Mwaliko Mkutanoni Finland

Nimepata mwaliko kwenda kushiriki mkutano wa wanataaluma Finland, katika chuo kikuu cha Turku. Mkutano ufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti na mada yake itakuwa The Role of Theory in Folkloristics and Comparative Religion." Nitakuwa mmoja wa watoa mada wateule, na mhadhara wangu utahusu "The Epic as Discourse on National Identity," kama ilivyotajwa katika programu hii hapa.

Mkutano huu wa wanataaluma umeandaliwa kwa kumbukumbu ya marehemu Profesa Lauri Honko, mmoja wa wataalam wakubwa kabisa duniani katika. Wa-Tanzania labda watafurahi kusikia kuwa Profesa Honko alifanya utafiti sehemu mbali mbali za dunia, ikiwemo Tanzania. Niliwahi kumwona,  na kuwa naye kwa wiki kama mbili hivi, wakati nilipohudhuria warsha ya watafiti ambayo aliiendesha Turku mwaka 1991. Alikuwa ni mtaalam sana, aliyekuwa anaongea kwa kujiamini kabisa, lakini mtu mtaratibu na mpole. Ukisoma vitabu vyake na makala zake, unaona wazi kabisa kuwa alikuwa mwenye mawazo mazito yenye kutoa mchango mkubwa kwa taaluma.

Kati ya mambo mengi aliyofanya, ikiwa ni pamoja na kuandika vitabu na makala na kutoa mihadhara, Profesa Honko aliisaidia UNESCO kwa kuandaa sera ya kuhifadhi utamaduni.

Sio jambo geni kwangu kupata mialiko ya aina hii. Najisikia raha kwenda kuuelezea ulimwengu fikra, mitazamo, na matokeo ya utafiti wangu. Papo hapo ni fursa ya kukutana na wataalam wengine na kubadilishana mawazo na uzoefu. Ndivyo taaluma inavyokua na kustawi.

Hata hivi, sitakuwa na raha sana kwenye mkutano huu wa Turku, kwani nitakuwa namkumbuka Profesa Honko.  Ni jambo jema kwamba mkutano utakuwa ni kwa kumkumbuka, lakinii papo hapo masikitiko ya kutokuwa naye yatakuwepo. Mungu amweke mahali pema Peponi.

Comments

Hongera kwa kupata mwaliko. Nakutakia kila la kheri. Usikose kupitia kwetu.
Mbele said…
Asante Dada Yasinta. Hii mialiko ina majukumu mazito, kwa maana ya maandalizi. Kwa muda huu niko katika maandalizi mazito.

Kisa ni kwamba huendi pale kuongelea au kukariri yale ambayo wanataaluma tayari wanayajua. Unatakiwa kuleta mawazo mapya, uchambuzi mpya, mwelekeo mpya. Unatakiwa kuisogeza taaaluma mbele.

Tunatakiwa kuandika makala, ambazo zitachapishwa kama kitabu. Hapo napo ngoma ni nzito.

Ukinipa simu yako, angalau nitaweza kukupigia nikusalimie. Kila la heri.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini