Wednesday, April 27, 2011

Maktaba ya Lushoto

Kila ninapokuwa Tanzania, najitahidi kutembelea taasisi za elimu kama vile shule na maktaba. Mwaka jana, wakati nipo mjini Lushoto, nilipata dukuduku ya kujua kama kuna maktaba hapo, na iko wapi. Nimeshaona maktaba za hata miji midogo kama Mbinga na Mbulu.

Niliulizia mitaani, na watoto wa shule ya msingi wakanionyesha maktaba ilipo. Hiyo ilikuwa ni tarehe 5 Agosti. Niliingia ndani nikaona vitabu vya aina aina, vya taaluma mbali mbali, kuanzia fasihi, hadi masuala ya jamii na maendeleo. Niliona hata vitabu viwili vitatu vya Karl Marx, Kwame Nkrumah, na Issa Shivji.

Ingawa maktaba hii haina vitabu maelfu na maelfu, nilipata hisia kuwa mtu anayeishi katika mji huu akiamua anaweza kujielimisha kiasi cha kueleweka kwa kusoma vitabu vilivyomo katika maktaba hii.

Niliongea na mama mhudumu wa maktaba. Alinieleza mazingira magumu ya maktaba hii, nami nilijionea mwenyewe. Niliona jinsi yanavyohitajika makabati bora, kwa mfano. Nilimwambia kuwa nami kama mwalimu naguswa na moyo wa kujitolea wa watu wa aina yake, kwani sote tuko katika kusukuma gurudumu la elimu kwa jamii. Alifurahi kusikia hivyo.

Jambo la msingi ni kuwa nawasifu walioanzisha maktaba hii, na wale wanaoiendesha. Changamoto iliyopo ni kwa jamii yetu kuboresha taasisi kama hii maktaba. Pesa tunazo. Tatizo ni vipaumbele. Tukiangalia bajeti ya ulabu, kwa mfano, kwa wiki, mwezi au mwaka, ni wazi kuwa tungeweza kuwa na maktaba nzuri katika kila mji.

5 comments:

Anonymous said...

Mara nyingi hujiuliza kuhusu elimu kwetu.Mfano mzuri ni hiyo maktaba ambayo hata bango halionekani au angalau kuwe na mvuto fulani ili kuwavutia wananchi na kuwa na shauku la kujifunza.Sasa sijui niseme labda serikali haina hamu ya wananchi kuelimika au wapo DISORGANISED kwa kutenga pesa za kusaidia maktaba ambazo iwajengee wananchi shauku la kujisomea.Au labda prof...unamawazo tofauti na mimi.Wewe unafahamu hapo ulipo na kuona maktaba zao zinavovutia.

Mbele said...

Asante mdau. Nimeandika sana kuhusu masuala haya, na lawama zangu huwa nazielekeza kwa serikali na kwa wananchi.

Uzembe wa serikali katika kutumia rasilimiali za nchi, au kutodhibiti hujuma, tunauelewa vizuri.

Uzembe wa wananchi ndio hatuuongelei pasavyo. Katika kila mji Tanzania utakuta baa nzuri, zenye viti, meza na makochi mazuri. Lakini unaweza kukuta karibu na hiyo baa kuna shule ambamo watoto wanakaa sakafuni na paa linavuja.

Wananchi hawaoni kabisa faida ya maktaba. Huwa nazungukia maktaba sehemu mbali mbali za nchi. Ukipita maktaba kuu ya Taifa pale Dar es Salaam, utawakuta watoto wa shule humo ndani.

Wakati huo huo kuna vijiwe hapo nje ambapo utawakuta watu wazima. Hawana habari kama humo maktabani kuna vitabu gani vipya. Ukipita maktaba ya mjini Tanga, ni hivyo hivyo, au Arusha, au Songea, na kwingineko.

Hiyo maktaba ya Lushoto iko bondeni sana, na nilivyoona mazingira yake, nilihisi kuwa wakati wa mvua panakuwa na mafuriko. Hali sio nzuri hata kidogo. Lakini pamoja na hivyo, kuna hivyo vitabu nilivyoviona. Nina hakika kuwa ukiwauliza watu mitaani Lushoto kama wanajua maktaba ilipo au kama wanaenda hapo kusoma, watabaki wanashangaa.

Ndivyo wananchi wa Tanzania walivyo. Nenda mji wowote halafu uwaulize baa maarufu ziko wapi. Watakufikisha. Ukiwaulizia maktaba, inaweza kuwa ni mtihani mgumu wa kuumiza kichwa.

Anonymous said...

Kuna maktaba karibu na kwako siku hizi pia. Itabidi utembelee Maguu utakaporudi tena.

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani kwa taarifa za Maguu. Nimekuwa nikifuatilia taarifa za maendeleo ya shughuli hizi za Maguu katika mtandao wa YouTube.

Kwenye mji wa Mbinga walianzisha maktaba miaka kadhaa iliyopita, na nafurahi kuwa niliwahi kuchangia vitabu. Orodha ya vitabu hivyo ninayo bado.

Kidogo kidogo, tutafika. Mimi mwenyewe nimekuwa nikipiga mahesabu ya kuanzisha kijimaktaba kijijini kwangu. Inawezekana, wala hakuna kipingamizi.

Maurus Mchimbi said...

Tumejenga Maktaba ya Jamii kijiji cha Matekela,kata ya Kambarage, wilaya ya Mbinga! Yaani ni pua na mdomo na kwako! Karibu utembelee siku moja!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...