Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare. Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii.
Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare.
Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo.
Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nakala sahihi ya mswada ulivyoridhiwa na mwandishi. Wakati wa Shakespeare, hapakuwa na utaratibu huo. Watu walikuwa wananakili andiko walivyoweza, na tofauti mbali mbali zilijidhihirisha kutoka kwa mnukuzi hadi mwingine.
Kadhalika waigizaji wa tamthilia majukwaani walikuwa wanatamka, pengine bila kujitambua, maneno yaliyofanana sauti, ingawa maneno ya mwandishi yalikuwa tofauti. Hiyo nayo ni sababu ya waandishi kuandika maneno tofauti.
Kwa hali hiyo, ni busara kuwa na nakala tofauti za kitabu hiki cha tungo zote za Shakespeare. Hata mtu ukiwa na kitabu cha tamthilia mojawapo tu, ni busara kuwa na nakala zilizohaririwa na wahariri tofauti wa kitabu hicho.
Faida nyingine ni kwamba baadhi ya nakala hizi zina maelezo ya wahariri juu ya mambo mbali mbali, yakiwemo maana za maneno na semi. Maelezo haya ni msaada mkubwa kwetu, kwani ki-Ingereza cha wakati wa Shakespeare kina tofauti nyingi na kiIngereza cha leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment