Wednesday, January 24, 2018

Mahagonny: Tamthilia ya Bertolt Brecht

Mwishoni mwa mwaka jana, mwanafunzi wangu mmoja hapa chuoni St. Olaf aliniomba afanye kozi ya kujitegemea chini ya usimamizi wangu. Tuna utaratibu wa kuwapa wanafunzi wanaohitaji fursa ya kufanya kozi za aina hiyo. Mwanafunzi anajitungia mada kwa kushauriana na profesa, na anaifanya kozi kwa kusoma vitabu na maandishi husika, kukutana na profesa mara kwa mara kujadiliana, anaandika makala na kufanya mitihani kadiri profesa anavyopanga.

Baada ya mazungumzo ya awali na mimi kuelewa alichotaka mwanafunzi huyu, kwamba alitaka kujielimisha kuhusu Marxism, na kwa kuzingatia masomo mengine anayosoma, katika sayansi ya jamii, nilimshauri kuwa mada ya kozi yake iwe  "Marxism, Alienation and Culture." Ingekuwa rahisi kwangu kuandika makala hii kwa ki-Ingereza, kwani sina hakika nitafsiri vipi dhana ya "alienation" kwa ki-Swahili.

Ili kuitafakari mada hii kinadharia, nilipendekeza mwanafunzi asome na tujadili ufafanuzi wa Marx na Istvan Meszaros kuhusu "alienation." Nilipendekeza tusome na kujadili jinsi dhana hii inavyotumiwa na Bertolt Brecht na inavyoweza kuhusishwa na riwaya ya Albert Camus, The Stranger.

Kwa kuwa Marx alijenga dhana ya "alienation" kwa kuihusisha zaidi na ubepari, nilipendekeza tusome tamthilia ya Bertolt Brecht iitwayo The Rise and Fall of the City of Mahagonny na tamthilia ya Arthur Miller iitwayo Death of a Salesman. Nilishauri pia tusome mawazo ya Ernest Hemingway kuhuru uandishi katika mfumo wa kibepari, alivyoandika katika Green Hills of Africa, na pia tusome shairi la Wordsworth, "The World is Too Much with Us," ambalo nililitaja katika blogu hii. Nilipendekeza pia tusome na kujadili pia ufafanuzi wa Walter Benjamin katika "The Work of Art in the Age of Mechanical Reproduction" na Raymond Williams katika "Culture is Ordinary."

Ingawa tumeshajadili mengi ya hayo maandishi, napenda kusema neno kuhusu tamthilia ya Brecht, The Rise and Fall of the City of Mahagonny. Niliona muhimu kumweka Brecht katika orodha, kwa sababu alielezea mbinu za utungaji na uigizaji wa tamthilia ambazo huitwa "alienation effects" zilizokusudiwa kuifanya tamthilia kuwa zana ya kuelimishia badala ya kuwa burudani tu na kichocheo cha hisia. Kwa kutumia mbinu hizo, Brecht alitaka watazamaji wa tamthilia wakumbane na masuala ya kufikirisha.

Brecht alikuwa na mwelekeo wa ki-Marxisti. Alifahamu jinsi ubepari unavyohujumu ubinadamu au utu. Hayo nilifahamu tangu nilipoanza kumsoma Brecht nilipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973. Miaka ile tulisoma Mother Courage and her Children na The Caucasian Chalk Circle, lakini tulifahamu pia kuhusu tamthilia zake zingine, kama vile Galileo. Nilivutiwa na Brecht kiasi kwamba nilijisomea The Rise and Fall of the City of Mahagonny.

The Rise and Fall of the City of Mahagonny inatuonyesha jinsi katika ulimwengu huu unaotawaliwa na pesa, hapendwi mtu, kama wa-Tanzania wasemavyo, bali ni pesa tu. Ukiwa na pesa, unakuwa na marafiki wengi. Ukiishiwa, huwaoni tena, na utajutia. Mhusika mmoja anasema: "What man's viler than a broke one?" yaani kuna mtu mbaya gani kumzidi aliyeishiwa? Tunaambiwa pia kuwa kuishiwa ni kosa la jinai na kwamba mtu asiye na pesa hastahili kuhurumiwa wala kusamehewa.

Pesa imekuwa kama ugonjwa ulioenea katika jamii. Hata mahakamani kumetawaliwa na pesa, kwani mahakimu na mawakili wananunulika. Ni kama alivyoandika Marx katika The Communist Manifesto: "The bourgeoisie has stripped of its halo every occupation hitherto honored and looked upon with reverent awe."

The Rise and Fall of the City of Mahagonny inatupa taswira ya jamii ambayo maadili yake yamevurugwa kabisa na suala la pesa.  Ingawa hapendwi mtu bali pesa, kwenye suala la pesa hakuna urafiki, kwa maana kwamba ukiwa na shida ya pesa, usimtafute wala usitegemee mtu wa kukusaidia. Hutampata, hata kama anazo. Tunashuhudia hayo yanavyomsibu mhusika aitwaye Jimmy. Tunamwona anavyowanunulia watu vinywaji wakati alipokuwa na pesa, lakini anapoishiwa na kujikuta matatani, watu wale wale wanamkwepa kabisa, bila aibu.

Tunakaribia kumaliza kozi yetu. Mada ya "Marxism, Alienation, and Culture" ni pana. Nategemea kuwa kwa siku chache zilizobaki, tutazama zaidi katika kile kinachoitwa "popular culture." Hata hivyo, tumeweza kuichambua kiasi cha kufahamu angalau vipengele vyake muhimu, hasa mitazamo juu ya dhana ya "alienation."

1 comment:

Anonymous said...

What a fantastic course the person had here, and the book Mahagonny sounds really like we all need to read it. What an honor to know you, Jospeh. I have not been commenting on your posts because my computer has been down. It is up again and running. Your students are blessed to have your depth of knowledge at their fingertips...plus your great and wonderful sense of humor..and peace. Blessings, Thank you for this post.. I so appreciate you..Merri

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...