Nimeteuliwa Kwenye Bodi ya Rochester International Association

Mwezi huu nimeteuliwa kujiunga na bodi ya Rochester International Association, ambayo makao yake ni mjini Rochester, Minnesota. Rochester International Association inashughulika na program mbali mbali za kujenga mahusiano mema miongoni mwa watu wa mataifa na tamaduni mbali mbali.

Moja ya programu hizo ni tamasha liitwalo World Festival, linalofanyika kila mwaka. Nimewahi kushiriki tamasha hili mara mbili, nikaelezea habari zake katika blogu yangu ya ki-Ingereza, na blogu hii ya hapakwetu.

Shughuli za bodi ni za kujitolea. Kwa miaka yote niliyoishi hapa Marekani, nimejionea jinsi wa-Marekani wanavyozijali shughuli za kujitolea, nami nimekuwa nikishiriki shughuli za aina hiyo, kama vile katika programu zinazowapeleka wanafunzi Afrika. Kujitolea kwa manufaa ya jamii kunaleta faraja na furaha moyoni.

Kushiriki kwangu katika Rochester International Association kutaniwezesha kuchangia mawazo katika masuala ya tamaduni kama nilivyoyaelezea katika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kwa bahati nzuri, baadhi ya wanabodi wa Rochester International Association wamesoma kitabu hiki na ndio maana wamenipokea kwa msisimko.

Kushiriki shughuli za Rochester International Association ni jambo la manufaa kwangu katika kujijenga katika shughuli zangu za kutoa ushauri ambazo ninafanya chini ya mwavuli wa kampuni ndogo ya Africonexion: Cultural Consultants. Vile vile ni fursa ya kuiwakilisha Tanzania na Afrika huku mbali Marekani.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini