Niko Dar es Salaam, kuanzia Machi 3, na kuanzia siku mbili zilizopita, kumekuwa na mgomo wa madaktari, kufuatia madai yao kuwa serikali haijatekeleza makubaliano yaliiyofikiwa wiki chache zilizopita. Nimesikiliza kauli za Waziri Mkuu Pinda pia.
Ninachoweza kusema, kwa ufupi kabisa ni kuwa serikali ya Tanzania imeamua kukiuka busara ya wahenga kwamba tusidharau wakunga na uzazi ungalipo. Ni jambo la ajabu na la kutisha kwa serikali au nchi kugombana na madaktari. Kwamba Tanzania imefikia hapo ni dalili tosha za kutowepo busara za kiuongozi.
Madai ya madaktari, tangu mwanzo nayaafiki. Madai hayo ni pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi mahospitalini, uwepo wa vifaa, madawa, na kadhalika. Vipato vya madaktari navyo ni duni sana. Tafsiri yangu ni kuwa madai ya madaktari hayahusu maslahi yao binafsi tu, bali maslahi ya wagonjwa. Tanzania, nchi yenye rasilimali nyingi, yenye serikali ambayo inafuja mali kwa namna mbali mbali, inaweza kabisa kutekeleza madai ya madaktari.
Nitoe mfano moja tu wa ufujaji unaofanywa na serikali. Wakati serikali hii ilipoanza kazi, Waziri Mkuu Pinda aliliambia Taifa kuwa alikuwa amenunuliwa gari la bei kubwa sana, na kwamba kutokana hilo, hakuwa tayari kulitumia. Binafsi najiuliza: je, waliofanya uamuzi wa kununua hilo gari waliwajibishwa? Na je, gari la fahari lililonunuliwa ni hilo moja tu? Na je, kwa nini serikali ya Tanzania isipige marufuku magari ya fahari? Nasikia Rwanda walishapiga marufuku magari hayo. Kwa nini serikali ya Tanzania isifanye hivyo hivyo. Huo ni mfano moja tu, lakini ningeweza kuandika zaidi.
Sote tunakubaliana na kuwa kazi ya udaktari ni nyeti kabisa, kwa maana kwamba inahusu uhai wa binadamu moja kwa moja. Hilo suala la unyeti wa shughuli za madaktari lilisisitizwa na Waziri Mkuu Pinda katika hotuba yake wiki hii. Hakuna ubishi hapo. Sasa basi inabidi tukubaliane kuwa ni muhimu maslahi ya madaktari ni lazima yawekwe mbele kuliko ilivyo sasa. Ni hatari kwa maisha yetu iwapo madaktari wako kazini huku wakihofia kodi ya umeme watalipaje au watoto wao watakula nini. Tufanye kila liwezekanalo ili daktari akiwa kazini, awe pale kwa roho moja, akitoa tiba.
Madaktari wamesema hawana imani na viongozi wawili wa wizara ya afya. Inashangaza kuona serikali ikipuuzia jambo hilo na kuliendesha kiubabe. Busara za kiuongozi zinaeleza kuwa morali ya watu ni jambo muhimu sana. Morali ya madaktari ingekuwa juu iwapo wangetekelezewa dai lao kuhusu kuondolewa kwa viongozi hao wa wizara.
Lakini serikali imeamua kuwakingia kifua watu wawili na hivi kudidimiza morali ya jumuia kubwa ya madaktari. Halafu, serikali inajaribu kujenga hoja kuwa madaktari hawathamini uhai wa wananchi. Hoja hii imenishangaza.
Kama kuna ambaye hathamini uhai wa wa-Tanzania ni serikali tuliyo nayo. Serikali hii imeacha wazi mianya ya rasilimali ya Taifa kuporwa, wakati rasilimali hii ingeweza kutumiwa kuokoa maisha ya watu mahospitalini kwa kununulia madawa na vifaa mbali mbali. Serikali inayofumbia macho ufisadi ndio mhujumu wa maisha ya wa-Tanzania. Hainiingii akilini kuwa serikali hii inajaribu kujifanya ndiyo ina uchungu na maisha ya wa-Tanzania.
Mambo mengine ya serikali hii yanachekesha. Pakitokea maandamano, kuanzia chuo kikuu hadi Songea, tunashuhudia jinsi polisi wanavyorusha mabomu na hata risasi. Hakuna siku tukasikia kuwa kuna upungufu wa mabomu na risasi. Serikali imewekeza katika mabomu ya kuwalipulia wananchi, wakati huduma za hospitali zina walakini. Ni ajabu na kweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment