Showing posts with label Changamoto: Insha za Jamii. Show all posts
Showing posts with label Changamoto: Insha za Jamii. Show all posts

Friday, February 17, 2017

Umuhimu wa Kuzifahamu Tamaduni za Wengine

Mada ya tofauti za tamaduni na athari zake duniani ninaishughulikia sana. Kwa mfano, nimeandika kitabu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimeongelea suala hilo pia katika kitabu changu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Vile vile ninaliongelea mara kwa mara katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Umuhimu wa kuzifahamu tofauti za tamaduni unaonekana wazi wazi wakati tunapokumbana na matatizo katika mahusiano yetu na watu wa tamaduni ambazo si zetu. Tusijidanganye kwamba jambo hilo ni la kinadharia tu na kwamba halituhusu. Miaka michache iliyopita, wafanya biashara wa Tanzania walikwenda Oman kushiriki maonesho ya biashara. Walipata shida kutokana na kutojua utamaduni wa watu wa Oman. Taarifa hiyo iliandikwa katika blogu ya Michuzi.

Suala hili haliwahusu wafanya bashara tu, bali wengine pia, kama vile wanafunzi wanaokwenda nchi za nje, wanadiplomasia, watu wanaokwenda mikutanoni, na kadhalika. Kwa kuzingatia hayo, na kwa kuwa nimekuwa nikifanya utafiti katika masuala hayo, nimekuwa nikipata mialiko ya kutoa ushauri kwa jumuia na taasisi mbali mbali hapa Marekani. Vyuo vya Marekani, kwa mfano, vinapopeleka wanafunzi nchi za nje, kama vile nchi za Afrika, vinazingatia suala la kuwaandaa wanafunzi kwa kuwaelimisha kuhusu utamaduni wa huko waendako. Mwaka hadi mwaka nimealikwa kutoa elimu hiyo.

Nimewahi pia kuendesha semina Tanzania, kwenye miji ya Arusha, Tanga, na Dar es Salaam. Vile vile, kwa kuombwa na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, niliwahi kutoa mihadhara Zanzibar na Pemba, juu ya utamaduni wa Marekani, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Kwa jinsi ninayofahamu umuhimu wa suala hili, nimekuwa nikikumbushia mara kwa mara kila ninapoweza. Kwa mfano, uhusiano ulipoanza kuimarika baina ya Tanzania na u-Turuki, nilikumbushia suala hilo katika blogu hii. Ningependa kuona suala hili la athari za tofauti za tamaduni linapewa kipaumbele katika maisha yetu kwani kulipuuzia ni kujitakia matatizo yasiyo ya lazima. Hii ndio sababu iliyonifanya nianzishe kampuni ya kutoa elimu na ushauri iitwayo Africonexion: Cultural Consultants.

Thursday, December 29, 2016

Vitabu Tulivyosoma Mwaka 2016

Zikiwa zimebaki siku mbili tu kabla ya kwisha mwaka 2016, nimeona wa-Tanzania kadhaa wakijitokeza katika mtandao wa Facebook na kutaja vitabu walivyosoma mwaka huu. Jambo hili limenifurahisha, nikizingatia kuwa nimekuwa nikihamasisha usomaji wa vitabu, kwa kutumia blogu yangu hii, blogu za wengine, na pia katika kitabu changu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Ninawapongeza watu hao kwa kuonyesha mfano mzuri. Ninawapongeza pia wasomaji waliojitokeza na kuchangia suala hili kwa namna mbali mbali, kama vile kuvijadili vitabu hivyo, kuulizia upatikanaji wake, au kupendekeza vitabu vingine. Kuhusu upatikanaji wa vitabu, watu wamepeana taarifa za maduka ya vitabu, na pia upatikanaji wa vitabu pepe mtandaoni. Ni jambo la kuvutia kwamba kuna wa-Tanzania wanaotambua matumizi ya manufaa ya tekinolojia ya mtandao.

Mazungumzo haya yameonyesha mambo kadhaa. Jambo moja ni kuwa wako wa-Tanzania wanaojibidisha kusoma vitabu. Jambo jingine ni kuwa wanasoma vitabu vya aina mbali mbali, kama vile vya siasa, ujasiriamali, fasihi, na maendeleo ya jamii au ya mtu binafsi. Vile vile wanasoma vitabu vya waandishi wa mataifa mbali mbali, vya ki-Swahili na vya ki-Ingereza. Jambo jingine ni kuwa wahusika wameonyesha moyo mkubwa wa kusaidiana, kama vile kwa kufahamishana vitabu bora na hata kuazimishana vitabu.

Ninawaenzi watu hao. Huenda wakawa chachu ya kustawisha utamaduni wa kusoma vitabu nchini Tanzania. Laiti watu wengi zaidi wangejumuika katika safari hii. Laiti kama watu maarufu nchini mwetu, kama vile wanasiasa na wasanii, wangejiunga na kuwa wahamasishaji wa usomaji wa vitabu. Kutokana na mvuto wa wasanii wetu, kwa mfano, wangeweza kuwa wahamasishaji wa watoto na vijana katika kupenda kusoma vitabu.

Kwa upande wangu, naona sihitaji kuorodhesha vitabu nilivyosoma mwaka 2016. Mara kwa mara, katika blogu hii au blogu ya ki-Ingereza, ninaandika taarifa za baadhi ya vitabu ninavyosoma. Vingine ni vile ninavyofundisha chuoni St. Olaf, na vingine ni vile ninavyojisomea mwenyewe. Ninapoandika  taarifa, ninajitahidi kuelezea upekee au ubora wa vitabu hivyo.

Tuesday, March 15, 2016

Kutana na Fundi Abdallah Ramadhani

Leo ninapenda kumtambulisha Abdallah Ramadhani, ambaye nimefahamiana naye siku chache tu zilizopita katika mtandao wa Facebook. Ilikuwa bahati tu kuwa nilianzisha mawasiliano naye, na ndipo nikaweza kujua habari zake. Nilivutiwa na shughuli za ufundi anazofanya.




Nilimwambia kuwa ningeweza kuzitangaza shughuli zake katika blogu yangu. Nilitambua tangu miaka iliyopita kuwa ninaweza kuitumia blogu yangu hii kutangazia shughuli za wa-Tanzania ninaokutana nao au ninaopata habari zao na kuvutiwa na namna wanavyojishughulisha. Ninawaunga mkono. Kwa mfano, niliwahi kuandika juu ya wajasiriamali wa Duka Asili na Super Muhogo.



Abdallah Ramadhani alizaliwa Temeke, Dar es Salaam, mwaka 11 Mei,1979.  Anatengeneza viatu vizuri kama inavyoonekana pichani katika ukurasa huu. Ufundi huu alijifunza kwa baba yake, ambaye alijifunza kwa wa-Hindi.

Wa-Tanzania tujijengee utamaduni wa kuvithamini vipaji vya wa-Tanzania wenzetu, na huduma wanazotoa. Tuwe na utamaduni wa kuzithamini kazi zao. Tuzithamini bidhaa zinazozalishwa nchini mwetu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii, na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Manufaa yake ni kwa hao wahusika na kwa Taifa.

Unaweza kuwasiliana na Abdallah kwa simu, namba  255-682-588-583 au 255-719-588-583


Tuesday, July 28, 2015

Kitabu Umechapisha, Kazi ni Kukiuza

Pamoja na kuandika vitabu, ninajitahidi kujielimisha kuhusu masuala yanayohusiana na uchapishaji, utangazaji, na uuzaji wa vitabu. Kwa bahati nzuri, kuna vitabu vingi na vingine vinaendelea kuchapishwa, na pia makala nyingi kuhusu masuala hayo.

Napenda kuongelea suala la kukiuza kitabu. Niliwahi kuongelea suala hili katika blogu hii. Nimeliongelea pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni suali linalonigusa na kunifikirisha daima, nami napenda kuwashirikisha waandishi wengine katika kulitafakari.

Usemi kwamba chema chajiuza, kibaya chajitembeza unaweza kuwa na mantiki nzuri kuhusiana na vitabu. Wateja wakiridhishwa au kufurahishwa na kitabu, hawakosi kuwaambia wengine. Aina hii ya utangazaji, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "word of mouth," ni muhimu sana.

Mimi mwenyewe nimeshuhudia hivyo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tangu nilipokichapisha kitabu hiki, mwaka 2005, wasomaji wamekuwa wakiwaambia wengine. Kwa lugha ya mitaani, wanakipigia debe.

Waandishi wengi hawajui kuwa baada ya kuchapisha kitabu, wana jukumu la kukitangaza na kukiuza. Wengi wanamtegemea mchapishaji afanye kazi hiyo. Hakuna shaka kwamba mchapishaji hujitahidi kukitangaza kitabu. Anawajibika kufanya hivyo, kwani anatafuta fedha za kugharamia uchapishaji, kuwalipa wafanyakazi wake, na kujipatia faida.

Lakini, waandishi tunapaswa kuona mbali zaidi. Kwanza, tusijiziuke. Mchapishaji hawezi kufanya kila kitu, hata kama angependa. Gharama za kukitangaza kitabu ni kipingamizi kwa mchapishaji, hasa yule ambaye si tajiri.

Pili, dunia inabadilika muda wote, nasi tunawajibika kujifunza mambo mapya muda wote. Leo hii kuna tekinolojia zinazomwezesha mwandishi kujichapishia kitabu chake. Katika mazingira haya, mwandishi anawajibika kubeba jukumu la kutangaza na kuuza kitabu. Si busara kutegemea "word of mouth" pekee.

Haikuwa rahisi kwangu kuanza kuvitangaza vitabu vyangu. Kutokana na malezi, mila na desturi, nilijiuliza italeta picha gani katika jamii iwapo ningekuwa natangaza na kuuza vitabu vyangu. Nilielezea wasi wasi huo katika blogu hii, na jinsi nilivyojikomboa.

Leo sioni tatizo kutangaza vitabu vyangu. Nimejifunza na ninaendelea kujifunza umuhimu na mbinu za kufanya hivyo, kwa kusoma vitabu na makala mbali mbali. Ndio maana mara kwa mara naandika katika blogu hii kuhusu matamasha ya vitabu ninayoshiriki. Kusoma kumenileta katika upeo huu mpya. Elimu ni mkombozi.

Tuesday, May 12, 2015

Vitabu vya Shaaban Robert

Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanzania wepi ambao wamesoma angalau vitabu vichache vya Shaaban Robert. Ni wangapi wamesoma au wanasoma mashairi yake, tenzi zake, insha zake, barua zake, na riwaya zake?

Ni wangapi wamesoma vitabu vyake vingine, kama vile Wasifu wa Siti Binti Saad, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, na tafsiri yake ya mashairi ya Omar Khayyam? Kama hatuna majibu ya kuridhisha, tuache kujigamba, kujidanganya na kudanganyana kuwa tunamwenzi mwandishi wetu huyu maarufu.

Ingawa kulikuwa na kipindi cha uhaba, leo vitabu vya Shaaban Robert vinapatikana kirahisi Tanzania, baada ya kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota kuanza kuvichapisha upya. Mwaka hadi mwaka, ninapokwenda Tanzania, nimekuwa nikijinunulia vitabu hivyo, kama hivi vinavyoonekana pichani, sambamba na vitabu vya waandishi wengine maarufu katika lugha ya ki-Swahili.

Imekuwa ni faraja kwangu kuvisoma, baada ya kuzinduka kutoka katika mazoea ya kusoma zaidi maandishi ya ki-Ingereza. Ninajiona kama vile nimeanza kujikomboa kimawazo. Lugha yako ni utambulisho wako, na kuifahamu na kuitumia vizuri ni ishara ya kuiheshimu lugha hiyo. Ni ishara ya kujiheshimu.

Pamoja na kununua na kusoma vitabu alivyoandika Shaaban Robert, ninajitahidi kupanua akili yangu kwa namna nyngine pia. Ninayo maandishi yanayochambua maandishi ya Shaaban Robert. Mfano ni vitabu vinavyoonekana hapa pichani, kimoja cha A.G. Gibbe, na kingine cha Clement Ndulute. Maandishi mengine yamo katika majarida na vitabu vingine ambavyo baadhi ninavyo pia.

Ninajitahidi, kwa uwezo wangu, kushiriki katika kuandika kuhusu kazi za Shaaban Robert. Nimechapisha insha juu ya Shaaban Robert katika Encyclopaedia of African Literature iliyohaririwa na Simon Gikandi. Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kuna pia insha yangu iitwayo "Shaaban Robert: Mwalimu wa Jamii." Kadiri nitakavyokuwa naendelea kusoma maandishi yake, nategemea kuandika zaidi. Nina nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwa kuwa ni mwalimu wa fasihi za kimataifa na nadharia ya fasihi.

Monday, April 6, 2015

Bemidji Yamwenzi Mary, Mke wa Hemingway

Jioni ya tarehe 4 Aprili, baada ya kurejea kutoka Leech Lake Tribal College karibu na mji wa Bemidji, niliingia mtandaoni nikiwa na lengo la kuona kama kuna taarifa zozote kuhusu mkutano wetu. Katika ukurasa wa Facebook wa Chuo, niliona taarifa na picha za mkutano ule:

Hilo lilinivutia. Lakini niliona pia taarifa nyingine, kuhusu namna mji wa Bemidji unavyomwenzi Mary Welsh, aliyekuwa mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mary Welsh alizaliwa karibu na Bemidji akakulia na kusoma mjini hapo.

Kisha alienda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern karibu na Chicago. Alikuja kuwa mwandishi katika magazeti hapo Chicago na hatimaye London, akajipambanua kama mwandishi wa habari za vita. Huko ndiko alikokutana na Ernest Hemingway na baadaye wakafunga ndoa.

Nilifahamu hayo yote na mengine mengi, kutokana na utafiti wangu wa miaka kadhaa. Nilifahamu tangu zamani kuwa Mary Welsh alizaliwa eneo la Bemidji, na nilikuwa nawazia kwenda kule kufanya utafiti juu yake. Mary Welsh Hemingway alitanguzana na Ernest Hemingway katika safari ya Afrika Mashariki mwaka 1953-54. Walizunguka Kenya, Tanganyika, hadi Uganda, ambako walipata ajali mbili za ndege, mfululizo.

Mary Hemingway alisafiri hadi Mbeya, na ameelezea hayo na mengi mengine katika kitabu chake kiitwacho How it Was. Nasikitika kuwa wa-Tanzania, kwa kukosa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, hawafahamu hayo. Wangekuwa wana utamaduni huo, wangeweza kutumia habari na maandishi kama haya ya Mary Welsh Hemingway na Hemingway mwenyewe kwa manufaa makubwa, hasa katika utalii. Hali ni mbaya kwamba wa-Tanzania hawashtuki wakielezwa habari za vitabu namna hii. Nimethibitisha hayo, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Wenzetu katika nchi kama Cuba, Hispania na Marekani wanafaidika sana na maandishi ya Hemingway. Cuba wanaitunza sana nyumba ya Hemingway, Finca Vigia, na hata baa alimokuwa anakunywa, mjini Havana, ni kivutio kikubwa cha watalii. Kule Hispania kuna mji wa Pamplona ambao ulipata umaarufu duniani na umaarufu huu unaendelea, baada ya Hemingway kuutembelea na kuangalia mchezo wa "bull fighting," akaandika juu yake katika riwaya iitwayo The Sun Also Rises. Maelfu ya watalii wanafurika Pamplona. Hapa Marekani, nyumba alimoishi Hemingway, kama vile kule Oak Park (Illinois)na Key West (Florida), ni vivutio vikubwa kwa watalii.

Hayo ndio yaliyonijia akilini wakati nasoma taarifa ya mji wa Bemidji kumwenzi Mary Welsh Hemingway. Jambo moja kubwa lililoelezwa katika taarifa ile ni utunzi wa tamthilia juu ya Mary Welsh Hemingway, unaofanywa na Catie Belleveau baada ya utafiti wa muda mrefu.

Hoja sio kwamba ni lazima nasi tujitose na kujishughulisha na Hemingway na mke wake, ingawa kufanya hivyo kungetuletea manufaa kama wanayopata wenzetu wa Cuba, Pamplona, Oak Park na Key West. Ninachotaka kusisitiza ni umuhimu wa kujifunza kutoka kwa hao wenzetu.

Sisi tunao waandishi maarufu kama Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utenzi wa Ras il Ghuli. Je, tunajua habari zake? Tunaye Shaaban Robert. Je, ni wa-Tanzania wangapi wanajua angalau mahali alipozaliwa, sehemu alimoishi, na mahali alipozikwa? Je? wahusika katika wizara za utalii na utamaduni wanafahamu habari hizo? Na je, wanafahamu kuwa taarifa hizo ni hazina ambayo tungeweza kuitumi? Binafsi ninatekeleza wajibu wangu kwa kuandika kuhusu mambo haya, kama nilivyofanya katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho nitashangaa kikipata wasomaji Tanzania.

