Friday, December 26, 2008

CCM: Ni chama cha Mapinduzi?

Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu.

CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya kuendeleza fikra na mwelekeo wa "Azimio la Arusha," "Mwongozo" na mengine yote niliyoyataja hapo juu, CCM ilitoa "Azimio la Zanzibar." Ingawa CCM haikutoa fursa iliyostahili kwa wananchi kuliangalia na kulijadili "Azimio la Zanzibar," habari zilizojitokeza ni kuwa Azimio hili lilikiuka yale yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha." Mwalimu Nyerere alilishutumu "Azimilo la Zanzibar" kwa msingi huo.

Kitu kimoja kilichokuja kufahamika wazi ni kuwa "Azimio la Zanzibar" lilibadilisha masharti ya uongozi yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo." Kwa mfano, "Azimio la Zanzibar" liliondoa miiko ya uongozi iliyokuwepo.

Baada ya CCM kuvunja misingi ya mapinduzi, kilichofuatia ni kuimarika kwa ubepari, matabaka, na ufisadi. Chini ya himaya ya CCM, "Azimio la Arusha" halisikiki, "Mwongozo" hausikiki, wala maandishi na hotuba zingine zilizofafanua maana ya mapinduzi hazisikiki. Inaonekana kuwa CCM ilikusudia tangu mwanzo kuwafanya watu wasahau hayo yote, ili iendelee na sera za kujenga ukoloni mamboleo nchini mwetu.

Inakuwaje basi CCM ijiite chama cha mapinduzi wakati inahujumu mapinduzi? Inakuwaje Watanzania hawahoji jambo hilo? Elimu ni ufunguo wa maisha; bila elimu kuna hatari ya kurubuniwa na kuburuzwa kama vipofu.

5 comments:

Bennet said...

Mi siijui siasa ila misemo kama KILIMO NI UTI WA MGONGO WA TAIFA na SIASA NI KILIMO ilisikika sana tangu zamani na hata sasa.

Kwa ninaovyoelewa mimi kilimo pamoja na ufugaji ni vitu vya kitaalam sana na vinahitaji uwekezaji wa pesa nyingi, hapa Tanzania wakulima tumezoeleka ni masikini na huwezi kuendesha kilimo cha kisasa bila pesa ya kutosha na mtaji.

China walipoamua kuendelea kama nchi enzi za Mao, walihakikisha kwamba watu wanashiba kwanza na wakaleta mapinduzi ya kilimo kwa kulima kwa kutumia mashine. hata ulaya mapinduzi ya viwanda yalifanikiwa baada ya kutokea mapinduzi ya kilimo.

Tatizo la Tanzania sera za kilimo na ufugaji zinaendeshwa kisiasa sana na si kitaalamu, ndio maana mabwana/mabibi shamba hawapatani na mabwana/mabibi mifugo, huu mgawanyiko uko kuanzia wizarani, vyuoni na mpaka field, matokeo yake ni kwamba tuna wizara mbili ya kilimo na ya mifugo na uvuvi. hii kitu haijawahi kutokea popote duniani kutenganisha hivi vitu viwili.

Mbele said...

Ni kweli kuwa Mwalimu Nyerere alitunga na kutumia sana hii dhana ya siasa ni kilimo. Sisi tuliokuwa tayari shuleni wakati wa Uhuru tulikuwa na fursa nzuri ya kufuatilia na kuelewa mkondo mzima wa fikra na siasa za Mwalimu Nyerere tangu wakati ule. Tulikuwa tunasikiliza wenyewe hotuba zake na huko mashuleni tulikuwa na fursa tele ya kusoma maandishi yake.

Kuifahamu dhana hii ya siasa ni kilimo, kama alivyokuwa anaitumia Mwalimu Nyerere ni muhimu kuiangalia katika mkabala wake mzima, inavyohusiana na sera zake kwa ujumla. Mwalimu alizingatia kuwa nchi yetu ni nchi iliyokuwa inategemea kilimo. Uti wa mgongo wa uchumi wetu ulikuwa ni kilimo. Asilimia kubwa ya wananchi wetu walikuwa ni wakulima.

Kutokana na hayo yote, Mwalimu alikuwa anatufundisha kuwa siasa itambue ukweli huo, na izingatie ukweli huo. Iwe inajihusisha na maslahi ya wakulima. Iwe inatafuta mbinu za kuboresha kilimo. Hapo ndipo ilipojengeka dhana na maana ya siasa ni kilimo.

