam, niliingia katika duka la vitabu, Dar es Salaam Bookshop, nikanunua vitabu kadhaa vya ki-Swahili. Vitatu vilikuwa vya Shaaban Robert, na kingine ambacho sikuwa nimewahi kusikia habari zake, kilikuwa juu ya Siti Binti Saad.
Kitabu hiki Mfinyanzi Aingia Kasri: Siti Binti Saad Malkia wa Taarab, kimeandikwa na Nasra Mohamed Hilal wa Malindi, Zanzibar, ambaye alikuwa mtangazaji wa Radio Tanzania Zanzibar kwa miaka 27. Kimechapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, 2007.

Kwa mujibu wa taarifa iliyo ukurasa wa nyuma ya kitabu, Bibi Nasra "(a)mefanya utafiti wa historia ya wanawake wa makabila mbali mbali walioishi mjini Zanzibar na kuacha nyayo zao juu ya mila, utamaduni na sanaa. Hivi sasa anakamilisha vitabu vingine viwili. Zaidi ya uandishi Bibi Nasra ni mtengenezaji wa filamu wa kujitegemea na amekwishatoa filamu tano fupi, zote katika Kiswahili."

Natoa pongezi na shukrani kwa juhudi za mama huyu. Kitabu chake hiki kinathibitisha juhudi yake katika utafiti, kwani amekusanya habari na kumbukumbu nyingi kutoka kwa watu mbali mbali waliomfahamu Siti Binti Saad, wakiwemo ndugu zake.

Amekusanya nyimbo mbali mbali za Siti Binti Saad, nyingine zikiwa mpya kwetu ambao ufahamu wetu wa Siti Binti Saad unatokana na maandishi. Tuna bahati ya kuzipata taarifa na nyimbo nyingi namna hii katika kitabu kimoja.

Kuna mengi ya kujifunza kutokana na maisha na tungo za Siti Binti Saad, ambaye alipambana na matatizo mengi katika maisha yake, lakini akawa shujaa mwenye kujiamini muda wote. Alituachia mafundisho mengi murua. Kwa mfano, katika wimbo wake moja alisema

Ukicha kutajwa
Hutotenda jambo....

Alimaanisha kuwa kama unaogopa maneno ya watu, hutafanya kitu cha maana maishani.

Kama tunavyofahamu, msingi wa utafiti juu ya Siti Binti Saad uliwekwa na Shaaban Robert, katika kitabu chake cha Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika kufuatilia habari za Shaaban Robert, nimeshangazwa na vipaji vyake. Kwa mfano, ingawa hakuwa na elimu kubwa ya shuleni, ikiwemo elimu ya utafiti wa masuala ya aina hii, Shaaban Robert alifanya kazi nzuri, akizingatia maadili ambayo leo tunafundisha vyuoni. Bibi Nasra ameutaja vizuri mchango wa Shaaban Robert na amemtolea sifa na shukrani ipasavyo.

Nategemea kupata wasaa wa kukichambua kitabu hiki cha Mfinyanzi Aingia Kasri siku zijazo na kuelezea maoni yangu vizuri. Kwa leo nimeona nikitaje tu, ili walimwengu wapate kufahamu uwepo wake.


















Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...