Sunday, March 25, 2012

Nimetua Safari Resort Dar es Salaam

Jana, Jumamosi, nilitua Safari Resort, eneo la Kimara, Dar es Salaam. Ilikuwa mchana, nami nilitamani kwenda tena mahali hapa, ambapo nilipapenda kuanzia miaka ya 1976, nilipoanza kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapo kushoto unaiona Safari Resort, ukiwa kwenye barabara iendayo Morogoro.






Hapo ndipo getini, palivyo siku hizi. Miaka ile, Safari Resort ilikuwa inavuma sana. Gwiji wa Muziki King Kikii alikuwa akiimba hapa na bendi yake,na kukonga nyoyo za wa-Tanzania kupita maelezo.








Sikwenda Safari Resort kuchapa ulabu. Wiki hii natumia dawa kutibu tatizo la afya lililonipata. Kwa hivi, sinywi bia kabisa. Nanywa maji tu. Hata hivyo, nimegundua kuwa kwenda sehemu za starehe kama hizo na kuishia kunywa maji haimaanishi kuwa unakaa hapa ukiwa na majonzi. Sio lazima ukienda mahali kama hapa upige ulabu hadi upotee njia, au uanzishe varangati ya kufa mtu, kama tufanyavyo wa-Tanzania. Maji yanatosha, na bado unafaidi kuangalia mazingira, kukutna na watu, kujikumbusha mambo kadha wa kadha ya zamani na kupiga picha.

Banda hili hapa kushoto linanikumbusha mbali. Mwaka juzi nilipata fursa ya kukaa kwenye banda hilo na Mheshimiwa Balozi Mstaafu Andrew Daraja, tukaongea kwa masaa manne, kuhusu masuala mbali mbali. Yeye tulifahamiana alipokuwa Balozi wetu Washington D.C. Wakati akiwa kule, alisoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kisha akanipigia simu ofisini kwangu, akionnyesha kufurahishwa na niliyoandika. Ni mtu makini, mwenye kuhamasisha wa-Tanzania wanaofanya mambo ya maana. Kwa mfano, msikilize Youtube, hapa. Balozi Daraja alinivutia kwa ufahamu wake wa mambo ya nchi hii na dunia, akaniacha hoi aliponukuu vifungu kutoka kwa Shakespeare. Kwangu mimi mwanafasihi, hii niliiona ni kali kabisa. Basi hizo ndizo kumbukumbu zilizonijia jana nilipokuwa naliangalia banda hili.

Watu wanaokaa Tanzania wanaweza wasielewe umuhimu wa blogu kuweka picha kama hizi ninazoweka hapa. Lakini wale wanaoishi ughaibuni, wanaguswa, kwani wako mbali. Mimi mwenyewe sikosi kungalia blogu kama ya Mjengwa, kwa jinsi inavyoleta picha kutoka sehemu mbali mbali hasa za Uswanzi za vijijini, pamoja na kule kunakovunjika jembe ukabaki mpini.

7 comments:

Rachel Siwa said...

Ahsante kwa kutuletea/kutukumbusha Safari Resort,Vipi kuhusu Bahama Mama bado ipo na jina ni lilelile?Uwe na wakati mwema Ndugu.

Yasinta Ngonyani said...

Picha nzuri na kumbukumbu nzuri sana. Ahsante sana ...Uwe wakati mzuri.. pamoja daima

Mbele said...

Asanteni kwa kunitembelea hapa kijiweni pangu. Dada Rachel, nimeanza kufuatilia suala la Bahama Mama. Nilimwuliza dada moja, akasema alisikia iko katika kukarabatiwa. Napangia kwenda kesho au keshokutwa, nikajionee. Kama iko bado inadunda, nitaleta picha.

Rachel Siwa said...

Ahsante sana Ndugu yangu,Mungu akubariki sana na uwe na wakati mwema.

Anonymous said...

rachel bahama mama ipo lakini sio kama zamani....

Rachel Siwa said...

Ahsante Anonymous kwa kunifahamisha.

Mbele said...

Sisi tulipofika pale kwenye kituo cha mafuta, tuliona Bahama Mama imezuiwa na ukuta wa mabati. Hatukuwa tena na wazo la kujaribu kutafuta kama kuna sehemu ya kuingilia, tukaamini inakarabatiwa.

Ningekuwa radhi kwenda tena kuangalia haya mabati yanafanya nini pale hata watu tudhani pamefungwa. Hali ilivyo ni kwamba najiandaa kwa safari ya kurejea ughaibuni wikiendi hii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...