Thursday, March 29, 2012

Profesa Anapotinga Baa

Kwa siku hizi ambazo nimekuwepo hapa Dar, nimekuwa nikitinga kwenye baa hii au ile, ingawa sinywi ulabu. Watu wengi hapa nchini wananifahamu kutokana na kuona taarifa zangu mtandaoni. Huko kwenye baa, wengine huambiwa na wenzao mimi ni nani.

Wadau wakishagundua kuwa mimi ni profesa, hupenda kuanzisha mijadala nami. Wanadadisi mambo mengi, yakiwemo yale ya Marekani. Nimejikuta nikilumbana na wadau wa aina aina, wakiwemo wale ambao wamelewa chakari. Ni burudani ya aina yake kuwashuhudia hao waliolewa chakari wakijibidisha kutema umombo ili ijulikane kuwa nao wamo.

Sasa, katika hizi siku zijazo, nataka kuanza kuwaambia hao marafiki zangu kuwa kwa kweli, mahali ambapo profesa anapaswa kuwepo ni maktabani, darasani, au sehemu ya utafiti wake. Anapaswa kuwa anatumia muda wake mwingi katika kusoma na kuandika makala na vitabu, si kukaa kaunta akitema cheche kwa wadau wa konyagi, Tusker, na Kilimanjaro za baridi.

Wadau kwenye baa hawatambui hilo. Hatari mojawapo ni kuwa watu wanadhani mtu kwa vile alishasoma sana na kumaliza shahada za vyuo, basi ameelimika kabisa na hahitaji wala kuwajibika zaidi ya pale. Wanaamini kuwa mtu aliyefikia cheo cha uprofesa amemaliza. Kwa hivyo hawaoni tatizo kuwa naye baa kila siku na kulumbana.

Kwa mtindo huu, Tanzania hatutafika. Tutashindwa kutoa mchango wa maana katika taaluma hapa ulimwenguni. Kiwango cha maprofesa kitaporomoka, kama hakijaporomoka tayari. Mimi mwenyewe, kwa siku chache hizi ambazo nimekuwa nikitinga baa badala ya kusoma vitabu na makala, najisikia kabisa kuwa nimedidimia kitaaluma kiasi fulani, kwa maana kwamba sijaandika lolote la maana kwa siku hizi kadhaa, wala sijasoma kitabu na makala katika taaluma yangu. Mihandara na malumbano yangu yote yamehamia baa. Nikiendelea namna hii kwa miezi au miaka, nitadidimia zaidi, ingawa bado wadau mitaani na kwenye baa wataendelea kuniona ni profesa maarufu. Hili ndilo tatizo la Tanzania. Kwa mtindo huu hatutafika kabisa.

Sio vibaya kwa profesa kuingia baa mara moja moja na kupata moja baridi. Lakini kukaa masaa humo baa, mara kwa mara, au kila siku, ni balaa tupu, wala tusidanganyane. Vile vile, kwa sisi tunaotafiti masuala ya jamii, baa panaweza kuwa sehemu moja muhimu ya kutafiti na kujifunza mengi. Ila, nadhani ili kufanikisha hilo, na kwa vile sisi ni waelimishaji, tunaopaswa kuwa mfano, tusiwe tunakata ulabu kama wadau wengine. Bia moja mbili sio mbaya.

11 comments:

Subi Nukta said...

Angalizo zuri hilo Prof. Mbele na kumbushio kwa wote. Shime tushikamane na elimu kuongeza ujuzi na maarifa ya kutusaidia kuishi vyema hapa duniani.

Wanywa ulabu waache ulabu uwalabue.

Anonymous said...

PROF NINGEKUOMBA UENDE PALE UDASA KAMA BADO KUPO UKAHUBIRI HAYA MAANA NI AIBU UKIENDA SEHEMU KAMA ILE KWA KWELI,MAANA HAPO NI SEHEMU YA ULABU YA WASOMI NA NAAM ULABU WAKATI MWENGINE HUMSHUSHA MTU HADHI YAKE.

Mbele said...

Da Subi, shukrani kwa ujumbe.

Anonymous, shukrani. Nawajibika kuelezea kuwa historia yangu ya ualimu ilianzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1976. Nilikuwa mwalimu pale hadi 1991.

Sasa basi, nami nilikuwa mteja mzuri wa UDASA Club. Ilikuwa kwamba kama mtu una pesa mfukoni, muda wa kukaa UDASA halikuwa tatizo, hata iwe masaa mengi. Kama faranga zilikubali, ilikuwa ni ulabu mtindo moja.

Lakini mwaka 1991 huo niliombwa kwenda kuanzisha na kufundisha masomo fulani kwenye chuo kimoja kule Marekani. Niko kule hadi sasa.

Tofauti ni kuwa pale nilipo hakuna utamaduni wa maprofesa kuwa baa namna hiyo. Kila mtu atakushangaa ukiwa wewe ni profesa wa kudumu ndani ya baa. Kila mmoja anachapa kazi ipasavyo, au anajibidisha kwa dhati kufanya hivyo. Hata kama kuna siku unajikuta una faranga za ziada, muda wa kukaa baa ni shida kupatikana. Nashukuru kuwepo mahali pa aina hiyo, kwani ni fursa ya kujifananisha na wengine, na kuona wapi nahitaji kujitahidi zaidi. Ni sawa na mwanariadha anavyohitaji ushindani mkal ili awe bora zaidi.

Hapa Tanzania hatushangai kabisa kumwona profesa aliyehamia baa. Tena, profesa ukifungua baa maarufu, ndio unaheshimika zaidi. Hata vigogo wa nchi watakuwa wanakata ulabu kwenye baa yako.

Anonymous said...

Hili angalizo limenigusa sana mzee Mbele. Nilipokuwa likizo huko nyumbani jioni moja nilitembelea pale SUASA (nadhani ni club ya wahadhiri wa SUA) pale Morogoro Hali ni hiyo hiyo! Kwa kweli inabidi watu wabadilike.

Anonymous said...

Wapendwa. Ni kwamba baada ya kukaa na kufanya kazi Magharibi imenidhihirikia kwamba mimi ni mgeni nyumbani Bongo. Utamaduni wa kazi, utamaduni wa kilaji kila siku, utamaduni wa sherehe nzito nzito, na hata utamaduni wa kusaidiana ni tofauti na ninavyofanya. Hata hivyo sidhani kama nimekuwa mtu wa magharibi kabisa. Sote tunapaswa kujichunguza.

Rama Msangi said...

heheheee....nicheke mie. Profesa, sisi wazalendo halisi huwa tuna misemo yetu siku hizi...."Kibongo bongo michongo na kila kitu ni bar"

Unknown said...

Mimi nashauri watu wa sosholojia wafanye utafiti kuhusu jambo hili la maprofesa kuhamia baa. Lakini pia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kunapaswa kuwa na chombo cha ushauri nasaha kwa hao maprofesa. Tumeona mara kadhaa wakiachwa wanakunywa weee hadi wanajifia. Mifano ipo. Tujue kuwa huo ni ugonjwa unaohitaji dawa. Labda kukemea ni hatua mojawapo tu, lakini sidhani kwamba kunalitibu gonjwa hili. Tujadiliane.

MICHUZI BLOG said...

Hahahahaa profesa kweli unafaidi vekesheni yako, japo umepatwa na tatizo la kiafya. Kila la heri nakutafuta leo, sijui nikukute baa ipi mida ya jioni, japo nami sipigi ulabu...

bibi Alesha said...

Kaka Joseph,

Natamani ningekuwa bongo twende sote nisikie michango ya wadau wa baa. Je umesikiliza hotuba ya mheshimiwa Lusinde kwenye kampein kuko Armeru?? Ni hit kwenye utube kwa waswahili. No comment!!Get well soon my brother.

Anonymous said...

Prof. njoo Morogoro ujionee maprofesa wenzio wa Sokoine University of Agriculture walivyowekeza kwenye ujenzi wa Baa na Guest Houses, kila mmoja kama hamiliki baa basi anamiliki guest house, badala ya kuwekeza kwenye ZOO au mashamba ya umwagiliaji ili Wakulima na Wafugaji waje kujifunza kwao,wao mapesa yao ya miradi waneona isiwe tabu wameamua huwekeza huko. kila wakisimama kwenye midahalo utawasikia kilimo kwanza sijui maneno hayo yanatoka kwenye mioyo yao au....... maana hatuwaelewi kabisa.

Mbele said...

Mahali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hapana utamaduni wa kujikosoa. Isipokuwa, jambo lolote likienda mrama nchini, waandishi wa habari wanakwenda pale kuulizia maoni ya wasomi. Lakini jamii ya wasomi yenyewe haina utamaduni wa kujikosoa namna hiyo, ingawa ina matatizo ya msingi na ya muda mrefu, yakiwemo haya ya watu kuhamia baa.

Miaka niliyosoma pale, kuanzia 1973 na kufundisha kuanzia 1976, angalau tulikuwa na jadi ya kufuata msimamo wa ki-Marx wa "criticism and self-criticism" yaani kuhoji, kukosoa, kujihoji na kujikosoa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...