Saturday, March 7, 2009

Mishahara Haitoshi

Katika nchi yetu ya Tanzania, watu wanalalamika muda wote kuwa mishahara haitoshi. Gharama ya maisha ni kubwa kuliko mishahara. Hata kwa kuzingatia mahitaji muhimu tu, watu wengi wana haki ya kusema kuwa mishahara haitoshi.

Malalamiko ya mishahara kuwa haitoshi yanasikika duniani kote. Hapa Marekani, shida kubwa inayowakabili watu ni kulipa bili na madeni mbali mbali. Marekani ni nchi ya madeni. Kutodaiwa popote ni sifa nzuri katika utamaduni wa Tanzania. Lakini Marekani, sifa inakuja kutokana na umakini wa kulipa madeni. Mishahara ya Wamarekani wengi inaishia kwenye kulipa madeni. Kwa hivi, nao wanalalamika kuwa mishahara haitoshi.

Wako Watanzania ambao wana mishahara ambayo ingeweza kutosheleza mahitaji muhimu. Tatizo ni kuwa dhana ya mahitaji muhimu ina utata.

Tunaweza kusema mahitaji hayo ni chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, na usafiri. Lakini, katika utamaduni wetu, orodha ya mahitaji muhimu ni kubwa zaidi ya hiyo. Kumlipia ada mtoto wa shangazi ni wajibu. Kuchangia gharama ya msiba kwa jirani ni wajibu. Kama una gari, kumpeleka mtoto wa jirani hospitalini ni wajibu.

Kwa msingi huo, hakuna Mtanzania ambaye anaweza kusema mshahara wake unatosha. Suala haliishii hapo. Je, ukitembelewa na marafiki, utakaa nao tu nyumbani na kuongea nao, au unatakiwa kuwapeleka mahali wakapate kinywaji? Je, unaweza kuacha kuchangia gharama za arusi ya rafiki yako?Tukizingatia hayo yote, mishahara haitoshi.

Watanzania wengi wana tabia ya kutumia fedha kwa mambo mengi mengine, ambayo umuhimu wake ni wa wasi wasi, kama vile bia. Kwa Watanzania wengi, bajeti ya bia ni kubwa sana. Kwa mtu anayekunywa sana bia, mshahara hauwezi kutosha. Lakini je, bia ni kitu muhimu namna hiyo?

Kwa upande wa pili, Watanzania tunapaswa kutafakari dhana ya mshahara. Mshahara unapaswa kuwa malipo muafaka ya kazi ambayo mtu anafanya. Kazi ndio msingi. Lakini, kuna tatizo kubwa Tanzania.

Watu wengi hawafanyi kazi kwa bidii. Muda mwingi wanatumia kwenye gumzo. Lakini wanategemea kulipwa mshahara, na wanalalamika kuwa mishahara haitoshi. Je, wanastahili hizo hela wanazopewa kama mshahara? Je, wakiongezwa mishahara, wataongeza juhudi kazini au wataendelea kukaa vijiweni na kupiga soga?

Huku Marekani, watu wanachapa kazi sana. Mshahara unatokana na kazi. Mtu asipofika kazini, halipwi. Akichelewa, malipo pia yanapunguzwa. Kwetu Tanzania mambo si hivyo. Mtu akishaajiriwa, anategemea kupata mshahara wake kila mwezi, hata kama anatumia masaa mengi kijiweni. Je, ni bora kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wafanyakazi kwa yale masaa wanayokuwa kazini tu, na kupunguza mshahara kwa masaa wanayokuwa kijiweni?

