Wednesday, April 27, 2016

"Kibwangai:" Shairi la Haji Gora Haji

Ninaleta hapa shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," ambalo limechapishwa katika diwani yake iitwayo Kimbunga. Shairi la "Kibwangai" ni chemchemi ya mambo mengi yanayosisimua akili. Mwenye ujuzi wa nadharia za fasihi na uchambuzi wa fasihi atajionea utajiri uliomo katika shairi hili.

Nitalitafsiri shairi hili kwa ki-Ingereza katika siku chache zijazo, ili kuwapa fursa watu wasiojua ki-Swahili fununu ya umahiri wa Haji Gora Haji kama mshairi.

Nimeshatafsiri mashairi yake mawili: "Kimbunga" na "Nyang'au." Kutafsiri shairi au kazi yoyote ya fasihi ni mtihani mgumu. Lakini ni njia ya mtu kupima ufahamu wako wa lugha na ufahamu wa lugha ya kifasihi. Kwa kuwa lugha inabeba hisia na mambo mengine yanayofungamana na tamaduni, kutafsiri ni mtihani ambao unahitaji umakini usio wa kawaida.

KIBWANGAI

1.    Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
       Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
       Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
       Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

2.    Nyani bada kugundua, watu wanawaviziya
       Sababu yake kwa kuwa, huila yao mimeya
       Na ndipo wakaamuwa, mwenzao kumtumiya
       Ende akawalimiye, mazao yalo muhimu

3.    Kwenye uamuzi huo, baada ya kukusudiya
       Kibwangai jama yao, wakamkata mkiya
       Unyani kwa mbinu zao, kwake ukajitokeya
       Akawa yeye si nyani, bali ni binaadamu

4.    Yalisudi watakayo, nyani wakafurahiya
       Yaliposadifu hayo, wote wakachekeleya
       Walidhani watakayo, atawakamilishiya
       Nyoyo zikategemeya, na nyuso kutabasamu

5.    Pana mmoja kasema, Kibwangai kumwambiya
       Kama tutalokutuma, weza kututimiziya
       Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu sikiya
       Wewe tumekuchaguwa, utumikiye kaumu

6.    Kibwangai akasema, hayo nimezingatiya
       Kidete nitasimama, jitijada kutumiya
       Kwa kusia na kulima, mpate jifaidiya
       Sitobadili mawazo, ilipwe yangu kaumu

7.    Kibwangai lipoona, ni mtu kakamiliya
       Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya
       Wala hakujali tena, wenzake walomwambiya
       Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu

8.    Kawa na tabia moja, nyani walipomwendeya
       Akajifunga mkaja, mijiwe kuwarushiya
       Hakujali zao haja, wala kuwahurumiya
       Kapiga na kukemeya, pia na kuwashutumu

9.    Nyani likawakasiri,  ghadhabu wakaingiya
       Wakafanyiza shauri, Kibwangai kumwendeya
       Kwa nguvu au hiyari, kumpa wake mkiya
       Ili awe nyani tena, asiwe binaadamu

10.  Mkia bada kumpa, mambo yakawa mabaya
       Nguo zake kazitupa, unyani kumrudiya
       Kaanza kuchupa chupa, mitini akarukiya
       Akawafata wenzake, akiwa nyani katimu

11. Wenzake wakamcheka, wote na kumzomeya
       Akakosa la kushika, kwa haya kujioneya
       Majuto yakamfika, akabakia kuliya
       Akarudia porini, iliko yake kaumu

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Profesa,

Haji Gora alikuwa gwiji, kusimulia hadith kwa njia ya ushari si lelemama. Kubwa Shairi hili linamafunzo, tujadili-nilojifunza ni kuwa, mtu kuwa uwavyo na badilika utakavyo,lakini wapo kaumu yako wanaokujuwa, wanaokuona, wanaokushangilia au watakao kuzomea, iwe kwa siri au dhahiri, muhimu binadamu sijisahau ulikotoka, siku ipo ya kurejeshwa-kwa mola.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Ni sawa usemavyo, kwamba Haji Gora Haji ni gwiji wa kusimulia hadithi kwa njia ya ushairi. Alilelewa katika utamaduni wenye utajiri wa sanaa kama vile ngoma na nyimbo na hadithi za jadi. Katika maandishi yake, anatumia urithi huo. Kwa mfano, mashairi yake kadhaa ni usimuliaji wake wa hadithi za jadi. "Kibwangai" ni moja tu ya mashairi hayo.

