Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena.
Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani.
Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu.
Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minnesota, katika tamasha la Afrifest. Huyu bwana, m-Marekani Mweusi, alikuja na watoto wake kwenye meza yangu, kuangalia vitabu. Watoto hao ni wadogo sana, na sijui kama walikuwa wanajua kusoma, lakini, nilivutiwa na kitendo cha baba yao kuwaleta kuangalia vitabu.
Kwa wa-Marekani, umri wa mtoto si tatizo. Wanawasomea vitabu hata watoto wadogo sana, hasa kabla ya kulala. Watoto wanapenda kusomewa vitabu. Hapa naikumbuka video ya kusisimua inayomwonyesha mtoto mdogo akisomewa vitabu, halafu anavyoangua kilio kila anapoambiwa kuwa hadithi imeisha. Hebu iangalie.
Nimeandika mara kwa mara kuhusu suala la elimu, sio tu katika blogu hii, bali pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kitabu ambacho nilitegemea kitasomwa na wa-Tanzania wenzangu, lakini mambo yamekuwa kinyume.
Kati ya mambo ambayo nimekuwa nikiyaongelea ni umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu, jambo ambalo limejengeka katika utamaduni wa wa-Marekani. Nimekumbuka yote hayo leo baada ya kusoma makala hii hapa
kama uthibitisho na changamoto.
Hili ni kati ya mambo ambayo wa-Tanzania tunapaswa kujifunza. Nimethibitisha mwenyewe kuwa watoto wa Tanzania wanapenda vitabu, bali, kadiri wanavyokua, mapenzi hayo huzimishwa na watu wazima na jamii kwa ujumla.
Kama wahenga walivyosema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Baada ya muda, watoto wa ki-Tanzania hufuata utamaduni wa jamii wa kutothamini vitabu, na Taifa linaendelea kuzorota kielimu., wakati wenzetu wa-Marekani wanawalea watoto wao katika kupenda vitabu.
Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha watu wawe na tabia ya kutafuta elimu. Alikuwa mwandishi na msomaji makini. Alionyesha mfano kwa vitendo. Aliongoza njia.
Leo tuna watu ambao tunawaita viongozi ambao sielewi kwa nini wanaitwa viongozi. Wangekuwa ni viongozi, wangetambua kuwa elimu ni msingi wa maisha na maendeleo. Wangekuwa wanaihamasisha jamii kwa kauli na vitendo katika kutafuta elimu. Lakini, badala yake, hawaonekani kujali kabisa kwamba wanachangia katika kuliangamiza Taifa badala ya kuliongoza, yaani kulipeleka mbele.
Leo, katika kuvinjari kwenye mtandao wa Facebook, nimeona video ya Rais Obama na familia yake. Wako bustanini wakiwasomea watoto hadithi.
Nimeguswa sana na video hii. Niliwahi kuandika makala kuhusu kuwasomea watoto vitabu. Katika makala hii nilielezea jinsi wenzetu huku Marekani wanavyojali suala hili, kuanzia watu wa kawaida hadi viongozi wa juu kabisa. Hata dakika ile Marekani iliposhambuliwa, tarehe 11 Septemba, 2001, Rais Bush alikuwa darasani na watoto wakisoma kitabu.
Makala yangu ile niliipanua na kuiboresha na imechapishwa katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Katika makala hiyo, na kila mara ninapoongelea masuala ya aina hii ya kutokuwa na utamaduni huo kama wenzetu.
Lakini haingekuwa vigumu kuuanzisha na kuujenga utamaduni huo. Ni faraja kuona kuwa wako wengine wenye mawazo hayo hayo, na hapo napenda kumtaja Dada Sophie Kagambo Becker, ambaye ameelezea hayo katika blogu yake.