Wednesday, March 23, 2011

Eti Wahadhiri Waeneza Siasa za Chuki Vyuoni

Niomeona taarifa hii hapa chini nikaona lazima niseme moja mawili, nikitumia wadhifa wangu kama mwanataaluma na mzoefu wa kufundisha au kutoa mihadhara vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia.

Sio kazi ya serikali kuingia darasani chuo kikuu ili kuchunguza mwalimu anafundisha nini au anafundishaje. Hii ni kazi ya wanataaluma na wahadhiri, kufuatana na taratibu zinazotambulika katika jumuia ya wanataaluma. Taratibu hizi ni za kulinda, kutathmini, kuratibu na kuboresha viwango vya utafiti, ufundishaji na taaluma kwa ujumla.

Serikali inapaswa kutambua kuwa dhana ya chuo kikuu, duniani pote, inaendana na haitengeki na uhuru wa kitaaluma. Walimu wa vyuo vikuu sio tu wana wajibu, bali uhuru wa kufukuzia taaluma bila vipingamizi, kwa mujibu wa vigezo vya taaluma hizo vinavyotambulika miongoni mwa wanataaluma kimataifa.

Kama kuna walakini katika utendaji kazi wa mwalimu wa chuo kikuu, kama vile kutofundisha somo inavyotegemewa, wanaowajibika kuchunguza ni wanataaluma wenzake, si serikali. Serikali haitegemewi wala kuruhusiwa kuingilia uhuru wa walimu na watafiti chuo kikuu katika kufanya utafiti, ufundishaji, uandishi na kadhalika kwa misingi na viwango vinavyotambuliwa kitaaluma.

Jambo jingine la msingi kabisa kuhusu chuo kikuu ni kuwa hapa ni mahala pa tafakari na malumbano kuhusu masuala mbali mbali, kwa kiwango cha juu kabisa. Ni mahala ambapo fikra za kila aina na hoja za kila aina zinapaswa kusikika na kuchambuliwa.

Chuo kikuu cha kweli, chenye hadhi ya chuo kikuu, ni maskani ya wachochezi wa fikra na hoja, katika taaluma mbali mbali, ikiwemo siasa. Huwezi kumwambia mtafiti au mhadhiri asiiponde serikali iliyoko madarakani iwapo utafiti na tafakari yake inampeleka huko.

Dhana ya kwamba kuna wanaoeneza siasa za chuki miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu ni dhana ya kusikitisha. Inamaanisha kuwa hao wanafunzi ni wajinga sana, au ni wavivu sana, ambao hawana uwezo au dhamira ya kujibidisha katika kusoma na kutafakari mambo ili waweze kugundua mapungufu ya hoja wanazosikia, na kupambana kwa hoja. Inamaanisha hao ni wanafunzi mbumbumbu, wasio na akili au wasiotumia akili. Kitendawili ni je, walifikaje hapo chuoni, kama si kwa njia za panya?

Wanafunzi wa chuo kikuu wanawajibika kuwa tayari na makini katika kupambana kwa hoja na wanafunzi wenzao na pia na walimu wao. Ni fedheha iwapo wanafunzi hao kiwango chao ni duni kiasi cha kuweza kupotoshwa na walimu wao. Hawastahili kuitwa wanafunzi wa chuo kikuu, na hicho chuo chenyewe hakistahili kuitwa chuo kikuu. Na ni fedheha kama tumefikia mahali ambapo serikali inaona ije darasani kuwanusuru hao wanafunzi feki.


------------------------------------------------------------------------------------
WAHADHIRI WAENEZA SIASA ZA CHUKI VYUONI


Chanzo:Habari Leo

Wahadhiri waeneza siasa za chuki vyuoni
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko; Tarehe: 23rd March 2011


SERIKALI inawachunguza wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wanaotumia muda mrefu madarasani kuzungumzia siasa badala ya kufanya kazi zinazohusu taaluma.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, Serikali ina taarifa kuwa, baadhi ya wahadhiri wanatumia muda wa kutoa mihadhara ya masomo kwa kuzungumzia siasa hasa kupiga vita Serikali iliyopo madarakani.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kuwabaini baadhi ya wahadhiri wanaojihusisha na siasa kwa kuingia madarasani na kuzungumzia siasa kwa dakika kumi kabla ya kuanza kufundisha,” amesema Mulugo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, lengo la wahadhiri hao ni kuwafanya wanafunzi kuchochea migomo na maandamano na kupandikiza chuki baina ya Serikali na wanafunzi.

Naibu Waziri ameyasema hayo katika mkutano kati ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Dar es Salaam.

Mulugo amesema, ingawa si katika chuo hicho, lakini kuna taarifa katika baadhi ya vyuo vikuu, wahadhiri wanafanya hivyo na kuwaonya kuwa kazi yao ni kuelimisha na si kuwavuruga wanafunzi akili kwa kuchanganya yale wanaojifunza na siasa na akawataka kujiepusha na siasa kwa kuwa wao ni wataalamu.

“Tena siasa zenyewe ni za kupiga vita Serikali iliyopo madarakani, tutawachukulia hatua,” alisisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri Kawambwa ambaye aliongeza kuwa wahadhiri wasipojihusisha katika siasa, watasaidia kuweka utulivu katika vyuo na kuepusha migogoro.

Awali, kabla ya onyo hilo, Dk. Kawambwa alisema Baraza la Mawaziri limeazimia kuanzia Machi mwaka huu wahadhiri wastaafu walipwe pensheni sawa na wastaafu wengine serikalini.

Alifafanua kwamba uamuzi huo unatokana na malalamiko ya wahadhiri wastaafu kwamba wanapata mafao finyu kutoka Mfuko wa Pensheni wa PPF tofauti na wanaostaafu kutoka Serikali Kuu ambao hupata mafao yenye neema kutoka Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GSPF).

Mbali na Dk. Kawambwa, pia Rais Jakaya Kikwete katika shughuli tofauti ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) jana, aligusia malalamiko ya wafanyakazi wote kuhusu tofauti kubwa ya sana katika utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni.

“Utakuta wafanyakazi wenye viwango sawa vya mshahara, muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata hadi mara tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine,” alisema Rais Kikwete.

Kutokana na tofauti hiyo aliyosema imelalamikiwa na vyama vingi vya wafanyakazi, Rais Kikwete aliagiza SSRA iangalie tofauti hiyo kwa makini na kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa mafao kati ya mfuko na mfuko, lakini akawataka pia wazingatie ustawi wa mfuko huo.

Lakini kuhusu maombi ya wahadhiri wa Muhas, kutaka kulipwa mafao kwa mkupuo kwa asilimia 50 ya mafao yao na kulipwa kwa miaka 15 baada ya kupokea mafao ya mkupuo, Dk. Kawambwa alisema bado yanafanyiwa kazi.

Kati hilo, Dk. Kawambwa alibainisha wataalamu wanaangalia suala la malipo hayo kwa kuwa limeonekana na utata unaoweza kusababisha baadhi ya mifuko kufa iwapo itapata wastaafu wengi hivyo unaangaliwa mfumo utakaotumiwa na mifuko yote.

Akizungumzia madai ya wahadhiri wa chuo hicho kuhusu posho ya nyumba ambazo hawajalipwa kuanzia mwaka jana, alisema hali hiyo ilitokana na ufinyu wa bajeti, lakini tayari wamepeleka malalamiko yao kwa Wizara ya Fedha ili walipwe katika bajeti ijayo.

Kabla ya kauli hizo za mawaziri, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Kisali Pallangyo alielezea changamoto anazopata ikiwemo ya miundombinu michache ya chuo hicho.

Kutokana na uhaba huo wa miundombinu, kati ya wanafunzi wanne wanaostahili kujiunga na chuo hicho, ni mmoja tu anayepata nafasi wakati Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya.

Dk. Kawambwa akijibu hoja hiyo, alisema, katika kuongeza wataalamu hasa katika masomo ya sayansi, Serikali imejipanga katika mpango wa maendeleo ya elimu ya juu kuboresha miundombinu ya vyuo hivyo ili wanafunzi wote wenye sifa wajiunge na vyuo stahili.

2 comments:

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Katu said...

Profesa Mbele...Niliandika maoni yangu kutoka kwenye hii habari yanye kichwa cha Habari "JK:anasikitishwa na Maprofesa" Niliandika hvi'Hizo Case study kujadiliwa mashuleni kama mbinu kujifunza elimu ya kisasa kujifunza maarifa endelevu ya wakati huu. Kwa sababu itaonekana kama kunyoosha vidole serikali ambayo imeisha onyesha haipendi kukosolewa.

Hivyo nafasi mwalimu au Mkufunzi au muhadhiri wa chuo kikuu ambaye anatumia hayo matukio yanatokea katika Tanzania ya leo kama somo la kufundishia shuleni hakika itakuwa chanzo cha kupoteza kazi au mengine mengi kutokea pia'.

Hiyo ndiyo hali halisi ya maisha sasa hapa Tanzania ya watu tunaoishi kwa kubahatisha kutoka ngazi zote za kijamii!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...