Friday, March 18, 2011

JK: Maprofesa Wananisikitisha

JK: Maprofesa wananisikitisha

Chanzo: Uhuru

NA JANE MIHANJI

RAIS Jakaya Kikwete amewataka maprofesa na wasomi nchini kutunga vitabu ili kukabiliana na tatizo la kushuka kiwango cha elimu, kunakochangiwa na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada.

Amesema anasikitishwa na kitendo cha maprofesa na wasomi chini kulalamikia upungufu wa vitabu katika fani mbalimbali, huku wakikwepa kutoa mchango wa kutatua tatizo hilo.

Rais Kikwete amewata kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anafanya jitihada za kuboresha elimu ili kuwa na kizazi kilichowiva kitaaluma.

Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Taarifa ya wizara iliyosomwa na waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, ilieleza uhaba wa vitabu ni moja ya matatizo yanayokwamisha sekta ya elimu.

Dk. Kawambwa alisema shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vitabu na katika baadhi, wanafunzi hutumia vya tofauti, tatizo linaloweza kupatiwa ufumbuzi kwa wasomi kujikita katika uandishi wa vitabu.

"Hili ni tatizo, wakati tunasoma Msoga kitabu cha Bulicheka, mwanafunzi aliyekuwa akisoma Lindi alikisoma, lakini siku hizi mambo yamebadilika," alisema rais Kikwete na kuiagiza wizara kutoa kipaumbele katika uchapishaji vitabu vya kiada na ziada.

"Lazima tupange kila mwaka bajeti ya kuchapisha vitabu vya watoto wetu, hatuwezi kuacha waendelee kuchangia vitabu kwa kuwa hili ni la kwetu, na hatuwezi kusubiri wafadhili," alisema.

Alionya fedha za vitabu, maabara na ujenzi wa nyumba za walimu zisipelekwe katika matumizi mengine.

Kwa upande wake, Dk. Kawambwa alisema wizara inakabiliwa na upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari, hususan katika mikoa ya pembezoni.

Alisema pia kuna tatizo la kiwango kidogo cha ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na ualimu, hususan masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza.

Waziri Dk. Kawambwa alisema ufinyu wa bajeti katika utekelezaji programu za elimu na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu pia ni tatizo kubwa.

Akizungumzia kiwango cha ufaulu, rais Kikwete aliwataka walimu wanaotunga mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo, kuacha kutunga migumu kupita kiasi, kwa kuwa yawezekana kuwa ndicho chanzo cha matatizo.

"Changamoto ya ufaulu mdogo kama mnavyodai katika masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza pengine inatokana na ugumu wa mitihani... lakini msitunge rahisi sana," alisema na kuongeza ni lazima wahitimu wawe na viwango vinavyostahili.

18 comments:

Mbele said...

Naafiki wito huu wa JK. Pamoja na maandishi mengine yote tunayotegemewa kuandika, ni muhimu tuandike aina ya vitabu anavyoongelea JK.

Binafsi, najikongoja, na baadhi ya vitabu vyangu ni hivi hapa.

Baahi ya vitabu hivi vinatumika vyuoni ughaibuni, na vinatakiwa viwepo pia katika vyuo vya Tanzania, kwani taaluma haijui mipaka ya nchi. Mfano ni kitabu hiki hapa.

Mimi sina uwezo wa kuvinunua kwa wingi na kuvisambaza kwenye vyuo vyetu. Tangu zamani nina utaratibu wa kununua vitabu viwili vitatu, sio hivi vyangu tu, na kuvibeba ninapoenda Tanzania na kuvigawa kwenye maktaba au vyuo.

Lakini uwezo ni mdogo, ingawa nia ninayo. Tena inakuwa ni uamuzi baina ya kupeleka vitabu au vipodozi. Sijui ni wangapi wanaoishi au kutembelea ughaibuni wanathubutu kurudi nyumbani na vitabu.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Prof. Mbele. Bado nakumbuka ule mkasa wako wa kurudi nyumbani na vitabu badala ya pick up kama wengi walivyotegemea.

Suala linalokatisha waandishi wengi - ambalo pia Mtanga amelizungumzia katika kibaraza changu - ni ukosefu wa wasomaji. Soko la kuaminika ni huko huko mashuleni ambako nako mpaka kitabu chako kikubaliwe na kuingizwa katika mitaala ni kizungumkuti kweli. Ya nini basi mtu uandike kitabu, uingie gharama ya kukichapisha na usipate cho chote? Jambo hili linakatisha tamaa sana. Kama kukiwa na utaratibu mzuri na unaoeleweka kuhusu uteuzi wa vitabu vya mashuleni pamoja na malipo mazuri kwa waandishi naamini kwamba vitabu vitaandikwa tena vingi sana.

Mimi nadhani pia kwamba hata suala la lugha nalo linachangia. Ukiandika kitabu cha Kiingereza na kwa bahati mbaya kisichaguliwe kutumika mashuleni basi hapo umeula wa chuya kwani wasomaji wa Kiingereza pengine ni wachache zaidi kuliko wale wa Kiswahili. Na naamini kwamba si maprofesa wote wanaweza kuandika vitabu katika nyanja zao kwa Kiswahili. Kuna mzunguko fulani hapa pia kuhusu suala hili la lugha.

Ndiyo maana watu wengi wanaamua kupita njia ya uhakika zaidi na kuamua kuandika vitabu vinavyotoa mwongozo wa jinsi ya kujibu maswali ya mitihani. Vitabu hivi vinanunuliwa sana na ndiyo maana watu kama akina Nyambari Nyangwine (sasa mbunge wa Tarime) wamajiwahi na kuanzisha makampuni ya uchapishaji ya vitabu vya kujibu maswali tu basi na wameweza kutajirika kwa haraka.

Naamini kwamba mwongozo wako wa Things Fall Apart ukiupeleka Tanzania utanunuliwa sana hasa kama kule mwishoni utaongezea mwongozo na mifano bora ya jinsi ya kujibu maswali ya fasihi ya kidato cha nne. Watoto watakuwa hawana tena haja ya kuisoma riwaya ya Things Fall Apart yenyewe na badala yake watasoma tu huo mwongozo na kutegemea kupata A katika mitihani yao. Ndiyo elimu yetu hiyo ilipofikia!

Kwa hiyo inawezekana ukawa umekalia utajiri na huo mwongozo wa Things Fall Apart.

Kuhusu hivyo vitabu vyako vingine hata kama angetokea mtu akakusaidia kuvipeleka Tanzania, nani atavisoma? Pengine mtu avilipie kabisa na wewe ukavigawe bure mashuleni. Hata hili likitokea, kama bado havijapendekezwa katika mitaala kusomwa huko ni kazi bure tu.

Mwaka huu nategemea kuchapisha vitabu vitatu - viwili vya isimu na kimoja cha sayansi kwa ajili ya shule za msingi Tanzania. Hiki cha shule za msingi nitakipeleka mwenyewe laivu kwa JK nikampe mkononi akisome ili aone mawazo na mapendekezo yangu kuhusu jinsi ya kuimarisha na kuwafanya watoto wetu wavutiwe na masomo ya sayansi. Huu ni mchango wangu kwa nchi yangu na hata kisipopendekezwa mashuleni ni sawa lakini nitakuwa nimeridhika na juhudi zangu za kujaribu kusaidia!

Mbele said...

Profesa Matondo, hayo unayosema ni muhimu, tena baadhi ndiyo yaliyonitokea.

Kwa mfano, baada ya kuandika hiki kijitabu kuhusu "Things Fall Apart," nikakichapisha Tanzania, jamaa walinishauri niandike pia masuali na majibu, ili kijitabu kiweze kutumika kwenye "tuition." Walininihakikishia kuwa nikifanya hivyo, kitakuwa na soko kubwa nami nitazoa pesa sana.

Tatizo la watu wa aina hii ni kuwa hawanielewi ni mtu wa namna gani. Hawaelewi ni kiasi gani ninavyothamini elimu. Siwezi kufanya mambo yanayohujumu elimu, hata kama yangeweza kuniletea utajiri.

Vile vile suala ulilogusia, kwamba hata vitabu vikienda Tanzania vitakosa wanunuaji na wasomaji ndio hali halisi. Nilishapeleka nakala kadhaa, na nimejionea hali halisi.

Tena wengine, badala ya kuzingatia kuwa suala la msingi hapa ni elimu, utawasikia wakisema kuwa unatafuta biashara ya vitabu. Yaani wa-Tanzania wengine ni wajinga kiasi kuwa hawakioni kitabu kwa mtazamo wa elimu bali pesa.

Kuhusu lugha ni kweli kuwa wasomi wengi wa Tanzania hawawezi kuelezea taaluma zao kwa ki-Swahili. Wala hawajitahidi kuondokana na tatizo hili.

Vile vile, hata ki-Ingereza ni shida. Ingekuwa wanaweza kujieleza vizuri kwa ki-Ingereza, wangeandika vitabu ambavyo vingetumiwa katika na shule za nchi za jirani au nchi za mbali pia.

Zamani, tulipokuwa tunasoma sekondari na kuendelea, vitabu vingine tulivyokuwa tunatumia, katika masomo kama ki-Ingereza, historia, na elimu ya viumbe ("biology"), vilikuwa vimeandikwa na watu kutoka nchi kama Ghana na Nigeria.

Ingekuwa wa-Tanzania ni makini, wangeandika vitabu vya masomo mbali mbali kwa ki-Ingereza pia, vikawa vinatumika huko Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, na ughaibuni.

Inavyoonekana, wasomi wetu wanategemea shule na vyuo vya nchini mwetu tu. Kumbe, inatakiwa waandike wakijua kuwa elimu haijui mipaka ya nchi. Kitabu bora hata kama hakitambuliwi na mfumo wa Tanzania kitatambuliwa kimataifa. Kwa hivi wajizatiti ipasavyo.

Mzee wa Changamoto said...

Nahisi kupanga safari za Minnesota na Florida kwa ajili ya MAHOJIANO MAALUM.
Sababu ninaijua mwenyewe.
Ila HAZINA hii si ya kupoteza

Koero Mkundi said...

Hata sijawaelewa, sasa mnatetea uandishi wa akina Nyambari Nyangwine au?

Christian Sikapundwa said...

Nakupongeza sana Profesa kama unauchungu na nchi yako,Rais ameona hayo na ameona mchango mkubwa unaoweza kufanywa na maprofesa wetu wa ndani na wanje.

Ukweli usio fichika tunaupungifu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada katika shule zetu.Wewe na maprofesa wenzako mjipinde muokoe jahazi hili.

Akina Nyangwine walifanya vyo na sasa ni wakati wa Maprofesa wengine wafanye vitu vyo.Suala la wapi vitabu vitauzwa sio la Mashaka cha msingi ni kuwasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hasa Afisa Eilimu Kiongozi.

Tunakutegemea sana katika mchango wako wa vitabu vya sayansi,Sayansi jamii na lugha.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mzee wa Changamoto - wewe si mtangazaji bwana. Bila shaka unajua kwamba siku hizi kufanya mahojiano na mtu siyo lazima kumfuata huko aliko, lakini unakaribishwa sana. Kuna ugali wa Kisukuma hapa tele; na jua limeanza kuwaka ile mbaya. Natumaini kwamba na nyie huko sasa barafu imeanza kuwaachia kidogo!

Koero - vitabu vya akina Nyambari Nyangwine, kwa maoni yangu vinadumaza elimu badala ya kuiimarisha. Badala ya kusoma vitabu (riwaya, tamthiliya na ushairi) vilivyopendekezwa wanafunzi wanapita njia za mkato na kusoma mwongozo wake na majibu waliyotafuniwa. Ndiyo maana nikasema kwa kejeli kwamba "ndipo elimu yetu ilipofikia!"

Mimi nilifundisha katika shule za sekondari za Jitegemee, Mwanza na Mwadui wakati ule nikisoma pale Mlimani. Wakati ule Mbunda Msokile ndiye alikuwa akitamba. Watoto walichokuwa wanafanya ni kusoma miongozo ya Mbunda Msokile na kukariri majibu yake kwisha. Hawana tena haja ya kuvisoma vitabu vyenyewe.

Nilipokuwa nyumbani mwaka jana pia nilitembelea vijana fulani hivi waliokuwa wakijiandaa kufanya mitihani ya kidato cha nne. Hawa walikuwa na vitabu vya Nyangwine vya kila aina. Nao waliniambia yale yale: kusoma riwaya nzima ni kupoteza muda tu kwani kila kitu wameshatafuniwa na Nyangwine. Cha kushangaza ni kwamba wote wamefeli. Mmoja tu katika kundi lile la watu sita amepata divisheni 4 ya point 28! Sasa sijui hawakukariri vizuri au pengine majibu ya Nyamgwine ndiyo yana matatizo. Kuna hata anayechunguza na kuyahakiki majibu yaliyotolewa katika vitabu hivi na kuona kama yanaendana na yale ya baraza la mitihani au? Kama majibu ya Nyangwine ni tofauti na yale ya baraza la mitihani basi sishangai kwa nini vijana wale wameambulia patupu. Na sijui ni wangapi ambao wamekumbwa na tatizo hili.

Kupendekeza kwangu kwamba Profesa Mbele aongeze majibu ya fasihi katika mwongozo wake wa Things Fall Apart kulikuwa ni uchokozi tu ili nimwone atasemaje. Ndiyo maana ukisoma vizuri utaona kwamba kuna utani utani hivi katika maelezo yangu!

Hili ni suala la muhimu, tuendelee kubadilishana mawazo.

NN Mhango said...

Wanaosikitisha si maprofesa wala waandishi na watunzi bali serikali isiyowajibika wala kuwa na sera ya kila kitu zaidi ya ufisadi.
Badala ya kulaumu watunzi na waandishi, Jakaya Kikwete angejilaumu mwenyewe kwa kutokuwa na visheni wala sera ya elimu na mambo mengine.
Nyerere alionyesha mfano wa uandishi na uongozi. Yeye Kikwete zaidi ya kukodisha watu wa kumwandika vizuri ameandika au kutunga nini?
Kuondokana na hili nashauri. Rais aondokane na ufisadi wa kiakili ambapo madili yamefunika maadili.Mie kama mtunzi huwa nashauri watunzi watunge si kwa ajili ya soko la leo bali kuacha urathi kwa jamii hapa watakapokuwa wameondoka. Shaban Robert alifanya hili.

Koero Mkundi said...

Matondo, nakubalianan na wewe kwa 100%, kwanza kama sikosei huyu Mbunda Msokile hatunaye tena.....Amekwihafariki kitambo kidogo au?

Kuhusiana na akina Nyangwine na akina Kadeghe na wengineo labda mimi na wewe tujiulize, ni nani wa kulaumiwa? ni wao, wanafunzi au serikali.

nitafafanua:

1. kwa upande wao yaani waandishi wa vitabu kama akina Nyangwine walijaribu kuangalia mahitaji ya wanafunzi kwa kipindi hiki na kuona kuwa soko lipo kwenye utunzi wa kujibu mitihani na ndio wakaona waelekeze nguvu zao huko

2. Wanafunzi nao waliona kuwa kinachotakiwa ni kufaulu na sio kuelewa na na ndio maan siku hizi hasa huku mijini madarasa ya Qualify Test (QT) yamejaa sana na kila mtu anataka asome hadi kwa kidato cha nne kwa miaka miwili tu na kidato cha tato na sita kwa mwaka mmoja tu... kinachotafutwa ni kujua namna ya kujibu mitihani na sio kuelewa.....

3. Kwa upande wa Serikali nayo ni kukaa kimya wakati upuuzi huu ukiendelea kutamalaki kila uchao, kwanza wao ndio wanaopitisha vitabu hivyo na kuvipa baraka, hivi hawajiulizi majaaliwa ya elimu yetu yatakuwa vipi kwa uandishi wa aina hiyo?
na ndio maan wakati mwingine huwa nashangazwa sana na baadhi ya maamuzi ya viongozi wetu, wa sasa, hayaoneshi hata chembe uadilifu. utakuata wananchi wamawatuhuku kuwa wamepewa 10%, mimi nasema, sio wote wanaopewa hiyo 10%, bali maamuzi yao yametokana na kiwango cha elimu walicho nacho, yaani elimu yao imeishia hapo....

tunahitaji mapinduzi makubwa sana kwa upande wa elimu

chib said...

Nakupongeza Prof Mbele kwa juhudi zako za kujaribu kuinua elimu ya Tanzania pasipo kukata tamaa, japo mazingira yanakatisha tamaa. Mimi ni muumini wa usemi wa kwamba, usikate tamaa kamwe. Nilikuwa naamini hivyo na ninaendelea kuamini hivyo hasa baada ya kufanya kazi huko umasaini na kwa wamng'ati vijijini kwa zaidi ya miaka 2.
Nakusifu pia Prof Matondo kwa juhudi za kutunga kitabu kunufaisha watotot wa kitanzania.
Nyumbani tuna matatizo makubwa 4
1. Hatuna sera za elimu, tunadandia tu
2. Ubinafsi, na kukubali kuhujumiwa na waandishi fulani ili wauze vitabu nchini na wizara kubadili mfumo na vitabu vinavyotumika ili mradi kukidhi asilimia kumi mtu aliyopokea
3. Watendaji wetu hawana upendo au sijui niiteje, I mean they are not proactive and serious .... kuhusiana na kiwango cha elimu na ubora wake
4. Watanzania wengi hawana utamaduni wa kupenda kusoma chochote, labda magazeti ya udaku, kwa sababu hakuna misingi imara ya watotot kufunzwa na kuelewa umuhimu wa kusoma vitabu au majarida ya kimaendeleo.
Wenzetu wakienda kutembea na watotot wakirudi nyumbani, wanawaambia waandike matukio yote waliyo yaona njiani na baadaye kuja kuwasomea wenzao ni nini walifanya wakati wakiwa mapumzikoni. Hii inajenga upendo na hamu ya kusoma.

Emmanuel said...

Ningefurahi kuona na JK akiandika kitabu hata cha hadithi za mwambao badala kuanza kuvurumisha lawama kwa wasomi. Kwahiyo yeye sio msomi? Tatizo letu tumekuwa tunacheza na mitaala hasa alipokuja Bwana Mungai kwa maslahi yake na sasa kila mmoja anafikiri hakuna tatizo. Vitabu vilikuwepo mpaka miaka ya tisini wakati mwenyewe nasoma Shule ya msing japo vingi vya magharibi. Sasa kumekucha ee..lakini lini atatekeleza haya maneno yake?

SIMON KITURURU said...

NImetatizwa na hoja ya JK ya kuomba MITIHANI isiwe migumu. Kwani ugumu kipimo chake ni nini?

Lakini maswala ya kutaka kujua majibu sio tatizo la Tanzania tu kwakuwa ukifuatilia Japan , KOREA kusini na CHINA katika elimu yao utastukia kukaririri majibu kupo sana na haionekani kuathiri sana kama ituathirivyo sisi.

Kwa hiyo naamini kuna zaidi ya kukariri tu majibu kuliko tatizo Tanzania.

Kwani si JK asemacho kuwa watu waandike hata katika maoni hapa najua watu wawili tayari ambao vitabu vyao kuchapishwa ilikuwa kasheshe na hao katika maoni haya ni Prof.Mbele aliyeamua kutumia Lulu na NN Mhango ambaye kitabu chake kipya sio muda mrefu kilikataliwa kwa kuwa kinapingana na ajenda za serikali?


Mie naamini Tatizo ni kubwa kuliko kukariri majibu kwa kuwa labda hata wasahihishao majibu nao hawakukariri vizuri ni nini JIBU!:-(

Nawaza tu kwa sauti!

Katu said...

Profesa Mbele!

mimi nadhani Rais amekimbilia kutoa majukumu tuu kwa maprofesa bila kuangalia mazingira halisi ya serikali na watendaji wake.

Yeye kama Rais watanzania anatakiwa kuhakikisha Kodi zinakusanya kama chanzo kimojawapo cha mapato serikali.

Na matumizi fedha umma yanakuwa makini kwa vipaumbele na siyo haya mambo yanayoendelea sasa ya ufisadi tena Rais akiangalia tuu bila kufanyia kazi kama serikali (Main drivers factors). Angalia sababu za

Maprofesa wa Kitanzania kuondoka Tanzania na kwenda ughaibuni. Baadhi yao wameondoka kutokana na ufisadi wa madaraka kwenye viongozi wa huko vyuo vikuu..