Kwa mtindo wake huu, tukitumia mtazamo wa fasihi linganishi ("comparative literature"), Haji Gora Haji yuko katika mkondo mmoja na waandishi kama Shakespeare, Lu Hsun, Wole Soyinka, Gabriel Garcia Marquez, na Chinua Achebe.

Kwa wale wanaosoma au kufundisha fasihi vyuoni, kuna wajibu wa kuangalia kwa undani na kwa umakini utungo kama huu. Ni muhimu kukiangalia kila kipengele na kujaribu kubainisha kinavyoshirikiana na vipengele vingine katika muundo wa shairi, na namna kila kipengele kinavyoshiri katika kuibua dhana, maana, na tafsiri ya shairi kwa msomaji.

Kuthibitisha kauli hii, napenda kutolea mfano ubeti wa tano, kwa kifupi kabisa:


5. Pana mmoja kasema, Kibwangai kumwambiya
Kama tutalokutuma, weza kututimiziya
Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu sikiya
Wewe tumekuchaguwa, utumikiye kaumu

Hapa tunasikia jinsi Kibwangai anavyokumbushwa wajibu wake. Lakini kuna utata katika ubeti huu. Tumeshaambiwa kabla kuwa baada ya kukatwa mkia, Kibwangai aligeuka binadamu. Iweje katika ubeti huu anaambiwa "ewe mwenzetu sikiya"? Iweje nyani wamwite Kibwangai mwenzao, wakati yeye sasa si nyani tena?

Pia, inakuwaje nyani waweze kuongea na Kibwangai ambaye si nyani tena? Ameshakuwa binadamu kweli, kama tulivyoambiwa, au tulivyoambiwa si kweli? Au Kibwangai sasa ni kiumbe ambaye ana hali mbili, yaani ya nyani na ya binadamu?

Maajabu haya ya binadamu kuongea na wanyama ni ya kawaida katika hadithi za fasihi simulizi ya jadi. Ni suala ambalo limejadiliwa na wataalam wengi. Hata mimi mwenyewe katika kitabu changu cha Matengo Folktales nimelijadili.

Tukilifuatilia zaidi suala hili katika shairi hili, tutaona kuwa tangu mwanzo, hao nyani si nyani tunaowafahamu, bali ni viumbe wa kubuniwa, ambao wana tabia za binadamu. Tangu mwanzo, tunawaona wanavyokaa kikao na kutoa maamuzi, sawa na binadamu, wanavyomcheka mwenzao, wanavyoonyesha uwezo wa kuona aibu, na kadhalika. Hao si nyani tunaowaona huko porini.

Kwa mtazamo huo, hii hadithi si juu ya wanyama, bali ni juu ya wanadamu. Na hapo ndipo kauli zako Ndugu Khalfan Abdallah Salim zinapoingia. Umelitafsiri shairi hili kama ujumbe wa wanadamu kwa wanadamu.

Nikirejea tena kwenye suala la utata katika shairi hili, napenda kusema kuwa utata huu hauko katika ubeti huu wa tano tu. Ni hali halisi ya muundo mzima wa hili shairi. Hapo nawajibika kusema kuwa wanafunzi na walimu wa fasihi vyuoni wana wajibu wa kusoma nadharia za fasihi.

Kuhusu suala la utata niliogusia hapa, ambao unajitokeza katika shairi hili, napendekeza watu wasome insha maarufu ya Cleanth Brooks iitwayo "The Language of Paradox." Humo kuna maelezo murua ya namna ushairi unavyokuwa umejengeka katika misingi ambayo kwa ki-Ingereza hujulikana kama "paradox," "irony," "denotation," na "connotation." Si jambo la kujivunia kwamba ki-Swahili changu bado hakijapevuka ipasavyo. Ninatambua kuwa bado nina wajibu wa kujifunza zaidi lugha hii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...