Monday, March 28, 2011

Dhana Duni ya Mfumo Kristo

Kila kukicha, unajitokeza ushahidi kwamba kiwango cha kufikiri miongoni mwa wa-Tanzania wengi ni duni. Siku hizi, kwa mfano, imeibuka hii dhana ya mfumo Kristo.

Walioibuni dhana hii na ambao wanaieneza wana ajenda ya kujenga hoja kuwa mfumo wa utawala na uchumi Tanzania unaendeshwa kwa misingi ya kiKristu, na kwa lengo la kuwanufaisha wa-Kristu na kuwakandamiza na kuwanyima wa-Islam fursa na haki wanazostahili, katika nyanja mbali mbali, kama vile elimu na uongozi.

Hii ndio dhana ya msingi ya hiki kinachoitwa mfumo Kristo. Wanaojenga hoja hii wanadai kuwa serikali ya Tanzania yenyewe inaendeshwa na maaskofu kama sehemu ya uendelezaji wa huu wanaouita mfumo Kristo.

Kwanza napenda kusema, kama ninavyosema daima, kuwa kila mtu ana uhuru wa kutoa mawazo yake. Uhuru huu ni pamoja na uhuru wa kuyahoji au kuyapinga mawazo ya wengine, kufuatana na mchakato wa kujielimisha na kutafakari masuala. Ni pamoja na uhuru wa kuyapinga mawazo yako mwenyewe.

Nashangaa kwa nini mfumo mbovu uhusishwe na jina la Yesu Kristu. Dini zote mbili, u-Islam na u-Kristu, zinamtambua na kumheshimu Yesu. Yesu anatambuliwa kama Mungu katika u-Kristu. Na katika u-Islam, anatambuliwa kama mtume maarufu. Dini zote zinamheshimu sana Yesu.

Kama mfumo wa Tanzania umeoza kama inavyosemwa, hauwezi kuwa mfumo Kristo. Kuuita mfumo Kristo ni dhihaka isiyo kifani. Huwezi kuuhusisha uchafu wowote na Mungu au mtume. Kama kweli maaskofu wanaendekeza na kuulinda mfumo wa dhuluma, wanakiuka mafundisho na maadili ya Kristo. Huu si mfumo Kristo. Mfumo Kristo ni mfumo wa haki na maadili aliyotufundisha Kristo.

Sidhani kama inahitaji akili ya pekee sana kuitambua hoja hii. Lakini ni wazi kuwa watu wengi Tanzania wana kiwango duni cha kufikiri au kuelewa mambo. Kwa dhana yao ya mfumo Kristo, wanaudhihaki u-Kristo, na pia wanaudhihaki u-Islam. Ila, kutokana na akili zao duni, hawatambui hilo. Kilichopo ni kuwaombea dua njema, waweze kujitambua na kujirekebisha.

16 comments:

Rhoda said...

Asante sana Prof Mbele..UBARIKIWE SANA!

Fadhy Mtanga said...

ni mada nzuri sana Prof Mbele. Nitarejea baada ya muda kiasi kuweka maoni marefu

Fadhy Mtanga said...

nimerejea.

Nakushukuru sana Prof Mbele kwa kulileta jambo hili jamvini.

Mara zote kumekuwa na malalamiko makubwa juu ya kutokuwepo kwa usawa katika nyanja ya elimu na maendeleo kwa ujumla baina ya kundi moja kiimani na kundi jingine.

Ukitazama, watu wengi wamekuwa wakihusianisha kuwa nyuma kielimu kwa Waislam, na ukatoliki katika mamlaka hapa Tanzania.

Mie kabla sijaitupia serikali lawama kwa kuiunga mkono hiyo dhana, najaribu kuitazama historia ya nchi nikiiunganisha na ujio wa waleta dini hizi zote mbili.
Tukitazama historia, Waarabu ambao ndio waliouleta uislamu hapa Tanzania, walifika miaka mingi sana kabla ya Wazungu ambao waliuleta ukristo.

Waarabu walipokuwa wakitawala ukanda huu wa Afrika Mashariki hawakuwa na mpango wa kujenga mashule ili kuwaelimisha Waafrika. Kipaumbele chao kikubwa kilikuwa ni biashara ya utumwa, pembe za ndovu na vinginevyo.

Lakini Wazungu walipoingia Afrika Mashariki mwishoni mwa karne ya 19, pamoja na mikakati yao kiuchumi, walijenga mashule kwa ajili ya kuwaelimisha Waafrika wachache ili wawatumie kuzinyonya nchi zetu.

Elimu ni elimu. Pamoja na elimu ile kuwekwa mahsusi kwa ajili ya uchumi wa kikoloni, bado ilisaidia jamii kwa kiasi kikubwa. Hata ukisoma historia ya mapambano dhidi ya ukoloni, utaona jinsi elimu ya kikoloni ilivyofanya kazi kubwa kuwafungua mawazo vijana wa Kiafrika.

Baada ya uhuru, tukiwa tumerithi shule za Kimishenari, serikali iliamua kuzitaifisha ili kuwapa nafasi Waislam kusoma kwa usawa. Nani hafahamu kuwa, maeneo mengi ya Pwani ambayo Uislamu umeenea zaidi, hata leo yangali nyuma kielimu?

Tazama udahili wa wanafunzi kwenye shule za kidini hata leo. Ukienda katika seminari ya Kikristo, utakutana na wanafunzi wa Kiislamu wengi tu, lakini katika seminari za Kiislamu, wanafunzi wa Kikristu ni wa kubahatisha.

Sasa tukisema Wakristu ndio maadui wa elimu kwa Waislamu, napata wakati mgumu kuafikiana na dhana hii kwa kuitazama historia.

Kwa mtazamo wangu, lawama zinapaswa kwenda kwa Waarab, ambao historia inatufundisha kuwa walijikita zaidi kwenye biashara na mambo mengine ambayo historia ni shahidi.

Niseme tu, huu si wakati wa kulalamika, bali kuinuka na kuisaka elimu ili kuikomboa jamii yetu.

Asalaam aleykum!

Haji said...

Unajua muandika mada hapo juu inawezekena umetunukuu vibaya. hatujasema mfumo yesu (ambaye kwa wakristo ni mungu na kwa waislam ni mtume) tumesema mfumo kristo ambayo ni dini kwa wakristo, au hujui ukristo ni dini? na mbona hilo halihitaji hata kuwa na darasa hata moja. pili maaskofu hujui kama ni viongozi katika ukristo? Fadhy hujui hata History inachakachuliwa? wewe hujui kama tanzania haikupewa uhuru wake 09/12? ukikalia history utaishiwa, hebu angalia nchi za magharibi na za mashariki wapi kuna mabaki ya watu weusi (watumwa) wengi? na nani alie abolish slave trade? hiyo ndo ujue aliekuwa mfanyaji ndo anaendika history nakuwatupia mzigo waarabu na ndiye aliezuia biashara.

Mbele said...

Ndugu Haji, kama nakuelewa vizuri, unachosema ni kuwa hii dini inayoitwa u-Kristo ndio tatizo. Unaihukumu dini hii kuwa ni mbaya.

Hebu nisaidie kama nimeshindwa kukuelewa vizuri. Hapa kwenye blogu yangu ni mahala penye uhuru wa kutoa maoni.

Nazingatia kwamba atakayetuhukumu kwa mambo haya ya imani, na mwenye hukumu ya haki na ya mwisho, si binadamu bali Muumba. Karibu sana.

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Haji,
Nakushukuru sana kwa mchango wako kwenye maoni yangu.

Ukiniambia kuwa Tanzania haikupewa uhuru wake Disemba 9, nitakuwa mwenye uelewa endapo utasema kuwa ilipata uhuru wake lini.

Tuyaache hayo.

Si kwa kuwa historia iliandikwa na watu fulani na kuwapa upendeleo. Lakini si kweli kuwa Waarab ndio waliotangulia kufika pwani ya Afrika Mashariki?

Maelezo ya safari za wazungu wa awali kufika pwani ya Afrika Mashariki, kina Batholomew Diaz na Vasco da Gama, yanaonesha kuwa waliwakuta Waarab tayari katika pwani hii. Hayo nayo yamechakachuliwa?

Kuwa Afrika iligawanywa kwa wakoloni panapo 1884-5 na kuzaliwa ukoloni nayo yana mashaka? Kuwepo kwa elimu ya kikoloni, nayo si sahihi?

Kuwa tulipopata uhuru, tulizikuta shule za Kizungu, mojawapo Mkwawa niliyoisoma mie, ambazo zikataifishwa ili kuruhusu watu wa dini zote kuweza kusoma, lina uchakachuzi?

Ninachojaribu kukizungumza hapa, ni kuonesha kuwa huu utofauti umechangiwa kwa kiasi kikubwa na historia za makundi haya ndani ya nchi yetu.

Si kwa kuchakachuliwa kwa historia. Kwa sababu tunaambiwa Waarab ndio walioeneza Kiswahili miaka mingi hapo nyuma. Mie nikiwa mshairi, nimesoma historia ya ushairi (sijui kama imechakachuliwa) na kuona lugha hii ilivyoenezwa na Waarab.

Lakini huwa nashangazwa na historia kuwa ni Wajerumani waliokifanya Kiunguja kuwa lahaja rasmi ya Kiswahili walipoitafsiri agano jipya.

Ahsante.

Muro said...

Watu nafikiri hawajui nini maana ya Mfumo Kristo. Mfumo Kristo ni maaskofu na mapadri kushiriki katika mambo ya serikali hasa katika kupinga lile ambalo waislamu wanataka ambalo kwa miaka mingi limefanyika pia Viongozi wa nchi ambao ni wakristo mara nyingi wamekuwa wakifanya upendeleo kwa wasiokuwa waislamu. Pia ni Serikali kuyapa Makanisa mabilioni ya Shilingi ili yaweze kujiimarisha huku Waislamu na Taasisi zao wakiambulia patupu kingine ni ushiriki wa wazi wa Waaskofu katika siasa! Pia bwana Mbele Ungekisoma Kitabu Cha Dr. Sivalon ambacho ameelezea kuhusu Kanisa katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953-1985. Ndani ya kitabu hico Bwana Sivalon amejaribu kuweka wazi ni jinsi nyerere aliwapendelea wakristo tena wa kanisa katoliki katika nafasi za uongozi serikalini

Mbele said...

Ndugu Muro, shukrani kwa ujumbe wako, na jitihada yako ya kufafanua dhana hii na matumizi yake. Najisikia katika nafsi yangu kuwa unaongea kwa dhati, nami naheshimu hilo. Ni muhimu tuwe na moyo wa kusikiliza duku duku na machungu ya wenzetu, kwani hata dini zetu zinatutaka tuwe na moyo huo.

Sasa nami napenda kuelezea yangu. Naamini kabisa kuwa baadhi ya watu, wakiwemo baadhi ya hao tunaowaita viongozi wetu, wanaojitambulisha kuwa waKristo, wamekuwa na hizo kasumba zinazolalamikiwa, au upendeleo unaolalamikiwa.

Watu hao, kwa kuwakosea haki wengine, wamekuwa wakikiuka misingi ya dini. Hakuna dini inayoruhusu kuwavunjia haki wengine. Iwe ni dini ya uIslam, au uKristo.

Ndio maana nasema watu hao wanaolalamikiwa, hata kama ni mawaziri au maaskofu, iwapo walikuwa au wamekuwa wakihujumu haki za wengine, wamekuwa wakikiuka uKristo.

Ndio maana nasema, naona si haki kuuita mfumo wowote wa kifisadi au wa dhuluma kuwa ni mfumo Kristo. Mfumo huo tuupe jina linalostahili.

Watu wanapoingiza jina la Kristo katika kuuelezea mfumo huo, ndipo roho yangu inapouma, kwa sababu hakuna haki wala ukweli.

Ili nieleweke vizuri zaidi, hebu nitolee mfano wa upande wa pili, kwa wenzetu waIslam.

Baadhi ya watu wanaojitambulisha kama waIslam nao wamekuwa wahujumu wa haki za wengine. Kwa mfano mfumo ulioko katika baadhi ya hizi zinazoitwa nchi za kiIslam, unahujumu haki za waKristu, iwe ni katika uhuru wa kuabudu au kupata nafasi za uongozi.

Vile vile, kuna baadhi ya watu ambao wanajiita waIslam ambao ndio wenye kuendesha mifumo kama Al-Qaida.

Kwa maoni yangu, hao wote wanakiuka misingi ya uIslam. Itakuwa si haki kuita mfumo wao kuwa ni mfumo Islam. Kufanya hivyo itakuwa ni kuudhihaki uIslam, dini ambayo inatetea yale yale ya msingi ambayo dini zingine zinatetea.

Kuthibitisha kuwa dini hizi mbili zinatetea yale yale ya msingi, napendekeza watu wasome vitabu kama vile vya Karen Armstrong, ambaye anaheshimiwa na watu wa dini zote kwa umahiri wake wa kutafiti na kuelezea masuala yetu.

Kama naelelezea mabaya wanayofanya watu katika mfumo wao, siwezi kusema ni mfumo Islam, wala siwezi kusema ni mfumo Kristo.

Tutumie lugha inayoelezea ukweli wa mambo, kwani kama wahenga walivyosema, kucha Mungu si kilemba cheupe. Maadam watu wamevaa majoho ya kiaskofu au vilemba, si kwamba wanafuata dini zao. Maadam wanaitwa Hussein au John haitoshi. Dini zetu zinatutaka tuwe watendaji wa kweli wa yale yanayofundishwa katika dini.

Tuendelee kuelimishana.

Blogu ya Mussa said...

Mbele nimefurahi kuisoma hii makala, na kimsingi imenipatia binafsi mtazamo mbadala wa namna ya kuliangalia hili suala la "Mfumo-Kristo". Mtazamo mpya ambao nimeupata - ambao ni wa msingi sana - kuuhusisha duhalimu, ukandamizaji, uovu, unyonyaji na Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye na waislamu pia wanaamini ametoka kwa Mungu.

Nadhani wote walioibua hii dhana wanapaswa kuelewa kwamba WAMEPOTOKA, WAMEPOTOSHA UKWELI na wanapaswa KUUREKEBISHA HADHARANI UPOTOSHAJI HUU...

asante

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe wako, Blogu ya Mussa. Nafurahi umetembelea hiki kijiwe changu na kuandika maoni. Kila la heri.

Blogu ya Mussa said...

Ndio "Mratibu" wa Hapa Kwetu... nilikuwa katika pita-pita nikakutana na tafakari yako ambayo iliniongezea "perspective" nyingine katika kuliangalia hilo suala.... huwa ninakuwa na tafakari zangu pia - hususan za kisiasa - japo sasa nimeanza kuliangalia hili suala la udini kwa karibu ili na lenyewe niliweke kwenye "spot-light".... tafakari zangu hupatikana kwa: msbillegeya.blogspot.com (ambayo ndiyo "Blogu ya Mussa")

Mbele said...

Ndugu Blogu ya Musa, shukrani kwa ujumbe wako. Nilishaanza kupita kwenye blogu yako tangu pale nilipoona tu ujumbe wako. Ni kazi muhimu.

Ninapangia kuandika makala nyingine hapa kijiweni pangu dhidi ya hii dhana inayoitwa mfumo Kristo. Kijiwe changu hiki ni uwanja huru, na yeyote anakaribishwa kutoa maoni.

Anonymous said...

Ingawa umejaribu kuonyesha kuwa huegemei upande wowote lakini ukweli wenyewe ni kuwa umeegemea zaidi katika Ukristo, na nina hofu kuwa ni upande ambao tayari ulishajichagulia kabla ya kutoa mada yako hii, hivyo kuifanya mada nzima kukosa mvuto.
Mfano ilikuwaje uwalaumu Waislamu kwa kulitumia neno Kristo vibaya huku ukiwaacha watuhumiwa wakuu wa huu mfumo wa dhulma yaani Maaskofu ambao wanautumia Ukristo kulichafua jina la Yesu?!
Be fair!

Mbele said...

Anonymous wa Agosti 11, katika masuala haya ya dini, ni kazi kubwa sana kujitoa katika mfumo ambamo mtu ulilelewa. Ninafanya juhudi kujitoa, ili niweze kuangalia mambo bila upendeleo.

Sikatai kauli yako ya kunikosoa. Yawezekana kabisa kwamba bado nina safari ndefu. Lakini ninafanya juhudi ya dhati.

Sasa basi, ningependa kusikia msimamo wako, na dhamiri yako kuhusu masuala hayo, nione kama mwenzangu umepiga hatua kunizidi au kama unaishia tu kunichambua mimi bila kujichambua wewe mwenyewe pia.

Kama wewe ni mu-Islam, ningependa kuona umefanya juhudi gani kujikwamua na mfumo huo na unawaonaje watu ambao si wa-Islam. Unawakubali kama ni binadamu sawa na wa-Islam au vipi?

Unaponihamasisha mimi nitumie haki sawa, nakubaliana nawe. Lakini napenda kuona ushahidi kwako pia, kama unatumia haki sawa kwa wote.

Halafu, nami napenda kukuuliza kwa nini usijitambulishe kinaganaga, bali unajiita anonymous. Unaweza kujificha sisi wanadamu tusikufahamu. Lakini je, kama unamwanini Allah, una sababu gani ya kujificha? Unadhani hatakufichua siku ya kiyama?

Khalfan Abdallah Salim said...

Imejidhihirisha kuwa Dhana ya mfumo Kristo, haina tafsiri moja. Inahitaji kuchunguzwa kwa umakini.

Katika kufutilia matumizi na maneno ya waislamu ambao ndio waliokuja na dhana hii, naelewa kuwa maana yake ni kuwa ' Ni mfumo wa uendeshaji wa serikali unaolenga kuwafurahisha/kuwanuafaisha viongozi wa Kikristo na wakristo zaidi hata kama jambo hilo ni kwa hasara ya watu wa dini nyingine hususan Waislamu." Mfumo Kristo, ni mkato wa Mfumo wa Kikristo, katika nukta hii waislamu wana mifano mingi na ushahidi. Mmoja wapo ni maandishi ya Sivalon.

Nikiijadili dhana ya mfumo Kristo, waislamu wanamini kuwa huo si mfumo wa Yesu kama ambavyo Prof. Mbele anavyoona, kwa sababu Ukristo huu uliopo kwa Waislamu haukuasisiwa na Yesu, bali na Paul. Ushahidi wa hayo unapatikana katika kitabu 'Jesus, The prophet of Islam' by Attau Rahim nakadhalika.

Kwa mantiki hiyo, Mfumo Kristo na Yesu ni vitu viwili tofauti kwa Waislamu. Ndio maana waislamu, hawapendezewi na mfumo huo, japokuwa wanamuamini na kupendezwa na Yesu kama mtume wa mungu.

Je dhana hii inaukweli, kuwa eti serikali inaendeshwa kwa kuzingatia maslahi ya wakiristo na viongozi wake? Hili ni swali pana lenye majibu tofauti; wapo wanaona kuwa hilo ni jambo la uzushi, na wapo wanaona kuwa hivyo ndivyo. Maoni yangu ni kuwa, kuna tofauti kubwa baina ya waislamu na wakristo linapokuja suala na maamuzi ya serikali, sioni kama inamaana sana kusema ni mfumo kristo lakini ni kuwa viongozi wa kikristo wanaushawishi mkubwa juu ya maamuzi ya viongozi wengi wa serikali na taasisi zake na wanapata wayatakayo wakati waislamu hawana nafasi hiyo. Jambo hili waislamu haliwafurahishi.

Japokuwa TEC imetaka serikali ikanushe uwepo wa Mfumo kristo, lakini hadi leo hawajafanya hivyo? Kwa nini? Kinmya hicho ni kishindo.

Funzo: Katika kuendesha dola ni udhaifu mkubwa viongozi wa serikali kuonesha waziwazi kuwa inasikiliza upande mmoja na inashindwa kusimama kwenye ukweli bali kufuata mtazamo wa dini moja. Mfano, serikali inatambua uwepo wa taasisi tofauti za Kikristo nna kuheshimu lakini kwa waislamu inaitambua BAKWATA pekee, taasisi isiyo na uwakilishi kamilifu wa waislamu. Hii ni dosari.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa mchano wako. Ni mchango uliojaa hoja na fikra. Ni mfano wa kuigwa, kwa yeyote mwenye nia ya kuelimishana, kwa kuheshimiana.

Napenda kuongelea kipengele kimoja tu, kuhusu Yesu na Kristo.
Umesema kuwa wa-Islam hawaamini kuwa Mfumo Kristo ni mfumo wa Yesu, kwamba u-Kristo hukuasisiwa na Yesu bali Paulo.

Jawabu langu ni kwamba, wa-Islamu hao waache kuingilia Imani za wengine namna hiyo. Sio jukumu lao, na hawana wadhifa huo.

Sio kazi ya mu-Islam kuingilia mafundisho ya vitabu vitakatifu vya wa-Kristo na kubeza chochote kilichomo. Wasipokanywa, kesho na keshokutwa watainglia vitabu vitakatifu vya wa-Hindu, wa-Buddha, na kadhalika. Ni uchokozi.

Wa-Kristu wanaposema Kristu, wanamaanisha Yesu. Hajalishi kama aliyeanzisha jadi hiyo ni Paulo. Kwetu wa-Kristu tunaposema Kristu tunamaanisha Yesu, na tunaposema Yesu tunamaanisha Kristu. Tunaweza kutumia jina lolote kati ya hayo mawili, na mara nyingi tunatumia yote kwa mpigo, "Yesu Kristu."

Hao wa-Islamu unaowaongelea wajifunze kuheshimu Imani za dini za wengine.

Wakristu nasi tunapaswa kuheshimu Imani za dini za wengine. Itakuwa ni uchokozi kufanya vingine, kama hao wa-Islam unaowaongelea wanavyofanya uchokozi.

Wakristu wakianza uchokozi wa kuikosoa imani ya dini ya u-Islam unadhani kitatokea nini?

Waumini wa dini zote tuheshimiane. Muumini wa dini ya Hindu anaamini kuwa ng'ombe ni kiumbe mtakatifu. Mimi na mu-Islam na muumini wa dini yoyote tunapaswa kuheshimu imani yao hiyo, kama wanavyoiheshimu wao wenyewe.

Mimi m-Kristu naamini Yesu au Kristu ni mwana wa Mungu. Nafahamu kuwa mu-Islam haamini hivyo. Kilichopo ni kuheshimiana, kila mtu na imani yake.

Tukitaka kufanya uchokozi, ni rahisi sana kwa yeyote kuifukua Quran na kuona vitu vya kujengea uchokozi. Ni rahisi sana kuchunguza ibada za u-Islam na kuona vipengele vya kuvifanyia uchokozi.

Je, turuhusu hayo? Au tuheshimu imani za kila dini, kama wenye dini zao wanavyoheshimu?