Mwalimu alifahamu fika kuwa elimu ni msingi wa kilimo bora. Alitambua kuwa sayansi na tekinolojia ni msingi wa kuendeleza kilimo. Alitambua umuhimu wa kilimo cha kisasa. Na si kilimo tu, bali uvuvi, ufugaji, na kadhalika, alitaka vyote viwe vinaboreshwa. Ukiangalia fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu elimu, utaona kuwa alijumlisha hayo yote, pamoja na hayo uliyotamka, ya kilimo au ufugaji wa kitaalam. Niliandika makala kwenye blogu hii, "Mwalimu Nyerere na Elimu," tarehe 15 Oktoba, 2008, ambamo nimegusia upana wa fikra za Mwalimu kuhusu elimu.

Sera ya Mwalimu ya Ujamaa Vijijini, ilifungamana na hayo yote. Mwalimu aliamini kuwa hii ndio njia ya kuleta maendeleo kwa wakulima, na vijijini kwa ujumla. Siasa ya vijiji vya ujamaa ililenga kuwaweka wananchi pamoja ili iwe rahisi kupata huduma kama shule, hospitali na kadhalika. Badala ya kuwa ni vishamba vidogo vidogo vidogo, yawepo mashamba makubwa, yenye kutumia zana za kisasa. Iwe rahisi kupeleka watalaam wa kilimo na mifugo. Mwalimu aliamini kabisa kuwa watu kukaa pamoja kungerahisisha mambo yote hayo na kuleta maendeleo.

Aliamini kuwa kuboresha kilimo kwa kutumia njia za kisasa kungeleta mafanikio vijijini kiasi cha kuzuia mkondo wa watu kuhamia mijini. Mwalimu alitaka huduma zinazopatikana mjini ziwepo vijijini pia. Leo, kwa vile tumepuuzia masuala hayo, watu wanahama vijijini na kukimbilia mijini. Kwa kiasi kikubwa haya ni matokeo ya kutofuata sera za Mwalimu Nyerere ambazo nguzo yake moja muhimu ni hii ya siasa ni kilimo.

Tatizo la viongozi wetu wengine ni kuwa ni wazembe. Wakati Mwalimu alikuwa anatumia juhudi kubwa kutafakari masuala na kuyaeleza kwa wananchi, hao wengine sana sana walikuwa wanafanya ukasuku.

Mwalimu Nyerere alipokaribia kung'atuka kwenye wadhifa wa mwenyekiti wa CCM, alizunguka nchi nzima kukagua kile kilichoitwa uhai wa chama hicho. Alijionea mwenyewe hali halisi ya huu uzembe. Kuna wakati, katika ziara yake hiyo, Mwalimu Nyerere alisema kuwa kuna watu ndani ya CCM ambao hata mtihani juu ya "Azimio la Arusha" hawawezi kupasi. Mwalimu alisema hivyo, na usemi wake uliripotiwa katika vyombo vya habari.

Kwa hivi, utaona kwamba kazi kubwa tunayo.

Mayenga Mabula Mbuzah said...

Miaka ikielekea tisa [9] sasa tangia Mwl Mbele, J uandike kuhoji huu 'umapinduzi' wa CCM kwa zama hizi unahalalishwa na nini, nikiri na mimi kusema kwamba CCM hii si ile ya tuliyoiasisi mwaka 1977!

CCM ya leo imetekwa na kijikundi cha Makada "wapiga-dili", wakiukuwadi utajiri wa raslimali wa sisi sote kwa "vibaka-wawekezaji", wanatutengenezea MIKATABA, Watendaji wetu wakiisaini hata ya bila kusoma vipengele cha MIKATABA hiyo, ili mradi 10% yao imeingizwa kwenye akaunti!

Itakumbukwa naye Mwenyekiti wa CCM katika Serikali ya Awamu III hakubaki nyuma naye akaimilikishia Kampuni yake na mkewe: AnBen Limited mgodi wa umma: KIWIRA COAL MINES kwa bro aliyojipangia na bila ya kujishindanisha na Wazabuni wengine!

Na katika kipindi cha Utawala wake, Makada waandamizi: Yusuf Makamba [wakati huo Katibu Mkuu wa CCM] na Rostam Aziz [Mwema Hazina wa CCM] na Mkurugenzi wa Sera za Uchumi wa Benki Kuu Bwana Peter Mayunga Noni wakapiga mabilioni toka akaunti za EPA pale BoT, ikisemwa, kwa baraka za Ikulu!

Kwa Nyerere yangelitokea matendo maovu sampli hiyo?

Mwalimu Mbele, J sie katika ACT Wazalendo bado tunalithamini Azimio la Arusha na ndiyo sababu kila Kiongozi ndani ya Chama chetu ni lazima atangaze Mali, Biashara na Madeni yake na vyanzo vyake!

Na ndiyo sababu waliotemwa na CCM hawakupata fursa ya kujichomeka kwetu!

Mbele said...

Mkuu Mayenga Mabula Mbuzah

Shukrani kwa mchango wako. Hii blogu yangu ni ukumbi huru wa watu kutoa mawazo na hoja zao. Ninauthamini sana mchango wako. Hapa kwangu, hoja hujibiwa kwa hoja, si kwa vitisho na mabomu ya machozi. Ni lazima tuonyeshe kuwa ni watu tunaothamini mijadala na hoja, ambayo ni chachu ya elimu.

Mimi ingawa si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ni mfuatiliaji wa siasa za Tanzania, kuanzia mikwamo ya CCM hadi misimamo ya wapinzani kama vile UKAWA na ACT Wazalendo. Nimekuwa nikifuatilia mipango ya ACT Wazalendo ya kufanya kumbukumbu kubwa ya "Azimio la Arusha" mjini Arusha. Ninawaheshimu kwa hilo, kwani hii ni sehemu ya mikakati ya kielimu ninayoipigania kwa ajili ya watoto na vijana wetu.

geoffnghumba2010@gmail.com said...

Nimeipenda Blogu yako Mwalimu Mbele.

Sijui kama nitakuwa ndani ya mukhtadha wa mada yenyewe kama nami nitasema haya yafuatayo.

Wakati wa wimbi la watu kutaka kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, Serikali ya Mwalimu iliamua kupitisha doroso lililoitwa 'White paper', lililohoji kwa kila liliyempitia kama alikuwa anakubaliana na mfumo wa Vyama Vingi au alikuwa anapinga.

Ilidaiwa kuwa ni asilimia 20% tu ya idadi ya waliopitiwa na doroso hilo, ndio walipendelea mfumo wa Vyama vingi kurejeshwa, huku wale asilimia 80% wakipendelea mfumo wa Chama kimoja uendelee!

Nilimsikia mwenyewe Mwalimu akishawishi kuwa, pamoja na ukweli kwamba asilimia kubwa ilipendelea mfumo wa chama kimoja uendelee, lakini alishauri wachache wale nao ilikuwa vema wasikilizwe.

Hivyo Wachache wale 20% wakasikilizwa kwa ushawishi wa Nyerere, na Nchi ya Tanzania ikarejea rasmi kwenye mfumo wa Vyama vingi.

Hata hivyo, pamoja na ushawishi huo wa Nyerere wa kuwapatia wachache walichokiomba, alitoa angalizo kwa Wananchi wote wa Tanzania kwamba, "Ninachokifahamu mimi kwa muda wote nilikuwa kiongozi wa Taifa hili, Watanzania wangu hawajui mambo ya Siasa na propaganda zake. Wao wanachojua ni hali bora ya maisha yao!"

Ndipo Vyama vyote vilivyoandikishwa, vilitakiwa kuwasilisha Katiba zao kwa Msajili wa Vyama vya vya Siasa.

Na kwa maneno yake Mwalimu, alikiri kuvutiwa na Katiba na Sera za CHADEMA.

Kwa ujumla, Vyama hivi tangu vipate usajili wa kudumu, vimekuwa vikiongeza wanachama wake kwa kasi ndogo sana, hali kadhalika kwa Chama cha Mapinduzi chenyewe, licha ya ukweli kwamba chama hicho kiliacha lango wazi kwa kila aliyehitaji kujiunga badala ya kuanza kupitia katika madarasa ya itikadi, wanachama wapya walipatiwa kadi kama njugu, siku ile ile ya tamko.

Pamoja na urahisi huo wa kujiunga katika vyama vya Siasa, bado Tanzania inayokisiwa kuwa na idadi ya watu wazima si chini ya 35m, walioko kwenye Vyama vya siasa ni chini ya 18m, huku CCM kikijiaminisha kuhodhi wanachama 10m kati ya hao, Huku idadi ya 8m inayosalia ndiyo inayojumuisha idadi ya wanachama katika Vyama vingine vya Siasa.

Kwa takwimu hizo (si rasmi, ni kwa makisio yangu) zinathibitisha bayana kwamba Watanzania wangu hawajui mambo ya Siasa, na wanachohitaji ni Hali bora ya maisha.

Hivyo ni kazi kwetu wanasiasa kuweza kuyaona na kuyahoji hayo tunayoyahoji, ikiwa CCM bado kinayaendesha Mapinduzi katika dhana ya Nyerere, au kimeshaachana na Mapinduzi hayo au la. Wananchi kwa ujumla wao wanahitaji HALI BORA YA MAISHA bila kujali yataletwa na Mapinduzi ya CCM au watayapata kupitia kwa Uongozi wa Vyama vya Upinzani.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...