Wa-Tanzania wenye vyama wakumbuke kuwa wao ni wachache kwa kufananisha na idadi ya wa-Tanzania kwa ujumla. Wafanye siasa zao, ila wasisahau jambo hilo. Nasema hivyo kwa sababu wana tabia ya kujiona kuwa wao ndio Tanzania, na Tanzania ni wao.
Kinachonikera zaidi ni fujo. Wa-Tanzania wenye vyama wana tabia ya kuleta fujo na kuhujumu amani, hasa kinapokaribia kipindi cha uchaguzi. Ni aibu sana kwamba, kutokana na fujo za wa-Tanzania wenye vyama, tumefikia mahali sasa ambapo watu wanasali na kufanya ibada kuombea amani. Hii ni fedheha ambayo tumeletewa na wa-Tanzania wenye vyama.
Ni sahihi kumwomba Mungu atupate mvua ya kutosha kwa mazao yetu. Ni sahihi kumwomba atuepushe na majanga kama vile matetemeko ya ardhi. Ni sahihi kumwomba atupe uzima siku hadi siku tuweze kujenga nchi yetu na kutimiza majukumu yetu mengine.
Lakini kuombea amani kwa kuwa inatishiwa na utovu wa nidhamu unaofanywa na wa-Tanzania wenye vyama ni jambo lisilokubalika. Kuombea amani kwa sababu ya utovu wa busara wa watu hao ambao wanadhani nchi hii ni yao peke yao, wanaodhani wana haki ya kujifanyia watakalo katika nchi hii, ni jambo lisilokubalika. Hili si suala la kuombea amani. Ni suala la kupambana na hao wahujumu wa amani.
Inashangaza kwamba hata Ikulu imeshindwa kutambua hilo. Haijawahi kutokea Ikulu ikawaita wa-Tanzania wasio na vyama kwa mazungumzo na mashauriano. Ikulu imekuwa tayari kuwaita wenye vyama na kuongea nao, lakini sio sisi tusio na vyama, ambao ndio wengi zaidi na ni mfano wa kuigwa.
Wa-Tanzania wenye vyama wazingatie kuwa sisi tusio na vyama hatujawahi na hatuna mpango wa kuhujumu amani ya Tanzania kama wanavyofanya wao. Tumetunza heshima ya Tanzania wakati wao wanaihujumu. Wajifunze kutoka kwetu ili wote tudumishe amani na tuipe nchi yetu heshima inayostahili.