Saturday, October 16, 2010

Maonesho ya Vitabu Minneapolis, Oktoba 16

Nimerejea jioni hii kutoka Minneapolis, kushiriki maonesho ya vitabu ambayo huandaliwa na jarida la Rain Taxi na kufanyika mara moja kwa mwaka.





Kama kawaida, nilipeleka vitabu vyangu. Nilikuwa nimelipia meza ndogo. Lakini hii ilitosha kwa vitabu tu, bila maandishi mengine. Kwa vile idadi ya vitabu vyangu si ile ile ya mwaka jana au mwaka juzi, siku zijazo itanilazimu kulipia meza kubwa ili niweze kuweka maandishi mengine pia.








Leo ninaleta hapa picha mbali mbali nilizopiga, kama mfano wa namna wa-Marekani wanavyojali suala la vitabu.








Kama nilivyosema siku zilizopita, wa-Marekani wanafurika kwenye maonesho ya vitabu. Wanafika tangu asubuhi, milango ya ukumbi inapofunguliwa. Na siku nzima watu wanakuwa wengi katika ukumbi, wakienda na kuja.







Wanafika watu wa kila rika: watoto, vijana, watu wazima, na waze, wanawake kwa wanaume.







Pamoja na hali ya uchumi wa Marekani kuwa mbaya miaka hii, watu wanavichambua vitabu na kuvinunua.







Wana dukuduku na hamu ya kusoma. Ukisikiliza maongezi yao, utawasikia wakiongelea sifa walizosikia kwa wenzao kuhusu kitabu hiki au kile. Au utawasikia wale waliosoma kitabu fulani wakiwaeleza wenzao na kuwahamasisha wanunue.



Mimi kama m-Tanzania ninashinda kwenye shughuli hizi nikiwa na masikitiko makubwa, kwani hali kama hii haiko Tanzania. Ninajua, kwa sababu ninashiriki maonesho ya vitabu kule, kama ninavyoripoti mara kwa mara katika blogu hii.






Ni wazi kuwa wa-Tanzania tumeshajichimbia kaburi katika dunia hii inayoendeshwa na elimu, ujuzi na maarifa. Tusijidanganye.







Kwa mtazamo wangu, dalili ya kuelimika ni kuwa na duku duku na hamu ya kudumu ya kujitafutia elimu. Shule inapaswa iwe ni chanzo tu na kichocheo cha duku duku na hamu hii ya kujitafutia elimu.






Kupata digirii, kwa mfano, si mwisho wa elimu, bali hatua moja au chachu katika safari ya kutafuta elimu. Hayo niliyaelezea pia katika mahojiano katika Kombolela Show.


Kama ninavyosema mara kwa mara, napenda sana kushirikia maonesho ya aina hii, kwani ni fursa ya kukutana na watu walio katika fani za uandishi, uchapishaji, uhariri na uuzaji wa vitabu. Kila mmoja wao ana jambo la kunichangamsha akili au kunipanua mawazo.




Kukutana na watu wanaotaka kununua vitabu ni jambo jingine linalonigusa. Wakati mwingi natumia kujibu maulizo ya watu wanaotaka kujua maandishi yangu yanahusu nini.



Watu wengi wanapoona kuwa natoka Afrika, wanapenda kuelezea vipengele vya maisha yao. Kama walishafika Tanzania au sehemu yoyote ya Afrika, wanaelezea. Kwa maana hiyo, kushiriki tamasha la vitabu ni kweli fursa ya kuonana na kufahamiana na watu wa aina mbali mbali.

4 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Natamani ningeshiriki. Japo watu wetu si wasomaji wa vitabu zaidi ya udaku, kuna haja ya kuendelea kuandika. Kuna siku watabadilika baada ya kugundua kuwa maisha huwa rahisi kwa wanaojisomea na kuandika. Kinachowazuzua kwa sasa ni kutokana kutawaliwa na mfumo wa kifisadi ambapo mtu ahitaji kufikiri wala kuchakarika kupata riziki. Mambo huenda yakibadilika. Hii ndiyo imani yangu. Waandishi tuandike kuibadili jamii na si kupata soko. Mie nimeandika vitabu viwili na sijapata wala senti. Sijutii hili. Najua kuna siku watu watalazimika kusoma kama walivyolazimika kuukubali utandawazi na utandawizi. Kusoma na kujisomea siyo suala la hiari huko tuendako bali kufa na kupona. Ngoja mifumo na serikali zinazowakingia kifua walioghushi hata shahada zipite uone. Big up ndugu MBELE endelea kusonga mbele wala usikwazwe na kutokuwa na wasomaji kwetu.

Mbele said...

Umenena. Sina la kuongeza. Nilitamani kuwa mwalimu tangu nilipokuwa mtoto mdogo, kabla ya kuanza shule. Kishapo nilikuja kuelewa hii dhana kuwa ualimu ni wito.

Tunatumia muda mwingi sana kujitafutia elimu, na kisha kuwagawia wengine yale tunayoyajua, iwe ni kwa mihadhara au kwa maandishi. Tunatumia muda mwingi sana kuandika.

Nikiangalia muda ninaotumia kwa shughuli hizi, sijui ni jamii ipi itakayoweza kunilipa, maana ni shughuli ya usiku na mchana, kila siku.

Umesema sawa, kuwa sisi tuandike, kuibadili jamii. Kwetu sisi walimu wa dhati, msimamo huu haubadiliki wala kutetereka.

Kuna kijitabu changu kimoja cha mwanzo mwanzo ambacho nilikichapisha pale Tanzania, halafu jamaa akaja na wazo kuwa nikirekebisha kwa namna fulani, atakipeleka kunakohusika ili kiingie mashuleni, na kwamba nitachuma hela sana.

Nilimsikiliza huku ndani ya moyo wangu nikisema laiti angenijua mimi ni nani. Siwezi kubadili kitabu nilichoandika kwa lengo la kuelimisha kikweli kweli, eti kwa ajili ya kujipatia mipesa.

Siwezi kuandika kitabu cha kuchumia pesa, wakati kitaaluma kingekuwa hakiniridhishi. Sizitaki hizo pesa, ingawa zingeniwezesha kupunguza shida za maisha. Siwezi kukiuka maadili ya taaluma na viwango vyake kwa ajili ya pesa.

Hapo ndipo tunapokubaliana. Tuukatae ufisadi muda wote.

Mbele said...

Luke Taylor wa Minnesota Public Radio, ambaye alinihoji wakati wa maonesho haya ya vitabu, ameniarifu sasa hivi kuwa ameandika makala kuhusu maonesho yale, hii hapa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ni makla mulua yenye kuelimisha na kujuza.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...