(Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Agosti 18-24, 2009)
Profesa Joseph L. Mbele
Katika makala zangu za hivi karibuni, nimegusia suala la kuiga mambo, kama vile mashindano ya urembo na suala la vyama vya siasa. Inaonekana suala hili litahitaji kushughulikiwa tena na tena. Katika makala yangu moja, niliongelea safari za JK nchi za nje, na baadhi ya watu walilalamika kuwa JK anasafiri mno. Walikumbushia kuwa viongozi wa nchi zingine za jirani, kama vile Kenya, hawasafiri hivyo, lakini nchi zao zinapiga hatua kutuzidi. Hitimisho likawa kwamba JK awaige viongozi hao; atumie muda mwingi nchini badala ya nje.
Wazo kuwa JK afanye kama wanavyofanya viongozi wa nchi zingine linahitaji tafakari. Napenda kuliongelea wazo hilo, kwa kutumia mfano huo wa Kenya na Tanzania. Je, kiongozi wa Tanzania anaweza kuiendeleza Tanzania kwa kuiga anayofanya kiongozi wa Kenya? Tanzania inaweza kuendelea kwa kuiiga Kenya?
Tanzania ni nchi yenye upekee. Kenya nayo ina upekee wake. Hizi nchi mbili zinatofautiana, kama zinavyotofautiana na Uganda, Rwanda, Congo, au Burundi. Tanzania ina historia yake, jadi yake, mtazamo wake, na malengo yake. Mahusiano ya jamii ndani ya Tanzania ni ya kiTanzania. Na Kenya ni hivyo hivyo. Kenya ina historia yake, jadi yake, na malengo yake. Mfumo wake wa uchumi na kijamii ni tofauti na wetu.
Mahusiano ya Kenya na nchi za jirani au nchi za mbali ni tofauti na mahusiano ya Tanzania na nchi za jirani yake au za mbali. Kenya inapakana na Somalia, Sudan na Uganda. Somalia kuna matatizo yanayoitishia Kenya pia. Masuala ya kiusalama yanayoihusu Kenya si sawa kabisa na yale yanayoihusu Tanzania. Tanzania ina utulivu kwa kiasi kikubwa, na hakuna mpaka wenye matatizo kwa wakati huu. Kiongozi wa Tanzania hakabiliani na hali halisi anayokabiliana nayo kiongozi wa Kenya.
Wakenya ni watu tofauti, na Watanzania ni watu tofauti. Sasa je, anayofanya kiongozi wa Kenya, au anayotakiwa kufanya kiongozi wa Kenya, yanaweza kutumika katika Tanzania? Au anayofanya kiongozi wa Tanzania, anayotakiwa kufanya kiongozi wa Tanzania, yanaweza kuwa sawa na yale ya Kenya. Kiongozi wa Tanzania anaweza kweli kuiongoza Tanzania kama vile ingekuwa Kenya? Au je, kiongozi wa Kenya anaweza kuiongoza Kenya kama vile ingekuwa Tanzania?
Mtu anayezunguka duniani ataona kuwa Wakenya wametapakaa duniani kuliko Watanzania. Mahali kama Marekani, kwa mfano, kama kuna chuo chenye waAfrika labda watatu au wawili, uwezekano ni mkubwa kuwa Mkenya yupo, na Mnigeria. Wakenya wanaoishi nje wanajituma katika masuala kama biashara na jumuia za kuleta maendeleo nchini kwao. Wanafanya mikutano, ambayo inahudhuriwa na viongozi kutoka Kenya, kwa madhumuni hayo. Nimewahi kuhudhuria hapa Minnesota.
Wakenya huku Marekani wanayo magazeti na vyombo vingine vya habari ambavyo wanavitumia kuitangaza nchi yao. Kenya imefanikiwa sana kujitangaza.
Serikali ya Kenya inashirikiana na hao waKenya waishio nje. Ilishaweka kitengo katika wizara yake ya Mambo ya Nchi za Nje cha kushughulikia masuala ya Wakenya hao. Kenya inajua kuwa waKenya hao wana mchango mkubwa katika uchumi wa Kenya. Hela ambazo waKenya walioko nje wanaingiza katika uchumi wa nchi yao ni zaidi ya mara nne kufananisha na zile wanazoingiza waTanzania walioko nje katika uchumi wao. Kwa kiasi kikubwa hii ni kwa sababu waKenya walioko nje ya nchi yao ni wengi zaidi kuliko waTanzania walioko nje ya nchi yao.
Mbele ya yote hayo, Rais wa Kenya ana sababu gani ya kuzunguka duniani kuitangaza nchi yake? Watu wake wanafanya hii kazi vizuri kabisa. Watanzania tunalalamika kuwa Wakenya wamefanikiwa hata kuutangazia ulimwengu kuwa Mlima Kilimanjaro uko kwao. Ni wazi kuwa, hata rais wa Kenya akikaa nchini muda wote, watu wake wako makini, walioko nchini na nje.
Sasa sisi Watanzania tukoje, hadi tudiriki kusema kuwa JK abaki nyumbani kama anavyofanya rais wa Kenya? Watanzania huku ughaibuni hatuwafikii waKenya katika masuala ya maendeleo ya nchi. Jambo hili nililitaja katika makala yangu kuhusu safari za JK nchi za nje. Watanzania tunakutana kwenye sherehe au misiba. Siku hizi, waTanzania walioko Ulaya, hasa Uingereza, wanajibidisha katika kufungua matawi ya CCM, badala ya kufanya shughuli za maendeleo na kuitangaza nchi kama wanavyofanya waKenya. Tunaanzisha matawi ya CCM badala ya kuanzisha angalau magazeti ya kuitangaza nchi.
Kwa upande mwingine, tofauti na ilivyo Kenya, Watanzania walioko nyumbani na wale walioko nje hawana mshikamano. Mtanzania wa nyumbani akisikia kuhusu Mtanzania anayeishi nje anamkejeli kuwa ni mlowezi au msaliti. Anaisema kuwa huyu aliyeko nje arudi nyumbani kujenga Taifa. Hata serikali yetu haijawa na mkakati wa kuwatambua hao waTanzania walioko nje na kuwashirikisha kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. Serikali haijawa na kitengo cha kushughulikia masuala ya waTanzania walioko nje. Ni wakati huu tu ndio tunasikia taarifa kuwa utaratibu wa aina hii utaanzishwa.
Kwa kifupi, Watanzania bado tuna njia ndefu. Simlaumu JK kwa kuzunguka duniani akijaribu kuitangaza nchi yetu. Wajibu wa kiongozi wa Tanzania ni kutathmini hali halisi ya nchi yake na kuamua nini kinachohitajika. Wiki chache zilizopita, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika kuongelea masuala fulani ya hapo Chuoni, ulisema kuwa unaona matunda ya ziara za JK nchi za nje. Nilitegemea wale ambao wamekuwa wakipinga sana ziara hizo wangetoa kauli. Labda bado wanatafakari. Papo hapo, kabla ya Chuo Kikuu cha Dodoma kutoa kauli hiyo, Mheshimiwa Charles Stith, aliyekuwa Balozi wa Marekani hapa Tanzania, naye alisema kuwa ziara za JK nchi za nje zina manufaa. Nilitegemea wapinzani wa ziara hizo wangejitokeza kuinga kauli hiyo, lakini hawajajitokeza. Kama wanaamini kuwa JK abaki nyumbani, kwa nini wasijitokeze na hoja yao wakati huu? Naamini kuwa kadiri siku zinavyopita, ukweli utaendelea kujitokeza, kuwa kiongozi wa Tanzania anapaswa kufanya yale yanayotokana na tathmini ya hali hali
si na mahitaji ya Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
6 comments:
Heshima kwako Profesa. Ningependa kunukuu kuwa "Serikali ya Kenya inashirikiana na hao waKenya waishio nje. Ilishaweka kitengo katika wizara yake ya Mambo ya Nchi za Nje cha kushughulikia masuala ya Wakenya hao."
Pengine tungeanza kujifunza kwa kufanya hili. Ni kweli kabisa kuwa serikali ya Kenya na Tanzania ni tofauti, na ni kwel kuwa ziara za Rais zinagharimu saana. Binafsi nadhani hili nililonukuu liwe la kwanza, pili apunguze TIMU anayosafiri nayo maana kuna wakati nadhani anakuwa na watu weni kuliko mahitaji HALISI ya wale aambatanao nao. Tatu, aainishe afanyayo. Tulishazungumza hili hapa mara nyingi kuwa matatizo ya serikali yetu ni kufanya HABARI MUHIMU KWA WANANCHI kuwa kama ZAWADI. Serikali haisemi Rais kafanya nini, kanufaisha nchi kivipi na ataiweka nchi katika uwezo gani wa kuendelea akindelea na ziara zake.
Nakubaliana na mengi usemayo, japo naamini RAIS ANASTAHILI KUPANGUA NA KUPANGA UPYA TIMU YAKE YA WASHAURI NA WATENDA KAZI HASA KATIKA UPASHANAJI HABARI.
Amani kwetu
Mzee wa Changamoto, shukrani kwa ujumbe. Napangia kuandika makala nyingine moja au mbili kuendelea kuelezea suala hili, na kujibu hoja za wapinzani. Kila la heri.
nimeongea na mdhungu mmoja kutoka ujermani na nimeanza kukubali kuwa ziara hizi zina manufaa japo mwanzoni nilimlaumu
Pia wahenga walisema mtembea bure si sawa na mkaa bure, ukikaa na kusubiri unachokihitaji ukipate bila kutoka kukitafuta utasubiri sana
Nyote mko sahihi kabisa. Kila mtu anajua kuwa Rais ana akili timamu na anajua kuwa kuna manufaa ya safari zake. Lakini bado nalia na WASAIDIZI WAKE. Jamani hawa wasaidizi wake hawaijulishi jamii kulikoni. Na hilo ndilo ninaloamini JK anastahili kuwajibika. Kama hajui kuwa anaangushwa na WASAIDIZI / WATENDAJI WAKE basi ni yeye wa kulaumiwa. Hatujulishwi kinachoendelea katika ziara zake. Na ndio maana nakereka kuona Prof Mbele ana mengi ya kueleza kuliko IDARA YA MAWASILIANO YA IKULU. Wangekuwa wanatu-keep up to date wengi wasingelaumu.
Amani kwenu
NAUNGA MKONO safari za nje za rais katika maana hiyo hiyo ya maendeleo lakini tahadhari lazima iwepo kuwa gharama zitumikazo wakati mwingine ni kubwa wataalam wanadai ni mamilioni ya fedha,kusafiri nimmuhimu lakini lazima uchambuzi kuntu wa gharama na hasara zinazopatikana lazima uzingatiwa ili kuleta maendeleo sufufu asante profesa kwa hoja tamu mimi ni TANDASI wa NDOTOYANGU-HARAKATI.BLOGSPOT.COM.
Post a Comment