Saturday, November 19, 2016

"Ozymandias:" Shairi la Shelley na Tafsiri Yangu

Percy Bysshe Shelley ni mmoja kati ya washairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza, ambaye nilimtaja jana katika blogu hii. Alizaliwa mwaka 1792 akafariki mwaka 1822. Ni mmoja wa washairi wanaojumlishwa katika mkondo uitwao "Romanticism," ambamo wanaorodheshwa pia washairi wa ki-Ingereza kama William Blake, William Wordsworth, Samuel Taylor Coleridge, na Lord Byron. "Romanticism" ni mkondo uliojitokeza katika mataifa na lugha zingine pia, kama vile Ujerumani na Ufaransa. Kwa waandishi wa Afrika au wenye asili ya Afrika waliotumia ki-Faransa, "Romanticism" ilijitokeza kama "Negritude," jambo ambalo nimeelezea katika mwongozo wa Song of Lawino.

"Ozymandias" ni shairi mojawapo maarufu la Shelley. Ninakumbuka kuwa nililisoma kwa mara ya kwanza nilipokuwa sekondari, miaka ya kuanzia 1967. Kitu kimoja kinacholitambulisha shairi hili kuwa ni la mkondo wa "Romanticism" ni ule mtazamo wake ambao Edward Said aliuita "Orientalism." Lengo langu hapa si kuongelea "Romanticism" wala "Orientalism," bali kutaja mambo mawili matatu yanayohusu shairi la "Ozymandias" na suala la tafsiri.

Suala la kutafsiri kazi za fasihi nimeliongea tena na tena katika blogu hii. Pamoja na ugumu wake, ninaona kuwa baada ya mahangaiko yote, inakuja raha ya aina yake. Sio raha au furaha inayotujia tunaposhinda shindano au mtihani, kwani katika kutafsiri hakuna ushindi. Kinachotokea ni kuwa mtu unafanikiwa kuuzalisha upya utungo unaowania kuutafsiri.

"Ozymandias" ni shairi ambalo ninalielewa vizuri kabisa lilivyo katika ki-Ingereza. Lakini, nilivyojaribu kulitafsiri, tangu jana, limenihangaisha. Nimejionea jinsi ufahamu wangu wa ki-Swahili unavyopwaya. Nimejikuta nikijiuliza iwapo madai yetu wa-Tanzania kuwa tunakifahamu vizuri ki-Swahili ni ya kweli au ni porojo. Nilipata taabu zaidi kutafsiri mstari wa tano na mistari mitatu ya mwisho. Pamoja na kwamba nimeweka tafsiri yangu hapa, siridhiki nayo.

Kuhusu dhamira, shairi la "Ozymandias" lina mengi ya kujadiliwa. Kwa mtazamo wa fasihi linganishi, dhamira ya kisa cha msafiri inajitokeza katika tungo nyingi za tangu zamani. Mfano moja ni hadithi ya Misri ya kale iitwayo "The Tale of the Shipwrecked Sailor." Kuna pia hadithi za baharia Sindbad. Pia kuna shairi la Samuel Taylor Coleridge, "The Rime of the Ancient Mariner." Tungo zote hizi zina mambo ya ajabu na mtazamo juu ya ulimwengu na tabia za binadamu.

Vile vile, "Ozymandias" ni shairi lenye ujumbe mzito. Ni onyo kwa wanadamu kuwa utukufu wa hapa duniani, uimara wa himaya au udikteta ni vitu ambavyo vina mwisho. Ujumbe huu umo pia katika tungo zingine maarufu, kama vile utenzi wa Al Inkishafi. Naishia hapo.
--------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ozymandias

Percy Bysshe Shelley, 1792-1822

I met a traveller from an antique land,
Who said: "Two vast and trunkless legs of stone
Stand in the desert.... Near them, on the sand,
Half sunk, a shattered visage lies, whose frown,
And wrinkled lip, and sneer of cold command,
Tell that its sculptor well those passions read
Which yet survive, stamped on these lifeless things,
The hand that mocked them, and the heart that fed;
And on the pedestal, these words appear:
'My name is Ozymandias, King of Kings;
Look on my Works, ye Mighty and despair!'
Nothing beside remains. Round the decay
Of that colossal Wreck, boundless and bare
The lone and level sands stretch far away."

Tafsiri

Nilimkuta msafiri kutoka nchi ya kale
Ambaye alisema, "Miguu miwili ya mawe mikubwa sana isiyo na kiwiliwili
Imesimama jangwani....Karibu nayo, mchangani,
Ukiwa umezama nusu, uso uliopasuka vipande umelala, mnuno wake,
Na mdomo uliokunyata, na dhihaka ya mamlaka yabisi
Vyabainisha kwamba mchongaji alizifahamu sawasawa hisia zile
Ambazo bado zimedumu, zikiwa zimebandikwa katika vitu hivi visivyo hai,
Mkono uliovidhihaki, na moyo uliovilisha,
Na kwenye sehemu ya kusimamia yanaonekana maneno haya:
'Jina langu ni Ozymandias, Mfalme wa Wafalme:
Yaoneni niliyofanikisha, enyi wenye mamlaka makuu, mkate tamaa!'
Hakuna kilichosalia, pembeni mwa uharibifu
Wa ile sanamu kuu iliyoporomoka, bila upeo bila chochote
Mchanga mpweke umetanda hadi mbali kabisa."

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...