Thursday, August 13, 2009

Tunahitaji Vyama vya Siasa?

(Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Agosti 11-17, 2009)


Profesa Joseph L. Mbele

Jamii yetu, kama jamii zingine, inatafuta namna ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Katika harakati hii, uamuzi ulifikiwa kwamba tuwe na vyama vya siasa, badala ya chama kimoja. Vyama vya siasa vinapiganiwa karibu kila mahali kwa imani kuwa ni njia muhimu ya kujenga demokrasia. Kama kuna nchi isiyo na vyama vya siasa, utawala wa nchi hiyo unahesabiwa kuwa si wa kidemokrasia.

Kwa maana hii, kuuliza kama tunahitaji vyama vya siasa inaonekana ni upuuzi. Lakini mimi sioni kama ni suali la kipuuzi.

Demokrasia ni nini? Ni aina ya utawala ambamo umma umeshika hatamu. Demokrasia ni utawala unaowakilisha na kuendeleza matakwa na maslahi ya umma. Hii ndio maana ya demokrasia. Dhana ya vyama haiko kwenye tafsiri hii, kwani sio msingi au uhai wa demokrasia. Ni namna gani demokrasia inaweza kujengwa? Ili demokrasia iwepo, ni lazima kuwe na vyama? Haya ndio masuali ya kujiuliza.

Huko Ulaya, katika historia yao na mazingira yao, waliamua kuwa mfumo wa vyama vya siasa ndio wanaouhitaji kwa kujengea na kuwezesha demokrasia. Huo ulikuwa uamuzi wao, kufuatana na hali halisi ya kwao.

Lakini je, Watanzania tulikaa lini tukatathmini historia na mazingira yetu, hadi kufikia uamuzi kuwa ili tuwe na demokrasia, tunahitaji mfumo wa vyama? Tumefanya hiyo tathmini au tumeiga tu? Je, kinachofaa au kuhitajika Ulaya ni lazima kiwe hiki hiki hapa kwetu? Hili ni suali muhimu.

Je, hatukuwa na historia na jadi yetu ambayo tungeweza kuitumia katika kujenga demokrasia yetu? Je, kwa nini tumeshindwa hata kuwazia hilo? Mataifa yanayotutawala kiuchumi nayo yanatushinikiza tuwe na vyama vya siasa. Je. huu si ukoloni mambo leo, ambao watu kama Frantz Fanon waliuelezea?

Vyama vya siasa tumevipata, na huenda vikaongezeka. Je, vimetusaidia au vimetuletea matatizo? Ni wazi kuwa katika nchi yetu, vyama vya siasa vimeleta mfarakano, ambao unazidi kuota mizizi. Kampeni za uchaguzi zinaendelea kuwa na sura ya magomvi. Kadiri siku zinavyopita, amani inazidi kuharibika. Hayo yote yako wazi, lakini wazo la kuhoji umuhimu wa vyama vya siasa halisikiki.

Mtu anaweza kusema kuwa tunaweza kuendesha siasa ya vyama vingi kwa amani na utulivu. Lakini hoja hii haitavunja hoja yangu ya msingi kuwa tumeiga mambo kikasuku.

Tunataka demokrasia. Hilo ni wazi. Ingekuwa bora iwapo tungetafuta mfumo tofauti wa kujenga na kuendeleza hiyo demokrasia, mfumo unaotufaa kwa mujibu wa historia, jadi na mazingira yetu. Mfumo huu ungekuwa ni wetu, usio na chembe ya kushinikizwa kutoka nje, kama ilivyo sasa.

Kuna tatizo gani, kwa mfano, kuwa na mfumo ambao ungetumia busara za wazee kama ilivyokuwa katika jadi zetu? Ingewezekana kila kijiji, tarafa, au wilaya kuwachagua wazee wenye busara na kukubalika, wakawa ndio wawakilishi kwenye ngazi hizo na kiTaifa pia. Kwa busara zao, hao wangewasilisha maoni na mahitaji ya jamii zao, kuanzia watoto hadi wazee, wanawake kwa wanaume.

Katika maisha ya kila siku ya jamii yetu, wazee wanashika wadhifa huo. Mbunge ambaye tunamchagua kwa mtindo huu wa vyama vya siasa anaweza kupotea muda mrefu, asionekane hadi wakati wa uchaguzi ujao, lakini masuala ya jamii anayopaswa kuiwakilisha yanatatuliwa na wanavijiiji wenyewe kwa njia zao za asili. Kuna wabunge ambao ni kama watalii kwenye majimbo yao ya uwakilishi, lakini maisha ya wanavijiji kwenye majimbo hayo yanaendelea kwa msingi wa utaratibu ambao si wa vyama, ikiwemo jadi ya kuwatumia wazee.

Miaka ya karibuni, tumeona kitu cha aina hiyo kikifanyika katika kutafuta ufumbuzi wa masuala ya bara la Afrika. Wazee kama Askofu Desmond Tutu, Jimmy Carter, na Kofi Annan, wamepekwa kushughulikia masuala kama yale ya Zimbabwe. Katika migogoro ya Somalia, mara kwa mara wazee wamekuwa ndio watafutaji wa suluhisho. Miezi kadhaa iliyopita, wazee hao walikusanyika Kenya, wakafanya mazungumzo ya muda mrefu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya nchi yao. Hapa Tanzania, tuliona jinsi Rais Ali Hassan Mwinyi alivyokuwa na utaratibu wa kuongea na wazee wa Dar es Salaam, kuhusu masuala muhimu ya kiTaifa. Binafsi, naona Mzee Mwinyi alikuwa na upeo mzuri ambao ungepaswa kuimarishwa. Mifano hii yote inaendana na hoja ninayojaribu kujenga hapa, kuhusu umuhimu wa waAfrika kutafuta mifumo inayofaa kwa demokrasia katika mazingira yetu.

Utawala wa nchi si lazima uwe kwa mfumo chama cha siasa au vyama vya siasa. Nchi inaweza kutawaliwa bila chama au vyama. Kuwepo au kutokuwepo kwa demokrasia ni suala ambalo si lazima lihusishwe na vyama. Unaweza kuwa na demokrasia bila vyama, kama ilivyokuwa enzi za mababu na mabibi zetu, kabla ya kuja wazungu. Hapakuwa na vyama. Lakini, kama Mwalimu Nyerere alivyoandika, wazee walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadiliana masuala hadi kukubaliana. Hii ilikuwa ni demokrasia, bila vyama.

Kinachohitajika ni sisi kufanya tafakari sisi wenyewe, si kudandia mambo ya Ulaya kama tunavyofanya. Uganda imeonyesha mfano, ina mfumo ambao inaona unafaa katika nchi ile, kufuatana na historia na mazingira yake. Mfumo wao unaweza kuwa na dosari, lakini angalau ni matokeo ya tathmini yao wenyewe. Wanaweza kuubadili wakaunda mwingine, kufuatana na hali halisi, bila kuiga kikasuku. Hizi ni fikra za watu huru. Kwa kutumia na kuthibitisha uhuru wa fikra na uamuzi, kila nchi katika bara letu, ingeweza kujitungia mfumo wa aina yake, kwa mujibu wa hali halisi ya nchi ile. Kwa mtindo huu, tungejenga demokrasia ya kweli, kudumisha amani na mshikamano, na kuleta maendeleo, sio fujo hizi tunazoziendekeza sasa kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa.

Tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao chimbuko lake na nguvu zake ni umma, mfumo ambao unasimamia na kuendeleza maslahi ya umma. Lakini je, ili hayo yawepo, tunahitaji vyama vya siasa? Hili ndilo suali linalohitaji jibu.

4 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

good article waweza kujiuliza kama kweli tuna hiyo demokrasia ya wazungu pia kwani inasemekana JK aliingizwa madalakani na kura zisizofika milioni kumi. kati ya watanzania wanaokadiriwa kuwa 40m, mnaongozwa na mtu mwenye vijikura kidogo.

tuliache hilo, prof unaonekana kujipendelea wewe kama mzee labda ndio maana unapedakeza wazee wenye busara pekee. lakini hata mabaraza ya vijana, nk yanaweza kuangaliwa katika mfumo unaoupendekeza kwani busara haina uhusiano kwa karibu sana na mvi kwani nyingine ni za kuzaliwa n azo zaidi kuliko kuzeeka nazo

Mbele said...

Luta, naona umetoa changamoto nzuri, kwa yote unayosema. Ndio faida na raha ya mijadala.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aiseee

mumyhery said...

Mimi nafikiri labada tungepatiwa elimu zaidi kuhusu suala hili

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...