Thursday, March 22, 2012

Nimeugua Dar es Salaam; Natibiwa Hapa Hapa, Sio India

Nimeugua Dar kuanzia siku chache zilizopita. Nimejikuta nikiwashwa hasa mikononi, miguuni, na mgongoni. Kwa siku mbili sikuweza kulala usiku. Katika kuulizia watu, nikaambiwa ni "allergy." Na mhudumu mmoja kwenye duka la madawa maeneo ya Sinza aliniambia niende Magomeni, kwenye hospitali ya Dr. Ole.

Nilienda hapo. Wakati wa kuchukuliwa damu ili ipimwe, mpimaji alinipiga mchapo kuwa isije ikawa nimewekewa sumu ya unga. Akazidi kutonya, huku akijifanya ananyunyizia unga mezani, kuwa kaunga kidogo tu kanatosha. Nami nilijibu kuwa mtu huwezi kujua, kwani Bongo haina dogo. Tukawa tunacheka.

Ni kweli daktari alipochunguza ripoti ya upimaji amegundua nina "allergy," na akanielezea sababu zake. Pia alisema kuna bakteria katika damu. Aliniandikia sindano na vidonge vya aina mbali mbali. Alisema kuwa hiyo dozi itafuta kabisa hili tatizo. Nimedundwa sindano jana na vidonge nikaanza. Tayari nimeshaanza kujisikia nafuu. Naendelea vizuri kabisa.

Nimeleta habari hii binafsi kwa sababu maalum. Kwanza, mimi kama m-Tanzania nina imani na madaktari wetu. Ninafundisha Marekani, na ninapougua kule natibiwa kule. Ninapougua Tanzania natibiwa hapa. Tena, miaka yote ya maisha yangu, kabla sijaenda Marekani nilikuwa natibiwa hapa Tanzania, bila matatizo.

Sioni kama kuna tofauti kati ya madaktari wa Marekani na wa kwetu. Kilichopo tu ni kuwa madaktari wa kwetu wapewe mahitaji yanayopasika katika kumshughulikia mgonjwa. Na hilo ni jukumu la serikali, wala isijaribu kukwepa, kwani Tanzania si nchi maskini. Nakerwa ninapowasikia viongozi wa nchi hii wakidai kuwa sisi ni nchi maskini. Juzi hapo nimemsikia waziri kwenye kipindi cha televisheni akitoa huo upupu kwamba Tanzania ni nchi maskini.

Nawashangaa wa-Tanzania waoendelea kuwapigia kura mbumbumbu wa aina hiyo, wasio na upeo kiuongozi, hawana fikra za kuijengea jamii ari ya maendeleo, badala yake wana upeo wa kudumaza na kukatisha tamaa. Nawashauri wajifunze kutoka kwa Rais Obama, ambaye katika mazingira yoyote yale, hawakatishi tamaa raia wake, bali anawahakikishia kuwa Taifa litapambana na litashinda, litafanikiwa. Lakini viongozi wa kwetu, kila kukicha ni vilio kuwa sisi ni nchi maskini!

Uwezo wa kuimarisha hali ya mahospitali yetu tunao, tukizingatia rasilimali nyingi tulizo nazo katika nchi hii. Pia, magonjwa mengi tunayopata hayahitaji daktari bingwa. Yanatibiwa vizuri, iwe ni Marekani au Tanzania. Tena yako magonjwa ambayo ni ya nchi kama zetu, ambayo wataalam wake ni hao madaktari wentu. Mifano ni malaria. Usidhani kuwa ukipata malaria, ukimbilie Marekani. Unaweza ukafia kule, kwa sababu sio madaktari wengi wanaijua malaria na namna ya kupambana nayo kama wanavyojua madaktari wa nchi kama Bongo. Hao madaktari wetu wanasomea magonjwa ya hapa kwetu. Ninavyofahamu, wanapoenda kusomea Ulaya, utakuwa wanasomea "tropical medicine" ambayo ndio uwanja wa mapambano katika nchi kama yetu.

Madaktari wetu wana ujuzi wa hali ya juu, utawakuta wako katika nchi mbali mbali. Ninawafahmu baadhi ambao wako Marekani, katika hospitali mbali mbali, kama vile Mayo Clinic, ambayo ni maarufu sana duniani. Yaani inashangaza kuwa ukienda hizo hospitali, unawakuta madaktari wengi wa kutoka Afrika, yaani madaktari kama hao wanaonyanyasika Tanzania kwa sababu ya viongozi wetu kutokuwa na upeo upasao.

Kwa hiyo, serikali yetu inachopaswa kufanya ni kuwekeza katika huduma za mahospitali yetu hapa hapa nchini. Iweke vifaa na miundombinu, ili madaktari wetu waweze kutumia ujuzi wao ipasavyo. Wakipata vifaa na miundombinu, na wakilipwa ipasavyo, watafanya yale yale ambayo baadhi ya watu nchini wanayatafuta India au ughaibuni. Tunapowapeleka watu nje eti kuchekiwa afya, wakati hizi ni taaluma za madaktari wetu pia, au tunawapeleka watu kutibiwa ugonjwa kama niliopata mimi wiki hii, ambao madaktari wetu wanajua namna ya kuutibu, ni kuwadhalilisha madaktari wetu, na mimi sitalilazia damu suala hilo.

Miezi michache iliyopita, nilipata fursa ya kumsikiliza Daktari m-Marekani, Mark Jakobson, ambaye ni mwendeshaji wa hospitali ya Selian, Arusha. Alikuwa akitoa mhadhara Minnesota, kuhusu shughuli za hospitali hiyo. Siku moja, Insh'Allah, nitaelezea hotuba yake katika hii blogu yangu. Jambo mmoja ninalokumbuka ni jinsi alivyowapigia debe madaktari wa ki-Tanzania wanaofanya naye kazi. Anatamani tu angekuwa na uwezo wa kuwalipa vizuri zaidi, ili wasipate vishawishi vya kwenda sehemu zingine.

Makala hii nimeiandika pia kwa sababu juzi hapo niliandika makala kuhusu mgomo wa madaktari nikaishutumu serikali kwa kudiriki kugombana na madaktari. Kwa hivi, nimejichukulia fursa hii kuelezea zaidi hisia zangu. Kati ya mambo niliyosema ni kuwa kisaikolojia, daktari anapaswa awe kazini akiwa amefurahi na moyo mkunjufu.

Huyu jamaa aliyenipima damu alitoa mchapo na tukacheka. Muuguzi au daktari anapokuwa na moyo mkunjufu na ucheshi, anapokuwa hana msongo wa mawazo, ni baraka kwa wagonjwa. Watafiti wa masuala ya saikolojia ya wagonjwa na matibabu wanathibitisha hilo. Ndio maana niliishutumu serikali kwa kutotambua umuhimu wa kuwaridhisha madaktari.

8 comments:

Fadhy Mtanga said...

Pole sana Prof Mbele.

MICHUZI BLOG said...

Pole sana Prof na Mungu akuafu

Yasinta Ngonyani said...

Pole sana Prof. Na twashukuru unaendelea vizuri.

Yasinta Ngonyani said...

Oh! nimerudi tena nilisahau kuuliza waligundua ni allegi ya nini?

Anonymous said...

pole sana profesa ni hali ya joto la dar,unavosema hata sisi wananchi tumeshaona madaktari wetu kama hawawezi kutokana na serikali yetu kuwadharau lakini wanaweza sana tena sana

Mbele said...

Dada Yasinta, kama tulivyo waSwahili, sikufuatilia vizuri vipengele ambavyo daktari alikuwa anavisoma kwenye chati yake iliyotoka maabara. Ila, nilimpata aliponipa huo muhtasari, akitaja allergy na bakteria.

Si unajua tena, sisi waSwahili tunachotaka ni kujua tu kama nitadundwa sindano au nitapewa vidonge. Wewe mwenzetu kwa vile uko kwenye taaluma hii ungeweza kuokota mengi zaidi.

Kama unavyokumbuka, hizo tabia zetu waSwahili nimezielezea kwenye kile kitabu changu cha "Africans and Americans: Embacing Cultural Differences."

Ndugu Anonymous, ni kweli hao tunaowaita viongozi wetu ni tatizo kubwa. Hebu fikiria, hivi karibuni, daktari mmoja wa Muhimbili alipata tuzo ya kimataifa kwa utafiti wake. Alienda kuichukua Ulaya. Halafu nchi yetu haiamini kuwa tuna mabingwa hapa nchini.

Katika utafiti wa virusi vya ukimwi, kumekuwa na ushirikiano baina ya madaktari wa Muhimbili na wale wa Harvard Medical School kwa miaka zaidi ya ishirini. Kwenye mwaka 1990, nilitembelea pale Harvard nikawaona hao madaktari wetu waliokuwepo pale wakati ule.

Lakini sisi wenyewe hatuwaoni kama wana ujuzi wa aina hiyo. Inatisha.

Anonymous said...

Hivi jamani ni mm tu au na wenzangu hili jambo mmeligundua, kuwa huku ulaya mtu ni tabu sabna kuandikiwa kudungwa sindano hata kama utaumwa vipi, sanasana utatiwa drip kwa muda na kuendelezwa na dawa baada ya hapo, sasa ni kwa nini nyumbani wanapenda kutumia sindano sanahebu jamani nielimisheni

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Pole mwalimu;

Pona na urudi nyumbani salama...

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...