
Nafanya shughuli hizi si kwa ajili ya kutafuta umaarufu, bali naamini ni wajibu kwa wanadamu kusaidiana katika maisha na kuifanya dunia iwe bora kuliko ilivyo.
Miezi ya karibuni nimejishughulisha sana na matatizo yanayowapata wahamiaji wa ki-Somali katika jimbo la Minnesota, ambalo linaongoza kwa idadi ya wahamiaji wa ki-Somali. Wasomaji wa blogu zangu watakumbuka taarifa za shughuli zangu katika mji wa Faribault.
Matatizo kama haya ya Faribault yako pia katika miji mingine, kama vile St. Cloud. Kutokana uzoefu nilioupata Faribault, nimeanzisha mawasiliano na ndugu Mohamoud Mohamed, mkurugenzi wa SASSO, jumuia inayoshughulikia masuala ya wa-Somali mjini St. Cloud.
Nilimpelekea nakala ya kitabu cha Africans and Americans, kama mchango wangu na changamoto. Jana ameniambia kuwa kitabu amekipata, anaendelea kukisoma, na anakipenda. Atawaonyesha wadau wa St. Cloud: halmashauri ya mji, shule na vyuo, idara ya polisi, mahospitali, na kadhalika. Nami nilimhakikishia kuwa ni jambo bora. Badala ya watu kununiana tu au kugombana, ni vema wakaanza utaratibu wa kuzungumzia matatizo kama ilivyofanyika Faribault, na ikapokelewa vizuri.
Kama ninavyosema katika mihadhara, blogu na maandishi mengine, matatizo ya aina hii yanayoikumba miji ya Faribault na St. Cloud yanajitokeza katika miji na jamii nyingine duniani: Afrika, Asia, Australia, Marekani, Ulaya, na kwingineko, na yataongezeka, kutokana na mwenendo wa utandawazi wa leo. Ninapokuwa Dar es Salaam, kwa mfano, nasikiliza na kutafakari minong'ono na majungu kuhusu wa-China, ambao wanaendelea kuja katika mji ule. Niliwahi pia kuongelea tafrani iliyotokea Zanzibar. Kinachobaki ni sisi kujizatiti kwa kuelimishana kuhusu tofauti zetu na kutafuta namna ya kuishi bila matatizo.
Najiandaa kushiriki katika masuala ya St. Cloud. Mbali ya umuhimu wake kwa jinsi hali ilivyo, ni fursa ya mimi kujiongezea ujuzi na uzoefu nitakaoutumia katika kuwasaidia wengine.