Thursday, May 15, 2014

Kitabu Kingine Kufuatia "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences"

Ni yapata miaka tisa sasa tangu nichapishe kijitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences
Kadiri siku zinavyopita, wazo la kuandika kitabu kingine cha aina ile linazidi kuimarika akilini mwangu.

Tangu pale nilipochapisha Africans and Americans, nilifahamu kuwa sijaongelea masuala yote ambayo ningependa au ningeweza kuongelea. Sikupenda kuandika kitabu kikubwa; ilinibidi nifanye uchaguzi wa mada na kuandika kitabu kidogo.

Wazo la kuandika kitabu hiki cha pili nimekuwa nalo kwa miaka mingi. Kuna wasomaji wa Africans and Americans ambao, tangu mwanzo, walinishauri niandike kingine, ili kuongelea masuala ambayo sikuwa nimeyaongelea. Nami niliafiki wazo hilo.

Vile vile, kwa miaka yapata saba hivi nimeandika sura ambazo zitakuwemo katika hiki kitabu kipya. Ingawa Africans and Americans kimejipatia sifa tele miongoni mwa wasomaji, nilipania kuwa kitabu hiki kinachofuata kiwe bora  zaidi.

Uwezo wa kuandika kitabu bora zaidi ninao.Mungu akinijalia uzima, nitakamilisha kazi hiyo. Sio kazi ya wiki chache, au miezi michache. Nahisi itachukua miaka, ingawa, kama nilivyosema, sura kadhaa nilishaandika. Nataka kutumia uwezo wangu wa lugha kwa ufanisi kuliko ambavyo nimefanya kabla. Kitabu hiki kitakuwa kimeandikwa kwa ki-Ingereza kizuri sana, mfano wa kuigwa. Uwezo wa kuandika hivyo ninao, bora tu niwe na muda wa kutosha. Kama Ernest Hemingway alivyotufundisha, uandishi bora ni kazi ngumu inayohitaji muda sana.

Halafu, sina haraka, tofauti na mazingira ambamo niliandika Africans and Americans. Niliandika kitabu kile kwa kusukumwa na maprofesa tuliokuwa katika bodi ya uongozi wa Associated Colleges of the Midwest, ambao ni jumuia ya vyuo kumi na nne maeneo haya ya katikatika ya Marekani (USA. Kwa kutambua changamoto za kuwaelimisha wanafunzi wanaoenda kusoma Afrika kuhusu tofauti za utamaduni, na kwa kutambua kuwa hapakuwa na kitabu cha mwongozo cha kufaa kwa shughuli hiyo, waliniomba na kunishinikiza niandike. Nami nilifanya hivyo, ili kuhitimisha andiko hilo kwa muda mfupi, lianze kutumika.

Ninaongea hivi kwa sababu nataka kuwashauri wengine umuhimu wa kujiamini. Vitabu mbali mbali ambavyo nimekuwa nikisoma kuhusu maendeleo na mafanikio binafsi vinasisisitza umuhimu wa kujiamini, sio kuangalia zaidi vipingamizi, na matatizo, bali uwezo na fursa. Kitabu kimojawapo ambacho ningeshauri kila mtu asome ni The Power of Positive Thinking, kilichoandikwa na Norman Vincent Peale (New York: Simon and Schuster, 2011) kikachapishwa  mara ya kwanza mwaka 1952.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...