Hiyo mitihani yenyewe sidhani hata inapotungwa inamjenga mwanafunzi maisha halisi ya kitanzani ya sasa. Sidhani hata mashuleni na vyuoni wanchukua matukio yanaendelea kujadili mashuleni kama Case Study!

Katu said...

Inaendelea Profesa Mbele!

Hizo Case study kujadiliwa mashuleni kama mbinu kujifunza elimu ya kisasa. Kwa sababu itaonekana kama kunyoosha vidole serikali ambayo imeisha oneha haipendi kukosolewa. Hivyo nafasi mwalimu au Mkufunzi au muhaziri wa chuo kikuu ambaye achukue hayo matukio yanatokea katika Tanzania ya leo kama somo kufundishia shuleni hakika itakwa chanzo cha kupoteza kazi au mengine mengi kutokea pia.

Nategemea Profesa atayetunga Ki-vi-tabu na kutumia maarifa yake kikamilifu ni vigumu sana kutunga kitabu bila kuhusisha hayo maufisadi na ubabe kuvuruga demokrasia yanayoendelea.....

Ni kweli wanatanzia wengi wetu ni wavivu wakujisomea..kwa sababu hiyo series ndefu sana katika maisha yetu ya kila siku hata hao wanaoshriki ufisadi ni matokeo ya uvivu wa kujitafutia...Hapa kuna tatizo la msingi(Responsibility and accountability.

Kupambana na kuondoa hilo Tanzania inahitaji viongozi wa juu serikalini wazalendo wa kweli kutoka Moyoni na siyo uzalendo wa Tabasamu na porojo kama huu wa sasa...

Katu said...

Tatizo linajitokeza sasa katika elimu limetengenezwa muda naona katika takribani miongo miwili iliyopita. na siyo kuanza kuwaptaia watu majukumu ya kutunga vitabu bila ya kweka mazingira yanaowajali watunga vitabu katika utendaji.

Katu said...

Hivi kweli profesa wa chuo Kikuu anayeishi tanzania anatunga hicho kiyabu katika mazingira haya mgao wa umeme!? Au mazingira gani!?

Mbele said...

Ndugu Katu, nafurahi kuona umeibukia tena kwenye hiki kiblogu changu. Ulikuwa msituni kwa kitambo. Pole na mgao wa umeme, ambao nahisi umechangia kuadimika kwako.

Napenda tu kutoa shukrani kwa mawazo yako. Ni changamoto nzuri.

Katu said...

Asante kunikaribisha hapa tena kutoa mchango wangu mawazo....Nilikuwa kimya kwa sababu matatizo mavuno yangu hayakuwa mazuri na serikali haina mikakati endelevu kulinda kipato cha m-wa-tanzania na wengine kwa ujumla hivyo iwapo mvua zinapokosean ama kunapotokea maafa ya asili basi hali inazidi kuwa mbaya.

Kingine kilichonifanya niwe kimya ni hali ya kukatisha Tamaa ya maisha ya sisi watanzania na kushindwa kujua umuhimu kupiga kura na maana yake.

Ni kweli vyama upinzani walisema CCM wamechachua kura. Kinachonishangaza mimi mikutano ya CCM ilikuwa ikijaa umati mkubwa hata kama wanapewa pesa, khanga, scafu na fulana ili kushiriki mikutano ya kampeni ya CCM. Nini kiliwashinda hao watanzania kuacha kwenda kwenye mikutano ya CCM...Naamini wangeweza kuchukua hizo za nguo na pesa na pia wasingefika kwenye mikutano ya CCM. Kimsingi kuna safari ndefu kwa sisi watanzania kutambua umuhimu siasa na maendeleo ya uchumi. Inafikia wakati viongozi wa juu wa serikali wanakosolewa wana sema hizo ni siasa...Sasa mimi haingii akilini wanatenganisha nini kati ya siasa na uchumi, Maana hivi vitu vinaenda pamoja! hapo ama wanaleta masihara katika mambo makini. Kama hivi JK anapowaambia Maprofesa kutunga vitabu...Yaani ni sawa kwa wale wanaoamini dini kwamba unamwambia muumini kutotenda dhambi bila ya kumweleza dhambi nini!?