Tuesday, March 15, 2011

Kichekesho: Eti Dr. Slaa Kama Savimbi!

KONA YA KARUGENDO

Chanzo: Raia Mwema

KICHEKESHO: ETI DR. SLAA KAMA SAVIMBI!

Watwambie ni kwa lipi wanafanana?
KAWAIDA ya mfa maji haishi kutapatapata, na katika hali hiyo ya kutapatapa anafanya mambo mengi na yasiyokuwa ya kawaida. Lengo zima likiwa ni kuyaokoa maisha yake.

Mtu anayetapatapa anaweza kuropoka na wakati mwingine kuupotosha umma. CCM ni kama mfa maji; wanatapatapa, wameanza kuropoka na kupotosha. Eti Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa ni kama Savimbi wa Angola. Kwa lipi?

Mbali na kwamba Savimbi alikuwa binadamu, na Dk.Slaa ni binadamu, Savimbi alikuwa Mwafrika na Dk. Slaa ni Mwafrika; hawana kingine cha kufanana! Savimbi alikuwa mwanajeshi, alipigana msituni zaidi ya miaka 20!

Aliendesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe; watu wengi walikufa. Wengine walipata ulemavu wa kudumu kutokana na vita alivyoviendesha Savimbi, na wengine waliikimbia nchi yao.

Savimbi alipora raslimali za nchi yake ili kuendesha vita hiyo iliyokuwa ndefu kiasi chake. Hadi leo hii wanahistoria wana kazi kubwa ya kutafiti na kuandika juu ya nia ya Savimbi ya kuendesha vita miaka 20 bila kuchoka wala kukata tamaa. Ni lazima alikuwa na lengo; nachelea kusema ni “uchu wa madaraka”; maana hata wale wasioingia msituni wana “uchu wa madaraka” kwa kutumia njia nyingine ambazo pia ni mbaya.

Kuvuruga uchaguzi kama ilivyotokea Kenya na Ivory Coast, ni mbaya zaidi ya kuingia msituni. Kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa kutumia nguvu za dola kama ilivyotokea kule Karagwe, ni mbaya; maana watu wanapoteza imani na zoezi zima la uchaguzi na labda ndo maana idadi ya wapiga kura katika nchi za Afrika inapungua kila mwaka.

Uchaguzi unakuwa hauna maana yoyote kama Tume ya Uchaguzi inaweza kutangaza jinsi inavyojisikia bila kufuata ukweli wa kura zilizopigwa. Watu wengi wanaamini Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010 Rais Kikwete angemshinda Dk. Slaa kwa kura chache za kuchakachua kiasi cha CCM kushindwa kuunda serikali bila kushirikiana na CHADEMA.

Hivyo kuna watu wenye uchu wa madaraka; hawaingii msituni – wanapambana kwa kuvuruga taratibu na kwenda kinyume na sheria; huku wakitumia vyombo vya dola kuwalinda.

CCM ilivuruga Uchaguzi Mkuu. Leo hii CCM inapiga kelele kwamba CHADEMA wanataka kuleta vurugu! Huwezi kuvuruga uchaguzi wa kidemokrasia ukategemea utulivu. Wale wote walioshiriki kuchakachua uchaguzi na kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa, baadhi si waaminifu kwa chama chao. Walifanya hivyo kupata fedha, na baadaye walivujisha habari za kuchakachua upande wa pili.

Watu makini ni lazima watahoji, ni lazima watafuatilia na kuhakikisha haki inatendeka. Harakati za kutafuta haki zisichanganywe na vurugu. CHADEMA wanajua CCM ilichakachua uchaguzi, wanajua ufisadi wote unaoendelea kwenye Serikali ya CCM – hayo ndo mapambano yao, na wala si vurugu wala vita.

Ikitokea watu wakahoji masuala hayo, utakuwa si uchochezi; bali ni ukweli wa wazi; maana yanayotendeka Watanzania wanaona na kushuhudia. Kila kitu kina wakati wake. Wananchi wakifikishwa mahali pa kuchoka na kukata tamaa, hakuna risasi wala mzinga utakaowanyamazisha. Natuombe Mungu nchi isifikishwe huko.

Kumlinganisha Savimbi na Dk. Slaa kama alivyofanya kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM katika mkutano wake na waandishi wa habari, ni kuropoka. Ni kupotosha na kumkosea haki mwanaharakati huyu shupavu anayepambana kwa nguvu ya hoja.

Wanasiasa wana maneno mengi; kuna kutambiana, kuna majivuno, kuna kutukanana, kuna kupotosha ukweli kwa lengo la kutaka watu wasahau yale yaliyo uwanjani – lakini maneno ya wanasiasa yanapovuka mpaka kiasi cha kumdhalilisha mtu ni lazima kuingilia kati.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii, viongozi wa dini, wanaharakati, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wasomi, ni lazima kuingilia kati na kuweka mambo sawa. Mwalimu Nyerere alitufundisha kwamba mtu anaweza kumvumilia kichaa; lakini kichaa huyo akizidi mipaka, ni lazima afungwe kamba.

Kumfananisha Dk. Slaa na Savimbi ni kuropoka kunakoelekea kwenye ukichaa cha kufungwa kamba! Savimbi alipambana msituni na kusababisha uhai wa watu wengi kupotea. Dk. Slaa yeye alipambana Bungeni, na sasa anapambana majukwaani!

Wakati Savimbi alitumia mtutu wa bunduki, Dk. Slaa anatumia nguvu ya hoja. Yeye anasema hata mende hajafa katika harakati za CHADEMA! Hakika huwezi kuwafananisha watu hawa wawili.

Savimbi aliwalazimisha vijana kuingia msituni – waliokataa waliuawa. Hatujamsikia Dk. Slaa akiwalazimisha vijana kujiunga na chama chake na wanaokataa kupoteza maisha yao. Vijana wanajiunga na CHADEMA kwa kuvutiwa na sera za chama hicho, na hasa harakati za kupambana na ufisadi. Hivyo kumlinganisha Dk. Slaa na Savimbi ni kuropoka.

Savimbi alitumia mtutu wa bunduki kuyalinda machimbo ya madini; si kwa faida na ustawi wa watu wa Angola; bali kutumia madini hayo kununulia silaha za kupambana na kulinda himaya yake. Madini ya Savimbi yaliwanufaisha watu wa nje; wawekezaje wa nje kuliko yalivyowanufaisha watu wa Angola.

Hatujasikia Dk. Slaa na CHADEMA yake kuwa wanamiliki mgodi wowote, hatujasikia kuwa wana silaha za moto zaidi ya hoja na maandamano. Katiba yetu inaruhusu maandamano na haki ya mtu kujieleza na kusikilizwa. Tunachokisikia ni mwanga wanaoutoa kwa wananchi juu ya ufisadi unaoendelea kwenye taifa letu - ufisadi ambao umeendekezwa na chama tawala CCM.

Dk. Slaa amekuwa mstari wa mbele kupigia kelele kashfa zote kubwa za EPA, Richmond na nyingine zote hadi ufisadi ndani ya halmashauri za wilaya.

Wanataka tufikiri kwamba Dk. Slaa anapenda vita kama Savimbi? Ni vita ipi ameianzisha Dk.Slaa? Labda vita dhidi ya ufisadi ambayo anaipigana kwa hoja na ukweli na si kwa mtutu wa bunduki.

Yaliyotokea Arusha ni kazi ya CCM. Kama taratibu za kumchagua meya wa Arusha, zingefuatwa – hakuna damu ingemwagika Arusha. CCM wanataka wakikosea taratibu na kwenda kinyume na sheria, watu wakae kimya kwa vile wao ni chama tawala? Enzi hizo zimepita!

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kama Tanzania tungekuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, CHADEMA ingeweza kujizolea wabunge wa kutosha kiasi cha kuizua CCM kuunda Serikali kwenye uchaguzi wa 2010.

Tulishuhudia wenyewe jinsi bunduki na mabomu ya machozi yalivyotumika kutangaza ushindi bandia wa mbunge wa Karagwe. Na kule Shinyanga jinsi mbunge wa CCM alivyoshinda kwa kura moja. Mkurugenzi wa Halmashauri alijificha baada ya kutangaza uongo.

Tuliambiwa walijiandikisha watu milioni 20 kupiga kura, lakini waliojitokeza kupiga kura ni milioni 8 tu! Kuna tetesi kwamba shahada nyingi ziliuzwa ili watu wasijitokeze kwa wingi kuvipigia kura vyama ya upinzani.

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete ametutangazia hali ya hatari kwamba CHADEMA wanataka kuipindua serikali yake. Mwenye akili za kutosha alielewa alichokuwa akilenga. Na sasa wapambe wake wanaingiza mpya ya kwamba Dk. Slaa ni kama Savimbi! Maana yake nini?

Maana yake akamatwe na kuwekwa ndani kwa kulinda usalama wa taifa? Maana yake ni nini? Kwamba huyu ni mtu wa hatari kama alivyokuwa Savimbi? Maana yake ni nini? Kwamba hata jumuiya ya kimataifa imuweke kwenye orodha ya watu hatari duniani?

Tumesikia msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa akitishia kukifuta CHADEMA. Ukichunguza utaona kuwa kinachoiponza CHADEMA ni kupambana na ufisadi; hivyo kama hakitaki kufutwa, basi, kiiache vita hiyo.

Kwa nini CHADEMA washinikizwe kuiacha vita hiyo?? Kwani sisi tunaupenda ufisadi? Kwa nini sisi tunamwona anayepora raslimali za nchi na kujiwekea vijisenti nchi za nje ndo mwanaume wa shoka? Mtu anayenunua shahada zetu wakati wa uchaguzi ndiye mwanasiasa bora? Kwani sisi tumezoea mikataba mibovu? Hatutaki umeme? Hatutaki barabara nzuri? Hatutaki maji?

Kwa taarifa ya wale wanaojifanya kutouona ukweli, ni kwamba hata CHADEMA ikifutwa na Dk. Slaa kuwekwa ndani, miti na mawe yatasimama na kuandamana! Kama Rais wa nchi anasimama na kusema sukari iuzwe si juu ya Shilingi 1,700 na leo hii sukari inauzwa Shilingi 2,000 hadi 2,300, unategemea nini? Wananchi wanaona kabisa kwamba Rais wao hana nia ya kweli kupunguza bei ya sukari. Je ni kweli Rais wa nchi hana uwezo wa kupunguza bei ya sukari? Rais ana vyombo vyote vya dola, ashindweje kupunguza bei ya sukari?

Rais anasema anapambana na ufisadi wakati mafisadi papa bado tunawaona mitaani wakitanua na kutembea vifua mbele. Inakuwaje Rais mwenye nguvu zote za dola na katiba yetu bado inampatia Rais nguvu kubwa, ashindwe kupambana na mafisadi hawa? Ni kweli anashindwa kupambana nao?

Je usalama wa taifa hawana habari za kutosha juu ya mafisadi hao? Ni kushindwa kupambana nao au ni kucheza siasa na kutaka kuwalinda maswahiba wao?

Sasa hivi mafuta yanapanda, umeme umepanda na kila kitu kitapanda – unga utapanda; maana mashine za kusaga zinatumia ama umeme au mafuta. Unga ukipanda, hakuna haja ya kumtafuta mchawi. Watu watajitokeza na kulalamika na pengine kuandamana kwa amani.

Kama Raisi Kikwete angekuwa na washauri wazuri wangemwambia kwamba badala ya kuiogopa CHADEMA, awaogope wananchi; maana hao ndiyo wenye uwezo wa kumwondoa madarakani kikatiba.

Watu wanaojitokeza kwa wingi kwenye maandamano ya CHADEMA si wanachama wa CHADEMA. Maandamano na migomo inayoendelea vyuoni si wanachama wa CHADEMA. Maandamano na migomo inayoendelea kazini si wanachama wa CHADEMA.
Inawezekana CHADEMA ina wanachama na washabiki wake, lakini si wengi kiasi cha wale tunaowaona kwenye maandamano. Tunachokishuhudia kwenye maandamano haya ni wananchi waliochoshwa na ugumu wa maisha. Wananchi wamechoshwa na ubabaishaji wa serikali. Wamechoshwa na ahadi hewa.

Tuliambiwa tatizo la umeme itakuwa historia, sasa tunaingia gizani. Tuliambiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, sasa kila kitu kinapanda. Nauli inapanda, karo inapanda, sukari inapanda, mafuta yanapanda, bei za matibabu zinapanda na maisha yanaendelea kuwa magumu.

Maisha yakiwa magumu, utulivu na amani ni ndoto. Ni kweli Tanzania ni nchi ya mani na utulivu, na hali hii haiwezi kuondolewa na CHADEMA. Si kweli kwamba CHADEMA wanacheza mchezo mchafu ambao ni mauti kwetu. Amani na utulivu vitatoweka kwa sababu ya maisha kuendelea kuwa magumu na Serikali ya CCM kuendeleza ubabaishaji.

Amani na utulivu vitaondoka kwa sababu ya wale wenye “uchu wa madaraka”. Nani hao? Si wengine bali CCM. Wamekuwa madarakani zaidi ya miaka 40, wanataka kutawala Bunge zima, wanataka kuongoza halmashauri zote, wanataka kushika nafasi nyeti zote katika taifa letu. Uchu wa madaraka wa CCM ni mauti kwetu!

Mwenye macho haambiwi tazama. Tishio kubwa la usalama wa taifa letu si CHADEMA wala Dk. Slaa, bali ni CCM chenyewe na serikali yake.

1 comment:

Mbele said...

Napenda niwe mtoa maoni wa kwanza. Nimeipenda makala hii kwa kuwa inafikirisha. Kwa ujumla, hoja zake zinaweza kumzindua aliyelala usingizi.

Hata kama kuna kitu kimoja au viwili ambavyo naweza nikawa na mtazamo tofauti na wa mwandishi wa makala hii, napenda kusisitiza hitimisho lake kwamba tishio la usalama wa Taifa letu ni CCM.

Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa na wazo hilo hilo kuhusu CCM, kama nilivyowahi kuandika hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...