Wednesday, April 1, 2015

Tunahitaji Demokrasia, Lakini Tunahitaji Vyama vya Siasa?

Bila shaka tutakubaliana kuwa tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao ni wa umma, unaendeshwa na umma, kwa maslahi ya umma. Kwa ki-Ingereza wanasema "rule of the people, by the people and for the people."

Hii ndio maana na tafsiri ya demokrasia. Lakini je, tunahitaji chama cha siasa? Tunahitaji vyama vya siasa? Ni lini wa-Tanzania walikaa na kulitafakari suali hili? Kwa kweli hawajawahi kufanya tafakari hii. Badala yake wamekurupuka na wazo la chama au vyama, kikasuku tu.

Hata wale tunaowaita wasomi wetu nao wameshindwa kuhoji hali hii. Wameshindwa kujinasua kutokana na mtazamo huu, badala ya kufanya kile kinachoitwa kwa ki-Ingereza "thinking outside the box."

Nimeelezea zaidi huu ukurupukaji, mkanganyiko, na ukasuku wa wa-Tanzania katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Tuesday, March 3, 2015

Utamaduni wa Kuwasomea Watoto Vitabu

Nimeandika mara kwa mara kuhusu suala la elimu, sio tu katika blogu hii, bali pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kitabu ambacho nilitegemea kitasomwa na wa-Tanzania wenzangu, lakini mambo yamekuwa kinyume.

Kati ya mambo ambayo nimekuwa nikiyaongelea ni umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu, jambo ambalo limejengeka katika utamaduni wa wa-Marekani. Nimekumbuka yote hayo leo baada ya kusoma makala hii hapa
kama uthibitisho na changamoto.

Hili ni kati ya mambo ambayo wa-Tanzania tunapaswa kujifunza. Nimethibitisha mwenyewe kuwa watoto wa Tanzania wanapenda vitabu, bali, kadiri wanavyokua, mapenzi hayo huzimishwa na watu wazima na jamii kwa ujumla.

Kama wahenga walivyosema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Baada ya muda, watoto wa ki-Tanzania hufuata utamaduni wa jamii wa kutothamini vitabu, na Taifa linaendelea kuzorota kielimu., wakati wenzetu wa-Marekani wanawalea watoto wao katika kupenda vitabu.

Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watu wawe na tabia ya kutafuta elimu. Alikuwa mwandishi na msomaji makini. Alionyesha mfano kwa vitendo. Aliongoza njia.

Leo tuna watu ambao tunawaita viongozi ambao sielewi kwa nini wanaitwa viongozi. Wangekuwa ni viongozi, wangetambua kuwa elimu ni msingi wa maisha na maendeleo. Wangekuwa wanaihamasisha jamii kwa kauli na vitendo katika kutafuta elimu. Lakini, badala yake, hawaonekani kujali kabisa kwamba wanachangia katika kuliangamiza Taifa badala ya kuliongoza, yaani kulipeleka mbele.

Friday, January 23, 2015

Kwa Anayewazia Kuchapisha Kitabu

Wazo la kuchapisha kitabu linawavutia watu wengi. Ni wazo lenye ndoto za mafanikio.Wako wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawapa umaarufu. Kuna wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea fedha nyingi. Wengi, labda wote, wanaamini kuwa wakisha chapisha kitabu, kazi yao inakuwa imemalizika; kinachobaki ni kungojea matokeo, kama vile umaarufu na fedha.

Ni bora mtu anayewazia kuchapisha kitabu ajielimishe zaidi kuhusu jambo hili, nami hupenda kuchangia yale ninayoyafahamu, kwa kadiri ya uwezo wangu. Vipengele ni vingi, lakini hapa nitaongelea vichache tu.

Mtu uandike kitabu kutokana na kujua kuwa una jambo la kusema kimaandishi. Uwe una jambo ambalo linakuelemea akilini mwako na kukusukuma uandike. Msukumo utoke ndani ya nafsi yako. Ukishaandika kitabu kwa msingi huo, utajisikia una raha sawa na mtu aliyetua mzigo. Kuridhika kwako ndilo jambo mihimu. Mengine yanafuata baadaye.

Huenda kitabu chako kitawavutia watu wakakinunua na kukisoma, au huenda kisiwavutie. Lakini sidhani kama hili ni tatizo lako, maadam umeshakidhi haja ya kutua mzigo uliokuwemo akilini mwako, na sasa uko huru kuwazia mambo mengine. Uhuru huu ni jambo muhimu.

Katika miaka yangu ya kuandika, na hata kuchapisha vitabu, nimekuwa nikisoma kuhusu uandishi, uchapishaji na uuzaji wa vitabu. Kitu kimoja mihimu nilichojifunza ni kuwa kuandika na kuchapisha kitabu sio mwisho wa kazi yako kama mwandishi. Kuna kazi kubwa mbele yako, kazi ya kuutangazia ulimwengu kuhusu kuwepo kwa kitabu chako, na kazi ya kukiuza kitabu chako.

Watafiti na waandishi wa masuala hayo wanasisitiza kuwa wajibu wa kuuza kitabu ni yako wewe mwandishi. Kabla ya kuanza kusoma mawazo haya, niliamini, kama wengi wanavyoamini, kwamba kazi ya kutangaza na kuuza kitabu ni ya mchapishaji. Kumbe, hata kama mchapishaji anaweza kuchangia katika jukumu hilo, mwandishi unawajibika sana, na pengine zaidi kuliko mchapishaji.

Kwa upande wa Tanzania, kwa hali ilivyo, tatizo kubwa ni kwamba utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ni hafifu sana. Watu wengi wanadhani kusoma vitabu ni shughuli ya wanafunzi, na hivi vitabu viwe vimo katika mitaala ya shule.

Kujisomea vitabu bila shinikizo la shule au mitihani ni utamaduni ambao unakosekana. Hii ni sababu moja inayonifanya nitoe angalizo kuwa mtu unaweza kuchapisha kitabu na kisiwe na wasomaji.

Masuala haya ya uandishi na uuzaji wa vitabu nimeyaelezea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika makala mbali mbali katika blogu hii. Ninaendelea kujielimisha kuhusu masuala hayo, na nitaendelea kuandika.

Wednesday, December 3, 2014

Wazo la Kutafsiri Kitabu

Kwa wiki kadhaa, nimekuwa nikiwazia kutafsiri kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu kitabu hiki katika blogu hii.

Nawazia kuzirekebisha insha zilizomo, na kuchapisha kitabu cha ki-Ingereza. Kufanya hivyo kutakipa kitabu hadhira kubwa zaidi kuliko ile ya wajuao ki-Swahili. Nina hakika, kwa mfano, kuwa wa-Marekani watakitafuta na kukisoma. Kwa ujumla wasomaji wa vitabu vyangu ni wa-Marekani.

Ninaposhiriki matamasha hapa Marekani, watu kadha wa kadha huja kwenye meza yangu na kuangalia vitabu, kuvinunua, au tu kuongea nami. Wako wanaoniuliza kama nimechapisha kitabu kingine, kwani vile vilivyopo mezani, vya ki-Ingereza, wanavyo au wamevisoma. Kauli hizi hata binti zangu, ambao hushirikiana nami, wamezisikia tena na tena.

Kwa miaka kadhaa, sijachapisha kitabu kipya. Sababu kubwa ni kuwa kuandika kitabu huchukua muda. Yaweza kuwa miezi au miaka. Kwa mfano, ilichukua miaka 23 hivi kuandaa kitabu cha Matengo Folktales. Vile vile, muda mwingi natumia katika kufanya utafiti na kuandika makala. Kutafsiri kitabu cha CHANGAMOTO, ni njia moja ya wazi ya kupatikana hicho kitabu kingine.

Kutafsiri CHANGAMOTO sio jambo la haraka. Kuna kitabu kingine katika lugha ya ki-Ingereza ambacho nataka kumaliza kukiandika kabla ya kuanza kutafsiri CHANGAMOTO. Hata hivi, siwezi kusema kuwa ni lazima ningoje. Muda wote ninakuwa na kazi kadhaa ninazoandika, na huwa sio rahisi kujua ni ipi itamalizika kabla ya ipi. Wanadamu tumejaliwa uwezo wa kufanya shughuli nyingi kwa pamoja, "multitasking" kwa ki-Ingereza. Ninachoombea ni uzima na akili timamu.

Thursday, November 27, 2014

Kitabu Changu cha Ki-Swahili

Kitu kimoja ninachojivunia kama mwandishi ni juhudi niliyofanya kwa miaka mingi katika kuandika kwa ki-Swahili. Aliyenihamasisha na kunisukumia katika uandishi wa ki-Swahili ni rafiki yangu Mugyabuso Mulokozi, ambaye sasa ni profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu tulipokuwa tunasoma wote "Mkwawa High School," aliona jinsi nilivyokuwa nimezama katika ki-Ingereza bila kujibidisha upande wa ki-Swahili.

Hatimaye, hasa tulipokuwa chuo kikuu, ambapo yeye nami tulikuwa tunafundisha, nilijitosa katika ulimwengu wa ki-Swahili. Kwanza nilisoma maandishi ya ki-Swahili, kisha nikaanza kufanya utafiti na kuandika makala magazetini. Kati ya maandishi niliyochapisha ni mapitio ya tamthilia ya Kijiji Chetu, iliyotungwa na Ngalimecha Ngahyoma.

Baadaye, nilianza utafiti kuhusu tungo za zamani za ki-Swahili, kama vile Utenzi wa Fumo Liongo, Al-Inkishafi na Utenzi wa Ras il Ghuli. Utafiti huu niliuendeleza nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, huku Marekani, miaka ya 1980-86.

Hatimaye, kwa kuombwa na Ndugu Maggid Mjengwa, mmiliki na mwendeshaji wa Mjengwablog, niliandika makala katika gazeti aliloanzisha, Kwanza Jamii. Baadaye, makala hizi nilizikusanya na kuzichapisha kama kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Nilipochapisha kitabu hiki, niliandika taarifa katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Kuandika kwa ki-Swahili ni namna ya kuienzi lugha hii. Lugha ni utambulisho wa utaifa na ni kielelezo cha jinsi mtu unavyoheshimu utaifa wako na unavyojitambua na kujiheshimu wewe mwenyewe, kama alivyobainisha Frantz Fanon hasa katika vitabu vyake viwili: The Wretched of the Earth na Black Skin, White Masks.

Ninajivunia kitabu hiki kwa vile kimenipa fursa ya kupima uwezo wangu wa kuandika ki-Swahili sanifu. Ingawa bado naandika zaidi kwa ki-Ingereza, sijarudi nyuma katika uandishi wa ki-Swahili. Mbali na hili suala la kujitambua na kujitambulisha kwa kuienzi lugha yetu kwa vitendo, kitabu hiki kilitokana pia na msukumo wa watu waliokuwa wananiuliza kwa nini naandika kwa ki-Ingereza tu. Watu hao waliniambia kuwa ingekuwa bora niandike pia kwa ki-Swahili, ili wa-Tanzania walio wengi waweze kuyaelewa mawazo yangu. Nami niliona hii ni hoja nzuri.

Hata hivi, kitabu hiki hakijapata wasomaji wengi. Labda hii ni kwa sababu nilikichapisha huku Marekani, mtandaoni. Kama hili ndilo tatizo, napenda kusema kuwa kitabu hiki, sawa na vitabu vyangu vingine, kinapatikana kutoka kwangu, kwa anwani hii: africonexion@gmail.com au simu namba (507) 403 9756.

Lakini pia kuna suala la kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu miongoni mwa wa-Tanzania, jambo ambalo limekuwa likisemwa na wahusika mbali mbali katika sekta ya vitabu. Tungekuwa na utamaduni huu, tungeona tahakiki na mijadala kuhusu vitabu, sio tu miongoni mwa wanafunzi na wasomi, bali katika jamii, kupitia vyombo vya habari, magazeti, na mitandao ya mawasiliano.

Thursday, July 3, 2014

Naulizwa Kama Nafundisha ki-Swahili Hapa Marekani

Mara kwa mara, ninapokutana na wa-Tanzania wasionifahamu vizuri, au wasionifahamu kabisa, wasikiapo kuwa nafundisha kwenye chuo fulani Marekani, wanauliza iwapo nafundisha ki-Swahili.

Suali hili linaweza kuonekana kuwa rahisi, lakini kwangu ni suali tata. Kifupi ni kuwa mimi nafundisha katika idara ya ki-Ingereza ya Chuo cha St. Olaf, hapa Minnesota. Idara hii ilinialika kuja hapa kuanzisha kozi katika somo la "Post-Colonial Literature," na pia kufundisha uandishi wa ki-Ingereza. Nilichukuliwa, mwaka 1991, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha katika idara ya "Literature."

Hakuna kozi ya ki-Swahili katika chuo hiki cha St. Olaf. Mbali ya ki-Ingereza, lugha zinazofundishwa hapa ni ki-Jerumani, ki-Japani, ki-China, ki-Spaniola, ki-Norway, ki-Latini, na ki-Griki cha kale.

Ninapotafakari suala la kufundisha ki-Swahili, najutia kwa nini sina ujuzi utakiwao, nikizingatia kuwa hii kwangu ni lugha karibu sawa na lugha mama. Nimeifahamu na kuitumia tangu utotoni. Lakini, lazima nikiri kuwa sina utaalam wa kuifundisha. Ningejivunia kuweza kufundisha ki-Swahili. Wazo hilo nimelielezea pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Mtu huwezi kukurupuka tu, ukafundisha ki-Swahili chuoni, au hata katika shule ya msingi. Lazima ujue mambo mengi yanayohusu lugha hiyo na uwe na utaalamu wa kuifundisha, ambao una vipengele vingi kufuatana na kiwango cha wanafunzi. Sikusomea taaluma hiyo, kwa hivyo siwezi kujitupa katika uwanja ambao siufahamu itakiwavyo.

Kwa kawaida, hao watu wanaoniuliza kama nafundisha ki-Swahili hapa Marekani nadhani wanaamini kuwa kwa mtu kama mimi kufundisha ki-Swahili Marekani ni jambo rahisi tu. Hawaonekani kufahamu hayo niliyosema hapa juu, kwamba inahitaji elimu ya pekee ya lugha husika na ufundishaji wake.

Wanashtuka ninapowaeleza kuwa nafundisha ki-Ingereza. Hawategemei kusikia m-Swahili anawafundisha wa-Marekani ki-Ingereza, ambayo ni lugha yao. Kwa upande wangu, kila ninapoulizwa kama nafundisha ki-Swahili hapa Marekani, huwa najichekea moyoni, ingawa sionyeshi kwao kwamba suali lao linanichekesha. Sio vizuri, wala uungwana kumcheka mtu, na kumfanya ajisikie vibaya, kwa suali kama hilo.

Tuesday, October 8, 2013

Tamasha Kubwa la Vitabu, Twin Cities, Oktoba 12

Lile tamasha maarufu kabisa la vitabu ambalo limefanyika mjini Minneapolis kwa miaka mingi, mara moja kwa mwaka, limekaribia kabisa. Kuanzia mwaka jana, tamasha limehamia mjii St. Paul, kwenye viwanja vya State Fairgrounds.

Hakuna tamasha kubwa zaidi ya hili katika eneo hili la Minnesota na majimbo ya jirani. Wanahudhuria watu yapata 7,000, wapenzi wa vitabu. Wanakuwepo waandishi, wachapishaji, wahariri, wachora picha za vitabuni, wahakiki, wauzaji wa vitabu na majarida. Wanahudhuria wazee, watu wazima, vijana, na watoto.

Nimeshiriki tamasha hili kwa miaka mingi, kama mwandishi wa vitabu na mwelimishaji katika chuo kikuu na jamii. Kila mara nimepata fursa ya kuongea na wasomaji wa maandishi yangu na watu ambao sijawahi kuwafahamu kabla. Wanakuja na maoni, taarifa, na uzoefu mbali mbali. Tunabadilishana mawazo. Inakuwa ni kama shule muhimu sana. Tamasha linapoisha, jioni, najiona nimeelimika sana.

Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuandika vitabu na maandishi mengine. Namshukuru kwa namna ya pekee kwa kuniwezesha kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho najua kimesomwa na bado kinasomwa na maelfu ya watu hapa Marekani, ambao huguswa na mawazo na ushauri niliotoa katika kitabu hiki.

Kwenye kila tamasha, ambamo kunakuweko vitabu maelfu kwa maelfu, unawajibika kushangaa wadau wanafikiaje uamuzi wa kununua kitabu fulani au vitabu fulani. Nina bahati kuwa kitabu changu, ingawa kimekuwepo sokoni kwa miaka mingi kiasi, hakijachujuka bali kinawavutia wateja. Ninachoweza kusema ni kimoja, kwamba yote ni mipango ya Mungu.

Baadhi ya watu ninaokutana nao ni waandishi chipukizi. Huniulizia namna ya kuchapisha kitabu. Nami huwahamasisha kufuatilia hali ya uchapishaji wa leo, unaotumia tekinolojia tofauti na zile tulizozizoea. Kwa taarifa, na kwa manufaa ya watu wanaoongea ki-Swahili, nimetoa maelezo na uzoefu wangu kuhusu uchapishaji huo na mikakati mingine inayohusika, katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Nimeshajiandaa vizuri kwa tamasha la tarehe 12. Nakala za vitabu vyangu ninazo, pamoja na matangazo na machapisho mengine. Nangojea kwa hamu kukutana na kuongea na watu wengi. Kwa namna ya pekee, nangojea kuongea na watoto. Insh'Allah, nitaandika ripoti ya tamasha, kama ilivyo jadi yangu. Kwenye tamasha hili, nimejisajili kwa jina la kampuni yangu ndogo iitwayo Africonexion: Cultural Consultants, ambayo nimekuwa nikijitahidi kuitambulisha Tanzania. Unaweza kuona jina hilo katika orodha ya wauza vitabu, ambayo hi hii hapa.

Monday, December 24, 2012

Shaaban Robert na Nyerere: Waandishi Muhimu kwa Kila m-Tanzania

Kwa miaka michache iliyopita, wakati nimejitosa katika kusoma maandishi ya Shaaban Robert, nimejiwa na mawazo mbali mbali ambayo naona ni muhimu. Kwa bahati nzuri, nimechapisha makala mbili juu ya Shaaban Robert, moja katika Encyclopedia of African Literature, na nyingine katika CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Napenda kunukuu machache niliyoandika katika Encyclopedia of African Literature:

Shaaban Robert displayed profound awareness of the human condition; he opposed injustice, championed freedom, and extolled the dignity of labour. He was sensitive to the condition of women. He wrote poems celebrating women, and a biography of Siti Binti Saad, the famous female taarab singer, recounting the meteoric rise to fame of this woman from a humble rural background in a male-dominated world which put incredible obstacles in her path. He was proud of his Swahili language and culture, which he understood very well, appropriated, and celebrated in and through his writings. However, he deeply respected other languages and cultures and appropriated whatever he could from them. If colonialism had not limited his educational opportunities, he would have explored this dimension to the fullest. He greatly admired world writers like Shakespeare, whose artistic mind he described as a great ocean whose waves touched the shores of the whole world....[Shaaban] Robert's poetic sensibility was deep and intertwined with his moral and ethical principles. Sensitive to the condition and plight of all creatures, he held that all things moved with the rhythm of poetry: the birds, streams, the sea, the wind and the thunderstorms, the seasons....His vision of a just society was part of the shaping of the dream for an egalitarian society, which became his country's policy. (p. 463)

Katika kusoma na kutafakari maandishi ya Shaaban Robert, ilifikia wakati nikajenga wazo kuwa kuna uwiano mzito baina ya mafundisho ya Shaaban Robert na yale ya Mwalimu Nyerere. Wakati Nyerere anaongelea sana masuala ya siasa, uchumi, nadharia mbali mbali kuhusu jamii na maendeleo yake, Shaaban Robert aliongelea masuala ya aina hiyo hiyo kwa kutuingiza katika hisia na mahusiano baina ya binadamu na binadamu mwenzake.

Kama Nyerere, Shaaban Robert alikuwa mchambuzi wa jamii na mwanafalsafa, lakini aliongelea masuala kwa kutumia wahusika maalum na matendo na masahibu yao, na hivi kutugusa moja kwa moja. Ningekuwa na madaraka ya kuamua masuala ya mfumo wa elimu Tanzania, ningehakikisha kuwa Shaaban Robert na Nyerere wamekuwa nguzo ya elimu ya kila m-Tanzania.

Sunday, May 8, 2011

Kikombe cha Mwenyekiti Maggid

Kama sote tunavyojua, wa-Tanzania tuko kwenye awamu ya vikombe. Waganga wamejitokeza nchini mwetu, wakiwa na vikombe vya kuponyesha magonjwa mbali mbali. Wateja wengi wanatoa ushuhuda kuhusu uponyaji wao.

Nami napenda kutoa ushuhuda kuhusu kikombe cha Mwenyekiti Maggid Mjengwa.

Nianze kwa kusema kuwa Mwenyekiti Maggid ni mwalimu, mwandishi na mwanablogu. Hajawa mganga wa kienyeji. Isipokuwa, kikombe ameninywesha. Tega sikio nikuhadithie.

Mwaka 2009 mwanzoni, Mwenyekiti Maggid alianzisha gazeti la Kwanza Jamii, akaniomba niwe mchangiaji. Nilikubali. Sikutambua kuwa nilijipalia mkaa, maana nilijikuta nahangaika kuandika hizo makala na kuzituma kwa muda uliotakiwa.

Ilikuwa ni kazi ya kuumiza kichwa. Kwanza kabisa, wakati mwingine nilikuwa sijui niandike kuhusu nini. Huku siku na saa za kuwasilisha makala zinaendelea kusogea, nami bila kujua mada ya kuandikia, nilibaki nimekodoa macho na jasho linanitoka. Mara kwa mara Mwenyekiti Maggid alikuwa ananiletea ujumbe usiku kwenye saa sita za hapa Marekani ya kati, iwapo nilichelewa.

Tatizo jingine nililopambana nalo ni kuandika kwa ki-Swahili. Nilizoea kuandika kwa ki-Ingereza, lakini kuandika ki-Swahili sanifu ulikuwa ni mtihani wa kuumiza kichwa.

Sisi wa-Katoliki, katika falsafa ya dini yetu, tunatumia dhana ya kikombe kuelezea magumu ya maisha au mateso ambayo Mungu anatuletea tuyakabili. Ni kama tunavyotumia dhana ya msalaba. Mungu ana malengo yake anapotutwisha msalaba maishani.

Napenda niendelee kufafanua falsafa za kidini zinazohusiana na mada yangu. Babu wa Loliondo ametueleza tena na tena kuwa kikombe si kikombe tu bali ni suala la imani, na uwezo wa kutibu ni wa Mungu, si binadamu.

Mungu anaweza kumtumia binadamu yoyote kuleta ujumbe au uponyaji duniani. Kwa imani yangu, ndivyo ilivyokuwa kuhusiana na hiki kikombe cha Mwenyekiti Maggid. Naamini kilipangwa na Mungu. Matokeo ya magumu niliyopitia, ambayo nayaita kikombe cha Mwenyekiti Maggid, yamekuwa mazuri. Makala nilizoandika zilisomwa na bado zinasomwa na watu wengi.

Makala mojawapo, baada ya mimi kuitafsiri kwa ki-Ingereza, ikachapishwa huku Marekani, ilimvutia Chad Brobst, mhariri wa jarida la Monday Developments. Aliiomba, nami nikairekebisha kidogo, akaichapisha. Kila toleo la Monday Developments huteua makala moja kama makala ya mfano. Kwa mwezi Aprili, iliteuliwa makala yangu. Watu wengi sana duniani wataiona.

Vile vile, makala nilizoandika katika Kwanza Jamii nilizikusanya nikazichapisha kama kitabu, CHANGAMOTO, ambacho watu waliokisoma wamekipenda. Ninajivunia kitabu hiki kwa vile ni kitabu changu cha kwanza kwa ki-Swahili.

Nimeshawahi kuandika kuwa wito wa Mwenyekiti Maggid kunitaka niandike makala za ki-Swahili ulisaidia kuniondolea kasumba tuliyo nayo wasomi wengi, ya kutoweza au kutotaka kutumia ki-Swahli ipasavyo. Nilifanya bidii kujiongezea ufahamu wa ki-Swahili. Nilisoma vitabu vya mabingwa kama Shaaban Robert na kujijengea nidhamu ya matumizi ya lugha.

Sisiti kukiri kuwa kikombe alichoninywesha Mwenyekiti Maggid kimechangia kunitibu ugonjwa sugu unaowaathiri wasomi wengi, mbali ya kuwaneemesha walimwengu kama nilivyoelezea.

Wednesday, February 23, 2011

Makala ya "Kwanza Jamii" Yaendelea Kupeta

Niliwahi kuandika kuhusu makala yangu ya kwanza kuchapishwa katika gazeti la Kwanza Jamii, "Maendeleo ni Nini," ambayo hatimaye ilichapishwa huku Marekani, baada ya mimi kuombwa niitafsiri kwa ki-Ingereza. Soma hapa.

Wahenga walisema: dunia ni mduara, huzunguka kama pia. Bila kutegemea, tarehe 20 Oktoba nilipata barua pepe kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mhariri mkuu wa jarida la Monday Developments. Ujumbe wa msingi wa barua yake ni huu:

We cover issues and trends in international development and humanitarian assistance, and are a publication of InterAction—an alliance of 200 U.S.-based international development organizations focused on the world’s poor and most vulnerable people.

One of our upcoming issues will be discussing the topic: Is development the new colonialism? While researching the subject, I came across your article “What is Development? Colonialism Deconstructed” and found it very refreshing. As a journal geared primarily toward global NGO staff, I thought your critique of the term and notion of development would be an interesting point of view to our readers—who often only see their side of the issue.

I wonder if you might consider adapting your article to run in our publication? Our readership includes NGOs, universities, the UN, World Bank, and offices of the U.S. government –exactly the audience who should be exposed to the points you raise.

Sikusita; nilikubali ombi la kuikarabati makala yangu na juzi nimeipeleka. Mhariri amejibu na kushukuru akisema, "You raise interesting points that our NGO readership should consider as they perform their work."

Makala hii, pamoja na zingine nilizochapisha katika Kwanza Jamii imo katika kitabu cha CHANGAMOTO, ambacho kinapatikana mtandaoni, kama inavyoonekana upande wa kulia wa ukurasa huu, na pia Dar es Salaam, simu namba 0754888647 au 0717413073. Nilikichapisha kitabu hiki ili kuwapa wa-Tanzania wengi iwezekanavyo fursa ya kuyafahamu mawazo yangu, kwa lugha ya ki-Swahili.

Nilifanya hivi ingawa najua kuwa vitabu havithaminiwi miongoni mwa wa-Tanzania. Nimejiepusha na lawama. Hatimaye nitapenda kukitafsiri kitabu hiki kwa ki-Ingereza, hasa baada ya kuona jinsi makala hii moja niliyoitafsiri inavyopokelewa na wale wasiojua ki-Swahili.

Naweka taarifa hii hapa iwe changamoto kwa watoto na vijana wetu. Wajizatiti na shule na elimu, kama nilivyofanya na ninavyoendelea kufanya maishani mwangu, bila kuyumbishwa na chochote. Manufaa yake huonekana baadaye.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...