Showing posts with label Kilimanjaro. Show all posts
Showing posts with label Kilimanjaro. Show all posts

Monday, May 23, 2011

Maktaba ya Mkoa, Kilimanjaro

Tarehe 3 Agosti, mwaka jana, nilikuwa mjini Moshi nikiwa na hamu ya kuufahamu zaidi mji huo. Lengo langu moja lilikuwa kuiona maktaba ya mkoa, kwani nilikuwa sijawahi kufika hapo.

Haikuwa vigumu kufika mahali hapo. Niliingia ndani nikaona kuwa ni maktaba yenye hali nzuri kwa ujumla, kwa upande wa vitabu na majarida, nikifananisha na maktaba kadhaa nilizoziona sehemu zingine za nchi.


Kwa kawaida, ninapoingia katika maktaba za Tanzania, nimezoea kuwaona zaidi wanafunzi. Katika maktaba ya Moshi, niliwaona watu wazima kadhaa wakisoma. Sijui kama hii ndio kawaida katika maktaba hii, lakini niliguswa na jambo hilo.

Kila maktaba duniani, hata kama ni bora namna gani, inahitaji vitabu na majarida mapya muda wote, pamoja na tekinolojia na vifaa vya kisasa vya kupatia maandishi na taarifa. Na ndiyo changamoto kwa maktaba za Tanzania. Nimeona niweke hii taarifa fupi na picha kwenye blogu yangu, ili wengine wapate angalau fununu kuhusu hii maktaba ya Moshi.

Monday, February 14, 2011

Mwanafunzi Wangu Kaniacha Hoi

Leo kaja ofisini mwanafunzi wangu ambaye amerejea siku chache zilizopita kutoka Tanzania, ambako alikuwa ameenda kujifunza masuala ya huduma za hospitali. Alikuwepo kule kwa mwezi moja.

Kabla ya kwenda Tanzania, alikuwa amechukua somo langu moja. Halafu, alipokuwa anaandaa safari ya Tanzania, tulikutana nikamweleza yale ninayowaelezea wa-Marekani kabla hawajaenda Afrika, kuhusu hali ya Tanzania, na hasa kuhusu tofauti za tamaduni kama nilivyozielezea katika kitabu cha Africans and Americans.

Alivyokuwa Tanzania, alikuwa akiangalia shughuli za madaktari katika hospitali moja mkoa wa Arusha. Kutokana na lengo lake la kuwa daktari, amejifunza mengi. Siku za mapumziko alisafiri hadi Dar es Salaam na Zanzibar, hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Lake Manyara. Pia alipanda Mlima Kilimanjaro.

Tulipomaliza maongezi, alinipa picha, bila mimi kutegemea, aliyopiga akiwa kileleni Mlima Kilimanjaro. Nimeguswa sana na zawadi hii. Raha moja kubwa ya ualimu ni kugusa mioyo, akili, na maisha ya wanafunzi. Nimevutiwa na ubunifu wa mwanafunzi huyu. Sikutegemea kuona jina langu linapepea juu ya Mlima Kilimanjaro. Labda ni changamoto, nijikongoje ili nami siku moja nikafike pale.

Thursday, February 3, 2011

Mji wa Moshi, Tanzania

Moshi ni mji maarufu kaskazini mwa Tanzania, chini ya Mlima Kilimanjaro. Siufahamu sana mji huu, ingawa nimepita hapo mara kadhaa, na hata kulala, mara mbili tatu.






Kama ilivyo katika miji mikubwa ya Tanzania, Moshi kuna hoteli nzuri za kufikia wageni. Wakati moja nililala katika hoteli hii hapa kushoto.









Moshi ni maarufu kwa usafi. Wa-Tanzania wanajua kuwa uongozi wa Moshi una sheria kali kuhusu usafi. Hapo kushoto nipo kituo cha mabasi, pasafi kama vile pamepigwa deki. Nilikuwa safarini baina ya Arusha na Dar es Salaam. Nimechoka, shaghalabaghala; msafiri kafiri na kitabu changu cha Under Kilimanjaro.

Tangu mara yangu ya kwanza kuingia mjini Moshi, nilivutiwa na msikiti unaoonekana kushoto, ambao uko pembeni mwa kituo cha mabasi.







Wakati mmoja nilikuwa Moshi na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, niliowaleta nchini kuwafundisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway alivyosafiri nchini mwetu akaandika juu yake. Niliwapeleka hadi Chuo cha Mweka, kinachoonekana kushoto. Kiko nje kidogo ya mji.

Ninapokuwa katika mji wowote napenda kujua maktaba ilipo. Hapo kushoto ni maktaba ya mkoa. Niliingia ndani, nikaona ilivyo nadhifu. Ina majarida na vitabu kiasi cha kuridhisha, nikifananisha na maktaba nilizoziona mikoani Tanzania. Nilivutiwa kuwaona watu wakisoma, sio watoto wa shule tu, kama ilivyo kwenye maktaba zingine.

Nilitembea kutoka Lutheran Uhuru Hostel kuelekea barabara kuu itokayo Arusha, nikaiona hoteli hii inayoonekana kushoto. Nilivutiwa na tangazo la mchemsho, ingawa sikupata kuingia ndani. Hamu ya kuingia nilikuwa nayo, kwa mategemeo ya kupata chakula cha ki-Chagga. Ni suala muhimu la kuzingatiwa siku za usoni, panapo majaliwa.

Saturday, April 10, 2010

Mpambano na Lonely Planet

Siku kadhaa zilizopita niliandika kuhusu msomaji wa kitabu changu cha Africans and Americans ambaye alisema kinafaa kuliko kile cha Lonely Planet. Bofya hapa. Nilitamka kiutani kuwa Lonely Planet wakae chonjo, maana wamepata mshindani.

Lakini baadaye, nililazimika kuandika tena kuhusu Lonely Planet, baada ya wao kuandika taarifa iliyoudhalilisha mji wetu wa Arusha. Bofya hapa. Hapo uzalendo ulinisukuma kusema kuwa hao sasa wanatuchokoza, na lazima tujizatiti kujibu mapigo.

Dada Subi, ambaye ni mfuatiliaji makini wa maandishi ya wanablogu wa Bongo na pia mshauri wetu tunayempenda na kumheshimu sana, kanibonyeza leo asubuhi kuwa kuna jambo limetokea Lonely Planet, yaani mteja anayepangia kwenda Tanzania anaulizia kitabu au vitabu vya kusoma, ambavyo si vya aina ya Lonely Planet.

Basi, hapo nimeona lazima niingie mzigoni na kuwachangamkia hao Lonely Planet. Sio kuwalazia damu; ni kuwavalia njuga tu. Nimefanya hivyo tayari, kwa kumpa yule mteja taarifa anazohitaji. Bofya hapa. Heshima na shukrani kwa Dada Subi, kama kawaida, na blogu yake maarufu hii hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...