12 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli kila mahali kuna malalamiko haya MISHAHARA haitoshi. Na kama ulivyosema mfano Tanzania ni kweli kabisa kuna wafanyakazi ambao kuanzia asubuhi mpaka jioni kazi yao ni kuzurura tu na hapo hapao analipwa kama kawaida. Hakuna anayefuatilia kama yupo kazini au vipi?. Ndio maisha yamepanda, na kila kitu kinapanda bei. Lakini kama mtu unaweza kuacha vile vitu ambavyo si muhimu basi nadhani unaweza tu kuyamudu maisha. Kwa nini ununue shati mpya wakati una mashati mengine matano kabatini? na kwa nini kila siku ule nyama wakati siku nyingine unaweza kula kisamvu. Kwa nini unywe bia kila siku wakati unaweza kunywa maji. Sawa, tunahitaji starehe, lakini ukipanga ufanye hivyo vitu kwa mwezi mara ngapi, nadhani haitakuwa mbaya sana. Ni mawazo yangu tu.

Subi Nukta said...

Nadhani imefika wakati sasa mfumo wa malipo ya wafanyakazi Tanzania ubadilike na watu walipwe kutokana na muda walioutumia kazini ikiwa ni pamoja na kuangalia matokeo ya muda uliotumika kazini wakati wa marejeo ya kila mwaka 'annual review'. Niliwahi kuuliza swali hili kwenye kundi pepe fulani ambalo ni mwanachama, kuwa, ni vigezo gani vimetumika kumpa mshahara mwajiriwa kila mwisho wa mwezi hata kama mwezi una siku 28, 29, 30 au 31 zikiwemo siku za sikukuu nk. lakini sikupata majibu wala kueleweshwa utaratibu huo. Je, si wakati sasa umefika kurejelea utaratibu huo na kuuboresha uendane na wakati wa sasa?
Hakuna kuwajibika (accountability) na mtu hajali kuwa ukifika mwisho wa mwaka wakati wa tathmini ya kazi yake kwa mwaka ataulizwa nini, kwa hivi haoni sababu ya kujishughulisha ili kutetea ajira yake, yeye anafahamu kuwa itakuwepo tu.
Haifai hivyo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nyie msituletee za kuletwa hapa kwetu tanzania.

yaani nyie kukaa sweden na marekani na kuona roho zao za kupenda na kuitukuza pesa basi mataka na kwenu tuige mambo ya wazungu? mtaiga mpaka lini nye wabongo msio fikiri?

mnadhani viwango vya mishahara vya huko utumwani mliko ni sawa na vya hapa tanzania?

boro kutawaliwa kimwili kuliko kutawaliwa kiakili na kiroho.

sasa kuna watu wanaolipwa shilingi lakini moja mpaka mbili kwa mwezi, huyu akiugua utakati shilingi ngapi kwa siku na abaki na kiasi gani na ataishi je?

kwa nini mnataka kuleta unyama wa huko utumwani hapa kwetu? mnataka kuleta mikono ya utumwa hapa ehe?

yaani mmewekewa mipaka ya kufikir kiasi kwamba hamna mwenye mawazo nje ya huo utumwa mnaouishi ehe?

kuweni makini mnapopendekeza upuuzi mwingine bwana. bongo binadamu wote ni sawa na ni ndugu na ndio maana unaweza kuwa huna ela lakini usife njee. kwa maneno mengine mshahra wa mtu mmoja unasaidia watu lukuki./
hapa ni ubinadamu kwanza mambo ya pesa na miliki za dunia hii ni baadaye.

kaeni utumwani na mfurahie maisha ya utumwani na msituletee mizizi ya utumwa kwetu
na kama mnaona maisha ya uko ni sawa poa tu kivyenu.


yainta unapoongelea sitarehe ya pombe, na wanaokunywa gongo ya shilingi hasini je? mnadhani wanakunywa kwa starehe au ugigili?
roho ya pesa imewatawala basi ni matatizo. kwani inamaana gani mtu akikaa ofisini mua mwingi na kuzalisaha kidogo na kukaamuda mfupi lakini kakafanya mambo makubwa?

familia kibao za kitanzania zina upungufu wa chakula na wengi hapa bongo wanaupungufa wa vyakula vya kutosha.
chakula kikipakuliwa, spidi yako ndiyo itakayokuonkoa, sasa muanze ujinga wa kupunguziana mishahara ili iweje? mnataka ndugu zenu wafe njaa ehe?

nasisitiza tena; SIO KILA MKIONACHO HUKO UTUMWANI KINAFAA KUIGWA, MENGINE NI HATARI KWA WATU WETU AU NDUGU ZENU

NB; mimi binafsi sjiaajiriwa na mtu yeyote na ninapata pesa kutokana na bidii yangu ya ufanyaji kazi, lakini ni lazima tuwe makini na maisha ya wakoloni

Mbele said...

Ndugu Kamala, shukrani kwa kutembelea blogu yangu. Masuali unayouliza ni mengi, na duku duku unazotoa pia. Nategemea zitawahamasisha wengine kutoka msituni na kuchangia.

Mbele said...

Ndugu Kamala

Leo nina fursa ya kuongelea masuali yako, kwani nilikuwa nimezidiwa na shughuli.

Mimi ni Mtanzania, kama wewe. Tanzania ni yangu, kama ilivyo yako, na sote tunawajibika kuichangia kwa hali yoyote tunayoweza.

Popote tulipo, tunawajibika kutafuta fursa ya kuichangia Tanzania. Ukifuatilia mawazo ya Mwalimu Nyerere utakuta alitoa mfano wa kijana anayepelekwa mbali akatafute chochote kwa ajili ya kijiji chake. Ni fundisho alilotoa, wakati anaongelea suala la kuwasomesha vijana na wajibu wa hao vijana wa kuchangia nyumbani. Cha muhimu ni ule moyo wako. Kama unaipenda nchi yako, utaitumikia popote ulipo.

Kwa mzalendo, kukaa nje si hoja. Nje kuna fursa tele za kuchangia, kwani fursa zilizopo nje hazipo nyumbani. Ninawafahamu Watanzania wengi huku Marekani ambao wanafanya makubwa kwa nchi yao kwa kutumia fursa zilizopo huku Marekani.

Kwa maana hiyo, kama wote ni wazalendo, hakuna sababu ya kuwatenga waliopo nje na walipo nchini. Haya mawazo uliyotoa hayatatufikisha mbali. Nchi za wenzetu, hata hapa hapa Afrika zinatambua hayo. Kenya, kwa mfano, ina kitengo katika wizara ya mambo ya nje, kinachoshughulika na watu wao waishio nje. Nchi ya Mali inayo wizara kamili ya kushughulika na wananchi wao wanaoishi nje. Nchi hizi zinatambua faida ya kuunganisha nguvu za hao walioko nje na wale walioko ndani. Tanzania tunajiumiza wenyewe tukiendekeza fikra kama ulizotoa.

Sisi hatupigi kampeni kuwa tuige mambo ya wazungu. Tumelenga kwenye suala la mishahara na kazi. Ndio mada pekee ambayo tumeongelea. Si haki kudai kuwa tunapiga kampeni ya kuiga mambo ya wazungu. Wazungu mambo yao ni mengi, mengine mazuri na mengine mabaya.

Kuhusu kufanya kazi kwa bidii, hatuna hata sababu ya kuwataja wazungu. Tulipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alituhimiza kwa usemi wa "Uhuru na Kazi." Na watu nchini kote waliitikia, wakawa wanafanya kazi sana. Sio suala la kuiga wazungu. Taifa letu lilianza na maadili ya kufanya kazi kwa bidii. Baadaye tumeingiza uzembe, na sasa watu wengi wanakaa vijiweni na kungoja mishahara hapo hapo kijiweni. Hili ndilo tatizo, wala si suala la kuiga wazungu.

Mtu yeyote anayeipenda Tanzania anawajibika kuunga mkono dhana ya kufanya kazi kwa bidii. Kutetea vijiwe ambavyo vinafanyika wakati wa kazi ni kuhujumu Taifa. Vijiwe vije tukishamaliza kazi, wakati tumechoka na tunahitaji kupumzika. Hapo ni sawa kwenda vijiweni kusogoa.

Kama tunakubaliana kuwa msingi huo wa Uhuru na Kazi ambao tulianza nao, ulikuwa sahihi, sioni kwa nini leo mtu akisema tufanye kazi kwa bidii iwe ni dalili ya kutawaliwa kiakili. Je, huyu Mwalimu Nyerere aliposema Uhuru na Kazi, alikuwa ametawaliwa kiakili? Wananchi nchini kote waliosikia wito wa Nyerere, walifanya vibaya?

Dunia ya leo, ya utandawazi, ina ushindani wa kutisha. Tusipofanya kazi hatutafika popote. Na kazi hizo si za kuzalisha tu katika uchumi, bali pia kujiongezea maarifa na elimu. Tusipopunguza vijiwe tutaangamia.

Ni kweli mishahara ya wengi nchini ni midogo. Lakini, dawa ya tatizo hili si kukaa vijiweni. Kufanya kazi ni njia ya kuinua uchumi na hii ndio njia ya kuinua kipato. Badala ya kukaa kijiweni, ni bora watu wawe wanajiongezea ujuzi na elimu, ili kujiweka katika nafasi ya kupata fursa bora kazini au kuweza kujiajiri. Ujasiriamali ni wazo ambalo wenzetu duniani wanatumia. Badala ya kukaa na kulalamikia mishahara midogo, ni bora kutafuta maarifa na ujuzi na kutafuta fursa za ujasiriamali. Vijiwe si dawa.

Mwishoni mwa ujumbe wako, umekiri kuwa wewe unajipatia kipato chako bila kuajiriwa na mtu, bali kutokana na juhudi yako ya kufanya kazi. Hujatuambia kuwa unashinda kijiweni. Sasa kwa nini unatulaumu sisi ambao tunasema hilo hilo unalosema, kuhusu umuhimu wa kufanya kazi? Kwa nini unatuambia sisi tuna akili za kitumwa, au tumewekewa mipaka ya kufikiri? Na wewe ambaye pia unazingatia kazi, tukuite una mawazo ya kitumwa au umepangiwa mipaka ya kufikiri?

Maadili ya kwetu ya kusaidiana ni mazuri, kama unavyosema. Hapa tunakubaliana. Ni jadi ya kuihifadhi. Mimi ni mwandishi, na nimeshaandika kuhusu tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mwamerika, na katika maandishi yangu huwa nataja mazuri na mabaye ya pande zote. Yako ambayo Waafrika tunaweza kujifunza kutoka kwa Waamerika, na yako ambayo wao wanaweza kujifunza kutoka kwetu.

Mimi ninawafahamu Wamarekani. NI watu kama sisi; wako ambao ni wema, na wako ambao ni wabaya. Hakuna tofauti na wanadamu wengine.

Mfumo wa uchumi wa nchi yao ni wa kibepari, na huu tunaweza kuuita unyama, kama alivyouita Mwalimu Nyerere, lakini si sahihi kuwaita Wamarekani wote kwa jina hilo. Wengi wao wanaupinga mfumo huo, kwani unawaumiza.

Binafsi, nachukulia maisha kuwa ni fursa ya kufanya mambo ya manufaa kwangu na wanadamu, sio fursa ya kustarehe. Suala unaloliongelea, la kufurahia maisha, halinihusu. Muda wangu mwingi natumia katika kujielimisha, ili niwe mwalimu bora zaidi na zaidi. Nikichoka napumzika kidogo, halafu naendelea na kazi. Dhana ya kufurahia maisha haina umuhimu kwangu.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

anony anayesingizia visa hajui mimi nimewahi kutembelea nchi ngapi mpaka sasa. anaona ni ukosefu wa visa tu na hajui nina uchaguzi gani katika maisha na labda sijui nini maana ya kuishi kama mfalme, wapi na vipi.

mbele, ni kweli uliyoyasema kwa kiasi kikubwa lakini mimi ninachokipinga ni tabia ya kuiga hata upuuzi na roho mbaya za wazungu.

kwa mfano kwanini tuanze na uwanyanyasa wafanyakazi kwa kuwanyima viisenti wanavyopata ambavyo hata hivyo haviwatoshelezi?

ni lazima tuanze na hiyo? kwani nyie mnaojiita wasomi na wataalamu wa dunia hii, hamna mawazo mapya na njia mpya za kujikomboa mpaka mfuurahie mfanyakazi wa bongo kunyimwa mshahara wake?

na je, pamoja na usomi wenu huo, unaonia ni sawa kwa bindamu mwenzako kunyimwa chakula (mshahala) wakati anaumwa? kama unaona nisawa, basi ukae tu ughaibuni.
na kama hayo ndio mawazo ya watu wa ughaibuni, basi mfilie huko huko hatuhitaji kuwa na wizara wala kitengo cha wakazi wa nje.

ninachosema hapa ni kwamba nchi kama yetu ambayo haina dira wala mwelekeo, watu watapata motisha gani wa kufanya kazi kwa bidii? watu wasiojitambua? wenye mawazo kama ya kwenu ya kukumbatia uzungu akija mzungu basi kuanzia kwa raisi mpaka mawazili wanachekelea?

kwani nyie hamuwezi kuja na njia mpya au hata kuwashauri wazungu kuachana na huo unyama wao na uuaji wakawa kama kwentu juu ya wafanyakazi wao wagonjwa, na kuwafikiria vyema kama watu wenzao?
upi utu kati ya wafanyiwavyo watanzania wagonjwa na wazungu au watumwa mlioko utumwani?

si kila kitu tutakiacha lakini ubinadamu wetu tutaondoka nao?

NB nayaongea haya lakini ninao ndugu wa kutosha huko utumwani, US na kanada na mipango yote ya mimi kwenda huko niliikataa mapema tu.

Mzee wa Changamoto said...

Alright!!
Amani, Heshima na Upendo kwenu nyote. Nami kama wengine ntawiwa kuikimbia mada na kutoa maoni kuhusu maoni maana ni sehemu kubwa na yenye nguvu kwenye ma-jamvi yetu haya.
Usomaji na utoaji wa maoni unatukutanisha na watu wenye uwezo, imani na mitazamo tofauti. Kwa hiyo kwangu naona kuna mawili kwa mtoaji na msomaji wa maoni hayo. Kwanza ni lazima kuzingatia kuwa hasira hupunguza busara. Namaanisha kuwa ukitoa ama kusoma maoni ukiwa na hasira kuna mengi utakayoshindwa kuwa nayo bayana. Na pili kwa msomaji kuna wakati yapaswa kuangalia zaidi "point of view" kuliko tone ya mtoa maoni. Na hili litasaidia maana kuna wengi wetu ambao huwa tunaandika kama tunavyoongea. Kwa hiyo kama hutazingatia hilo waweza kupata shida kiasi.
Na sasa nirejee ktk maisha ya kutatua tatizo kwa namna tulionavyo. Nilifundishwa kuwa katika kila linaloonekana kama jambo baya kuna uzuri ndani yake.
Nadhani wapo waliokerwa na maoni ya Kamala lakini nadhani kwa ujumla tunapaswa kujiuliza maswali ambayo yanapelekea kuwepo kwa mgongano wa mawazo hapa. Kwa mfano maoni ya Ndg Kamala yananipa CHANGAMOTO kujiuliza MAANA YA UTUMWA KATIKA ULIMWENGU WA SASA, YUPI MTUMWA NA VIPI UNATENDEKA.
Kwa hali ilivyo ntakubaliana kutofautiana na Kamala kuwa Utumwani ni huku. Na hata kama ni huku naamini kuwa utumwa ulioko nyumbani ni m'baya zaidi. Na pia sidhani kama kuna makosa ya kuiga mfumo unaoweza kuwa bora kutoka mahala ambapo unaamini si bora. Hata kama si masuala ya mshahara, lakini kuna mengi mema ambayo yanatendeka kuwawajibisha wanaofanya yasiyofanyika. Ukiangalia katika haki za wananchi, huduma za wateja (customer services), siasa na mengine mengi utagundua kuwa hatua waliyofikia huku ni kubwa ukilinganisha na nyumbani na sidhani kama tunaweza kupinga kujifunza kwa kuwa tu "tutaiga toka utumwani."
Utumwa unaofanywa na viongozi wetu kwa wananchi wetu nadhani ni wa kinyama kuliko uliofanywa na watu ambao lengo lao lilikuwa kuja kutenda hilo. Sasa hivi watu wanahenya kufanya kazi, kuonekana wanajenga nchi na kisha matokeo yake pesa inaingia kwenye akaunti za watu ambao wanatenda makosa hayo huku wakipindisha katiba tena kwa makusudi na kisha wanatumia kinga za kikatiba kutokwenda kujibu mashitaka. Huwezi fanya hayo huko unakokuita "utumwani".
Huku "uhuruni" ambako watu wanajilimbikizia mali kwa mshahara usiojulikana tena akiwa kwenye nafasi ya kuitumikia jamii na hakuna mwenye uwezo wa kumuuliza, huwezi kufanya hivyo ukiwa huku "utumwani."
UKWELI NI KWAMBA TAFSIRI YA UTUMWA IMEBADILIKA NA SASA TUNAKUWA WATUMWA WA KAKA NA DADA ZETU HUKU WANAOPANGA HAYO WAKISTAREHE NA KUSHEREHEKEA HAYO NJE YA NCHI.
Utumwa wa zamani ulikuwa nyumbani ukitendwa na wakoloni lakini UTUMWA ULIOSEMA KUWA NI M'BAYA ZAIDI ni huu unaotendwa na viongozi wetu wanaosema kuwa WANAWAPENDA NA WAKO HAPO KUTETEA MASLAHI YA NCHI YETU ilhali hakuna wanalofanya zaidi ya kuiba na kutumikisha jamii.
Naomba kuwakilisha kipande hiki. Ni mtazamo wangu kulingana na namna nionavyo tatuizo, na naendelea kutunza haki ya kukosea na kukosolewa.
Blessings

Sophie B. said...

Wow! nina mengi ya kuandikia kuhusu suala la mishahara ila kwanza nitatoka nje ya topic niongezee kidogo kuhusu issue aliyoi-rise Ndugu Kamala kwamba "mbele, ni kweli uliyoyasema kwa kiasi kikubwa lakini mimi ninachokipinga ni tabia ya kuiga hata upuuzi na roho mbaya za wazungu"
Mie nafikiri si sahihi kujumuisha watu (wazungu in this case)na kuwaita wapuuzi na kuwa wana roho mbaya. Hili si kwa wazungu tu bali kwa binadamu yeyote si utu wema,si sheria na wala hata dini zote haziruhusu. Binadamu wote ni sawa tukumbuke hili.
Pia napenda kui-back comment yangu kwa maelezo kuwa baadhi ya fursa tulizonazo watanzania zimetokana na misaada ya kutoka Magharibi na ikapokelewa na Rais wetu kwa mikono miwili kuwa itakuwa na faida kwa maendeleo yetu watanzania na nchi yetu kwa ujumla. Mwaka jana 2008 Mh. Rais Kikwete alipokea American aid worth nearly $700 million. ikiwa na lengo ya maendeleo kwa kila mtanzania including mimi na Ndugu Kamala.
Ifuatayo ni riport ya makabidhiano hayo:

"US boosts aid to Tanzania
Posted Mon Feb 18, 2008 12:44am AEDT

On his second day in Africa, US President George W Bush has signed an agreement with Tanzania to provide American aid worth nearly $700 million.

The five-year aid package is seen as a mark of approval for Tanzania, for observing democratic principles and sound economic policies.

Tanzanian President Jakaya Kikwete promised to justify the confidence America had placed in his country by approving the aid.

"Today with the signing of the MCA compact you are making it possible for the people of Tanzania to chart a brighter future ... by growth, opportunity and democracy," he said.

"We owe it to you and indeed to the American people that this compact meet its objectives and becomes a source of pride and satisfaction for our two governments and peoples

Source:http://www.abc.net.au/news/stories/2008/02/18/2164964.htm

Ikumbukwe kuwa hii ni pesa ya Wamarekani(WAZUNGU na wamarekani weusi). Hao hao wanafanya kazi kwa bidii, wanakatwa makato tunapata misaada Je ni haki sie tuendelee kukaa vijiweni ,kuwaita majina mbalimbali na kutofanya kazi kwa bidii?
Prof. nakupongeza kuleta mada muhimu naamini namna hii tunajifunza na kuelimishana mengi. Naamini Tanzania itaendelea tutapofikia ku-debate mambo muhimu pasipo hasira wala chuki wala kunyosheana vidole bali kwa kutoa hoja zenye nguvu na hii ndiyo sifa kubwa ya best debators. Nawasilisha.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

prof, mbele

umesoma ukweli alioutoa Evarist? umeiona mipaka ya kufikiri uliyokuwa nayo wewe na ninayoiongelea? umekubali kwamba japo nilionekana kuropoka kwani msema ukweli sikuu zote huanza kwa konekana mlopokaji, lakini umedhibitisha kwa macho yako mipaka hiyo ya kifikara?

je wewe pamoja na u-prof wako, umeona kuwa bado unapaswa kujifunza mengi kutoka kwetu kizazi kipya kisichokuwa na elimu ya kitumwa na ya kikoloni na iliyopitwa na wakati kama ya kwako?

ebu kuwa muwazi basi, ikopi comment ya everist na kuipaste hapa ili uanike mipaka yako na uvivu wako wa kufikiri ndugu yangu.

ni enzi za ukweli na uwazi sio vinginevyo.

maprofessa wengine bwana, mna mawazo yenu. kumbuka ni vizuri kujieleza kwani tutaujua uwezo wako wa kufikiri na kung'amua mambo kwa kusikiliza maongezi yako na kuangalia uwezo wako wa kutafsiri na kujua mambo.

Christian Bwaya said...

Kamala,

Naomba nikushauri jambo moja.

Lugha unayotumia inaweza kumzuia kabisa msomaji, ambaye bila shaka unamkusudia, ashindwe kukuelewa. Hoja yako nzuri inaweza kufifiishwa na baadhi ya maneno ambayo, kwa bahati mbaya hukuyachagua kwa makini.
Matokeo yake, mbadala wa hoja yako unaikwepa hadhira.

Pamoja na haki ya kusema unachoona kinastahili, ni vizuri kukwepa maneno fulani fulani yanayoweza ama kumfedhehesha huyo unayemlenga au kumfanya msoma maoni hayo kupata hisia zilizo za kweli pasipo ulazima wowote.

Mbele said...

Ndugu Kamala, nilishasoma maoni ya Ndugu Evarist kule kwa Dada Yasinta, na bila kuchelewa nilimshukuru, nikisema kuwa amenipanua mawazo. Sijui kama hukuona ujumbe wangu huo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Mbele,

nimekubali umekua kidemkrasia vinginebyo ungeleta ubaba hapa wa kuanza kunipangia maneno ya kutumia. nashukuru kwamba umenielewa hata kama natumia maneno makali kama anavyosisitiza bwaya, lakini unaheshimu uhuru wa kusema chochote kwa lugha yoyote bila kulazimishwa kuchagua sura ya maneno.

bwaya, wewe weka mwongozo kuwa wanaotumia maneno fulani katika mijadala, hupendi kuwaona na wala hutamani kuwasikia na zaidi katika blog yako. vinginevyo sijasomea lugha na wala sijalelewa na wazazi, ni mtu wa kijiweni na lugha yangu ni yakijiweni zaidi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...