Showing posts with label elimu ya juu. Show all posts
Showing posts with label elimu ya juu. Show all posts

Tuesday, August 18, 2015

Warsha Kuhusu Jamii na Taaluma Inaendelea

Siku chache zilizopia niliandika katika blogu hii kuhusu warsha tuliyokuwa tunaisibiri hapa chuoni St. Olaf juu ya jamii na taaluma. Warsha hiyo ilianza jana; tulijadili sura kadhaa za kitabu cha Martha C. Nussbaum, Not for Profit: Why Democracy Needs the Humanities.

Kitabu hiki kinaelezea namna mwelekeo wa elimu ya juu unavyochepuka kutoka katika hali yake ya asili na unavyoingia katika mkondo wa kibiashara. Malengo ya elimu, ambayo yanapaswa kuwa kumjenga mtu na jamii katika tabia ya kutafakari, kuhoji mambo, kujitambua, na kuwa na mahusiano mema, ya ushirikiano na kusaidiana, yamekuwa yakibadilika. Malengo hayo sasa ni kuwaandaa watu kwa ajira na uzalishaji wa mali.

Not for Profit kinaongelea umuhimu wa elimu katika demokrasia. Kwa kuiingiza elimu katika mfumo wa biashara, tunahujumu demokrasia na mahusiano bora ulimwenguni. Nilifurahi kusoma katika kitabu hiki nadharia za mabingwa niliowasoma nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Socrates, Jean Jacques Rousseau, Johann Pestalozzi, na John Dewey. Ningefurahi zaidi iwapo nadharia za Paulo Freire zingekuwemo pia, kwani huyu ni mwelimishaji maarufu aliyeonyesha njia ya kuifanya elimu kuwa nyenzo ya mapinduzi.

Nilifunguka akili niliposoma kuwa Rabindranath Tagore alikuwa mwelimishaji, sio tu kinadharia, bali kwa kuanzisha na kuendesha vyuo. Tangu zamani nilimfahamu Tagore kama mwandishi maarufu wa riwaya, tamthilia na mashairi, aliyepata tuzo ya Nobel mwaka 1913. Niliwahi kufundisha kitabu chake maarufu, Gitanjali, hapa chuoni St. Olaf. Lakini sikuwa nimefuatilia mchango wake ulivyoelezwa katika Not for Profit.

Leo tumejadili sura kadhaa za kitabu cha Stanley Fish, Versions of Academic Freedom: From Professionalism to Revolution. Fish anafafanua vizuri dhana ya uhuru wa taaluma, kwa kuangalia mitazamo mbali mbali iliyopo kuhusu dhana hiyo. Ameweka wazi masuali muhimu kuhusu dhana ya uhuru wa taaluma. Kwa mfano, uhuru wa taaluma ni haki ya kikatiba? Kwa nini waalimu katika elimu ya juu wanaamini wana haki ya kuwa na uhuru wa taaluma mpana kuliko uhuru walio nao wananchi wengine? Wanafunzi nao wanao au wanastahili uhuru huo?

Fish anaongelea pia masuala ya mtazamo wa kisiasa wa waalimu katika vyuo vikuu, na uhusiano wa maadili na uhuru wa taaluma. Tulipokuwa tunajadili suala hilo la maadili, profesa mwenzetu mmoja alielezea alivyowahi kukataa kuchora michoro ya kuboresha muundo wa ndege za kivita za jeshi la Marekani.

Kama ilivyokuwa jana, mjadala wa leo ulikuwa mzuri na wa kuelimisha. Nimefurahi kuvisoma vitabu viwili nilivyovitaja hapo juu. Kesho tutajadili Professors and their Politics, kitabu kilichohaririwa na Neil Gross na Solon Simmons.

Monday, September 10, 2012

Ziara Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki, Songea

Kama nilivyoelezea tena na tena, napenda kutembelea vyuo ninapokuwa Tanzania. Soma kwa mfano, hapa. Ni fursa ya kujiweka sawa katika ufahamu wa nini kinachoendelea, changamoto zilizopo, mikakati ya kuboresha elimu ya juu. Napata fursa ya kujadiliana na wahusika namna ya kushirikiana na kuchangia vyuo hivi. Tarehe 21 mwezi Julai, mwaka huu, nilitembelea tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin, mjini Songea. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin ni mradi wa Kanisa Katoliki Tanzania. Ni mtandao ambao tayari una vituo sehemu mbali mbali za nchi. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Hapa kushoto naonekana na Profesa Donatus Komba, makamu wa mkuu wa chuo hicho mjini Songea. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu siku ya ziara yangu, akinitembeza kila mahali na kunipa maelezo.








Hapa kushoto naonekana nikitia sahihi katika kitabu cha wageni.


Hapa kushoto ni jengo la utawala. Chuo cha Mtakatifu Augustin kina mipango mikubwa ya kupanua mtandao wake. Kwa upande wa Songea, tayari Seminari Kuu ya Peramiho imeshafanywa sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo ya falsafa. Wanaofahamu taratibu za seminari za Katoliki wanajua kuwa tangu zamani, mapadri walitakiwa kusoma masomo ya kawaida tunayosoma sisi wengine, na baada ya hapo kwenda seminari kuu kusomea masomo ya teolojia na falsafa.  Basi Peramiho sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo haya ya falsafa.

Kanisa Katoliki jimbo la Songea limetoa majengo yaliyowezesha chuo hiki kuanzishwa. Chuo kina mipango ya kuongeza majengo. Nilionyeshwa sehemu mbali mbali, kama vile madarasa, kumbi kubwa, na maktaba. Nilivutiwa kusikia kuwa, mapadri wastaafu wamekuwa wakichangia hazina ya vitabu vyao katika juhudi za kuitajirisha maktaba.


Tayari, chuo kikuu cha Songea kinaendesha masomo ya aina mbali mbali. Mimi kama mwalimu wa "Literature" nilifurahi kusikia kuwa hilo ni somo mojawapo katika chuo hiki, na nilifurahi kukutana na mhadhiri wa somo hili.



Kwamba hiki ni chuo cha Kanisa Katoliki haimaanishi kuwa wanaosoma, kufundisha, au kufanya kazi hapo, ni wa-Katoliki tu. Chuo hiki kinawapokea watu wa dini na madhehebu mbali mbali. Angalia, kwa mfano, orodha ya wanafunzi wapya kwa mwaka huu.

Nilijifunza mengi katika ziara yangu hii, na hapa juu nimetoa dondoo chache tu.







Mdau jipatie taarifa zaidi kwa kuangalia video hii inayoelezea ufunguzi wa chuo hiki:

 

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...